Uchakavu wa mabehewa, hujuma vyasababisha usafiri TRL vurugu tupu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uchakavu wa mabehewa, hujuma vyasababisha usafiri TRL vurugu tupu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Oct 12, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 12, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,534
  Likes Received: 81,951
  Trophy Points: 280
  Date::10/11/2008
  Uchakavu wa mabehewa, hujuma vyasababisha usafiri TRL vurugu tupu

  [​IMG]
  Usafiri wa reli ya kati baada ya kuwa mikononi mwa wawekezaji toka India bado umekuwa wa mashaka has kutokana na uchakavu wa mabehewa ya abiria ni hadi huduma kwa ujumla.

  Na Reginald Miruko
  Mwananchi

  UCHAKAVU wa mabehewa na vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi ni miongoni mwa mambo yanayoididimiza Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambayo imetimiza mwaka mmoja tangu kukabidhiwa uendesheji wa lililokuwa Shirika la Reli nchini(TRC).

  Mwandishi wa Mwananchi Jumapili aliyesafiri na treni ya kampuni hiyo kutoka Dar es salaam hadi Mwanza wiki iliyopita, alishuhudia uchakavu wa mabehewa na jinsi baadhi ya watumishi wanavyojinufaisha badala ya kuliingizia mapato shirika.

  Malalamiko makubwa zaidi yalikuwa kwenye kituo cha Mwanza ambapo tiketi zinadaiwa kulanguliwa na kuuzwa kwa bei ya kuruka.

  Mwandishi wa habari hii akiwa na abiria wengine waliohitaji tiketi Oktoba 8, mwaka huu kwa ajili ya usafiri wa siku iliyofuata, walielezwa na wauzaji tiketi kuwa zimekwisha na gari limejaa hadi Oktoba 16, mwaka huu.

  Ubao wa matangazo katika stesheni hiyo ulieleza kuwa tiketi za daraja la pili zingeweza kupatikana kuanzia Oktoba 16, wakati zile za daraja la kwanza na tatu zingepatikana Oktoba 23, mwaka huu.

  Waziri Omari, mkazi wa Ilemela aliyetaka kumsafirisha baba yake kutoka Mwanza kwenda Manyoni mkoani Singida, alisema hali hiyo imemsikitisha kwa kuwa mipango yake ilikuwa imevurugika.

  Kwa upande wake Kawikele Luchanganya aliyetoka Bariadi, Shinyanga kuwakatia teketi watu watano wa familia yake waliokuwa wanahamia Morogoro, alisema angekaa hapo kumsubiri mkuu wa stesheni, ili kuomba msaada wake kwa sababu asingeweza kusubiri zaidi ya wiki nzima ili apate usafiri.

  "Mimi nitakaa hapa kumsubiri 'stesheni masta' ili nimuombe aangalie namna ya kunisaidia, kwani sitaweza kusubiri wiki nzima," alisema.

  Uchunguzi wetu ulibaini kuwa hali hiyo inawaumiza zaidi maskini, lakini wenye pesa wameshaizoea kwani tiketi za kusafiri siku hiyo au inayofuata hupatikana kupitia mlango wa nyuma kwa kuongeza dau.

  Baada ya kupata fununu hiyo, mwandishi wetu alimfuata kijana mmoja ambaye baadaye alijitambulisha kama mtumishi wa stesheni hiyo, akamuuliza jinsi ya kupata tiketi ya kuondoka siku iliyofuata.

  "Tiketi (daraja la tatu) inapatikana, itabidi ulipe Sh22,000 badala ya Sh16,900," alisema kijana huyo na baada ya kukubaliana na mwandishi wetu, alimtaka akae mahali fulani kwa muda, ili kumsubiri mkatishaji wa tiketi aliyekuwa amekwenda kula.

  Baadaye kijana huyo alimfuata mteja wake (mwandishi) na kumtaka ampatie jina kamili na fedha. Alipopatiwa fedha hizo na kipande cha karatasi cha jina kamili, kijana huyo aliingia ndani ya chumba cha kukatia tiketi, na aliporudi alimletea mwandishi tiketi yake namba 04483 ya kuondoka Mwanza Oktoba 9, mwaka huu.

  Baadhi ya abiria waliohojiwa na gazeti hili walisema hali ni mbaya na kama marekebisho hayatafanyika haraka kampuni hiyo itaendelea kudidimia kiuchumi.

  Msuya Mbuko, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt Augustine cha Mwanza, alilalamikia kuchanika kwa baadhi ya viti na vitanda, vyoo kukosa maji pamoja na milango na madirisha kuwa mabovu.

  "Ninachoona tofauti baada ya shirika kubinafsishwa ni kujali muda, lakini treni nzima bado ni chakavu na hakuna mabadiliko yaliyofanyika. Ukiangalia kitanda hiki kilivyochanika (anaonyesha), huwezi kuamini kuwa ni cha daraja la pili," alisema.

  Mwananchi Jumapili lilishuhudia uchakavu huo katika madaraja yote, huku mende wadogo wadogo wakitembea hadi kwenye vyumba vya daraja la kwanza, la pili na kwenye mghahawa.

  Uchunguzi umebaini pia kuwa treni hiyo bado inajaza abiria kupindukia hadi wengine kukaa kwenye vyoo, lakini si makusanyo yote ya nauli za abiria wanaoingilia njiani yanalifikia shirika hilo.

  Moses Methew, abiria aliyetoka Kigoma kuelekea Mwanza alilieleza Mwananchi Jumapili kuwa baadhi ya abiria wanapoingia kwenye mabehewa hulipa fedha na kupewa utambulisho fulani badala ya stakabadhi inayopelekwa kwenye shirika.

  Juhudi za kuwapata maafisa wa TRL kuzungumzia hali hiyo zimekwama baada ya Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Midladjy Maez aliyekutwa ofisini kwake Alhamisi wiki hii kudai yuko likizo.

  Badala yake, Maez alimwelekeza mwandishi aache maswali kwa afisa aliyebaki, Mohamed Mapondela ambaye wakati huo hakuwa ofisini, hakuonekana ofisini siku iliyofuata na ilielezwa kuwa hana simu ya mkononi.
   
 2. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #2
  Oct 12, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,534
  Likes Received: 81,951
  Trophy Points: 280
  Kuna haja ya kuwakokota Kikwete na Pinda wakaone hali ya mabehewa hayo ili waseme kama yana hadhi ya kusafirisha binadamu na pia kama hao wahindi walistahili kuendelea na mkataba wa kuendesha TRC pamoja na kuonyesha hawana uwezo wa kifedha. Wameshasaini mkataba hakuna anayefuatilia kama TRC inakidhi mahitaji ya watumiaji wa usafiri huo na kama hao wahindi wanatimiza masharti waliyopewa.
   
Loading...