Elections 2010 Uchakachuaji wa kura ni uhaini

Susuviri

JF-Expert Member
Oct 6, 2007
3,713
888
Uchakachuaji wa kura ni uhaini
Prudence Karugendo
Tanzania Daima


Tumemaliza Uchaguzi Mkuu, tumempata rais, wabunge na madiwani. Kwa upande wa Tanzania Visiwani wenzetu wamenufaika zaidi kwa vile wana vitu viwili zaidi ambavyo sisi, watu wa Bara, hatuna.

Wamempata rais wao na wawakilishi wakati sisi Bara tunampata rais wa muungano peke yake. Nani atabisha kwamba wao hawaufaidi Muungano zaidi yetu?

Nani atabisha kwamba wao hawayapati matunda ya Muungano wakati sisi Bara tukiyasikia tu kwenye maneno? Hilo tuliache, lengo la makala hii ni kuuangalia Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika mala yangu ya juma lililopita nilimpongeza Maalim Seif Shariff Hamadi, ambaye kafanywa Makamu wa Kwanza wa Rais, Tanzania Visiwani, badala ya kumpongeza Rais Ali Mohamedi Shein.

Ni imani yangu kwamba maelezo niliyoyatoa kuhusu uamuzi wangu huo yalijitosheleza. Pia leo nasema sitampongeza Rais Jakaya Kikwete, kama wengi wanavyofanya, kwa kinachoitwa “ushindi wake” kutokana na sababu nitakazozieleza hapa chini.

Nakumbuka Rais Kikwete, mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, alisema wazi kwamba asingefurahia watu wa kumficha ukweli kwa lengo la kujipendekeza kwake, kwa maana ya wanafiki.

Sina hakika kama amebadilisha msimamo wake huo hata kama naona rundo la wanafiki limemzunguka kila upande kwa sasa, hata hivyo ukweli huo haunifanyi niamini kwamba wanafiki hao anawafurahia.

Inawezekana wanafiki hao ni matokeo ya hali halisi ambayo Kikwete, kama binadamu, hana uwezo wa kuigeuza iwe jinsi anavyotaka yeye.

Tendo la kupongeza linafuatia mabadiliko chanya yanayokuwa yamepatikana. Kwa lugha nyepesi ni kwamba haiwezekani kumpongeza mtu aliyeuza gari, hata kama ni mkweche, ili kununua baisikeli mpya. Kwa vyovyote vile pongezi zinazoweza kufuatia kitendo hicho hawezi kumfurahisha mhusika maana ni pongezi kwa hatua kubwa anayokuwa ameipiga kwa kurudi nyuma, kitu ambacho ni lazima akione kama dhihaka.

Ukweli ni kwamba hatupongezani kwa kurudi nyuma, kurudi nyuma si mafanikio, mafanikio ni lazima yaonekane kwa kwenda mbele. Kiungwana mtu anayerudi nyuma anapewa pole siyo pongezi.

Tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, ambao chama tawala kilitumia kaulimbiu ya “ushindi ni lazima”, tena ikiwa inajionyesha mikakati ya ajabu ajabu ya kuulazimisha ushindi huo, mwaka 2005, mkakati pekee uliotumiwa na CCM ni sura ya Kikwete.

Kwa hilo tu CCM ilikuwa inasema kwamba “ushindi ni wazi”, tena siyo ushindi wa kawaida, ushindi wa kimbunga au Sunami. Na ndivyo ilivyokuwa kwa vile wananchi walikuwa wamekubaliana na kilichokuwa kimejitokeza, haiba ya Kikwete.

Kwa hiyo uchaguzi wa 2005 ukafanyika bila matatizo yoyote, hatukusikia tahadhari ya vyombo vya usalama wala kitu chochote cha kutia mashaka.

Mambo yalienda kwa maana halisi ya amani na utulivu. Kura zikapigwa, zikahesabiwa na matokeo kutangazwa bila mizengwe yoyote katika amani na utulivu. Walioshindwa hawakulalamika kwa vile walikuwa tayari wameishaona kuwa ushindi kwa CCM ulikuwa wa wazi.

Rais Kikwete akaibuka na asilimia 80 ya kura zote halali. Ulikuwa ushindi uliofurahiwa hata na wapinzani wake, ushindi wa kimbunga. Kusema ukweli Kikwete alikuwa na kila sababu ya kupongezwa.

Tofauti kabisa na uchaguzi huo, uchaguzi wa mwaka huu mambo yamebadilika kabisa, kimbunga kimeelekea kwake. Badala ya kaulimbiu ya ushindi ni wazi ikaja kaulimbiu mpya na ya kibabe ya ushindi ni lazima.

Kaulimbiu hiyo ikatengenezewa mikakati ya kila aina ya kuhakikisha ushindi unalazimishwa. Hii tunaweza kuiita mikakati ya kuokoa maisha kutokana na hali iliyovurugika, kwa vile ni kufa na kupona, ni lazima tuseme kupona ni lazima.

Hakuna tena kujiamini hivyo hatuwezi kusema kupona ni wazi kutokana na tishio linaoonekana kwa mbele linalotokana na kuvurugika kwa hali ya hewa. Kujipa moyo ni kujikakamua kwa kusema kupona ni lazima.

Kwa hiyo katika hali kama hii ambayo mtu anaonyesha kuporomoka kwa kiasi cha kutisha anawezaje kuifurahia pongezi utakayompatia? Unampongeza kwa kuporomoka!

Unampongeza kwa kuuza gari na kununua baisikeli! Kinachofaa hapa ni pole, pongezi ya aina yoyote ni dhihaka.

Kikwete wa ushindi wa kimbunga cha Sunami asilimia 80 anawezaje kupongezwa kwa ushindi wa upepo wa kupulizwa kwa mdomo wa asilimia 60?

Hivi wanaompongeza hawaelewi alikotokea? Hawaelewi kuwa mtu huyu alikuwa anaendesha gari mpaka wampongeze kwa kununua baisikeli hata kama ni mpya na nzuri?

Tuache unafiki, tuwe waungwana na tumpe pole Kikwete.

Kusema ukweli Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulikuwa umegubikwa na kila hofu ya kushindwa. Ni kutokana na hali hiyo usalama ukawa tete kiasi cha uchaguzi kuonekana kama unaendeshwa kijeshi. Hali ya askari kutanda kila mahali kwa kisingizio cha kulinda amani wakati hakuna tishio lolote la kuvamiwa imedhihirisha kuwa kumbe matakwa ya wananchi wakati mwingine nayo yanaweza yakaonekana kama tishio la uvamizi hasa kwa wanaokuwa madarakani.

Nashindwa kuamini kwamba uchaguzi wa mwaka huu umefanyika katika hali ya utulivu na amani. Ni utulivu gani ambapo askari wanawatimua wananchi wasilinde kura zao kwa kuwafyatulia moshi wa sumu?

Ni amani gani ambapo wahusika wa kusimamia uchaguzi wanapata kigugumizi cha kuwatangaza washindi kwa zaidi ya siku mbili pale ambapo wananchi wanakuwa wameamua kinyume na matakwa ya watawala?

Lakini zaidi ya yote kaulimbiu ya mwaka huu ya chama tawala ya “ushindi ni lazima” inatupa picha gani?

Neno ushindi ni lazima lina maana gani na lina uhusiano gani na demokrasia? Binafsi nalichukulia neno hilo kama mpango maalumu wa kuwapora wananchi utashi wao, maana katika demokrasia ya kweli ni vigumu kutumia ulazima.

Sanasana linaweza likatumika neno ushindi ni muhimu kwa maana ya kuwashawishi wananchi kwa hali yoyote ili wakupe ushindi.

Lakini linapotumika neno “lazima” maana yake ni kwamba umeshindwa kuwashawishi wananchi ili wakupatie kile unachokihitaji kufa na kupona na hivyo unaamua kuwapora kwa nguvu.

Ni katika ulazima huo, kunamojitokeza usemi kama uliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu, kuchakachua kura au matokeo.

Kuchakachua kura ni mchakato wa kubadilisha matakwa ya wananchi ili yaonekane yanaendana na ya wale wanaosema ushindi ni lazima.

Hapa kura zitapigwa za bandia au matokeo kubadilishwa. Ushahidi wa haya upo mwingi na mkubwa katika uchaguzi huu ulioisha.

Na matokeo ya uchafuu wote ni nchi kutawaliwa kinyume na utashi wa wananchi katika kile kinachohimizwa na kaulimbiu ya ushindi ni lazima.Madhara ya kaulimbiu ya ushindi ni lazima ni kudumaa kwa usitawi wa wananchi kwa vile kile walichokiamini kwamba kingeufanya ustawi wao ushamiri kinaondolewa kwa mabavu na kuwekwa wasichokiamini.

Vivyo hivyo kile kilichowekwa kwa mabavu hakiwezi kuujali usitawi wa wananchi zaidi ya kuangalia na kujali tu faida ya nguvu iliyokiweka pale.

Ushindi ni lazima, ni hasara kwa wananchi.

Mpaka hapa nautazama uchakachuaji wa kura kama uhaini. Iwapo kitendo cha kuiondoa serikali inayokuwa madarakani kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria kinajulikana kama uhaini, kwa nini kitendo cha kubadilisha uamuzi wa wananchi wa kuiweka serikali halali madarakani kisihesabike nacho kuwa ni uhaini?

Serikali inayokuwa madarakani, hata kama ni ya kijeshi iliyojiweka yenyewe bila ridhaa ya wananchi, ukitokea mpango wa kuiangusha mpango huo unajulikana kama uhaini.

Kama mpango huo haukufanikiwa na wahusika kukamatwa, adhabu yake ni kubwa mno, kifo.

Sasa kwa nini hawa wanaofanya uchakachuaji wasihesabike kama wahaini kutokana na kuyabadilisha matakwa ya wananchi kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi?

Mtu mmoja mwenye mawazo ya uchakachuaji tuliyekuwa tunabishana kuhusu matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu, yeye alidai kwamba Rais Kikwete kwa mwaka huu angepata zaidi ya asilimia 100, mimi nilimkatalia na kumueleza kwamba nyinyi wanafiki mmemuharibia kwa hiyo hawezi kufikia hata kiasi alichofikia uchaguzi wa 2005, aliniambia kwamba angenipeleka kunionyesha matunda ya uchakachuaji aliyopata tangu mwaka 2005, siyo ya Kikwete bali ya kwake binafsi!

Ni matunda binafsi, siyo matunda ya nchi wala wananchi. Huyu ni mchakachuaji ambaye naamini kwa kiasi kikubwa amechangia kuporomoka kwa Kikwete.

Mchakachuaji huyo, mwenye akili za kufumba macho na kuamini kwamba watu wote wamefumba macho na hivyo kutouona uchafu wake, haongei kitu kuhusu mafanikio ya Kikwete kama kiongozi wa nchi katika miaka yake mitano ya kwanza zaidi ya kuongelea faida aliyoipata yeye binafsi.

Hawa wanafiki wanachokiangalia ni namna gani watamtumia rais au jina lake kutunisha matumbo yao hawafikirii kumsaidia kwa njia yoyote kufanikisha majuku yake kwa wananchi. Na hawa ndio wanaofanya kila linalowezekana na lisilowezekana ili mtu fulani awe rais. Mbinu hii ya kishetani inanifanya niamini kabisa kuwa wanachokuwa wamekilenga wachumia tumbo hawa ni kumtoa rais kafara huku wakimkenulia meno ili awaamini kuwa wako naye.

Na mambo yanapokuwa yamebadilika na kuwa mazito ndio wanaomshauri rais kutumia nguvu za dola kuzima hasira za wananchi, lakini mambo yakizidi kuwa mazito zaidi wao ndio watakaokuwa wa kwanza kusema asulubiwe. Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Nicolae Ceausescu wa Romania .

Kwa hiyo, ingetungwa sheria kali kama ile ya uhaini itakayoyafanya matokeo ya uchaguzi wetu kutochezewa kwa namna yoyote na wadau wote wanaohusika katika mchakato wa uchaguzi.

Sheria hiyo ndiyo itakayoufanya uchaguzi kuwa mchakato mtakatifu wa wananchi kuamua namna ya kuiendesha nchi yao.

Nimalizie kwa kusema pole sana Rais Kikwete. Walikupokea ukiwa na haiba yako nzuri wakakuchafua, sasa wamehangaika kukusafisha kwa gharama ya wananchi, ulipaswa kujihadhari na hawa akina Brutus.

My take:

Nadhani makala hii inaibua suala moja nyeti lakini muhimu na linalohitaji mjadala wa kina. Kwani swali la kwanza: uhaini ni nini? Je uchakachuaji ni uhaini?
 
kama uchakachuaji unasababisha mtu ambaye hakushinda uchaguzi kuingia katika nafasi ya ushindi nadhani ni hatari zaidi. Lakini utakuwaje uhaini endapo watu wengi zaidi wameridhia au wamekubali matokeo ya uchakachuaji huo kama umefanyika?
 
kama uchakachuaji unasababisha mtu ambaye hakushinda uchaguzi kuingia katika nafasi ya ushindi nadhani ni hatari zaidi. Lakini utakuwaje uhaini endapo watu wengi zaidi wameridhia au wamekubali matokeo ya uchakachuaji huo kama umefanyika?

Kwani uhaini unaofanywa wa kijeshi si huwa nayo wanaafiki wananchi wakati mwingine. Tuchukue mfano wa Jerry Rawlings alipindua nchi kwa hiyo huu ni uhaini, lakini wananchi wakamkubali.
In this case hatuna uhakika kama wananchi wamekubali kwani wapo wananchi ambao hawana taarifa ya uchakachuaji na ndio maana wamepokea matokeo.
Pia sheria ya nchi imeshindwa kutoa remedy katika kura za urais kwa hiyo hata uhaini ukifanyika (institutionalized) hakuna njia ya kuyapinga.

Lakini tukibaki katika maelezo ya Karugendo, uchakachuaji ni uhaini au la?
Mi nakubaliana nae na ktk thread nyingine niliandika kuwa kiongozi hawezi kutawala bila ridhaa ya wananchi isipokuwa kwa nguvu. Je JK atalazimika (sooner or later) kufanya hivyo?
Ila kama tutakubaliana kuwa ni uhaini basi ni muhimu mhimili wa pili wa serikali yaani Bunge ianze inquiry kwani ni kitendo cha kutisha!
 
kama uchakachuaji unasababisha mtu ambaye hakushinda uchaguzi kuingia katika nafasi ya ushindi nadhani ni hatari zaidi. Lakini utakuwaje uhaini endapo watu wengi zaidi wameridhia au wamekubali matokeo ya uchakachuaji huo kama umefanyika?

Ibara ya 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema:

28.-(1) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.

(2) Bunge laweza kutunga sheria zinazofaa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa.

(3) Mtu yeyote hatakuwa na haki ya kutia sahihi kwenye mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Jamhuri ya Muungano au wa sehemu yoyote ya ardhi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania eneo la taifa na, bila ya kuathiri Katiba hii na sheria zilizowekwa, hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Jamhuri ya Muungano kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi.

(4) Uhaini kama unavyofafanuliwa na sheria utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Muungano.

Mimi ninakubaliana na Karugendo. Uhaini ni kosa kubwa kushinda yote katika nchi yetu na kwa kweli adhabu yake ni lazima iwe kifungo cha maisha(kwani ninapinga adhabu ya kifo). Licha ya watu kukubali au kumezea wizi wa kura hiyo haihalalishi vitendo vichafu vya wezi hao. Kwa mtu ambaye anafahamu kuwa watu hao ni wahaini ana haki kabisa ya kuendelea kudai kuwa ni wahaini. Katika nchi za kidemokrasia uongozi lazima utokane na matakwa ya watu na kama si hivyo basi hiyo si demokrasia na hatuwezi kuitetea.

Kikwete, Makame, Kiravu, Ikulu, CCM na mtandao wao wanajua kabisa nini walikifanya hadi wakapata "ushindi wa lazima". Je huko si kukiuka katiba ya nchi ambayo ibara ya nane inasema:

8.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo -
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;
(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Ni lazima tufike mahali tuweke wazi kabisa na ili ni lazima liwe dai la kudumu la watu wote wanaopigani demokrasia kuwa wizi wa kura au kuchakachua uchaguzi ni kosa la uhaini na adhabu yake ni moja tu ni kifungo cha maisha ambacho hata Raisi hatakuwa na uwezo wa kutoa msamaha kwake. Hatuwezi kukubali kutawaliwa na watu ambao hawaheshimu matakwa na utashi wa wananchi. Katika barua ya Taasisi yangu ya Mtetezi nilimweleza wazi kabisa Makame. Lakini kwa kuwa yeye amezoa kuibeba CCM hakuona shida kuendelea kuchakachua matokeo.

Wakati ninakubaliana na Karugendo kuhusu suala la uhaini, sikubaliani naye kuwa uchaguzi wa 2005 ulikuwa huru na wa haki kwani uchakachuaji ulikuwepo kwani Kikwete alipewa ushindi hata maeneo hakushinda kama jimbo la Hai ambalo Mbowe alikuwa anatoka. Ni kweli kuwa kama uchaguzi ungekuwa wa haki Kikwete bado angeshinda lakini si kwa kiwango kile cha asilimia 80. Vitisho vilikuwepo na CUF iliendelea kutajwa kuwa ni chama cha udini. Wizi katika viti vya ubunge ulikuwa si wa kawaida muulize Dr. Slaa na Mnyika. Ninasema kwa nguvu zote kuw uchaguzi katika nchi yetu tangu imeingia katika mfumo wa vyama vingi tena chini ya Makame na Kiravu haujawahi kuwa huru na wa haki hata kidogo. Ila kilichidhihiri mwaka huu ni kuwa sasa watu wengi wanajua kuwa wizi wa wazi umefanyika na siri za wizi huo ziko hadharani. Wahaini hawa ni lazima wawajibishwe.. Na sisi ndio ambao tunatakiwa kuwawajibisha.
 
kama uchakachuaji unasababisha mtu ambaye hakushinda uchaguzi kuingia katika nafasi ya ushindi nadhani ni hatari zaidi. Lakini utakuwaje uhaini endapo watu wengi zaidi wameridhia au wamekubali matokeo ya uchakachuaji huo kama umefanyika?

Kwani uhaini unaofanywa wa kijeshi si huwa nayo wanaafiki wananchi wakati mwingine. Tuchukue mfano wa Jerry Rawlings alipindua nchi kwa hiyo huu ni uhaini, lakini wananchi wakamkubali.
In this case hatuna uhakika kama wananchi wamekubali kwani wapo wananchi ambao hawana taarifa ya uchakachuaji na ndio maana wamepokea matokeo.
Pia sheria ya nchi imeshindwa kutoa remedy katika kura za urais kwa hiyo hata uhaini ukifanyika (institutionalized) hakuna njia ya kuyapinga.

Lakini tukibaki katika maelezo ya Karugendo, uchakachuaji ni uhaini au la?
Mi nakubaliana nae na ktk thread nyingine niliandika kuwa kiongozi hawezi kutawala bila ridhaa ya wananchi isipokuwa kwa nguvu. Je JK atalazimika (sooner or later) kufanya hivyo?
Ila kama tutakubaliana kuwa ni uhaini basi ni muhimu mhimili wa pili wa serikali yaani Bunge ianze inquiry kwani ni kitendo cha kutisha!

Kama Rugemeleza alivyoonyesha hapo juu, uchakachuaji wa kura unasababisha kuwapo kwa serikali ambayo haikupata mamlaka yake kutoka kwa wananchi. Kwa lugha nyingine, ni kughaili mamlaka ya wananchi. Kwa hiyo ninakubali wazi kabisa kuwa huo ni uhaini.

mapinduzi ya kijeshi pamoja na mambo mengine huwa yanafa\uta kabisa katiba iliyopo na hivyo kuhalalisha vitendo vyao. Ila katika baadhi ya sehemu, serikali za kiraia zinaporudishwa na hivyo kurudisha katiba, kumekuwa na mashtaka ya uhaini dhidi ya walioenedesha mapinduzi yale, ingawa wengine huwa wanaingia mkataba wa kupewe imunity kabla hawajabidhi mamlaka kwa serikali ya wanachi tena.
 
Uhaini ni kosa lolote kubwa sana dhidi ya mamlaka ya wananchi juu ya serikali na taifa la jamuhri ya muungano wa Tanzania. ------ haya ni maoni yangu tu siyo ya kisheria.

Uhaini ni kosa la kutaka kupindua au kupindua au kuasi juu ya mamlaka ya halali ya nchi yoyote. Ni kosa ambalo ni kubwa kushinda makosa yote katika nchi kwani linakiuka mamlaka na mfumo mzima wa utawala wa nchi. Kingereza neno lake ni "treason". Hivyo hata kitendo cha kufanya ujasusi dhidi ya nchi yako mwenyewe ni uhaini. Vilevile kushiriki kumuua mtawala au kiongozi halali wa nchi ni uhaini.
 
Kwa misingi hiyo hapo juu, licha ya katiba kutunyima FURSA ya kuhoji uchaguzi wa raisi unapokwenda mrama kama ambavyo ilivyotutokea hapa kwetu, je sheria inatuambia nini pindi tunapobaini kwamba HASWA kuna MHAINI ambaye ndiye anaishi pale Ikulu Magogoni wakati Mshindi halisi pengine anakaa Sinza???

Je, inatupasha sie vijana tukaupitie huo ufungu wa makazi yetu yale kwa wakati na staili zetu za kitaa kwenda kumuomba aliyekua mheshimiwa akatukadhi funguo au mpaka Dr Masumbuko Lamwai, Dr Mvungi na wengineo kama wao wawepo??

Na kwa upande mwingine, pindi Katiba inapotuzuia sisi kama walipa-kodi tusihoji mahakamani mwenendo mzima wa kuchaguliwa kwake rais ilhali bado anaenda kutumia kodi zetu huko huku akijua vema kwamba hana ridhaa yetu; maana yake ni nini hasa hapa?? Je, inamaana kwamba huenda KATIBA yetu, kwa sasa, pengine huenda inatuambi bila kupanua kinywa sana ya kwamba mpangazi kama huyu pengine tutumie MIGUVU kama njia mbadala ya kumfanya akampishe mgeni rasmi mwenye stahiki na sehemu yake??

Hivi kwa kweli, bila hata ya kuhitaji kupevuka sana kisheria, mgombea tena wa ngazi ya juu kabisa kama raisi (mwenye kuwania dhamana kubwa sana ya nchi) anapobainika kwamba kwa zaidi ya wiki 3 aliwahi kufikiri, kujadili, na hatimaye kuagiza kutekelezwa kwa harakati za KUIBA KURA na kuwapokonya raia haki ya msingi kuchagua viongozi kwa hiari yao wenyewe; mpaka hapa bado tu hakuna uhaini tu kweli ?????? Chonde tueleweshane kiundani kidogo hapo jamaa.
 
Kutokana na nidhamu yetu ya uwoga hasa pundits wetu kukosa ujasiri wa kujadili masuala kama haya katika vyombo vya habari , hivi sasa JK amekosa kabisa uhalali yaani legitimacy ya kuwa rais machoni mwa raia wake.
Naamini kuwa kama kutatokea mabadiliko ya kweli kama yaliyotokea huko Romania baada ya Ceausceau na mafaili ya mashushu kuwekwa wazi tutakuja kuona kuwa mazungumzo yetu hapa jamvini yalikuwa yanagusia suala nyeti sana. Hivi sasa wapo hata watu wa usalama wa taifa, wafanyakazi wa serikali ambao wanaongea wazi kuwa walichakachua matokeo hususan ya urais katika vituo na hata katika majumuisho. :A S 13:
Hii ni hatari na ina maana kuwa kuna uwezekano kuwa tumetawaliwa kwa mabavu na si kwa ridhaa yetu. Kwa mantiki hii kuna tofauti gani kati ya Mubarak na Kikwete? Kwani hata Misri walidai kuwa na demokrasia na uchaguzi wa vyama vingi kama hapa lakini siku zote alikuwa anashinda Mubarak, hapa kwetu siku zote ni CCM hata kama mgombea wao ni weak kama JK! Hebu tuwaze kidogo...
 
Back
Top Bottom