Uchahuzi Kinondoni, Siha ni kipimo mtanzania anavyofikiri

Tee Bag

JF-Expert Member
Dec 21, 2013
7,200
5,553
UCHAGUZI KINONDONI, SIHA NI KIPIMO MTANZANIA ANAVYOFIKIRI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza kuwa itatumia Sh1 bilioni kugharamia uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam. Wakati huohuo, Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, imejengewa kwa msaada, jengo la upasuaji, lenye thamani ya Sh420 milioni. Ujenzi wa jengo hilo umegharamiwa na kampuni ya GSM kwa asilimia 100.

Hesabu hiyo ni kuonesha kwamba fedha ambazo zinagharamia uchaguzi mdogo Kinondoni, zingeweza kujenga majengo mawili ya upasuaji Mwananyamala na Sh160 milioni zingebaki. Ingewezekana kabisa kuokoa wagonjwa wengi, hasa akina mama wajawazito na watoto, kwa kuboresha uzazi salama.

Kinondoni ni moja ya majimbo ya Dar es Salaam ambayo mvua ikinyesha kidogo, maji hujaa barabarani na mitaani kutokana na ubovu wa miundombinu. Nyakati za mvua maisha huwa magumu mno kwa wakazi wake, maana maji huingia mpaka ndani ya nyumba wanazoishi. Unaweza kujiuliza Sh1 bilioni zingesaidia kiasi gani kupunguza tatizo?

Kinondoni ni mjini, na kwa eneo jimbo hilo ni dogo. Kama Sh1 bilioni zitatumika kufanikisha uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo, maana yake pengine yangekuwa majimbo ya Kawe, Mbagala, Temeke, Ukonga, Ubungo, Kibamba, Ilala na Kigamboni, gharama zingekuwa kubwa zaidi kutokana na ukumbwa wa majimbo na wingi wa wapigakura.

Kwa mantiki hiyo, bila shaka kwa sababu za Kijiografia, fedha nyingi zaidi zitatumika kufanikisha uchaguzi Siha. Sababu ni ukubwa wa jimbo lakini pia mazingira. Kama Dar es Salaam ambalo ndilo jiji lenye maendeleo zaidi, lililo na miundombinu bora zaidi ya kimawasiliano, Sh1 bilioni itatumika, ni wazi Siha ni zaidi.

Sasa basi, uchaguzi mdogo wa ubunge majimbo ya Siha na Kinondoni yana maana zaidi ya uchaguzi. Ni kipimo cha namna wakazi wa majimbo hayo wanavyofikiri na kufikia uamuzi. Matokeo ya uchaguzi kwenye majimbo hayo yatakuwa kielelezo cha jinsi walivyowapima wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sababu zao.

Uchaguzi wa Siha na Kinondoni ni kipimo cha gharama zinazotumika kufanikisha uchaguzi dhidi ya sababu ambazo wagombea wa CCM walizitoa walipokuwa wabunge tayari kwa tiketi za vyama vya Cuf na Chadema, kisha kuamua kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM ambako wamerejeshwa kugombea tena majimbo hayo.

Je, sababu ambazo Maulid Mtulia na Godwin Mollel, walizitoa walipokuwa wanajiuzulu ubunge na kujivua uanachama wa vilivyokuwa vyama vyao, zina uzani mkubwa kuliko kiasi cha fedha kitakachotumika kufanikisha uchaguzi wa majimbo hayo? Jumlisha matumizi ya rasilimali nyingine zisizohusiana na fedha.

Kuna suala la muda. Wananchi leo inabidi kujitokeza kwenye mikutano ya hadhara ili kusikiliza maelezo ya wagombea. Uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika Februari 17, mwaka huu. Siku hiyo itafika na wananchi watalazimika kupanga foleni kwenye mistari.

Wananchi watanyoosha mistari kwenye vyumba vya kupigia kura. Hivyo, muda watakaotumia, usumbufu wa kusimama kwenye foleni, jua litakalowaunguza kufanikisha sauti zao kusikika, wananchi watapaswa kupiga hesabu jumla ya gharama za uchaguzi dhidi ya sababu ambazo Mtulia wa Kinondoni na Mollel wa Siha walizitoa walipojiuzulu ubunge.

Je, ni sahihi kutumia fedha nyingi kiasi hicho kufanya uchaguzi mara mbili baada ya miaka miwili, badala ya miaka mitano? Ambatanisha na sababu ambazo Mtulia na Mollel walizitoa kujiuzulu ubunge pamoja na gharama za uchaguzi kwa jumla. Baada ya hapo wakazi wa Siha na Kinondoni watakuwa waamuzi.

NI KIPIMO CHA UBONGO

Naam, Mtulia na Mollel walijiuzulu ubunge Desema mwaka jana. Ni kwa kujiuzulu kwao ndiyo maana majimbo hayo yanafanya uchaguzi wa marudio ili kujaza nafasi ambazo waliziacha. Na kwa vile baada ya kuhamia CCM, chama hicho kimewarudisha tena kwenye majimbo hayohayo ili wakishinda waendelee kuwa wabunge, sasa basi lipo lingine la kujadili.

Mtulia na Mollel walipokuwa wakijiuzulu, sababu kubwa zaidi waliyoitoa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, kwamba anafanya kazi nzuri sana ya kupambana na ufisadi, vilevile kuwaletea Watanzania maendeleo. Katika hili, ubongo wa watu wa Siha na Kinondoni utapimwa.

Kipimo cha ubongo kinaanzia kwenye kuujua urais na ubunge kisha kuoanisha na sababu ambazo Mtulia na Mollel walizitoa. Urais ni utawala, ubunge ni uwakilishi. Rais ni mkuu wa utawala, mbunge ni mwakilishi wa wananchi. Rais anaongoza Serikali inayowatala wananchi. Mbunge anatumwa na wananchi kwenda kuisimamia Serikali ili itende kazi yake kwa masilahi ya wananchi.

Rais amepewa mamlaka ya kikatiba kukusanya mapato na kuihudumia nchi. Amepewa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kila nyenzo kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo, vilevile wananchi wanakuwa ni wenye amani na usalama. Mbunge amepewa wajibu mkubwa muhimu; kumchunga Rais anavyofanya kazi, kumbana na kumdhibiti inapobidi.

Katika kumpa meno mbunge kikatiba, mbunge amepewa Bunge ambalo limepewa nguvu katika ibara ya 46A, kifungu kidogo namba 1 na 2, ya kumwondoa Rais madakarakani pale atakapoonekana anavunja Katiba, anakiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma au anakwenda kinyume na sheria yenye mwongozo wa vyama vya siasa, iliyotajwa ibara ya 20(2) ya Katiba.

Hoja ya nyingine ambayo Bunge limepewa meno ya kumwondoa Rais madarakani ni pale anapoonekana amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpaka hapo unaona kwamba hachaguliwi mbunge tu kwenda kutunga sheria, bali kumsimamia Rais na Serikali yake.

Tafsiri hapo ni kuwa anahitajika mbunge ambaye anakuwa macho dhidi ya Serikali. Anayemkagua Rais na Baraza la Mawaziri kwa ukaribu. Japo Rais na Serikali yake wawe wanafanya kazi kubwa na nzuri kiasi gani, Bunge halipaswi kubweteka na kushangilia, bali lifuatilie kuusaka ubaya ndani ya uzuri unaoonekana.

Baada ya tafsiri hiyo, rejea kwenye hoja za Mtulia na Mollel kwamba walijiuzulu ubunge ili kumuunga mkono Rais Magufuli anavyofanya kazi. Kwa maana kwamba walipokuwa wapinzani walikosa uhuru wa kumuunga mkono na kumtia moyo jinsi anavyofanya kazi na anavyopambana na ufisadi.

Hivyo basi, wamejiunga CCM ili kumuunga mkono au kumshabikia waziwazi. Ni sawa na kusema kwamba wakishinda ubunge watakwenda kutimiza kile ambacho walishakitamka kwamba ni kumuunga mkono Rais. Hapohapo rejea tafsiri ya uwepo wa Bunge kama mhilimili huru wenye wajibu wa kuisimamia na kuidhibiti Serikali.

Ifahamike kuwa suala la kuisimamia Serikali ni wajibu wa Bunge na siyo suala la vyama. Kwa maana hiyo wabunge wa chama tawala kama ilivyo CCM kwa sasa, hawatakiwi kuwa wapiga makofi na wapaza sauti za ndiyo kupitisha hoja za Serikali, bali lazima watende kazi ya kuisimamia Serikali ili kulipa hadhi Bunge na heshima ya uwepo wake kama mhimili unaotimiza wajibu.

Sasa basi, wakazi wa Siha na Kinondoni watapiga kura, kisha uamuzi wao utachora mstari jinsi wanavyofikiri. Wanavyoubeba umuhimu wa Bunge kama chombo chao cha uwakilishi na aina ya wawakilishi wanaowataka. Tutajua mengi kutoka kwenye fikra zao.

Je, wananchi wa Kinondoni na Siha wanataka Rais Magufuli aungwe mkono mpaka Bunge lipoteze maana na uzani wake? Hiyo ndiyo sababu nimetangulia kueleza kwamba Siha na Kinondoni ni zaidi ya uchaguzi. Februari 17, mwaka huu, kitakuwa kipimo cha jinsi wananchi wa majimbo hayo wanavyofikiri.

IPO FAIDA NAIONA

Hoja mbalimbali za kiuchambuzi zinakosoa Mtulia na Mollel kusimamishwa kugombea Kinondoni na Siha kwa sababu walikuwa wabunge wa majimbo hayo, hawakufukuzwa na vyama vyao, ila wenyewe kwa ridhaa yao walijiuzulu kwa kuambatanisha sababu ambazo nimeshazigusia.

Kwamba Mtulia na Mollel hawakupata kuwa na mgogoro kwenye vyama vyao kwa kumuunga mkono Rais Magufuli. Hawakuwahi kufunua vinywa kupongeza mazuri ya Rais Magufuli kisha viongozi wa vyama vyao wakawa mbogo na kutishia kuwafukuza. Hivyo kuhama kwao kulijaa mshangao. Kwa maana hiyo, nchi imeingia kwenye uchaguzi kwa mshangao.

Pamoja na kila sababu yenye kutolewa, mimi naona sawa Mtulia na Mollel kurejeshwa kugombea Kinondoni na Siha. Maana inawezesha kutambua kwa ukaribu kile ambacho wananchi wanakitafsiri kutokana na matukio ya kisiasa yenye kuendelea. Hiyo ndiyo faida ninayoiona.

Endapo Mtulia na Mollel watashinda kwa uchaguzi huru, wazi na haki, utakuwa ni ujumbe kwamba wananchi wanataka Rais Magufuli aungwe mkono, japo uungaji mkono unawagharimu kiasi gani. Ikiwa Mtulia na Mollel watashindwa, itakuwa ni alama kuwa hoja zao za kuachia ubunge na kutimkia CCM hazikupata baraka zao na zilijaa kichefuchefu.

Lipo muhimu pia la kusoma. Ni kama idadi ya wapigakura (turnout) itapungua kutoka Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Kutakuwa na fundisho kwamba ama wananchi wamekerwa kurejea uchaguzi bila sababu zilizowatosheleza au kukatishwa tamaa na vyama vya upinzani kususia uchaguzi.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vikiongozwa na Chadema, vilevile Chaumma na ACT-Wazalendo, viligomea uchaguzi mdogo wa majimbo matatu ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido pamoja udiwani kwenye kata sita, uliofanyika Januari 13, mwaka huu. Hivi sasa Chadema wamerejea kugombea Siha na Kinondoni. Wananchi wanapokeaje hiyo kususia na kurejea? Tutajifunza.

Ndimi Luqman MALOTO
 
Ni kipimo sahihi ikiwa tu uchaguzi utakuwa huru na haki. Matokeo yataakisi mawazo halisi ya wapiga kura!
 
Uchambuzi mzuri sana. Wenye akili tulishajua konachoendelea. Ombi la kwanza kwa kila mpiga kura wa Kinondoni na Siha liwe TUGAWANE KILE MTULIA NA MOLLEL WALICHOPEWA THEN NDO TUWAKAANGE KWENYE SANDUKU LA KURA.
 
Kama vile sijakuelewa!!! Uchaguzi ni takwa la demokrasia,na tunajua unagharama.Kukosa kutimiza takwa hilo pia ungelidai.
1:je ungependa uchaguzi usiwepo?
2:Au ungependa uwepo lakini tumchague mtu kutoka chama kisichokuwa CCM?
3:Ungetamani mbunge aliyekuwepo asijiuzuru? Kwa maana ya kumnyima haki yake ya kiraia ?
Yote kwa yote Lazima uchaguzi ufanyike na pesa itumike.
Katika swala moja kama tingelibahatika kuwaza sawa,nakuunga mkono nalo ni matumizi yasiyo ya lazima ya rasilimali watu/fedha. Hili ni tatizo la kitaifa kuanzia ngazi ya mtu binafsi,familia,kaya mpaka taifa. Priority zetu hazieleweki..wala hazina faida hata kidogo.


Sent from my TECNO 7C using JamiiForums mobile app
 
Hii nchi ina watu wa ajabu kweli kweli, Watanzania huwa hawajui maana ya kupiga kura, na hawajui wanachoenda kuchagua. Kwa mtu anayejitambua hawezi kumpigia kura Mtulia wala Molel.
 
Back
Top Bottom