UCHAGUZI UJAO KENYA UNATUFUNDISHA SISI LOloTE???

KIMOSTODO

Member
Jun 1, 2012
9
1
HARAKATI za wataka urais wa Tanzania mwaka 2015 sasa zimeingia bungeni ambako baadhi ya wabunge wanajipanga kwenye makundi mithili ya ambayo yamekuwa yakionekana katika siasa za Kenya.
Raia Mwema limeambiwa kwamba yapo mawasiliano miongoni mwa wabunge na wanasiasa na baadhi yao wana mawasiliano na wataalamu kutoka Kenya, ambao kwa pamoja wanaandaa mikakati inayoweza kuanza kutekelezwa kwenye mkutano ujao wa Bunge.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya vikao mbalimbali vya wahusika hao, baadhi ya wanasiasa wamekwishakujipanga kuanza kutangaza nia zao hizo wakati wowote kuanzia sasa.
“Wakati wowote (anamtaja kwa jina) atawasiliana na mmoja wa wanasiasa ambaye anatajwa sana kuwania urais lakini anazidi kuporomoka kwa sababu za kuchafuka kisiasa na kuzorota kwa afya yake. Atamjulisha (anamtaja jina) na kumwambia akiona anaelemewa ahamie kambi yake.
“Kwa ujumla wameshaanza kujipanga na watakuwa na wabunge kama 100 wenye nguvu ili ikibidi wakiwa na nguvu waweze kufuatwa na wagombea wengine kama wataona umuhimu ama wawe na sauti katika uchaguzi ujao na baada ya uchaguzi wakati wa kuunda serikali,” anaeleza mtoa habari wetu aliye karibu na mpango huo.
Baadhi ya wabunge wakiwamo mawaziri wa sasa wanajiandaa kutumia Bunge lijalo kuungana bila kujali tofauti za vyama vyao, wakiiga mfumo huo kutoka Kenya ambako kwa sasa, Serikali na Bunge la nchi hiyo ni vipande vyenye kiu ya kupigania wagombea urais na si kutumikia wananchi.
Kasi hiyo itakapokuwa ikishika moto, mambo yatakayokuwa yakijitokeza ni pamoja na kauli za baadhi ya wasemaji kulitumia Bunge kuwakandamiza baadhi ya viongozi wanaodhamiwa ni hatari kwa kambi zao za urais na hasa kama ikijitokeza watu hao hatari kwa kambi zao ni sehemu ya mawaziri.
Hali hiyo inajitokeza huku tayari kukiwa na malalamiko miongoni mwa watumishi wa umma kwamba, Bunge limeanza kujiendesha kwa kuingilia muhimili wa utendaji ambao ni Serikali.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge wamekuwa wakiwaunga mkono baadhi ya viongozi waastafu wa Serikali wenye nia ya kuwania urais mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wenzao ambao hawana uamuzi kuhusu nani wamuunge mkono.
Taarifa inasema ni mambo hayo ambayo yamesababisha kutolewa kauli kama ile ya Rais Jakaya Kikwete kwa wakuu wa mikoa na wilaya waliokutana mjini Dodoma kwa ajili ya mafunzo maalumu ya kuwataka wasiwe madalali wa wanasiasa na badala yake wafanye kazi ya kutawala na kuwatumikia wananchi.
“Uungwaji mkono wa namna hiyo unahusisha mambo mengi, mojawapo ni kuhakikisha yule hasimu wetu mkubwa kuelekea kinyang’anyiro cha urais anashughulikiwa na hasa anapowasilisha hoja zake bungeni,” anaeleza mtoa habari wetu.
Kwa sasa, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kinachoonekana kuwa na kambi za wagombea urais ambazo zimekuwa zikichuana katika siasa za ndani ya chama hicho na hasa wakati wa uendeshaji wa vikao vyake vya juu vikiwamo vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC).
Wakati mwingine matokeo ya michuano hiyo ya kambi imekuwa ikikigharimu chama hicho kiasi cha kupoteza baadhi ya majimbo ya uchaguzi, ngazi ya ubunge ambako kambi moja inaposhindwa kupitishiwa mgombea wake huunga mkono kwa siri mgombea wa chama pinzani, hali ambayo imekuwa ikinufaisha zaidi kambi ya upinzani.
Lakini viongozi mbalimbali wa CCM wamenukuliwa wakisema mvutano uliopo ndani ya chama hicho kikongwe nchini unahusisha kurejea kwa vitendo misingi ya chama hicho jambo ambalo limekuwa likipingwa na wenzao na hivyo kuibua mvutano.
Hayo yakiendelea, mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya nao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kuleta changamoto na mshawasha wa aina yake katika makundi yanayowania urais wa 2012.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa na wengi kuwamo katika katiba mpya ni pamoja na ruksa kwa ushiriki wa wagombea binafsi, mapendekezo ambayo gazeti hili limepata kueleza kuwa unaridhiwa pia na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwapo kwa hofu kwamba mjadala wa kuundwa kwa katiba mpya unaweza kuvurugwa na matakwa ya makundi yanayowania urais mwaka 2015.
Kati ya hayo ni taarifa ambazo zinasema ya kuwa sasa ipo hoja kwamba kama Muungano unadumu licha ya sekeseke linaloendelea sasa Zanzibar, basi suala la urais wa Muungano kwa zamu liingizwe kwenye katiba ijayo.
Katika hoja zinazotolewa kuhusiana na kupokezana zamu inaelezwa kwamba kwa sasa ni vyema kuipa nafasi Zanzibar kutokana na kupamba moto kwa mjadala wa uhai wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Ukiacha hayo, orodha ya wawania urais imekuwa ikikua kila mara, sasa majina yanayotajwa yakiwa ni ya Edward Lowassa aliyejizulu uwaziri mkuu katika kashfa ya mradi wa umeme wa dharura wa Richmond, spika mstaafu wa Bunge na Waziri wa Maendeleo ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Wengine wanaotajwa kuwamo katika harakati hizo ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Wanaotajwa kutoka nje ya Serikali ni waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na aliyepata kuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro.
Kwa upande wa Zanzibar, wanaotajwa ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein; rais mstaafu, Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais wa Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Katika Upinzani wamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa; Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Maswa, John Shibuda; Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed ambaye taarifa zinasema kufika 2015 anaweza kuwa amepata chama kingine nje ya Chama cha Wananchi (CUF).
 
Back
Top Bottom