Uchambuzi wa Bajeti ya Elimu kwa mwaka wa fedha 2023/24

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
609
1,540
Uchambuzi wa Bajeti ya Elimu kwa mwaka wa fedha 2023/24

Utangulizi.
Leo, tarehe 17 Mei 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaenda kuhitimisha mjadala wa bajeti ya waziri ya Elimu kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa jana. Tunafahamu kuwa bajeti ni nguzo muhimu sana katika kugharamia utoaji wa huduma ya elimu hapa nchini. Kutokana na umuhimu wake, bajeti ya Sekta ya Elimu imekuwa ikifuatiliwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali na wadau wamekua wakitoa maoni yao kuhusu vipaumbele vya bajeti.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa Elimu tumefanya uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23. Uchambuzi wetu utahusisha maeneo nane (8) kuhusu bajeti ya Elimu ya mwaka huu. Pamoja na kubaini maeneo nane (8) tuliyoyafanyia uchambuzi wa kina, masuala ya jumla kuhusu bajeti.

Mosi, kuhusu muundo wa wizara na majukumu yake haukidhi mahitaji katika kusimamia sekta ya elimu kwa ufanisi uliokusudiwa. Kumekuwepo kwa mwingiliano na mgongano wa majukumu kati ya kusimamia Elimu hususani maeneo ya Usimamizi (utawala), Ujenzi wa Miundombinu na utoaji wa miongozo.

Pili, kuendelea kuwepo kwa bajeti kiduchu ya maendeleo hususani kwenye maeneo ya utafiti na uajiri katika ngazi ya vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na taasisi za elimu.

Tatu, bajeti ya elimu kwa kawaida inashughulikiwa na wizara mbili, Wizara iliyo chini Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Tayari Chama Chetu kimeshatoa mtazamo wake na maeneo ya kipaumbele kupitia Msemaji wa sekta ya TAMISEMI na Maendeleo Vijijini baadhi ya mambo yanayoangukia kwenye sekta ya Elimu. Leo tutazungumzia Sekta ya Elimu kwa muktadha wa majukumu na vipaumbele kutokana wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

1. Marekebisho ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu nchini.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 iliweka kipaumbele cha kukamilisha mchakato wa marekebisho ya Sera ya Elimu ya 2014 toleo la 2023. Sisi ACT Wazalendo, tumepata nafasi ya kushiriki mjadala wa kupitia Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 pamoja na Rasimu ya Mitaala ya Elimu ya Awali, msingi na ualimu (Umahiri Mkuu na umahiri Mahususi kwa kila somo) katika Kongamano la wadau Jijini Dodoma lililofanyika tarehe 12 hadi 14 Mei, 2023.

Maoni yetu ya jumla, pamoja na hatua nzuri ya kuanzisha mchakato huu yapo maeneo bado marekebisho haya mapya haijaondoa utata ama kutoa mwongozo mzuri;

Mosi, suala la ugharamiaji wa Elimu na Mafunzo. Sera haijaonesha nani atagharamia upatikanji wa Elimu katika kila ngazi, ijapokua imeonesha wazi juu ya uhaba wa bajeti na ongezeko na mahitaji, Tamko la Sera kuwa "Serikali itahakikisha kuwa Ada na Michango katika ngazi mbalimbali za Elimu inazingatia misingi ya Elimu Bora na endelevu wa uwekezaji katika Sekta ya Elimu" inaacha maswali makubwa. Kwamba, elimu bora itatokana na ada na michango, kwamba bila ada na Michango hakuna Elimu Bora? Eneo la ugharamiaji wa elimu ni nyenzo muhimu katika kuleta usawa wa fursa ya kupata elimu kwa kigezo cha uwezo wa mtu.

Gharama za elimu zimekuwa kikwazo kikubwa na mstari unaochora wenye nacho na wasio nacho kwenye kupata fursa ya elimu nchini. Kuendelea kutekeleza sera iliyotengeneza matabaka ni kuendeleza ubaguzi na kuzuia usawa wa fursa ya kupata elimu kwa wote.

Pili, kuhusu lugha ya kufundishia katika shule na vyuo Sera ya Elimu haijaweka bayana juu ya lugha ya kufundishia kati ya Kiswahili na Kiingereza bado inaendeleza utata wa kutumia Lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya awali na elimu msingi halafu katika ngazi ya sekondari na chuo kutumika kiingereza.

Kibaya zaidi kwenye maelezo ya sera yanaonyesha kwamba Kiingereza ndio chanzo cha maarifa. Mtazamo huu umejawa na kasumba ya utumwa na fikra za kikoloni katika jamii iliyotangazia uhuru kwa zaidi ya miaka 60. Si kweli kwamba "Kingereza ni chanzo kikuu Cha maarifa katika Kufundishia" kama inavyoelezwa na maelezo ya Sera.

Tatu, kuhusu falsafa ya Elimu ya kujitegemea. Kwa maoni ya awali, tunaona falsafa hii imeegeshwa tu lakini sio mwendelezo wa dhana na shabaha ya Elimu ya kujitegemea iliyokuwa inatekelezwa kwa msukumo wa Azimio la Arusha.

Falsafa ya Elimu ya kujitegemea kwa msukumo wa Azimio la Arusha ililenga kumwezesha binadamu kujitambua, kujikomboa na kushiriki katika kuikomboa jamii yake. Katika muktadha wa Afrika na Tanzania ni elimu inayomtoa Mwafrika kutoka mawazo na tabia za kukubali mazingira yanayomnyanyasa na kupunguza utu wake na hadhi yake kana kwamba hayabadilishiki na hana uwezo juu ya mazingira hayo. Elimu ya kukataa ubinafsi, umimi, unyonyaji, ukandamishaji na hali ya unyonge unatokana na athari za utumwa, ukoloni na ukoloni mamboleo.

Dhana ya kujitegemea inayoelezewa kutokana na msukumo wa mantiki ya utawandawazi na soko huria ni kuifanya elimu kukidhi maslahi binafsi, kukuza na kutukuza mafanikio binafsi na kufanya maarifa na mtu mwenye maarifa kuwa bidhaa inayothaminiwa na soko kama ilivyo kwa pamba, kahawa au madini ya Tanzanite.

Falsafa hii itawaweka tayari vijana kuwa watumishi wema, watiifu, wasiouliza maswali, na wavumilivu wa mfumo ya unyonyaji, ukandamizaji alimradi anapata kipato stahiki. Elimu yetu itaendelea kuwa mradi wa mataifa tajiri wa kuendeleza unyonyaji, ukandamizaji na kutukalia hata baada ya uhuru wa kisiasa.

Hivyo kwenye suala la marekebisho ya Sera tunapendekeza hatua zifuatazo;

Kwanza, Serikali iondoe maelezo ya kuwa Kingereza ndio chanzo kikuu cha maarifa (hakuna lugha bora kuliko nyengine) msingi wa maarifa ni ufahamu na uelewa.

Pili, Sera iweke wazi kuwa Kiswahili kiwe lugha rasmi ya kufundishia na Lugha zingine zifundishwe kama somo. Kubadili lugha ya kufundishia ni hatua muhimu ya msingi katika kuboresha elimu. Kwa kuwa lengo la elimu ni kuwaandaa vijana kuwa sehemu ya jamii ni vema maandalizi hayo yakafanywa katika lugha kuu ya jamii. Matumizi ya Lugha moja katika elimu na jamii inaimarisha uhusiano kati ya jamii na shule au vyuo.

Tatu, dhana ya falsafa ya elimu ya kujitegemea inapaswa kwenda sambamaba na Kujenga aina gani ya jamii tunayoitaka.

2. Usimamizi usioridhisha wa Sera ya Elimu bila malipo.

Mwaka 2016, Serikali ilianza kutekeleza mpango wa elimu ya msingi bila malipo. Huu ni mkakati mzuri wa Serikali kuhakikisha kwamba watoto wote wa kitanzania wanapata elimu ya msingi bila vikwazo vya ada. Katika utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi na Sekondari bila malipo jukumu la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni pamoja kutenga fedha kwa ajili kuthibiti ubora; Kutenga fedha za kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa sera hizo ili kuchukua hatua stahiki. Aidha, wizara inafanya majukumu ya kutenga fedha kwa ajili mitihani ya upimaji wa kitaifa na ununuzi wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia.

Ingawa, wizara ina majukumu haya tumebaini kutotekelezwa kikamilifu kwa majukumu haya suala linaloathiri dhana, shabaha na matarajio ya elimu bure na ubora wa Elimu yetu nchini. Kwa muda mrefu kumekuwepo kilio cha wadau kuwa Serikali imeshindwa kufanya ukaguzi kwa ufanisi kwenye shule za msingi na sekondari ili kukagua na kutazama ubora wa elimu inayotolewa.

Hoja hii imethibitishwa pia na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge kwamba kuna udhaifu katika uthibiti bora mashuleni kwa kuwa shule nyingi hazikaguliwi. Kwa mfano, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, ni asilimia 26.4 pekee shule za msingi zilizopangwa kukaguliwa zilikaguliwa.

Kwa mujibu CAG inaonyesha kuwa ili kukidhi mahitaji ya vitabu kwa wanafunzi katika shule za msingi za Serikali vilihitajika vitabu 6,323,566 kwa mamlaka 22 za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, ni vitabu vya kiada 1,467,829 (sawa asilimia 23) vilisambazwa katika mwaka huo ikionesha upungufu wa vitabu 4,855,737 vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.42. Utoaji pungufu wa vitabu kwa shule za msingi na sekondari kunaathiri matokeo ya kitaaluma ya mwanafunzi.

Kutosimamiwa vizuri kwa Sera hii ndio maana kumeibuka wimbi kubwa la michango inayoelekezwa kwa wazazi kwenye shule mbalimbali nchini. Wazazi wanachangishwa fedha kwa ajili ya mitihani, vitabu, chakula, walinzi, ukamilishaji wa madarasa na kadhalika. Vilevile, ni dalili za wazi ruzuku na bajeti ya Serikali haijitoshelezi kufikia lengo la kutoa elimu iliyo bora bali ni bora elimu.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kutenga bajeti ya kutosha kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sera ya elimu kwa ajili ya ukaguzi na uthibiti ubora wa shule.

Pili, tunaitaka Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha shilingi 25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Shilingi 58,000 kwa mwanafunzi wa sekondari.
Aidha, Serikali ilipe fidia ya ada na michango mengine ili kuwezesha uendeshaji wa shule kwa kuwa tathmini zinaonyesha ruzuku hii haikutokana na tathimini ya gharama halisi za uendeshaji.

3. Mgongano kati ya Wizara ya Elimu na Wizara nyengine.
Katika utekelezaji wa sera ya Elimu kumekuwa na mwingiliano wa wizara hii ya elimu na mafunzo ya ufundi na wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa na wizara ya Maendeleo ya jamii jinsia na makundi maalumu, mwingiliano huu upo katika utawala wa elimu, ujenzi wa miundombinu na utoaji wa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa elimu nchini.

Usimamizi wa miradi ya elimu, na utekelezaji wa sera, masuala ya Takwimu za elimu zinatoka TAMISEMI ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa ngazi ya hadi sekondari ya juu ni TAMISEMI, uajiri wa waalimu na watumishi wa elimu ni TAMISEMI, huku Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ikisimamia utekelezaji wa sera kwa eneo dogo na mitaala, pamoja na uthibiti ubora. Mgongano huu unapunguza ufanisi kwa kiwango kikubwa, Sekta ya Elimu ni Sekta Nyeti ambayo inapaswa yenyewe kujitegemea kama ambavyo Sekta nyengine zinajitegemea na kuwe tu na ushirikiano wa Kisekta, Mgongano huu unaacha maswali ambayo Wizara ya Elimu haiwezi kujibu na mengine ambayo Wizara ya TAMISEMI haiwezi kujibu mathalani changamoto ya uhaba wa waalimu na miundombinu kwa shule za msingi na sekondari Wizara ya Elimu inategemea Bajeti ya TAMISEMI.

Nchi hii ina uhaba mkubwa wa miundombinu ya madarasa, uhaba mkubwa wa walimu, matundu ya vyoo, vitabu, maabara, na maktaba ambavyo ni vitu vya elimu lakini havipo katika utekelezaji wa Wizara ya elimu.

Mgongano wa kimaamuzi, Walimu Wamekua wakipokea Amri na matamko mbalimbali kutoka katika Wizara hizi mbili tofauti. Mathani katika utitiri wa Michango mashuleni, ni Waziri wa TAMISEMI ndie aliyeelekeza Kuwa wanafunzi wachangie chakula shuleni, hii inaifanya Wizara ya Elimu kukosa uhuru wa kimaamuzi katika usimamizi wa Sera.

ACT Wazalendo tunashauri Wizara ya elimu na Mafunzo ya ufundi iachiwe majukumu yote yanayohusika na Masuala ya elimu kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu ili iweze kuwajibika ipasavyo kuhusu Wizara hiyo, Wizara ifanye kazi zake kupitia taasisi zilizochini yake katika Kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora kulingana na wakati.

4. Kukithiri kwa upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari, walimu wa mafunzo ya amali na wakufunzi wa ualimu
Tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi , sekondari za umma na vyuo vya ualimu linazidi kukua kutokana na jitihada ndogo za Serikali kuajiri. Katika uchambuzi wetu wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 tulieleza masikitiko yetu makubwa juu ya mwenendo usioridhisha wa Serikali katika kuajiri walimu ukilinganishwa na mahitaji. Bado tunaona Serikali imeamua kupuuza vilio vya wadau mbalimbali ili kuboresha elimu ya nchi hii.

Kuna uhaba mkubwa hususani katika masomo ya Sayansi, amali, lugha na hisabati, kwa takwimu za mwaka 2021/2022 kwa shule za sekondari tu zilikuwa na uhaba wa walimu 12,577 wa somo la Fizikia, walimu 13,686 wa hisabati, walimu 12,027 wa Baiolojia na walimu 10,600 wa somo la kemia huku kwa elimu ya juu Takwimu za 2021 zinaonesha kuna uhaba wa wanataaluma 3,639.

Takwimu za mwaka huu 2023/2024 zinaonyesha upungufu wa walimu 186,325 kwa shule za msingi sawa asilimia 51.44 (mwaka jana ilikuwa asilimia 36.7) na upungufu kwa sekondari ni walimu 89,932 sawa na asilimia (51.5) ikilinganishwa na mwaka jana upungufu ulikuwa wa asilimia 47. Vilevile, mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa Shule za Msingi ni walimu 4,462 ambapo waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,945 sawa na asilimia 66. Kwa sasa, inafanya upungufu wa walimu kufikia walimu 279,202 kwa ajili ya shule za msingi, sekondari na zile za mahitaji maalumu.

Mwaka wa fedha 2022/23 Serikali iliajiri walimu 9,800 tu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari na mwaka huu imeweka mikakati ya kuajiri walimu 13,000. Kwa mwenendo huu Serikali inatuambia kuwa itachukua zaidi ya miaka 20 kumaliza tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari ambao ni walimu 279,202.

Katika ngazi ya vyuo vya ualimu 2022/2023 Serikali imesajili jumla ya wanafunzi 22,802 (Wanawake 11,641na Wanaume 11,161) katika Vyuo vya Ualimu vya Serikali na visivyo vya Serikali ambapo Astashahada ya Elimu ya Msingi 15,177 (Wanawake 8,406 na Wanaume 6,771), Stashahada ya Ualimu 2,787 (Wanawake 1,076 na Wanaume 1,711) na Stashahada maalumu ya ualimu wa sayansi sekondari wa miaka mitatu 4,838(Wanawake 2,159 na Wanaume 2,679). Bado kiwango hiki ni kidogo sana kulingana na mahitaji.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza idadi ya ajira za walimu kwa mwaka hadi kufika walimu 30,000. Pia, Serikali irudishe utaratibu wa kutoa ajira za moja kwa moja za walimu kila mwaka. Wakati kuna vijana wengi sana takribani 123,000 waliohitimu ngazi mbalimbali waliosomea ualimu hatupaswi kusumbuliwa tena na tatizo la upungufu wa walimu katika shule zetu.

Pili, tunarudia Rai yetu kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwamba Serikali iajiri angalau wakufunzi na wahadhiri angalau 5000 ili kupunguza uhaba wa walimu vyuoni na vyuo vikuu.
5. Uthibiti wa ubora katika Elimu ya ufundi na Mafunzo ya ufundi stadi haupewi kipaumbele nchini.

Wizara ya Elimu kupitia Baraza la Taifa la Elimu linasimamia elimu ya ufundi nchini. Katika uchambuzi wetu wa hotuba ya wizara tumeona kuna udhibiti mdogo sana wa ubora kwa kuwa kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ukaguzi hakiwezeshi wizara kutekeleza majukumu yake. Kwa miaka zaidi ya sita kuanzia 2016 hadi sasa kiwango cha bajeti kwa ajili ukaguzi huwa ni hafifu mno.
Ubora wa vyuo vya ufundi unaathiriwa kutokana na upungufu mkubwa wa wakufunzi na walimu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Vilevile, uwezo mdogo wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kudahili wanafunzi. Idadi ya wanafunzi wanaohitimu shule za msingi na sekondari na kukosa fursa ya kuendelea na masomo ni kubwa ni wastani wa wanafunzi milioni moja huku uwezo (wanafunzi wanaodahiliwa ni 266,000.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iongezwe bajeti ya ukaguzi na udhibiti ubora wa shule na vyuo vya amali ili kuwawezesha wakaguzi kuzifikia shule na vyuo vyote kila mwaka. Pili, Serikali itenge bajeti ya kuongeza idadi ya vyuo vya amali (kati) ili kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa kwa ufanisi zaidi.

6. Wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kumaliza Elimu msingi (Darasa la Saba) na Kidato cha nne
Taarifa ya utekelezaji ya wizara na takwimu mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kwa ngazi ya darasa la kwanza, kwa miaka kadhaa. Pamoja na ongezeko kubwa la udahili bado Serikali imeshindwa kufuatilia anguko kubwa la Watoto wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi darasa la saba (7).

Aidha ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023 imebainisha kuwa Katika Halmashauri 11, kati ya 2015 na 2021 Wanafunzi 19,945 (25%) kati ya 78,786 waliosajiliwa mwaka 2015 hawakuhitimu darasa la saba na katika Mamlaka 19 za Serikali za Mitaa; Wanafunzi 22,039 sawa na asilimia 28 kati ya 82,236 waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 hawakufanikiwa kufanya mtihani na kupata cheti cha kuhitimu kidato cha nne.

Katika uchambuzi wetu pia tumebaini kuna kukatisha masomo kwa wanafunzi wengi kabla ya mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili mathalani kwa miaka miwili tu yaani 2021 na 2022 kuna wanafunzi zaidi ya laki mbili na arobaini (240,000) hawakufanya mtihani wa darasa la nne licha ya kusajiliwa kufanya mitihani hiyo huku zaidi ya wanafunzi 55,211 hawakufanya mtihani wa kidato cha pili licha ya kusajiliwa kufanya mitihani hiyo.
Sababu za kukatisha masomo zilikuwa ni pamoja na ujauzito kwa wanafunzi wa kike, umbali mrefu kutoka makaazi ya wanafunzi hadi shuleni, malezi ya familia na sababu binafsi.

Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 haijaweka mkazo wa namna ya kukabiliana na hali hiyo mbaya ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki ya elimu kama mpango wa maendeleo miaka mitano 2020/21 hadi 2025/26.

ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kike aliyepata mimba akiwa shule anamaliza elimu yake kama ilivyokusudiwa kwa kusimamia utekelezaji wa ahadi ya kuruhusu kumrejesha mtoto wa shule shuleni.

Pili, kukomesha ukali dhidi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakuwa huru kushiriki na kupata elimu.

Tatu, kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kujenga shule kuongeza idadi ya shule maeneo ya karibu ili kupunguza umbali, mwisho tunatoa rai kwa wazazi wote kuhakikisha wanasimama kidete kuhakikisha watoto wote wanapata elimu na kumaliza kama ilivyokusudiwa.

7. Mapitio ya utekelezaji wa bajeti fedha za miradi ya maendeleo ya Elimu
Katika mwaka wa fedha 2022/23 wizara ilipitisha bajeti ya Shilingi trilioni 1.5 ambapo Shilingi trilioni 1 zilikua ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo bilioni 652 zimetumika kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Serikali inafanya makusudi kuchanga fedha za mikopo ya elimu ya juu katika fedha za maendeleo kwa kuwa fedha hizo huonekana kuwa ni nyingi lakini fedha zinazokwenda kutekeleza miradi halisi ya maendeleo ni kidogo sana. Kwa kutazama fedha hizo kwa mwaka jana fedha za mikopo zinachukua asilimia 57 ya fedha zote za miradi.

Katika mwaka wa fedha 2023/24 Wizara imeomba kuidhinishiwa Shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, kiasi kinachoenda kuhudumia gharama za mikopo kitaendelea kupanda na kuwa Bilioni 652 kutokana kuongezeka kwa idadi ya wahitimu kidato cha sita mwaka huu na kuongezwa kwa kiwango cha pesa ya kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

ACT Wazalendo tunapendekeza kutenganishwa kwa fedha za miradi halisi ya maendeleo katika bajeti na fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa kuzianzishia fungu maalumu ili fedha za miradi halisi ya maendeleo ziweze kuonekana na kufuatiliwa utekelezaji wake.

8. Udhibiti usioridhisha wa vyanzo vya Mionzi nchini
Juhudi zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania katika kudhibiti na kukuza matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia nchini haziridhishi.

Katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) imebaini mambo kuwa Wastani wa 66% ya vituo vya vyanzo vya mionzi vilivyosajiliwa nchini havikuwa na leseni ya kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania: Ukaguzi ulibaini kuwa, vituo vyenye vyanzo vya mionzi vilivyopatiwa leseni na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania vilianzia 31% hadi 37% katika kipindi cha miaka 4 iliyopita kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2021/22, ambapo kiwango cha juu cha idadi ya leseni zilizotolewa kilikuwa 37% katika mwaka 2020/21. Kwa wastani, 66% ya vituo vilivyosajiliwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) havikupewa leseni katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2021/22.

Kukosekana kwa mfumo mzuri wa leseni ulisababisha Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kupoteza wastani wa shilingi milioni 424.7. Aidha, ukaguzi ulibaini kuwa hatua za utekelezaji za kusimamisha vituo visivyokuwa na leseni za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi hazikutekelezwa ipasavyo na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania. Mathalani, 94% ya vituo vilivyokuwa na mapungufu hayo viliendelea kufanya kazi bila kuchukuliwa hatua na Tume kwa kipindi cha 2018/19 hadi 2021/22.

ACT wazalendo tunaitaka Serikali kupitia Tume ya nguvu za atomiki iimarishe udhibiti wa matumizi ya mionzi ya nyuklia nchini kwa kuweka mikakati ya makusudi ya kutoa leseni na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepuka upotevu wa mapato nchini na kuhakikisha matumizi sahihi kwa kuzingatia usalama.

Hitimisho:
Kwa kuhitimisha, Usimamizi wa sekta ya Elimu kugawanywa katika wizara takribani zaidi ya tatu yaani, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya TAMISEMI na wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na watoto (kwa baadhi ya masuala) kuna fanya mpango wa bajeti kwenye sekta ya Elimu kuyumbishwa kwa vipaumbele vyake. Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha sekta ya Elimu inasimamiwa na wizara moja.

Pia, changamoto nyingi za kibajeti na kisera zinatokana na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa juu ya aina ya Elimu tunayoitaka, hivyo ni muhimu mchakato wa Mapitio ya Sera iwahusishe wadau wote.

Tunatambua hatua za Serikali kukamilisha marekebisho ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu, ni muhimu kuwe na mwafaka wa kitaifa juu ya masuala kadhaa yakiwemu lugha ya kufundishia na kujifunzia, mfumo wa upimaji, tathimini na utambulizi (awards), uwezo wa uongozi, usimamizi na utawala wa elimu, ubora wa mitaala pamoja na ithibati na udhibiti wa ubora wa shule na vyuo katika ujumla wake.

Imetolewa na;
Ndg. Riziki Shahari Mngwali
Twitter: @rizikishahari
Waziri Kivuli wa Elimu
ACT Wazalendo.
17 Me, 2023.
FB_IMG_1684392984244.jpg
 
Back
Top Bottom