Uchaguzi 2020 Uchaguzi Tanzania 2020: Kwanini kumekuwa na ugumu wa ushirikiano wa CHADEMA na ACT-Wazalendo?

wahid1

JF-Expert Member
Jun 26, 2014
225
279
Baada ya Vyama vya CHADEMA na ACT Wazalendo kuwapitisha Tundu Lissu na Benard Membe kuwa wagombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, itakuwa vigumu kuwa na mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama hivyo viwili katika ngazi hiyo.

Ni vigumu lakini si kwamba haiwezekani kabisa.

Kwa miezi kadhaa kabla ya mikutano ya wiki hii iliyowapitisha wagombea hao, vyama hivyo vikuu vya upinzani nchini Tanzania kwa sasa, vilikuwa na mazungumzo yasio rasmi baina yao kuhusu ushirikiano kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vilisimamisha mgombea mmoja wa urais; Edward Lowasa, kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliyepata kura zaidi ya milioni sita - mara ya kwanza kwa mgombea wa upinzani kupata idadi hiyo ya kura.

Mafanikio ya Ukawa ya mwaka 2015 ndiyo yalikuwa kichocheo kikubwa cha wapinzani kuona umuhimu wa kuungana dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, ambaye alipata kura zaidi ya milioni nane kwenye mchuano wake na Lowassa.

Kitendo cha CHADEMA kufanya Mkutano Mkuu na kumpitisha Lissu huku ACT-Wazalendo nayo ikifanya hivyohivyo kumpata Membe, kinaonyesha kwamba mazungumzo yaliyofanyika hayakufikia mwafaka kwenye suala hilo.

Kwa uzoefu wa mwaka 2015, vyama vilivyomuunga mkono Lowassa; NLD, NCCR Mageuzi na CUF havikuwa vimewatangaza wagombea wake kabla ya Chadema kumpitisha Lowassa na ilibidi CUF imruhusu aliyekuwa mwanachama wake mashuhuri, Juma Duni Haji, ajiunge na Chadema ili awe mgombea mwenza.

Na kabla ya hapo, Ukawa ilikuwa imetengenezwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi - umoja ukiundwa wakati wa mchakato wa kutafuta Katiba Mpya ya Tanzania kupitia Bunge la Katiba. Mpaka wakati uchaguzi wa 2015 unafika, vyama hivyo rafiki vilikuwa tayari na walau mwaka mmoja wa kufanya kazi na kujiandaa kwa ushirikiano.

CHADEMA tayari imetangaza kwamba Lissu atachukua fomu Agosti 8 mwaka huu huku Membe akitarajiwa kuchukua fomu hizo siku moja kabla - yaani Agosti 7 mwaka huu.

Ili Lissu au Membe abaki peke yake, ni lazima kimojawapo ya vyama hivyo kifanye uamuzi wa kuacha kuwania na jambo hilo litakuwa sawa na ukaidi kwa vikao vya juu vya chama vilivyofanya uamuzi wa kuwapitisha wagombee katika nafasi hizo.

Kwanini kumekuwa na ugumu wa ushirikiano wa CHADEMA na ACT?

Kufahamu kwanini hali imefikia katika hatua hii, ni muhimu kufahamu asili ya vyama hivi viwili na uhusiano wa kibinafsi baina ya viongozi wa juu wa vyama hivi.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ni zao la CHADEMA. Alianza siasa zake ndani ya chama hicho na kupanda kutoka mwanasiasa anayechipukia hadi kuwa mbunge na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.

Msuguano wake na CHADEMA ulijitokeza mwaka 2009 wakati alipotangaza nia ya kutaka kuwania wadhifa wa Mwenyekiti wa chama hicho. Jambo hilo lilileta hali ya sintofahamu ndani ya chama kiasi kwamba ilibidi wazee wa chama hicho wakiongozwa na Bob Makani, wamwombe Zitto asigombee na akakubali.

Hata hivyo, jambo hilo likawa limeharibu uhusiano baina yake na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe. Yeye na wafuasi wake walichukulia uamuzi huo wa Zitto kama kitendo cha utovu wa shukrani na utiifu kwa mtu aliyempika katika siasa na kumpa umaarufu.

Sintofahamu hiyo iliendelea hata baada ya Zitto kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho na ilifikia kilele mwaka 2013 kwa CHADEMA kumfukuza uanachama mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini pamoja na watu waliodaiwa kuwa naye karibu kisiasa ndani ya chama hicho.

Mmoja wa viongozi wa Chadema waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha Zitto anafukuzwa Chadema kwa madai ya usaliti dhidi ya chama hicho alikuwa ni Tundu Lissu ambaye sasa ndiye ametangazwa kuwa mgombea wa Chadema mwaka huu.

Baada ya kufukuzwa, ndipo Zitto aliamua kujiunga na ACT Wazalendo kilichokuwa kimeanzishwa na baadhi ya waliokuwa maswahiba wake wa kisiasa alipokuwa Chadema.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyoyafanya miaka michache iliyopita, Zitto alitaja uamuzi wake wa kuwania Uenyekiti wa Chadema kama jambo analojutia zaidi kuwahi kulifanya na kwamba kama nyakati zingekuwa zinarudi nyuma, asingechukua uamuzi ule na pengine leo angebaki kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa chama hicho.

Ingawa ACT imepata usajili miaka sita tu iliyopita, kwa sasa kinatajwa kuwa chama kinachokua kwa kasi zaidi hapa nchini - hasa baada ya kufanikiwa kupata wanachama wa kariba ya Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Membe aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania.

Chadema kinaiona ACT Wazalendo kama mshindani wake halisi katika nafasi yake kama chama kikuu cha upinzani hapa nchini na historia ya nyuma baina ya viongozi wa vyama hivyo imefanya uhusiano wao binafsi kuwa wa kutoaminiana.

Tatizo kubwa kuliko yote katika jambo la ushirikiano baina ya vyama hivi viwili liko katika jambo moja tu; kuaminiana. Chadema hawaamini kwamba ACT inawatakia mema na ACT inaamini Chadema inataka chama hicho kife.

Lissu anataka, Membe anataka
Jambo moja kubwa la msingi kuhusu wateule hawa wawili wa Chadema na ACT Wazalendo ni kwamba hakuna aliyelazimishwa kuwania nafasi hiyo kwa sababu wote wawili wanaitaka nafasi hiyo kwa dhati kabisa.

Membe amekuwa na nia ya kuwa Rais wa Tanzania kwa takribani miaka kumi sasa. Ingawa alichukua fomu ya kutaka kupitishwa na CCM kuwania urais mwaka 2015, alishafanya uamuzi wa kutaka nafasi hiyo miaka kadhaa nyuma.

Kwa wasifu wake kama mbunge kwa takribani miaka 15, waziri kwa takribani miaka kumi, ujasiri wa kukemea maovu hata wakati akiwa ndani ya CCM - jambo lililomletea matatizo na kusababisha afukuzwe uanachama mwaka huu na ubobezi na mtandao wa marafiki ndani na nje ya nchi, Membe anaamini kwamba ana sifa zote za kuwa mgombea wa upinzani.

Kwa upande wake, Lissu anaamini kwamba kama mgombea aliyepitishwa na chama kikuu cha upinzani nchini, anatakiwa kuwa mgombea wa upinzani.

Kwa historia yake kama mwanaharakati dhidi ya uonevu wa serikali kwa takribani miaka 15 kabla hajawa mbunge, uzoefu wake bungeni na ukweli kwamba inaonekana ana upepo wa wafuasi wanaovutiwa na ujasiri wake na uwezo wa kujenga na kupangua hoja, Lissu anaoana anafaa kupeperusha bendera ya upinzani.

Tofauti na mwaka 2015 au katika uchaguzi mkuu wowote uliofanyika nyuma, upinzani una wagombea wawili wenye sifa zinazotosha kupeperusha bendera -hazifanani lakini muunganiko wake unatengeneza ukamilifu.

Kama kusingekuwa na suala la Muungano linalohitaji vyama viwe na mgombea au mwenza wake katika tiketi ya kuwania urais, Membe na Lissu wangeweza kutengeneza timu nzuri ya Rais na Makamu wa Rais; mmoja 'anatema cheche', mmoja mwanadiplomasia; mwengine mtu anayejua mfumo, mwingine kutoka nje ya mfumo - jasusi na mzua balaa, mtulivu na machachari bila kusahau mtu mzima na mwandamizi.

Kwa bahati mbaya, mfumo wa nchi ya Tanzania hauruhusu jozi ya Lissu na Membe kuingia kwa tiketi moja.

Nini kinaweza kufanyika
Membe na Lissu wanachukua fomu za kuwania urais wiki hii mjini Dodoma. Kati ya leo na Agosti 26 ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itapitisha majina ya wagombea urais, kuna muda wa takribani wiki tatu za kuangalia la kufanya.

Kisheria, ili kubadili mgombea au kufanya maamuzi ya kumuunga mkono mgombea mwingine, vyama vinatakiwa kuitisha mikutano mingine ili kutengua maamuzi yaliyofanywa.

Mwanasheria wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban, alinieleza wiki hii kwamba utaratibu huo utahusisha kuandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa taarifa hiyo. Katika muda uliobaki, uwezekano wa Chadema au ACT Wazalendo kurejea kwenye mchakato huu ni mdogo.

Hata hivyo, kwa wiki nzima iliyopita, viongozi wa vyama hivyo viwili wamekuwa wakizungumza hadharani kuhusu umuhimu wa kuwa na timu moja katika uchaguzi wa mwaka huu uliopangwa kufanyika Oktoba 28.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chadema uliofanyika Agosti 4 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ACT, Maalim Seif Shariff Hamad, alimwambia Mbowe mbele ya wajumbe wa chama hicho kwamba jukumu la kuhakikisha vyama hivyo vinashirikiana liko kwenye mabega ya wawili hao; Mbowe na Seif.

Kwa sababu suala la ushirikiano huu ni la kisiasa zaidi kuliko kisheria, kama litakuwapo, litahitaji kushughulikiwa kisiasa na kuna namna kadhaa za kufanya.

Namna ya kwanza ni kwa mmoja wa wagombea hawa kuchukua fomu lakini asirudishe na hivyo kuwa amejitoa rasmi. Hili linaweza kufanyika endapo chama ambacho mgombea wake amejitoa, kitakuwa kimeambiwa katika mazungumzo ni kwa namna gani kitafaidika na uamuzi wa namna hiyo.

Njia ya pili ni kufuata njia ya Malawi ambapo katika uchaguzi uliofanyika takribani miezi miwili iliyopita, wapinzani wawili; Lazarus Chakwera (aliyekuja kuwa mshindi) na Saulos Chilima, waliungana dhidi ya Rais Arthur Peter Mutharika na kumshinda.

Katika uchaguzi wa kwanza uliopingwa mahakamani, Chilima na Chakwera walipata asilimia 35 na 20 dhidi ya Chakwera aliyepata asilimia 37. Kukiwa na mkakati, wapinzani wawili wanaweza kuungana dhidi ya Rais aliye madarakani kwa kushambulia kutokea pande mbili tofauti.

Huu ni mkakati ambao baadhi ya viongozi wa vyama hivyo viwili wameniambia uko mezani na unaweza kujadiliwa. Kufanikiwa kwake kunategemea ni kwa namna gani vyama hivi viwili vitatengeneza mkakati wa kupambana pasipo kugombana wenyewe.

Endapo hatimaye ACT Wazalendo na Chadema vitaamua kwenda kwenye uchaguzi mkuu pasipo mpango wa kufanya kazi pamoja; ni wazi CCM itaibuka na ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Chadema ndiyo itaathirika zaidi kwa sababu ACT angalau ina uhakika wa kupata viti vya ubunge kutoka Pemba na Unguja ziliko ngome zake na kwa vyovyote vile kitaingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar; kama mshindi au mbia kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar.

Mpira uko mikononi mwa Chadema.

Chanzo:

Ni Membe au Lissu 2020? - BBC News Swahili

_113818659_527561d3-bce9-4346-83b4-6e58b8c259f1.jpg
 
Chadema inao mtaji wa kutosha bila kuungana. hivyo bora Chadema waende wenyewe kama Chademasababu vyama vingine vishinde visishinde hawana wanachopoteza sababu hawana nguvu yoyote kwa raia.
 
Kwa Maoni yangu Kila chama (Ccm na Chadema) kinapaswa kutafuta kura zao (walizopata na walizopoteza ) 2015 ziliko !
Hiki ndicho kipimo halisi cha kuanzia.

Niinavyo 2020 Act inachoweza ni kupunguza kura za ccm kupitia Wana ccm Wanaopenda Bernard na. Wapizani Wanaopenda Zitto lakini 2015 walimpa Magufuli kwa hasira ya Lowasa na Dr Slaa. Kwa hiyo huu sio uchaguzi wa kushinda saa nne asubuhi kwa sababu kura hutafutwa !
 
Back
Top Bottom