Uchambuzi Wa Kitabu; Own the Day, Own Your Life (Miliki Siku Yako Kuyamiliki Maisha Yako)

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,070
own your day.jpg

Kila mtu anapenda kufanikiwa kwenye maisha, kila mtu anapenda kupiga hatua zaidi kwenye kila eneo la maisha yake, kuanzia kwenye afya, kazi, biashara na hata mahusiano.

Ni rahisi sana kuweka malengo na mipango ya muda mfupi na muda mrefu, lakini inapofika utekelezaji wa mipango hiyo, ndipo ugumu na changamoto hujitokeza. Katika hali hiyo ndiyo wengi hukata tamaa na kuona kufikia maisha wanayotaka ni kitu kisichowezekana.

Mwanafalsafa Confucious alinukuliwa kusema safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja. Na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha na mafanikio. Chochote unachotaka kufikia, unaweza kukifikia kama utakuwa tayari kuanza kwa hatua ndogo.

Na ili kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa, maisha unayoyamiliki wewe, sehemu muhimu ya kuanzia ni kumiliki siku yako. Kwa maisha ya mafanikio siyo chochote bali mkusanyiko wa siku zenye mafanikio. Hivyo kama unataka kufanikiwa, kama unataka kuwa na maisha bora, unahitaji kuanza kwa kuimiliki siku yako, kuifanya kuwa siku bora kabisa kwako. Kisha unarudia zoezi hilo moja kila siku, na utashangaa unapiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Mwandishi Aubrey Marcus kupitia kitabu chake cha OWN THE DAY, OWN YOUR LIFE anatushirikisha jinsi ya kuimiliki siku, kuanzia unapoamka, unavyofanya kazi, unavyojifunza, unavyokula, unavyofanya mazoezi, unavyofanya mapenzi na unavyolala. Aubrey amegusia kila eneo la maisha yetu tunaloliishi kwenye siku yetu moja na jinsi ya kulifanya kwa ubora wa hali ya juu ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Badala ya kukazana na siku nyingi kama mipango mingi ya maisha ya mafanikio inavyoonesha, Aubrey anatuambia tukazane na siku moja, tuhakikishe tunayatumia vizuri masaa 24 ambayo tunayo kwenye siku yetu kitu kitakachopelekea tupige hatua kubwa.

Karibu sana kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha OWN THE DAY, OWN YOUR LIFE, tujifunze mambo muhimu ya kufanya kwenye kila eneo la maisha yetu kwenye siku moja ya maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa.

MOJA; MAJI, MWANGA, MWENDO.

Unapoianza siku yako, kuna mambo matatu muhimu sana unapaswa kuyafanya kama unataka kuimiliki siku yako. Mambo hayo ni rahisi kufanya na hayahitaji uwe na chochote cha ziada. Ukiyafanya vizuri unaitengeneza siku yako kuwa bora na yenye uzalishaji mkubwa. Mambo hayo matatu ni kama ifuatavyo;

1. Kunywa maji ya kutosha.

Unapoamka asubuhi, unakuwa umekwenda muda mrefu bila ya kupata chochote, hivyo mwili wako unakuwa na ukosefu wa maji, kitu ambacho kinaufanya uwe kwenye hali ambayo siyo nzuri. Hivyo kitu cha kwanza kufanya unapoamka ni kunywa maji na kiasi cha kunywa ni angalau theluthi moja ya lita ya maji. Maji yanapaswa kuwa kwenye joto la chumba, hivyo yasiwe baridi sana wala moto sana.

Unaweza kuongeza madini kwenye maji unayokunywa ili kuupa mwili nguvu zaidi.

2. Pata mwanga wa jua.

Mwanga ndiyo msingi mkuu wa maisha, bila ya mwanga mimea haiwezi kuishi na hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wanyama na kwetu binadamu. Mwanga wa jua unapeleka taarifa kwenye akili zetu kwamba kumekucha na siku imeanza. Pia mwanga wa jua ndiyo unatengeneza mfumo wa kulala na kuamka kwenye miili yetu. Bila ya kusahau, mwanga wa jua la asubuhi, unapofika kwenye ngozi unasaidia ngozi kutengeneza vitamin D ambayo ni muhimu sana kwa kujenga na kuimarisha mifupa. Hivyo pata mwanga unapoamka, ni muhimu kwa afya yako.

3. Uweke mwili kwenye mwendo.

Unapofika muda wa kuamka asubuhi, ni rahisi kutamani kuendelea kulala. Kwa sababu mwili wako umepumzika kwa muda mrefu, na kwa sheria ya mwendo, kitu kilichopumzika huwa kinaendelea kupumzika na kitu kilichopo kwenye mwendo huendelea na mwendo.

Unapoamka, unahitaji kuuondoa mwili wako kwenye hali ya kupumzika na kuuweka kwenye hali ya mwendo. Hivyo unahitaji kufanya kitu kinachouweka mwili kwenye mwendo. Siyo lazima yawe mazoezi makali, lakini mazoezi madogo madogo kama kukaa na kuinuka, kurukaruka kunaufanya mwili uanzishe mwendo ambao ni muhimu kwenye kuiendea siku ya mafanikio.

MBILI; PUMUA KWA KINA, BARIDI KALI.

Umeshaamka, umeshaupa mwili maji, mwanga na umepata mwendo, sasa unahitaji kuufanya mwili kuwa vizuri zaidi kwa ajili ya siku ndefu iliyopo mbele yako. Hapa kuna vitu viwili muhimu sana unahitaji kufanya, ambavyo ni kama ifuatavyo;

4. Pumua kwa kina.

Pumzi ndiyo njia kuu ya kuupa mwili hewa ya oksijeni ambayo ndiyo inatumika kuupa mwili nguvu na kuondoa hewa ya kaboni ambayo ni uchafu mwilini. Watu wengi wamekuwa wakipumua kwa mazoea, hivyo hawapati hewa ya oksijeni ya kutosha, na hivyo mwili haupati nguvu ya kutosha, na kibaya zaidi, hewa chafu inajikusanya mwilini kitu kinachopelekea mwili kuwa na uchovu.

Unahitaji kupumua kwa kina, ili kuingiza hewa ya oksijeni ya kutosha, na kuondoa hewa chafu ya kaboni. Unapopumua kwa kina, vuta pumzi ndefu, kwa pua, mpaka tumbo lako liingie ndani kabisa, kisha toa pumzi hiyo kwa pua mkapa tumbo lirudi juu. Fanya hivyo kwa kuhesabu mara 30 mpaka mara 50. Baada ya pumzi hizo za kina, unaweza kuendelea kupumua lakini sasa unashikilia pumzi baada ya kutoa hewa. Yaani unavuta pumzi mpaka mwisho, kisha unaitoa mpaka mwisho, kisha unabana pumzi, huingizi hewa, unafanya hivyo mpaka pale unapoona huwezi kuendelea kushikilia pumzi zaidi, hapo unavuta pumzi kwa kina na kutoa. Unaweza kurudia hilo mara nyingi uwezavyo.

Zoezi hili la kupumua kwa kina linaupatia mwili hewa safi ya kutosha, kuondoa hewa chafu na pia kuituliza akili yako.

5. Oga maji baridi.

Kitu cha pili kufanya ni kuoga maji baridi, maji baridi sana, ambayo yakifika kwenye ngozi yako unasikia kama yanakukata. Faida ya kuoga maji baridi ni kuupa mwili msongo wa muda mfupi, na hivyo kuufanya utengeneze kinga na kujiweka kuwa imara zaidi. Tumezoea kuiweka miili yetu kwenye misongo ya muda mrefu ambayo ni mibaya kiafya, na ndiyo inaleta magonjwa. Lakini misongo ya muda mfupi, kama unaotengenezwa na maji baridi ni muhimu kwa afya.

Kama upo eneo ambalo huwezi kupata maji baridi kwa urahisi, unaweza kuweka barafu kwenye maji ya kuogea na ukaoga maji hayo baridi kwa asubuhi, inauandaa mwili kwa mchakamchaka wa siku nzima.

TATU; MAFUTA ZAIDI, SUKARI KIDOGO AU USILE KABISA.

Harakati za afya na tafiti mbalimbali za kiafya zimekuwa zinakosea eneo moja muhimu, kuonesha kwamba mafuta ni mabaya, mafuta ndiyo yanaleta unene, presha na kisukari. Lakini tafiti za kina, zinaonesha kati ya mafuta na sukari, sukari ni mbaya sana. Sukari ndiyo unasababisha magonjwa mengi mno kuliko aina nyingine yoyote ya chakula. Na tunapozungumzia sukari, hatumaanishi ile unayoweka kwenye chai pekee, bali kundi zima la vyakula vya wanga, hivyo kuanzia ugali, wali, mkate ni kundi la vyakula vya sukari.

Katika kuifanya siku yetu kuwa bora, Aubrey anatupa misimamo mitatu muhimu sana;

6. Usitumie sukari asubuhi.

Kifungua kinywa unachopata asubuhi, kile unachoanza nacho siku yako, hakikisha hakina sukari. Kama tulivyoona, sukari inamaanisha kundi zima la vyakula vya wanga. Ubaya wa kupata sukari asubuhi ni kwamba inapelekea sukari kuongezeka kwa haraka kwenye damu, kisha mwili unazalisha homoni ya insulini ambayo inaondoa sukari kwenye damu, kitu ambacho kinapelekea sukari kupungua sana. Hii ndiyo ile hali inayosababisha kujisikia kuchoka sana saa moja mpaka mawili baada ya kunywa chai au hata kula.

Ukiepuka sukari asubuhi, unaepukana na hali hiyo ya kuchoka, na pia akili yako inakuwa kwenye hali ya kuweza kufanya maamuzi bora na mwili kuweza kuchukua hatua sahihi.

7. Tumia mafuta.

Tofauti na ilivyozoeleka, mafuta hayasababishi unene au ugonjwa wa moyo. Kinachosababisha unene ni sukari, ambayo ukitumia kwa wingi, mwili unakwenda kuihifadhi kama mafuta pale ambapo haitumiki.

Faida ya kutumia mafuta asubuhi, ni kwamba yanachelewa kumeng’enywa na hivyo sukari kwenye damu haiongezeki haraka, hivyo mwili wako unakuwa unapata virutubisho muhimu kwa wakati sahihi na kiwango sahihi.

Fanya kifungua kinywa chako kiwe na vyakula vya mafuta zaidi kuliko vya sukari, na utaianza siku yako ukiwa vizuri. Vyakula vizuri vya mafuta ni kama mayai, siagi, karanga, parachichi, nazi, samaki na nyama.

8. Usinywe chai kabisa.

Swali linakuja, kama njia pekee ya kupata kifungua kinywa ni kutumia sukari, je mtu ufanyeje? Aubrey anasema, usitumie kifungua kinywa kabisa, na siyo Aubrey tu, bali tafiti zinaonesha, kuliko kutumia sukari kwenye kifungua kinywa, ni bora usile chochote kabisa.

Hapa pia kuna mengi tumekuwa tunadanganywa, ile dhana kwamba kifungua kinywa ndiyo chakula muhimu zaidi kwenye maisha yako siyo kweli. Kifungua kinywa ni muhimu, lakini siyo muhimu sana kiasi kwamba ukikosa kifungua kinywa afya yako itatetereka.

Unaweza kuacha usitumie kifungua kinywa na ukajiandaa kupata mlo kamili mchana kama huwezi kuepuka sukari asubuhi. Hii itaufanya mwili wako kuwa kwenye hali ya ufanyaji mzuri wa kazi bila ya kuingiliwa na madhara ya sukari ya asubuhi.

9. Mpango mzuri wa kufunga.

Kufunga kunausaidia mwili kuwa imara, kutumia chakula ulichohifadhi mwilini na pia kujijengea nidhamu. Zipo aina nyingi za kufunga kulingana na utamaduni wa watu na hata dini pia.

Lakini mpango mzuri wa kufunga ni ule wa kuupa mwili muda fulani wa kutokuwa na chakula na muda fulani wa kuwa na chakula. Mpango huu wa kufunga unaitwa INTERMITTENT FASTING. Kwa mpango huu, unakula ndani ya masaa nane, kisha kufunga ndani ya masaa 16. Hivyo unaweza kupanga muda wa kula ukawa kuanzia saa sita mchana mpaka saa mbili usiku, kisha huli chochote kuanzia saa mbili usiku mpaka kesho yake saa sita mchana. Huu ni mpango mzuri kwa wale ambao hawawezi kupata kifungua kinywa kisicho na sukari. Wakati wa mfungo unaweza kunywa kinywaji chochote kisicho na virutubisho vya chakula.

NNE; VIRUTUBISHO MUHIMU.

Chakula tunachokula, mara nyingi huwa hakijitoshelezi, hakina kila aina ya madini na vitamini tunazohitaji ili kuwa na ufanisi bora kwenye maisha yetu. Hivyo tunahitaji kuongeza virutubisho hivyo kwenye chakula au maji tunayokunywa.

Unahitaji kuongeza vitamini B na vitamini D kwenye vyakula au maji, pia unahitaji kuongeza madini muhimu kama ya chumvi na madini joto ili mwili uweze kujiendesha vizuri.

TANO; MUDA WA KUENDESHA, MUDA HAI.

Muda ambao unaondoka nyumbani na kwenda kwenye kazi zako, iwe unatumia usafiri binafsi au usafiri wa uma, ni muda ambao kwa wengi huwa muda uliokufa. Ni muda uliokufa kwa sababu hawana cha kufanya na muda unakuwa unapotea, hasa kama unakaa kwenye miji yenye foleni za magari. Ili kumiliki siku yako, usikubali kuruhusu muda wa kwenda au kutoka kwenye kazi yako kuwa muda mfu, badala yake ufanye kuwa muda hai kwa kufanya mambo mawili muhimu sana;

10. Tuliza akili yako.

Akili zetu zimekuwa hazipati muda wa kupumzika, kwa sababu kila wakati kuna kitu tunafikiria au kitu tunahofia. Unahitaji kupata muda wa kutuliza akili yako na hata kufanya tahajudi au kutengeneza uwepo kiakili kwenye chochote unachofanya.

Kwa kuwa siyo rahisi kupata muda wa aina hiyo unapokuwa kazini, au hata nyumbani, tumia muda unaokuwa kwenye safari ya kwenda kazini au kurudi nyumbani kutuliza akili yako.

Kama unatumia usafiri binafsi, fanya zoezi la kupumua kwa kina, kuhesabu pumzi zako. Zoezi hili rahisi litatuliza sana akili yako. Kama huwezi kufanya zoezi hilo, na kama unatumia usafiri wa umma, tumia dakika chache kuifanya akili yako iwe pale ulipo, kwa kuangalia kila kinachoendelea, maeneo unayoyapita. Hili ni zoezi la uwepo kiakili ambalo ni aina ya tahajudi.

11. Lisha akili yako.

Kitu cha pili muhimu kufanya unapokuwa kwenye usafiri ni kulisha akili yako. Watu wengi hutumia muda wa usafiri kama muda wa kufuatilia habari, kuperuzi mitandao na mambo mengine yasiyo na tija. Kama unataka kumiliki siku yako na maisha yako kwa ujumla, usipoteze muda wako kwa mambo hayo.

Badala yake lisha akili yako, muda wa usafiri ndiyo muda mzuri kujifunza. Unaweza kusoma kitabu muda huo, na kama unaendesha au unatumia usafiri wa umma ambao ni vigumu kusoma kitabu, labda umesimama, basi sikiliza kitabu kilichosomwa (audiobook). Hii ni njia rahisi sana ya kujifunza ambayo haihitaji nguvu kubwa wala gharama kubwa, unaweza kutumia simu yako kusikiliza vitabu vilivyosomwa.

12. Chuo kikuu kinachotembea.

Unaweza kuifanya simu yako kuwa chuo kikuu kinachotembea, kwa kuweka kila aina ya maarifa na mafunzo unayotaka. Unaweza kuwa na vitabu vya kujisomea, vitabu vya kusikiliza, video za kuangalia na hata mahojiano mazuri unayoweza kusikiliza na kujifunza. Kama una simu, ifanye kuwa chuo kikuu kinachotembea, na ni rahisi sana kwa zama hizi tunazoishi.

SITA; MIMEA YENYE NGUVU KUBWA.

Maisha yetu hapa duniani, yanategemea mimea, bila ya mimea hakuna maisha, kwa sababu mimea ndiyo inatumia nguvu ya jua kutengeneza chakula, na sisi tunakula mimea hiyo, au tunakula wanyama ambao wanakula mimea. Lakini umuhimu wa mimea hauishii kwenye chakula pekee, bali ipo mimea yenye nguvu kubwa za kutuwezesha kutumia akili zetu. Kuna mimea mitatu yenye nguvu hizi kubwa;

13. Kahawa.

Kahawa ni mmea ambao unazalisha mbegu ambazo zikikaangwa na kusagwa, zinatoa kinywaji ambacho kinachangamsha akili, kuondoa uchovu na kufanya akili ifikiri vizuri. Kahawa imekuwa na manufaa makubwa kwa wengi na imewawezesha wengi kufanya kazi kwa muda mrefu.

14. Tumbaku.

Mmea wa tumbaku umekuwa na sifa mbaya sana kwa sababu sigara ambazo zinatengenezwa kwa tumbaku ndiyo kitu kinachoongoza kwa kuua watu wengi. Kila aina ya kansa inasababishwa na uvutaji wa sigara, iwe moja kwa moja au siyo moja kwa moja.

Tumbaku mbaya ni ya kuvuta kama sigara au njia nyingine. Lakini mmea wa tumbaku unapotumika ukiwa mbichi, na ukatumika kwa kutafunwa na siyo kuvutwa, unaipa akili nguvu ya kufanya makubwa.

15. Huperzia.

Huperzia ni aina ya mimea ambayo huwa inaota maeneo yenye vyanzo vya maji au kuwa na maji muda mrefu. Mmea huu umedhibitishwa kuchangamsha akili na kuongeza uwezo wa kufikiri bila ya kuwa na hatari ya kuwa na uteja kama ilivyo kwa madawa ya kulevya.

SABA; KUFANYA KAZI.

Kinachotufanya sisi kuwa watu, ni kazi ambazo tunafanya. Tumetengenezwa kwa namna ya kufanya kazi, jinsi miili yetu ilivyo na hata mikono yetu ilivyoumbwa ni mahususi kwa ajili ya kufanya kazi.

Katika kumiliki siku yako ili kumiliki maisha yako, kazi ni sehemu muhimu ya maisha yako. Huwezi kufanikiwa bila ya kufanya kazi. Hivyo usijidanganye na chochote cha kukwepa kazi, au kutafuta mafanikio bila ya kazi, penda kazi, fanya kazi na siku yako itakuwa bora, kitu kitakachopelekea maisha yako kuwa bora.

16. Usitumie muda kupima kazi.

Moja ya vitu vinavyofanya watu wengi wachukie ajira, ni pale kazi zinapopimwa kwa muda. Kwamba lazima ufike kazini saa mbili asubuhi na usiondoke mpaka saa kumi jioni. Unahesabiwa kufanya kazi kwa muda uliopo kazini, na hili limesababisha wengi kuwa na maisha ya ajabu. Kwa sababu kazi za watu wengi, zinaweza kufanyika kwa muda mfupi, hivyo wanatumia muda unaobaki kufanya mambo ya hovyo, yasiyo na maana kwao au kwa waajiri wao. Unafikiri kwa nini maeneo mengi ya kazi yana majungu? Kwa sababu watu wana muda mwingi kuliko kazi walizonazo, hivyo wanapata muda wa kuanza kujadili wengine.

Usipime kazi zako kwa muda, bali panga kwa ufanisi, panga kwa kile unachotaka kukamilisha. Panga ni nini unataka kufanya, kisha weka juhudi kukifanya, bila ya kuangalia ni muda gani unaotumia. Kama kitu ni muhimu, unapaswa kukifanya, na vingine visubiri mpaka ukamilishe hicho muhimu.

17. Unapofanya kazi, usiahirishe chochote.

Kuna kitu watu wamekuwa wanajidanganya kuhusu kazi, kwamba kama watajitesa na kuvumilia kwa muda mfupi, wakafanya kazi ngumu na kupata fedha, basi wataweza kuyafurahia maisha ya starehe baadaye. Huo ni uongo na usiendelee kujidanganya. Kazi yoyote unayochagua kufanya, jua utaifanya kwa maisha yako yote, hivyo wakati unafanya sasa, usiahirishe chochote. Fanya kazi yako na ishi maisha yako, maisha hayajagawanyika kwamba kwa sasa ni kazi na baadaye ni mapumziko. Kazi ni sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo maisha mengine lazima yaende.

18. Watu wenye furaha wanafanya kazi bora, na kufanikiwa pia.

Dhana ya furaha na mafanikio bado imekuwa inawachanganya wengi. Wengi hufikiri wakifanikiwa ndiyo watakuwa na furaha, lakini ukweli ni kinyume cha hilo, ukiwa na furaha ndiyo unakuwa na mafanikio. Furaha inaanza kabla ya mafanikio.

Kadhalika kwenye kazi, ukiwa na furaha, kazi inakuwa bora, na furaha siyo zao la kazi, bali kazi bora ni zao la furaha.

19. Kuwa na kitu kinachokusukuma kwenye kazi.

Kila aina ya kazi ni ngumu, inachosha na kuumiza. Kama unafanya kazi kwa sababu tu unataka ufanye kazi, au kama unafanya kwa sababu unataka upate fedha, itafika hatua hutaweza tena kuvumilia maumivu na mateso ya kazi unayofanya. Unahitaji kuwa na kitu cha ziada kinachokusukuma kufanya kazi. Unahitaji kuwa na maono makubwa unayoyafanyia kazi, unahitaji kuona thamani kubwa unayotoa kwa wengine na hilo litaipa kazi maana, litafanya mateso unayopata yawe na maana kwako na kwa wengine pia.

20. Miliki eneo lako la kazi.

Mazingira unayofanyia kazi, yana mchango mkubwa sana kwenye ufanisi wako wa kazi. Kama kazi yako inahitaji kufikiri kwa kina, kuwa kwenye eneo lenye kelele kutakuzuia kufanya kazi iliyo bora. Miliki eneo lako la kazi, yafanye mazingira yako ya kazi yakupe hamasa ya kufanya kazi na siyo kukukatisha tamaa au kukufanya uahirishe.

NANE; KULA CHAKULA CHA AJABU.

Ulaji wa chakula kwa wengi umekuwa kama kazi, kwa sababu vyakula ni vile vile ambavyo watu wanakula kila siku. Aubrey anatuambia, kama tunataka kufurahia chakula tunachokula, basi tunahitaji kula chakula cha ajabu, chakula ambacho siyo tulichozoea kula kila siku.

Kwenye chakula, kama ilivyokuwa kwenye kifungua kinywa, punguza sukari na weka mafuta zaidi. Andaa chakula chako mwenyewe kama huwezi kupata chakula bora kwako na hifadhi kwenye chombo kisichopooza.

21. Usiangalie wingi, angalia ubora.

Watu wengi wamekuwa wakichagua chakula kulingana na wingi wa kalori kwenye chakula husika. Hilo halina msaada kwenye kuifanya afya kuwa bora. Njia bora ya kuchagua chakula ni kuangalia ubora, na hapo unaangalia virutubisho na madini muhimu yanayopatikana kwenye kila chakula unachotumia.

22. Kula vyakula hai.

Zama tunazoishi sasa, ni zama ambazo kila aina ya chakula imetengenezwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kwa muda mrefu. Nyama inachinjwa na kuhifadhiwa kwenye makopo kwa matumizi ya muda mrefu. Hichi siyo chakula cha afya. Kazana kula vyakula ambavyo ni hai, vyakula ambavyo havijahifadhiwa kwa muda mrefu tangu kuandaliwa. Pia epuka vyakula vilivyowekwa kemikali za kuvitunza kwa muda mrefu.

TISA; MUDA WA KUSINZIA.

Tunaishi dunia inayoenda kasi, dunia ambayo mtu akilala muda mrefu anaonekana ni mzembe, na ukilala mchana basi unaonekana hujui unachofanya. Lakini kila mmoja wetu anajua kitu kinachotokea baada ya kula chakula cha mchana, mwili huwa unachoka na akili haifikiri vizuri. Huu ni muda mzuri wa kila mmoja wetu kupata muda mfupi wa kupumzika na kusinzia ili kuchaji akili zetu, kama ambavyo mtu unachaji simu pale inapopungua chaji.

23. Usikilize mwili wako.

Miili yetu huwa inatusemesha kwa njia ya dalili mbalimbali. Unaposikia uchovu, ni mwili unakuambia kwamba unahitaji mapumziko. Kadhalika pale unaposinzia, mwili unakuambia kwamba akili imechoka na inahitaji kupumzishwa. Unapojisikia kusinzia, tenga muda mfupi wa kulala, hasa mchana, ukiamka kwenye mapumziko hayo, utakuwa na nguvu ya kuendelea na kazi zako vizuri.

24. Urefu sahihi wa kupumzika.

Kupumzika mchana, au kusinzia siyo kitu cha kuonea aibu, kwa sababu ni kitu kinachokuwezesha kufanya kazi vizuri baadaye. Mfumo wetu wa usingizi una hatua nne, ambazo zinachukua dakika tisini kukamilisha mzunguko wa usingizi. Katika mzunguko wa usingizi, kuna wakati unakuwa kwenye usingizi wa juu juu na kuna wakati unakuwa kwenye usingizi wa kina. Unachopaswa kuepuka unapolala mchana, ni kuingia kwenye usingizi wa kina, maana ukiamka katikati ya usingizi wa kina, unakuwa umechoka sana.

Ili kuepuka kuingia kwenye usingizi wa kina, usilale kwa zaidi ya nusu saa. Dakika 20 mpaka nusu saa ni muda mzuri wa kulala mchana, ukiamka unajisikia ukiwa na nguvu zaidi na kuweza kufanya kazi zako vizuri.

Kulala huku haimaanishi mpaka uwe kitandani, unaweza kuegemea meza yako na kusinzia kwa dakika 20 mpaka 30 na kuamka kuendelea na kazi zako.

25. Njia nyingine ya kupumzisha akili bila ya kulala.

Kama haupo kwenye mazingira yanayokuruhusu kulala mchana, ipo njia nyingine ya kupumzisha akili bila ya kulala. Njia hiyo ni kusikiliza sauti ambazo zinachangamsha mawimbi ya akili yanayohusika na kupumzika. Akili zetu zina mawimbi mbalimbali, yapo mawimbi yanayohusika na kazi, na yapo yanayohusika na kupumzika.

Zipo sauti na miziki mingi inayoweza kutuliza akili bila ya kulala. Miziki hii inaitwa binaural beats. Unaweza kutafuta miziki hiyo na kuisikiliza, itakusaidia kupumzisha akili na kukuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

KUMI. MAZOEZI.

Hujaimiliki siku yako kama hujaupa mwili wako mazoezi. Unahitaji kutenga muda kwa ajili ya mazoezi ya mwili, mazoezi hasa, ambayo yanaufanya mwili kushughulika na kutoka jasho la kutosha. Unaweza kuweka muda huo asubuhi au jioni kulingana na mazingira yako.

26. Dawa ya maajabu inayotibu kila ugonjwa.

Mazoezi ni dawa ya maajabu, inayotibu kila aina ya ugonjwa kwenye mwili wa binadamu. Mazoezi yanaimarisha kinga ya mwili na hivyo kuufanya mwili kupambana na kuzuia magonjwa. Mazoezi pia yanaifanya akili kuwa makini na kuweza kufikiri kwa usahihi.

Ukosefu wa mazoezi, umekuwa chanzo cha matatizo mengi ya kiafya ambayo watu wanapitia kwenye maisha yao.

27. Huhitaji kutumia fedha nyingi kwa ajili ya mazoezi.

Wapo watu wanaoacha kufanya mazoezi kwa sababu wanaona hawawezi kumudu gharama za mazoezi. Watu wamedanganyika kwamba mazoezi ni mpaka watumie vifaa vya kisasa, vinavyoweza kuhesabu kiasi cha mazoezi ambacho wamefanya. Usidanganyike na hilo, wewe tumia njia za asili kufanya mazoezi. Una uwanja au barabara zinazokuzunguka ulipo, kimbia kwenye barabara hizo. Tengeneza uzito kwa njia za asili na beba uzito huo. Popote ulipo, unaweza kufanya mazoezi ya kutosha bila ya kuingia gharama za ziada.

28. Anza kidogo na kua kadiri muda unavyoenda.

Kosa kubwa wanalofanya wengi kwenye mazoezi ni kutaka matokeo ya haraka. Mtu anataka siku ya kwanza ya mazoezi aweze kufanya kila aina ya mazoezi na kwa viwango vikubwa. Wanapojaribu kwa hamasa kubwa wanayokuwa nayo, wanafanya makubwa leo, lakini kesho yake wanaamka wakiwa na maumivu makali, kitu kinachowafanya wasiendelee tena na mazoezi yao.

Anza kidogo na kua kadiri muda unavyokwenda. Kama hujawahi kukimbia kabisa, tembea mita kadhaa, kisha kimbia mita hizo, halafu kimbia kilomita moja na endelea kuongeza kadiri muda unavyokwenda na mwili unavyozoea.

KUMI NA MOJA; PUMZIKA NA TENGENEZA MAHUSIANO.

Siku ya kazi inapoisha na ukarudi nyumbani, unahitaji kujua huo ni wakati wa kupumzika, acha kazi eneo la kazi na rudi nyumbani kwa mapumziko na kutengeneza mahusiano yako na wale ambao ni muhimu kwako.

29. Tenga muda kwa ajili yako.

Siku nzima umeitumia kufanya kazi na mambo mengine, ambayo hayakuwa yanakuhusu wewe moja kwa moja. Lakini kumbuka wewe ni mtu muhimu kwako, hivyo unahitaji kutenga muda kwa ajili yako. Huu ni muda muhimu, ambapo unafanya chochote ambacho ni muhimu kwako, unapenda kukifanya lakini siyo kazi. Inaweza kuwa kucheza au kusikiliza muziki, kutumia vyombo vya muziki au hata kujisomea. Chochote unachopenda kufanya, tenga muda wa kukifanya kwenye siku yako.

30. Tenga muda kwa ajili ya wale ambao ni muhimu kwako.

Kuna watu ambao ni muhimu kwako, ambao wanayafanya maisha yako kwenda vizuri. Familia, jamaa na marafiki ni watu hao. Tenga muda kila siku kwa ajili ya watu wa familia yako. Wape muda wako, ambao hausumbuliwi na chochote. Hapa unahitaji kuwa mbali na simu au mitandao ya kijamii ili uweze kuwa na muda bora na wale ambao ni muhimu.

Kadhalika kwa jamaa na marafiki, tenga muda wa kukutana nao kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yenu.

KUMI NA MBILI; KULA CHAKULA CHA USIKU KAMA MFALME.

Chakula cha usiku ni muhimu sana kwa afya yako. Pia kinakuandaa kwa zoezi litakalofuata kabla hujalala. Hivyo unahitaji kuchagua vizuri vyakula gani unakula usiku, na muda sahihi wa kula ili mwili wako uwe na afya bora.

31. Unaweza kula chochote unachotaka kula, lakini kwa kiasi.

Kwenye kifungua kinywa na hata chakula cha mchana, tumeona unahitaji wa kuchagua kwa makini vyakula unavyotumia. Hii ni kwa sababu baadhi ya vyakula, kama sukari, vinauchosha mwili na hivyo unashindwa kufanya kazi vizuri.

Chakula cha usiku unaweza kula chochote unachotaka kula, lakini kwa kiasi. Hivyo kwenye chakula cha usiku unaweza kutumia sukari, kwa kiasi. Na kama unafanya mazoezi jioni, basi kula sukari kwenye chakula cha usiku hakuna madhara makubwa. Na kwa sukari namaanisha vyakula vyote vya wanga na sukari yenyewe.

32. Muda sahihi wa kula.

Muda sahihi wa kula usiku, ni angalau masaa mawili kabla ya kulala. Kadiri unavyokula mapema zaidi ndivyo chakula kinatumika vizuri na kujenga afya nzuri. Hivyo angalia muda unaolala, kisha hakikisha masaa mawili kabla ya muda huo unakuwa umeshamaliza zoezi lako la kula kwa usiku.

33. Vitu vya kuepuka wakati wa kula.

Usile chakula na kunywa maji baridi kwa wakati mmoja, au kunywa maji muda mfupi baada ya kumaliza kula. Maji yanaenda kupunguza makali ya tindikali iliyopo tumboni ambayo inameng’enya vyakula. Hii inapelekea vyakula visimeng’enywe na hivyo kushindwa kukupa virutubisho muhimu.

34. Kula taratibu, tafuna vizuri.

Watu wengi wamekuwa wanakula kwa haraka, hawatafuni vizuri na hilo linachangia matatizo mengi ya kiafya. Unapokula, kula taratibu, tafuta chakula chako taratibu mpaka kilainike chote kabla ya kumeza. Zoezi hilo linarahisisha umeng’enywaji wa chakula ambao unatokea tumboni.

KUMI NA TATU; KUFANYA MAPENZI BORA.

Kila unapoangalia, kila mziki, kila tangazo, kila tamthilia, nguzo kubwa ni ufanyaji wa mapenzi. Unafikiri kwa nini matangazo yanawekwa wasichana warembo au wanaume watanashati? Kwa sababu msukumo wa mapenzi ni mkubwa kwa kila mtu. Ufanyaji wa mapenzi ni moja ya eneo la kuzingatia ili kumiliki siku yako. Unahitaji kufanya mapenzi bora ili mwili wako uwe bora.

35. Faida za kufanya mapenzi.

Ukiacha raha mtu unayopata unapofika kwenye kilele wakati wa tendo, kufanya mapenzi kuna faida nyingi kwenye mwili. Kunapunguza msongo wa mawazo na mwili, kunachochea kuzalishwa kwa homoni muhimu kwenye mwili, kunaimarisha kinga ya mwili, kunapunguza sonona, kunasaidia vidonda kupona, kunapunguza mwili kuzeeka na kuongeza uvumilivu kwenye maumivu.

Baada ya mazoezi, ufanyaji wa mapenzi ni dawa nyingine muhimu sana kwa afya yako, na tafiti za kisayansi na kitabibu zinadhibitisha hilo.

36. Mapenzi bora ni yanayowaridhisha washiriki wote wawili.

Watu wengi huwa na ubinafsi kwenye ufanyaji wa mapenzi, hujiangalia wao zaidi kuliko wale wanaofanya nao mapenzi. Hilo limekuwa tatizo kwenye mahusiano mengi. Tafiti zinaonesha kwamba, matatizo mengi ambayo yanapelekea ndoa nyingi kuvunjika, yanaanzia kwenye ufanyaji wa mapenzi. Inatokea mmoja ana mapungufu na hajui au hayupo tayari kuyafanyia kazi, ufanyaji wa mapenzi unapungua, msongo unaongezeka na ndoa inaingia kwenye matatizo.

Hakikisha mwenza wako anaridhika kwenye tendo la ufanyaji wa mapenzi mnaloshiriki. Hivyo kila mmoja anapaswa kujifunza njia bora za kufanya mapenzi ili kuridhika yeye pamoja na mwenza wake.

37. Tiba kwa wale wenye matatizo kwenye ufanyaji wa mapenzi.

Kuna watu wana matatizo mbalimbali kwenye ufanyaji wa mapenzi. Wapo ambao wanakuwa hawajisikii tu kufanya, hasa kwa wanawake, na kwa wanaume, changamoto kubwa ni kushindwa kusimamisha uume kwa muda mrefu au kufika kileleni mapema. Sehemu kubwa ya matatizo haya huwa inatengenezwa na hofu, kukosa maandalizi ya kutosha na pia akili kuwa mbali.

Mnahitaji kujiandaa kwa tendo, kwa kushiriki vitu vingi kabla ya tendo husika, na pia kuhakikisha akili na mawazo yote yapo kwenye tendo mnalofanya. Usiruhusu akili ihame na kuanza kufikiria vitu vingine, hapo utakosa hamasa ya kuendelea na tendo hilo au kufika kileleni haraka.

Kwa wale wanaofika kileleni haraka, pia unaweza kuhamisha akili yako pale unapokaribia kufika kileleni ili kuzuia kufika kileleni.

KUMI NA NNE; ZIMA VIFAA NA WASHA MWILI.

Siku hizi kumekuwa hakuna tena mpaka kati ya mwili na vifaa tunavyotumia. Simu zetu zimekuwa kama zimenaswa kwenye mikono yetu, maana tunaenda nazo kila mahali, mpaka kitandani.

Hiki ni kitu unapaswa kukiepuka sana. Saa moja kabla ya muda wa kulala ni muda wa kuandaa mazingira ya kulala. Unahitaji kuzima kila aina ya kifaa unachotumia ili kisikatishe usingizi wako. Pia unahitaji kupunguza mwanga unaoingia kwenye macho yako muda mfupi kabla ya kulala ili uweze kupata usingizi haraka.

Kamwe usiingie na simu kitandani, usiangalie tv ukiwa kitandani na unapolala, zima kila aina ya mwanga.

Piaa tumia muda mfupi kabla ya kulala kufanya zoezi la kuitafakari siku yako, na kupangilia siku inayofuata. Fanya hivyo kwa kuandika kwenye kijitabu chako. Hili ni zoezi lenye manufaa makubwa sana kwako kiakili na hata kiafya.

KUMI NA TANO; KULALA.

Kulala ni sayansi ambayo wengi hasa zama hizi hatuielewi. Kwenye kila aina ya jamii, zamani wakati sayansi haijakua, watu walikuwa wanalala na kuamka na jua. Watu walienda kulala giza linapoingia, na kuamka jua linapochomoza. Lakini sasa hivi, watu wanaweza kufanya kazi usiku na mchana, kitu kinachovuruga mazoea ya miili yetu kwenye kulala, na hili linaleta matatizo makubwa sana kiafya. Watu wengi hawapati usingizi wa kutosha, na hilo linaleta madhara makubwa kwenye kazi zao na wale wanaohusika na kazi zao.

38. Jinsi ya kupima muda wa kulala.

Kama tulivyojifunza, mzunguko wetu wa usingizi una hatua nne, ambazo zinachukua dakika 90 kukamilisha mzunguko. Ukiamka katikati ya mzunguko, hasa wa usingizi wa kina, unakuwa umechoka sana. Hivyo unapopanga kulala, zingatia mzunguko wa dakika 90, yaani saa moja na nusu. Hivyo unapolala, unahitaji kuamka baada ya mzunguko kuisha, hivyo labda baada ya saa moja na nusu, masaa matatu, masaa manne na nusu, masaa sita, masaa saba na nusu na kuendelea.

Umelala masaa mangapi siyo muhimu sana, muhimu ni mizunguko ya usingizi uliyolala, kwa wiki unahitaji kupata mizunguko isiyopungua 35, angalau mizunguko mitano kila siku.

39. Jinsi ya kulala.

Kuna sayansi kwenye ulalaji, ndiyo maana wengi huwa wanapata shida kwenye kulala na kuamka. Unapolala, lalia upande, mmoja, hiyo ndiyo njia salama ya kulala. Usilalie mgongo na wala usilalie tumbo. Hizo ni njia zisizo salama za kulala, ambazo zinaweza kukuletea matatizo mbalimbali kiafya.

40. Mazingira yawe bora.

Usiwe na mwanga wakati unalala.

Joto liwe wastani, kusiwe na joto sana.

Godoro unalolalia liwe linapumzisha kweli na siyo kuumiza.

Utulivu uwe wa hali ya juu.

KUMI NA SITA; HITIMISHO.

Kumiliki siku yako, kwa namna ambavyo tumejifunza kwenye kitabu hiki, siyo kitu rahisi. Siyo kitu ambacho unaweza kufanya kila siku, kwa sababu siku hazilingani. Hivyo kitu cha kwanza ni uwe tayari kujisamehe. Hata ukipangilia siku yako vizuri kiasi gani, kuna mambo yatatokea ambayo hukutegemea na yakavuruga. Unapokutana na nambo kama hayo, usikate tamaa na kuacha kumiliki siku zako, bali kazana kufanya kilicho sahihi. Na siku mpya inapoanza, ianze siku hiyo kwa umiliki.

Tengeneza kauli fupi zitakazokusukuma mambo yanapokuwa magumu. Kadiri unavyokwenda, utakutana na magumu, na wakati wa ugumu siyo wakati mzuri wa kuanza kufikiria. Unahitaji kutengeneza kauli ambazo utakuwa unajikumbusha kila mara, ambazo zitakupa sababu ya kupiga hatua zaidi. Kauli kama NITAFANYA KILICHO SAHIHI MARA ZOTE, NITATIMIZA NINACHOAHIDI, NAKAZANA KUWA BORA, zitakusaidia sana kwenye safari yako ya kumiliki siku yako na kumiliki maisha yako pia.

Miliki siku yako, na utaweza kuyamiliki maisha yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kitabu hiki kimesomwa na kuchambuliwa na Dr. Makirita Amani ambaye ni Daktari wa Binadamu, Kocha wa Mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Kama unapenda kupata vitabu vizuri vya kujisomea pamoja na chambuzi za kina, karibu ujiunge na channel maalumu ya TELEGRAM inayoitwa TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA. Kupitia channel hii, kila juma kwa majuma 52 ya mwaka utapata vitabu, uchambuzi wa kina na mafunzo ya ziada yanayopatikana kwenye vitabu mbalimbali.

Kujiunga na channel hii tuma ujumbe kwa kutumia app ya TELEGRAM MESSENGER wenye maneno TANO ZA JUMA kwenda namba 0717396253. Karibu sana.
 
HONgera kwa kazi nzuri. Ujumbe sahih hufikishwa kwa kutumia lugha sahihi
 
Hongera kwa uchambuzi mzuri. Kama kawaida ya JF uzi mzuri namna hii haupati washabiki!
 
View attachment 1039891

Shukrani sana
 
14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom