Uchaguzi wa Igunga na Juhudi za Kukandamiza upigaji kura

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,461
39,928
a-woman-holds-up-her-voter-card.jpg

Uchaguzi mdogo wa ubunge huko Igunga utaamuliwa kwa namba. Utaamuliwa kwa idadi ya watu watakaojitokeza kupiga kura na siyo watu wanaojitokeza leo hii kwenye mikutano ya kampeni. Utaamuliwa na watu ambao wataamua kuacha shughuli zao siku hiyo na kwenda kutumbukiza karatasi moja kwenye sanduku la kura. Kuanzia mwanzoni mwa wiki hii inayoisha nimekuwa nikujiulzia ni kitu gani kitawapa wapinzani ushindi na ni kitu gani kitawarudishia CCM ushindi. Jibu ni lile lile – namba.

Nimejiuliza mwanzoni mwa wiki kwanini CCM imejikuta ikidaiwa kufanya vitu vile vile tulivyovisikia huko nyuma – kuulizia ni nani kajiandikisha kupiga kura. Kwa watu wengi hili linaonekana kama njia ya "kuiba kura" lakini kwa mtu yeyote anayetengeneza mikakati ya ushindi ya uchaguzi ni muhimu sana kujua nani kajiandikisha kupiga kura. Kuna maswali muhimu ambayo mpanga mikakati yeyote ya uchaguzi (political strategist) anajiuliza mapema.​
a. Watu wangapi wamejiandikisha kupiga kura kwenye jimbo au eneo linalogombewa?
b. Kati ya waliojiandikisha ni wangapi wanachama wa chama chako?
c. Kati ya wanachama wako waliojiandikisha ni wangapi wanapanga kupiga kura siku ya uchaguzi?
d. Ni wangapi wanapanga kumpigia kura mgombea wa chama chako?​
Maswali haya manne ni muhimu sana kwa uchaguzi wowote wenye kuhusisha chama zaidi ya kimoja au zaidi ya mgombea mmoja. Lengo la kutaka majibu kwenye maswali haya ni kutaka hasa kujua mwelekeo wa wapiga kura siku ya uchaguzi ukoje kwa kadiri chama chako kinahusiska. Kwa mfano, kama watu wengi sana wamejiandikisha kupiga kura na kati yao wengi wanapanga kupiga kura siku hiyo ya uchaguzi basi mwanamkakati wetu atatakiwa kufanya juhudi kubwa sana ya kutaka kujua kati ya hao ni wangapi ambao ni wanachama wa chama chake. Hivyo, juhudi kubwa itawekwa kwenye kuhamasisha wanachama kujitokeza zaidi kupiga kura – kama wamejiandikisha kwa wingi.​
Kwa mfano, kwenye uchaguzi ambapo watu 100,000 wamejiandikisha kupiga kura, utafiti unaonesha kuwa karibu 60,000 ni wanachama wa chama kimoja. Sasa Chama kinahitaji kujua kati ya hao 60,000 ambao ni sawa na asilimia 60 waliojiandikisha kupiga kura ni wangapi kati yao wanapanga kupiga kura siku hiyo. Lengo ni kujaribu kuhamasisha kwa kadiri inavyowezekana wanachama kujitokeza kupiga kura. kama asilimia hamsini tu watajitokeza kupiga kura ina maana ya kuwa vyama vingine vitagawana kura zilizobakia.​
Lakini kuna lengo la pili vile vile la kutaka kujua idadi hizi. Lengo pia huwa katika kile kinachojulikana kama voters suppresion – yaani kugandamiza upigaji kura. Kama chama chenye nguvu/tawala kinaona kuwa kinaweza kikapoteza kura endapo wapiga kura wengi watajitokeza basi mbinu hutafutwa za kugandamiza upigaji kura. Katika uchaguzi wa mwaka jana nilikuwa miongoni mwa watu wachache tulioweza kuonesha kuwa CCM ingeweza kushinda uchaguzi endapo kungekuwa na ugandamizaji kura. Siyo kusudio langu hasa kuanisha mbinu mbalimbali zinazotumika duniani kugandamiza kupiga kura. Lakini ni muhimu kutambua kuwa mbinu kubwa iliyotumika ni kuhakikisha kuwa wengi waliojiandikisha kupiga kura hawajitokezi kupiga kura.​
Mbinu kama vitisho (umwagikaji damu, jeshi, n.k) zinatumika kuwafanya watu wahofie kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi. Mbinu za kutisha watu zilifanikiwa sana kuhakikisha kuwa katika historia ya Tanzania mwaka jana ndio watu wachache zaidi walijitokea kupiga kura. Tangu uhuru hatujawahi kuwa na chini ya asilimia 69 (wastani ni asilimia 70) ya waliojiandikisha kupiga kura kupiga kura. Mwaka jana ilikuwa chini ya asilimia 45. Niliandika wakati ule kuwa kama upigaji kura utakuwa chini ya asilimia 70 CCM itashinda.​
Lakini kwa vyama vya siasa pia ni muhimu kupata picha ya kundi la wapiga kura ili kujua ni ujumbe gani unataka kuufikisha wakati wa kampeni. Kama katika kufanya utafiti chama kinagundua kuwa wapiga kura wake wengi wako mjini, ni wanaume, na wana kazi rasmi ujumbe wao ni lazima utakuwa ni tofauti zaidi wa kuwahamasisha. Huwezi kwenda kuwahubiria wafanyakazi wa maofisini sera za kilimo! Hawa watapenda kujua kuhusu haki za kazi, pensheni, usalama kazini, mafao mbalimbali n.k Lakini vile vile unapoenda kuhutubia kwenye maeneo ya vijijini ambako wafanyakazi wake wengi ni wenye ajira binafsi au wakulima wa kujishikiza ujumbe wako kwao utakuwa tofauti vile vile. Hawa labda watahitaji kujua zaidi mipango mbalimbali ya kuboresha kilimo, afya ya msingi, elimu n.k​
Hivyo basi utaona kuwa japo kwa baadhi ya watu wanaweza kushtuka kuona chama kinafuatilia kujua nani kajiandikisha kupiga kura na nani mwanachama – mbinu ambazo binafsi ninaamini zinakubalika kisiasa kama hazihusishi wizi, vitisho au geresha ya aina fulani – ukweli ni kuwa hii ni mbinu ya kisiasa ya uchaguzi na wakati umefika kwa vyama vya upinzani navyo kujua mapema namna ya kuzitumia. CCM inafanya kile ambacho hakikatazwi kisheria – kwa kadiri nijuavyo. Upinzani unahitaji kujua jinsi ya kuhamasisha kujiandikisha; kujua idadi ya wanachama wake waliojiandikisha, na vile vile kuweza kufahamu ni kiasi gani kati yao wana uwezekano wa kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi.​
Bila kupata majibu ya maswali haya na hasa kwenye mfumo wetu ambapo wapiga kura wote watakaopiga kura kwenye uchaguzi huu mdogo ni wale tu waliojiandikisha mwaka jana basi kazi ya kushinda uchaguzi kwa chama kama CDM, CUF au NCCR haviwezi kuwa rahisi kama inavyodhaniwa. Vyama hivi vya upinzani vina kazi kubwa kubwa ya kuweza kupata kura za wanaCCM hasa ukizingatia kuwa kwenye uchaguzi wa mwaka jana CCM ilipata kura 35,674wakati CUF ilipata kura 11,321.
Kwa upinzani kushinda Igunda ni lazima igeuze hizo namba zilizokwenda CCM wakati kwa upande wa CCM inahitaji kura kidogo kutoka upinzani kuweza kuziba jaribio lolote la kuangushwa. Kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa Rais ni ishara kuna uwezekano mkubwa wa kura nyingi za CUF zikaenda kumpa nguvu kura za CCM na hivyo kupunguza athari yoyote ya kura za CCM kupungua kutokana na hasira za kuondoka kwa Rostam.​
Lakini namba hizi mbili hazina maana kubwa bila kujua idadi ya waliojiandikisha kura Igunga. Ni idadi hiyo kwa kweli ndio itakayoamua ni nani atakuwa mshindi kwani kama wanachama wengi walioiunga mkono CHADEMA mwaka jana hawakupata nafasi ya kupiga kura (kwa sababu hakukuwa na mgombea wa CDM) basi watu hawa wanaweza kujitokeza zaidi safari hii kwani mgombea "wao" amepatikana. Swali kubwa ni kiasi gani cha waliopigia kura CCM na CUF mwaka jana watahama na kwenda kuipigia kura CDM?​
Idadi hiyo ni ipi?
Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya kuaminika watu waliojiandikisha kupiga kura mwaka jana huko Igunga ni 170,586. Hii ni idadi kubwa sana. Lakini kwa kuiangalia idadi hii na kulinganisha na watu waliojitokeza kupiga kura mwaka jana ni rahisi kwa namna fulani kuweza kutabiri mwelekeo wa uchaguzi mdogo wa Igunga kwa kuangalia namba. Kama mwanamkakati wa kisiasa kuna vitu naweza kuvisema kwa uhakika kuhusu nani ataelekea kushinda. Lakini hebu tuangalia hizi namba kwa ukaribu kidogo.​
- Waliojiandikisha kupiga kura mwaka jana = 170, 586
- Walioipigia kura CCM = 35,674
- Walioipigia kura CUF = 11, 321
- Kura zilizoharibika = 2018
- Jumla ya kura zilizopigwa = 49,013.​
Hivyo: Waliopiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwenye kura za wabunge ni asilimia 28.73 ya wale waliojiandikisha kupiga kura. Kwa maneno mengine asilimia 71 ya waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza kupiga kura (hii ni karibu kabisa na theluthi mbili ya wapiga kura waliojiandikisha).​
Kwa kulinganisha kidogo tunaweza kuona kuwa kura za Urais za Igunga kati ya wagombea 7 ambao majina yao yalikuwepo kwenye karatasi ya kura mgombea wa CCM alipata kura: 24,945, wa CUF= 7,355, CHADEMA =6,815 na wagombea wengine 521. Jumla ya kura zote pamoja na zilizoharibika zilikuwa 40,412. Hivyo, waliojitokeza kupiga kura za urais ni sawa na asilimia 23.69 ya wale waliojiandikisha kupiga kura.​
Namba hizi zinatuonesha vitu kadhaa:​
1. Karibu watu 10,000 walioenda kupiga kura za wabunge hawakupiga kura za Rais.
2. Mgombea wa Urais wa CCM alipoteza kura 10,729 kulinganisha na kura alizopata mgombea wa Ubunge wa CCM
3. Mgombea wa Urais wa CUF alipoteza kura 3966 kulinganisha na kura alizopata mgombea wa Ubunge wa CUF
4. Mgombea wa Urais wa CHADEMA alipata kura 6,815
Swali hapa la msingi ni kukosekana kwa mgombea wa Ubunge wa CHADEMA kule Igunga kuliathiri kwa kiasi gani kura za mgombea wa Urais hasa tukiangalia jinsi ambavyo matokeo ya ubunge ya CCM na CUF yanavyoonekana kuwa juu ya yale ya Rais? Je yawezekana kama mwelekeo huo ungeendelea yawezekana mgombea Ubunge wa CDM angepata kura zaidi ya zile za Rais? Je kura alizopata Dr. Slaa ni sehemu ya kura ambazo Kikwete na LIpumba walinyimwa au zilikuwa ni kura za wale ambao walikuwa ni nje ya hao wapiga kura wa CCM na CUF? Kama ni hilo la pili, ni kwanini karibu watu elfu 13 ambao walipiga kura za Ubunge kwa vyama vyao hawakupigia kura urais wa vyama vyao?​
Siri itakuwepo kwenye kuzuia watu kujitokeza kupiga kura
Ni wazi kabisa – angalau inapaswa kuwa wazi – kuweza kuona kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo yatategemea sana upigaji kura. Hadi hivi sasa mojawapo ya taarifa ninazozisikia kutoka Igunga ni kuwa vituo vya kupigia kura viko mbalimbali sana kiasi kwamba inataka moyo kwa mtu kwenda kupiga kura. Hii yaweza kuwa ni mbinu ya "kijiografia" ya kugandamiza upigaji kura. Ni kitu gani kitamfanya mzee atembee maili moja au mbili au zaidi kwenda kupiga kura?​
Katika hili vyama ni lazima vijipange kuhamasisha wanachama wake na mashibiki wake kujitokeza kupiga kura na kujitolea usafiri wa kupelekana kwenda kupiga kura na kurudi. Sheria ya Uchaguzi (ambayo niliibeza tangu ilipoanza kufikiria na kuja kupitishwa) inakataza watu kukodisha magari kwa ajili ya kupeleka watu na kuwarudisha kutoka vituo vya kupigia kura (Ibara 23:3,4). Lakini sheria hiyo hiyo (ibara ya 23:5) inaruhusu wapiga kura wenyewe kwa kutumia gharama zao wenyewe (joint cost) kusaidia kupelekana kwenye vituo vya kupigia kura na kurudisha. Lakini vile vile sheria hiyo inatoa jukumu kwa serikali kuhakikisha kuwa usafiri unakuwepo kwa wale wote (bila kujali vyama au siasa) wanaotaka kufika mahali pa kupigia kura endapo kutokana na sababu mbalimbali vituo vya kupigia kura viko mbali na makazi yao.​
Hii ina maana ya kwamba, hoja ya kuwa watu hawakuweza kufika kwenye maeneo ya kupigia kura kwa sababu ya umbali, mto au daraka haina nguvu kwani vyama vinatakiwa vipange na sreikali na kuhamasisha wanachama wao kujipatia usafiri wao kwenda vituo vya kupigia kura. Kwa vile haki ya kupiga kura ni haki ya msingi ni muhimu wananchi watambue kuwa serikali inaweza kukodi au kuhakikisha kuwa mabasi na vyombo vya usafiri vinakuwepo kwa watu wanaotaka kupiga kura.
Kwa ufupi ni kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga yatategemea sana hisabati na jinsi namba zinavyoweza kutumika. Tuangalie wiki moja iliyobakia kuweza kuona ni kwa kiasi gani kura zinagandamizwa na ni kwa kiasi gani watu wanajipanga kujitokeza kupiga kura au kusaidiwa kujitokeza kupiga kura ili watu wasiwe na udhuru. Upinzani utafanya vizuri endapo watu wengi watajitokeza kupiga kura na CCM itafanya vizuri kama watu wachache watajitokeza kupiga kura.​
Imeandikwa na M. M. Mwanakijiji
SOMA MAKALA HII YA KUCHANGAMSHA AKILI: Uchaguzi Igunga utaamuliwa na namba siyo vilemba! | Fikra Pevu | Kisima cha busara!
 
Jimbo la Igunga lina vijiji vipatavyo 98, kata 26 na tarafa 3 Nimejaribu kupitia mitandao kujua idadi ya wapiga kura Jimbo la Igunga, mwaka 2005 waliopiga kura ni zaidi 75,000 ambapo ni wastani wa wapiga kura 765 kila kijiji na 2800 hivi kwa kila kata au 25,000 kwa kila tarafa.

Mwaka 2010 idadi ya wapiga kura karibu 47,000 ambopo ni sawa wa wastani wa wapiga kura 479 kwa kila kijiji ambapo kwa kila kata ni 1807 na kitarafa ni wastani wa 1566 hivi.

Kwa takwimu hizo chama chochote kikicheza kara vizuri na kupata kwa uchache wa wapigipa kura 400 kwa kila kijiji kwa kuangalia idadi ya wapiga kura 75,000 waliojitokeza 2005 watajihakilishia ushindi wa zaidi ya %50.

Tukichukulia takwimu za 2010 ya wapiga kura 47000 wanahitaji wastani wa wapigakura 240 kila kijiji kujìhakikishia ushindi wa % 50.

CDM wakiweza kulinda mtaji wa kura alizopata Dr Slaa 8800 watahitaji wapiga kura 150 wapya toka katika vijiji 98 kujihakikishia ushindi wa % 50.
Nawakilisha.
 
Good analysis, chupi zinawabana na presha inapanda presha inashuka....kazi kwao
 
Mkuu upo sahihi kabisa, wingi wa watu ktk mikutano sio sababu ya ushindi maana wengine wanaenda kusikiliza sera tu.
 
Sasa kama uchaguzi utaamuliwa kwa kura itakuwaje kwa ccm waliokwisha nunua kadi za wapiga kura na tayari wanazo?
Inavyoonyesha ni kwamba tayari wameshapiga kura na sanduku zimefichwa darini, zitashushwa baada ya watu kupiga kura.
 
Nakubaliana na wewe MKJJ kuwa uchaguzi wa Igunga na wowote ule huamuliwa kwa watu waliojitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi kama tu uchaguzi unakuwa free and fair, lakini mimi huwa nakataa watu wanaposema hautaamuliwa na mikutano inayofanyika leo. Nafikiri waliopanga kuwe na kampeni kabla ya kupiga kura walijua kabisa kampeni au mikutano ni factor au catalyst tosha ya kuonyesha mwelekeo wa ushindi. Nchi za wenzetu kama huko US na UK huwa wanajua matokeo hata kabla ya kupiga kura kutokana na kampeni zinavyofanyika, siku ya kupiga kura sana sana huwa ni kwa undeciided voters(narudia tena kwa nchi za wenzetu).

Kama usipofanya kampeni kwa kusubiri siku ya kupiga kura sijui maswali yako uliyo uliza yatajibiwa vipi, utajuaje chama chako kinapendwa jua ushabiki na shamra shamra pia zina msaada wa kuongeza wapiga kura ndio maana tunaona CCM wanajitahidi kuwapeleka kina Joti na kina Dokii kule, ingekuwa ni suala la kujua idadi tu na kuridhika tayari CCM kina wanachama wengi kule na kama ni data tayari uchaguzi uliopita CCM ilipata zaidi ya kura 40,000. Kwa hiyo suala hapa si kujua una wapiga kura wangapi je wako active? isije siku ya kupiga kura ukajiridhisha niliandikisha wapiga kura 10,000 lakini ukashangaa umepata kura 2,000.
 
sisi wa2 waigungawenyewe, ndo2na tamaa, 2nauza kadi alafu 2najifanya ha2taki umasikini namanyanyaso ya ccm,je sisi sio wanafiki? Enyi chadema endeleeni ku2hamasiha, mpaka 2015 2takua tumekua wajanja. Chadema, halaaaaa big up, wa2wangu
 
Sasa kama uchaguzi utaamuliwa kwa kura itakuwaje kwa ccm waliokwisha nunua kadi za wapiga kura na tayari wanazo?
Inavyoonyesha ni kwamba tayari wameshapiga kura na sanduku zimefichwa darini, zitashushwa baada ya watu kupiga kura.

Mungi hii ndio maana yake; kama ni kweli CCM wananunua "kadi za wapiga kura" wanachofanya ndicho nakionesha kwenye makala hii kwamba lengo ni kupunguza watu watakaojitokeza kupiga kura. Kama huna kadi ya kupiga kura ni vigumu kuamka asubuhi na kwenda kupiga kura. Hivyo, kama strategists wa CCM wanaamini wanaweza kutumia shilingi 10,000 kwa kila kadi kununua kadi kadhaa hasa za maeneo sema ya mjini basi wanaweza sana kuathiri upigaji kura. Fikiria kama watatumia shilingi milioni 500 kwa zoezi hilo wanaweza kuondoa karibu kadi 50,000!

Hata hivyo siamini kama CCM inaweza kwenda na kutumia kiasi hicho kwani tofauti ya kura itakuwa kati ya mshinda na anayefuatia naamini itakuwa +- 15,000 hivi.
 
Nakubaliana na wewe MKJJ kuwa uchaguzi wa Igunga na wowote ule huamuliwa kwa watu waliojitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi kama tu uchaguzi unakuwa free and fair, lakini mimi huwa nakataa watu wanaposema hautaamuliwa na mikutano inayofanyika leo. Nafikiri waliopanga kuwe na kampeni kabla ya kupiga kura walijua kabisa kampeni au mikutano ni factor au catalyst tosha ya kuonyesha mwelekeo wa ushindi. Nchi za wenzetu kama huko US na UK huwa wanajua matokeo hata kabla ya kupiga kura kutokana na kampeni zinavyofanyika, siku ya kupiga kura sana sana huwa ni kwa undeciided voters(narudia tena kwa nchi za wenzetu).

Kama usipofanya kampeni kwa kusubiri siku ya kupiga kura sijui maswali yako uliyo uliza yatajibiwa vipi, utajuaje chama chako kinapendwa jua ushabiki na shamra shamra pia zina msaada wa kuongeza wapiga kura ndio maana tunaona CCM wanajitahidi kuwapeleka kina Joti na kina Dokii kule, ingekuwa ni suala la kujua idadi tu na kuridhika tayari CCM kina wanachama wengi kule na kama ni data tayari uchaguzi uliopita CCM ilipata zaidi ya kura 40,000. Kwa hiyo suala hapa si kujua una wapiga kura wangapi je wako active? isije siku ya kupiga kura ukajiridhisha niliandikisha wapiga kura 10,000 lakini ukashangaa umepata kura 2,000.

unachosema ni kweli lakini x factor ya uchaguzi wetu nyumbani ni mfumo mbaya uliopo sasa. Watu watakaopiga kura Igunga ni wale tu ambao walikuwa wamejiandikisha mwaka jana. Hakuna kujiandikisha upya. Kwa maneno mengine vijana wote waliofikisha miaka 18 kuanzia Oktoba 29 mwaka jana na hadi sema Septamba 30 mwaka huu hawawezi kupiga kura! Wanaweza kuja kwenye maandamano, wanaweza kuvaa rangi za chama, wanaweza kuzungumza kwa hamasa kubwa lakini THEY WILL NOT VOTE.

Sasa kama hili ni kweli ni lazima turudi kwenye uchaguzi ule wa mwaka jana. Waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 170,586 lakini siku ya kupiga kura walijitokeza kama 49 elfu hivi ambayo ni chini ya asilimia 30 ya wapiga kura. Hii ni chini ya national average ya nchi nzima ambayo ilikuwa around 42 percent ambayo nayo ni chini ya election average ya chaguzi zote kumi zilizopita ambayo ilikuwa inaelea kwenye asilimia 70!
 
Kwa mwenendo wa mikutano hii CDM wameifanya mpaka sasa inaonyesha dhahiri wananchi wameamka sana na obvious watataka mabadiliko. Shaka yangu ni Je,, CDM wamejiandaaje kukabiliana na faulo/uchakachuaji unaoweza kujitokeza, maana tayari tushaona DC akifanya faulo, shahada za kupigia kura zikinunuliwa
 
CCM wasipochakachua kwa idadi yoyote itakayojitokeza CDM itashinda kwani watu wameelimika vya kutosha.
 
CCM wasipochakachua kwa idadi yoyote itakayojitokeza CDM itashinda kwani watu wameelimika vya kutosha.

Usijidanganye hivyo; kinyume na watu wanavyofikiria uchaguzi hucheza sana na hesabu kuliko mikutano ya kisiasa. Usiamini hata kidogo idadi ya watu wanaojitokeza wakiwa wamevaa nguo za rangi ya chama! Ukiweza kumanipulate namba ya wapiga kura unaweza ukaamua nani awe mshindi.
 
Kete za CCM zilizobaki ni kuwatisha wapiga kura wasijitokeze na kuwanunua mawakala. Watamwagiana tindikali, watachomeana nyumba na mwisho Watauana wenyewe kwa wenyewe. Hawatafuti kura za huruma na hawana muda wa kuwadhuru wana CHADEMA maana wanajua wakiwadhuru itajulikana ni wao wamefanya hivyo. Wao wanaviziana wenyewe kwa wenyewe wakati hamna mashahidi na kutoana kafara. Ukisikiliza kampeni zao hawaongelei sera isipokuwa kulalama kwamba kuna hatari ya kufa mtu Igunga. Uvumi ni kuwa wametenga sh 150,000 kwa kila wakala. Sasa CHADEMA ili kushinda lazima iwajaze ujasiri wananchi wajitokeze kupiga kura na iwe na mawakala wasionunulika. Zaidi ya hapo hamna ushindi.
 
Mkuu upo sahihi kabisa, wingi wa watu ktk mikutano sio sababu ya ushindi maana wengine wanaenda kusikiliza sera tu.

Lakini pia kama watu hata kwenye hiyo mikutano hawaji sitarajii watakuja kukupigia kura
 
Wakuu, free and fair elections katika mazingira ya kifisadi na ukosefu wa maadili ni ndoto.
 
unachosema ni kweli lakini x factor ya uchaguzi wetu nyumbani ni mfumo mbaya uliopo sasa. Watu watakaopiga kura Igunga ni wale tu ambao walikuwa wamejiandikisha mwaka jana. Hakuna kujiandikisha upya. Kwa maneno mengine vijana wote waliofikisha miaka 18 kuanzia Oktoba 29 mwaka jana na hadi sema Septamba 30 mwaka huu hawawezi kupiga kura! Wanaweza kuja kwenye maandamano, wanaweza kuvaa rangi za chama, wanaweza kuzungumza kwa hamasa kubwa lakini THEY WILL NOT VOTE.

Sasa kama hili ni kweli ni lazima turudi kwenye uchaguzi ule wa mwaka jana. Waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 170,586 lakini siku ya kupiga kura walijitokeza kama 49 elfu hivi ambayo ni chini ya asilimia 30 ya wapiga kura. Hii ni chini ya national average ya nchi nzima ambayo ilikuwa around 42 percent ambayo nayo ni chini ya election average ya chaguzi zote kumi zilizopita ambayo ilikuwa inaelea kwenye asilimia 70!

Mzee Mwanakijiji; matokeo ya Igunga yapo kinachosubiriwa ni siku ya zoezi la upigaji kura, mfumo mzima wa uchaguzi ni wa kilaghai, inakuwaje kusiwepo na zoezi la uandikishwaji upya kwa wapiga kura? Wapo wapiga kura waliohama Igunga na wapo wageni waliohamia vile vile wapo vijana waliofikisha umri wa miaka 18, kimsingi kila mkazi wa Igunga mwenye umri wa 18 na zaidi anahaki ya kuchagua mwalikilishi wake bungeni sasa je iweje litumike daftari la zamani? Malalamiko mengi yalitokea kuhusu madaftari ya wapiga kura kwenye uchaguzi wa raisi, je serikali inataka kusema daftari la Igunga ni safi kiasi cha klifanya litumike? Je ni nani alilihakiki? Kimsingi matokeo tutaambiwa chama chetu kitukufu kimeshinda uchaguzi kwa asilimia kati ya 1% hadi 3% hivi, hii ni kutaka kufanya uchaguzi uonekane ulikuwa competitive na kila chama kilikuwa na nafasi ya kushinda.

Chama
Gongo la Mboto DSM.
 
MwanaKijiji,
Igunga watasahihisha makosa ya 1994, 1995, 2000, 2005 na 2010? Makala yako kwenye TD ya leo natamani ingesomwa na WanaIgunga kwa visiku hivi vichache vilivyobaki. Hofu yangu kubwa ni kuwa kama wapiga kura ni walewale wa mwaka jana, matokeo yatakuwa yaleyale.
 
13 Reactions
Reply
Back
Top Bottom