Uchambuzi: Ambacho Watanzania hatutajifunza miaka 60 ya uhuru

IslamTZ

JF-Expert Member
Nov 22, 2010
309
182
1.jpeg

ABUU KAUTHAR

Moja ya msingi mkuu wa demokrasia ni mamlaka kwa umma. Ina maana, mamlaka yapo kwa wananchi ambao wamekasimu madaraka kwa viongozi waliowachagua katika uchaguzi huru na wa haki ili kutenda kwa niaba yao.

Nchi ambazo mamlaka hayatoki kwa wananchi ikiwemo zile zinazoongozwa na mfalme ambaye pia ni kiongozi wa serikali, haziwezi kuwa za kidemokrasia kwani mtu mmoja au kikundi cha watu huamua kila kitu na wananchi hawana mamlaka ya kuwahoji.

Lakini hutokea pia katika baadhi ya nchi katiba na sheria vinawapa mamlaka wananchi lakini hawayatumii kwa sababu ya elimu ndogo ya uraia, mwamko duni na kadhalika.

Tanzania ni nchi ya kidemokrasia lakini kwa kiasi kikubwa raia zake hawajahamasika au hawajelimika vya kutosha kuhusu mamlaka na nguvu yao katika uendeshaji wa nchi. Nikitafakari miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, naona kuwa hilo ndio jambo kubwa ambalo Watanzania tunahitaji kulirekebisha katika nukta hii ya historia yetu.

Hoja yangu hii imesadifu vema katika miaka 60 ya Tanganyika (sio Tanzania) kwa sababu kuna tofauti kubwa ya kujitambua, kuelimika na hamasa ya kisiasa kati ya Tanganyika na Zanzibar. Kwa ujumla, wengi watakubaliana nami kuwa, Wazanzibari wanajitambua zaidi, kisiasa.

;
4.jpeg
5.jpeg

Kioneshi cha tatizo

Unajua kiwango cha kujitambua/ au kutojitambua kwa watu kisiasa kwa namna wanavyoweza kuhusianisha maisha yao na siasa za nchi. Unapokuwa na idadi kubwa ya watu katika jamii ambao wanakwambia, ‘Mi sipendi siasa’ kama vile ambavyo anaweza kuchagua kutopenda michezo au muziki, au Yanga au Simba, unajua hapo kuna tatizo. Bahati mbaya, tuna Watanganyika wengi wa hali hiyo.

Jambo la kusikitisha ni kuwa mifano ipo wazi ya namna maisha yetu yanavyoathiriwa na maamuzi ya wanasiasa. Kipindi cha marehemu rais wa awamu ya tano, John Magufuli, maisha yalibadilika mno, kwa uzuri au ubaya, ukilinganisha na kipindi cha mtangulizi wake, Jakaya Kikwete. Lakini ni kura za Watanzania ndio zilizomfikisha JPM Ikulu akiwaangusha wwagombea wengine katika chama na katika uchaguzi mkuu. Maamuzi yote aliyoyafanya yalitokana na wingi wa kura alizopata na kumfanya rais wa Tanzania.

Katika kipindi hicho cha awamu ya tano, watu walibomolewa nyumba zao bila kulipwa, maelfu waliachishwa kazi katika sakata la ‘wafanyakazi hewa’ lakini kwa upande mwingine migao ya umeme ilipungua, nidhamu kwenye ofisi za umma ilipanda na wamachinga walilindwa. Maamuzi yote hayo yaliathiri moja kwa moja maisha ya watu. Katika kipindi hiki cha Rais Samia Suluhu Hassan, baadhi ya watu wanamkumbuka JPM wakiamini kuwa angeishi mpaka sasa kusingekuwepo na migao ya maji na umeme.

6.jpeg

Tukizungumzia kuhusu migao ya umeme na maji, kuna somo kubwa. Kijana wangu mmoja wa kiume, miaka 20, huwa anapenda kunung’unika kila ninapoweka habari kwenye televisheni muda ambao yeye angependa kuangalia igizo la Bondita, akidai haoni siasa zinamgusa na kumuathiri vipi.

Wiki mbilizilizopita ameanza kuchota maji kwenye ndoo kuleta nyumbani baada ya kuanza mgao ambao huku kwetu ni kama tumetolewa kabisa katika mfumo. Siku hizi, aghlabu hutokea mwishoni mwa wiki umeme hakuna na hivyo hawezi kuangalia mipira. Nami nikachukua nafasi hiyo kumuelewesha namna siasa zinavyoweza kuathiri maisha yake.

Ukiangalia nchi hii kupitia mitandao hasa iwapo watu unaosuhubiana nao ni wanaharakati, unaweza kudhani watu wengi wameerevuka sana. Lakini kaa mtaani uishi na vijana katika maskani zao ujue nini hasa wanafikiri. Siasa, uongozi, mustakabali wa nchi, si katika vipaumbele vyao!

Na ukichunguza zaidi, hata huko mitandaoni, ni asilimia chache ya watu ambaa wana muamko wa kufikiria siasa na uongozi wa nchi yao, zaidi kule Twitter na ClubHouse, vinginevyo kule Instagram na Facebook ni umbea, miziki, maisha binafsi ya ‘mastaa’ ndio mada kuu.

Ukifanya fikra tunduzi, hali hiyo haishangazi sana. Vyombo vya habari vikuu vyenye ufuasi mkubwa katika jamii yetu ya Kitanzania, ukipanga tatu bora, ni vya udaku, watangazaji wa vipindi vyao maarufu wanaitwa ‘chawa’ wakifanya jukumu ‘muhimu’ la upambe na kuzungumzia maisha binafsi ya wasanii. Mada nyingine kubwa mitaani ni Yanga na Simba, Manchester na Liverpool vikiunganishwa na masuala ya kamari za ‘betting.’

Bahati mbaya sana ni kuwa hata hao wachache waliohamasika kisiasa waliopo mitandaoni wamegeuza siasa kuwa ushabiki, ubora wa hoja zinazotolewa katika mijadala upo chini sana, na hata kuna muelekeo wa kidikteta, unyanyasaji wa kimtandao na mashambulizi binafsi.

Hatima ya yote haya ni kutamalaki kwa udikteta wa viongozi, kushamiri kwa ufisadi na kukomaa kwa tabia ya viongozi kutojali, wakisema kwani watafanya nini? Hii demokrasia nusunusu, inatugharimu sana kama nchi na inabidi tunapoanza miaka 60 ijayo tubadilike
 
Back
Top Bottom