Uchambuzi wa Hotuba ya Kenani Kihongosi Chuo Kikuu Mzumbe (Morogoro)

Almalik mokiwa

Senior Member
Jun 5, 2020
147
157
Anaandika Almalik Mokiwa

Tarehe 4/02/2023 katibu mkuu wa vijana UVCCM, Kenani Kihongosi alitembelea chuo kikuu Mzumbe kuzungumza sera na itikadi za chama cha mapinduzi (CCM)

Waliohudhuria walikuwepo wanachama wa CCM na wasio wanachama. Nilikuwepo kujifunza nikiwa kama muumini wa "Nyutro gang" kwa lugha nyepesi, mtu asiyeamini katika chama chochote cha siasa. Nime-bold ili nieleweke zaidi kuwa, mimi sio muumini wa chama chochote kile cha siasa.

Hotuba ya Kihongosi ilipambwa na maneno ya kutia moyo vijana, kusimamia wanachoamini, kuzingatia na kuchangamkia fursa bila kujali nani anafikiria nini kuhusu wanachokifanya hasa hasa linapokuja suala la uongozi na ujasiriamali.

Mbali na yote, alizungumza mengi kuhusu itikadi na historia fupi ya chama cha mapinduzi na kuwaasa vijana wake kuwa WAZALENDO. Aliwataka vijana kuingia CCM na kukitumikia chama kwa uzalendo mkubwa na sio kufata fursa.

Alizungumza kuhusu uimarishwaji wa demokrasia unaofanywa na chama cha mapinduzi huku akivikosoa vyama vingine vya upinzani kama ACT, CHADEMA, CHAUMA na CUF. Ambavyo mara nyingi vimekuwa vikiongozwa na mwenyekiti mmoja kwa muda mrefu akilinganisha na chama chake (CCM) ambacho kimeongozwa na wenyekiti sita tangu kuundwa kwake februari 5, 1977.

Kama ilivyo kawaida kwa wana-CCM kuhamasisha wasio wanachama kujiunga na CCM kwa jina la sehemu salama. Kenani Kihongosi alitumia sehem ya muda wake ndani ya hotuba yake kuwahamasisha vijana kujiunga na CCM

Pia alikosoa vikali tabia ya wanachama wa vyama pinzani kukosoa kila kitu kinachofanywa na serikali ya CCM. Namnukuu "Wapinzani wmetusaidia kwa namna flani, lakini wamekuwa wakipinga kila kitu. Nyakati flani walikuwa wakipinga suala la Tanzania kutokuwa na ndege wakati ni nchi kubwa. Serikali ikaleta ndege 11 na bado wakarudi kupinga kwa kusema kuwa ndege sio ajenda ya msingi. Lakini wanazipanda na tunaona"

SEHEMU YA UCHAMBUZI WANGU:

Wakati wa hotuba yake, alikuwa akiwaasa vijana kuingia CCM sio kwa kufata FURSA bali kwenda kukitumikia chama kwa UZALENDO. Lakini katika sehemu ya mazungumzo yake aliwapa moyo vijana na kuwaambia kuwa kuna siku watateuliwa kama yeye, ila wahakikishe wanabaki kwenye chama. Alidai kuwa hakuna teuzi zinazotoka nje ya mfumo wa chama cha CCM. Kauli hii inapingana na kauli yake ya kuwahamasisha vijana kuingia CCM kwa kutofata FURSA bali uzalendo.

Iko hivi; Katika kusanyiko lile kulikuwepo na mchanganyiko wa vijana wenye itikadi mbali mbali wakiwemo waumini wa vyama vingine vya siasa (tofauti na CCM) pamoja na vijana wasio na vyama. Matamanio ya vijana wengi ni kufika mahala ambapo watapewa heshima na kuwa na uchumi unao eleweka.

Kuna vijana wasio wanachama wa CCM wanatamani nao siku moja wapigiwe salute kama wakuu wa wilaya au mikoa. Wawe wakurugenzi au mawaziri. Kupitia hamasa iliyo amshwa na Katibu mkuu wa vijana UVCCM wengi wakajikuta wanajisajili na ili kuchukua kadi za CCM kwa hisia na matamanio ya kufika mbali na sio kwa 'Logic' na uzalendo kama alivyo asa Kihongosi katikati ya hotuba yake. KIMANTIKI, CCM leo imeongeza namba kubwa ya watu wanaowaza maslahi yao zaidi kuliko maslahi ya wanao piganiwa na CCM (wananchi).

Katika hotuba yake pia nilimsikia akiwaambia vijana kuwa, watu wanalalamika kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa. Alisema kuwa, wapinzani wanatumia mfumuko huo wa bei kama ajenda kwa kuambatanisha na katiba mpya. Namnukuu "....bei za bidhaa zimepanda alafu wapinzani wanadai kuwa kutokana na bidhaa kupanda bei, suluhisho ni katiba mpya. SASA KATIBA MPYA NA KUPANDA KWA BEI ZA BIDHAA WAPI NA WAPI? Yaani ni mbingu na ardhi"

NAKOSOA vikali dhana hii, Kenani Kihongosi alizungumza kauli za kebehi kuhusu umuhimu wa katiba mpya akidhani anazungumza na maamuma na kujisahau kuwa anazungumza na wasomi wa chuo kikuu. Katiba mpya ingeweza kuleta viongozi wawajibikaji na waadilifu ambao wangeweza kudhibiti mfumuko wa bei. Kupanda kwa bei ya bidhaa ni matokeo ya athari nyingi ikiwemo UONGOZI tulio nao. Viongozi wetu wana uwezo wa kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unadhibitiwa. Kushindwa kudhibiti kupanda kwa bei za bidhaa kunaonyesha matobo na mianya inayotakiwa kuzibwa kupitia katiba mpya.

Pia, Kihongosi alizungumza kuhusu usimamiaji na uimarishwaji wa demokrasia na chama cha mapinduzi. Hapa sijaelewa ni demokrasia ipi aliyokuwa anaizungumzia, labda demokrasia ya kufunga mikutano ya hadhara kwa wanachama pinzani, kinyume na katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Demokrasia ya kuwabambikizia watu kesi na kuwashurutisha kukiri makosa na kutaifisha mali zao kupitia kivuli cha "plea bargaining", demokrasia ya kuminya uhuru wa habari na haki ya kutoa maoni.

Demokrasia gani inayominya dhana ya ukosoaji? Hakuna demokrasia ya kuwanyanyasa wapinzani.

Demokrasia ya kuwan'gan'gania na kuwalipa kodi zetu wabunge haramu wa COVID 19 (wabunge wasio na chama) imeambatanishwa na kifungu gani cha sheria?? Hapa Kihongosi "alitupiga za kichwa'' tukasukumia na maji tukameza shwaaa.

Naandika kwako Kenani Kihongosi; Jikite katika kututetea vijana, vijana wengi hawana ajira, tumegubikwa na huzuni kubwa, maisha yetu ni papatu papatu, ifike wakati usimame kuwatetea vijana hadharani. Hata lile suala la Tanesco kuingia mkataba na India na kuwanyima vijana wetu fursa tulisubiri useme kitu, ukakaa KIMYA, tukaugulia maumivu mpaka yakapoa.

Hata lile Azimio la wabunge kuhusu waliohusika na mkataba wa SYMBION na kusababisha serikali kulipa mabilioni ya fedha, fedha ambazo zingeweza kusaidia maendeleo ya vijana, tulitegemea useme kitu. Ukakaa KIMYA tukafa moyo, ila tukajiponya na kusema kuwa "Hata mh Jakaya aliwahi kusema UVCCM iko salama chini ya mikono ya Kenani Kihongosi" tukasema wakubwa hawakosei. Tukapiga moyo konde.

Mh, Kenani Kihongosi; sisi vijana tumeamua kujikita zaidi kufanya biashara zetu mtandaoni, tunafanya matangazo ya bidhaa zetu kupitia mitandao. Kuna vijana wengine wanafanya kazi za ufundi wa kuunganisha vyuma, wasaga mashine, wauza muvi na wanaofanya kazi za 'steshenari' wote wanategemea umeme ndio wapate KULA. Suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara linawakosesha vijana ulaji, tumesubiri kauli yako kutusemea vijana. Ukakaa KIMYA.

Tunaomba ujikite kutusemea vijana, wewe UNASIKIKA ZAIDI. Tunajua unakuwaga na mawasiliano direct na mh rais. Nenda katusemee. Hii itachora tafsiri halisi ya KATIBU MKUU WA VIJANA UVCCM. Lakini pia, sio UVCCM pekee hata sisi tusiokuwa na chama NI WAKWAKO tukumbuke na Katupiganie.

MWISHO:
almalikmokiwa98@gmail.com
 
Kenani kihongosi nakumbuka alituhumiwa na Gambo kule chuga kwamba aliingiziwa hela kinyume na utaratibu kupitia akaunti ya mtu wake wa karibu. Mbona hajawahi kukanusha huyu jamaa na anahubiri uadilifu kila siku?
 
Back
Top Bottom