Uchaguzi mkuu na tafiti za kinafiki | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uchaguzi mkuu na tafiti za kinafiki

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Jumakidogo, Oct 29, 2010.

 1. Jumakidogo

  Jumakidogo R I P

  #1
  Oct 29, 2010
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 1,859
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  REDET, SYNOVATE na, wagombea wametugeuza watanzania ‘ndondocha’


  Wagombea wote watakaoshindwa kutimiza ahadi zao washitakiwe kwa makosa ya utapeli na udanganyifu
  Na Juma Kidogo


  Ni matumaini yangu kuwa asilimia kubwa ya watanzania ambao ni wapenzi na wasomaji wazuri wa makala ni wazima na bukheri wa afya. Kwa mara nyingine na wakati mwingine tena tunakutana na kuzungumza pamoja kwa njia hii ya maandishi.
  Kuna mambo mengi sana ya kuzungumza na kujadili wakati huu wa mpito kuelekea uchaguzi mkuu ambao utafanyika siku ya jumapili ya tarehe 31 mwezi wa 10 mwaka huu wa 2010.
  Kampeni zimeendelea kushika kasi kupasua anga na, kuchanja mbuga hasa kwa wagombea wa uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  Wanaendelea kufanya kampeni huku wakimwaga makumi kwa mamia ya ahadi kila pembe ya nchi, ahadi ambazo ni imani yangu kuwa hata wakipewa miaka 40 ya kutawala nchi hawatazitekeleza zote.
  Ndugu zangu ahadi ni deni kama walivyosema wahenga,yawezekana wagombea wetu hawa wa uraisi wamesahau kuwa ahadi ni deni na kipindi cha miaka mitano ni michache sana kwa kuyakamilisha yote wanayoyaahidi.
  Hawa hawaogopi dhambi kuwadangaya wananchi, hawaogopi kushukiwa na ghadhabu za Mungu kwa tamaa yao ya kujipatia madaraka kwa njia ya udanganyifu. Nadhani ingekuwepo sheria ya kuwashitaki kwa makosa ya udanganyifu na utapeli wagombea ambao wanashindwa kutimiza yale waliyoyaahidi kuwa watayatekeleza katika kipindi cha miaka hiyo mitano akiwepo Raisi mwenyewe.
  Kuwepo kwa sheria hiyo kungefanya wagombea kuwa waoga kwa kuheshimu sheria na hatimaye wangekuwa wanaahidi ahadi ahadi zenye ukweli.
  Tuchukue mfano huu rahisi. Tuchukulie kuwa mgombea amefanya mikutano ya kampeni 300 tu nchi nzima, japo anaweza kuwa amefanya zaidi ya hapo, hiyo ni kwa uchache tu. Na tuchukulie kuwa katika kila mkutano mgombea ameahidi ahadi mpya 5 tu, japo ni hesabu ndogo sana kulingana na ahadi zinazotolewa katika kila mkutano. Sasa chukua mikutano 300 zidisha mara 5, unapata ahadi 1500.
  Ahadi hizo 1500 gawanya kwa miaka 5 ili upate kila mwaka mgombea atatakiwa kushughulikia na kukamilisha ahadi ngapi.
  Gawanya 1500 kwa 5 unapata ahadi 300. Ni kweli serikali itakayoundwa na mgombea gani inaweza kutekeleza yote hayo katika kipindi cha mwaka mmoja tu au watatumia majini na nguvu za giza?
  Lakini nadhani pia kasoro ipo kwa wananchi wenyewe ambao ndio wanaotarajiwa kuwa wapiga kura siku ya uchaguzi ikifika.
  Wanakubali kuahidiwa ahadi lukuki huku wakishangilia kwa vifijo na mbinja kila wahudhuliapo mikautano hiyo ya kampeni.
  Sisi watanzania ni sawa na mandondocha, ‘’Misukule’’ tulioharibiwa na kupumbazwa akili na hivyo kuona kila kipitacho mbele ya macho yetu ni sawa. Ndondocha ni sawa na zumbukuku au jitu fumbakalomo ambalo halijui wala kuelewa chochote kinachoendelea.
  Kila kifanywacho na viongozi wetu ni sawa hata kama ni cha ovyo bila kufikiria wala kupima madhara yanayoweza kutupata kutokana na undondocha wetu huu.
  Yapo mengi ya kusema na kuandika ili watu wasikie au wapate kuyasoma lakini yatosha tu kusema kwamba, kabla ya kufika mwisho wa makala haya.
  Nafsi yangu haitasafishika kama sintatoa dukuduku langu kwa kujadili na kuchangia haya yafuatayo kuhusu baadhi ya taasisi zainazoibuka katika miaka ya uchaguzi mkuu na kuanza kutoa porojo za kuwahadaa wananchi. Hapa nazitaja mbili maarufu yaani REDET na SYNOVATE.


  Hapo juu nimedokeza kuwa watanzania ni
  ‘’ndondocha’’
  nikiwa na maana kuwa, wale waliokubaliana na matokeo ya tafiti za taasisi mbili ambazo zimetoa matokeo ya bandia kuhusu mwelekeo wa matokeo ya uchaguzi mkuu yatakavyokuwa yanatia mashaka kuhusu ukamili wa akili zetu sisi watanzania.
  Tasisi hizo ambazo zinajitokeza hadharani kusema na kutangaza matokeo ya uongo mbele ya halaiki ya watanzania zinapewa na nani kiburi na ujasiri wa kufanya hivyo? Au ni mwendelezo ule ule wa sanaa kama zinazofanywa na wagombea katika mchakato wa kutoa ahadi hewa?.
  Kama wananchi wanaamini kuwa matokeo hayo ni ya kweli,basi watanzania hawatakuwa na sababu ya kusimama mbele na kuukana undondocha wao.
  Kama watanzania watakuwa wakiamini kuwa utafiti huo ulifanyika kweli,watakuwa hawana haki ya kujitokeza na kusimama mbele kuukana usukule wao. Na kama watanzania wanayaamini na kuyakubali matokeo hayo basi ni aibu kujitokeza mbele na kukanusha kuwa wao si wajinga.
  Nizungumzie upuuzi wa SYNOVET pekee kwani hakuna sababu ya kuwazungumzia wote kutokana na kuwa kwa kiasi fulani matokeo yao na yale ya REDET hayatofautiani sana na inaonyesha kuwa wote walipita katika mlolongo mmoja kwa sababu walikuwa wametumwa kuropoka kwa maslahi ya kundi la watu fulani na siyo kwa faida ya watanzania wote. Haihitaji akili nyingi katika kubaini uongo wa taasisi hizi.
  SYNOVET bila aibu wanatuambia kuwa utafiti wao wameufanya katika wilaya 63 na kati ya hizo wengi wa waliohojiwa ni wananchi wa vijijini kwa asilimia 60 ya watu 2000 ambao wanadai walihojiana nao.
  Kwa mantiki hiyo wanataka kutuambia kuwa walifika pia katika mikoa ya mbali na Dar Es Salaam ama waliwahoji wapiga kura hao kwa kutumia simu zao za mkononi?
  Nasema hivyo nikiwa na maana kuwa kwa uhalisia mtu hawezi kutumia gharama kubwa kusafiri kutoka Dar Es Salaam mpaka Kigoma kwa ajili ya kwenda kumuhoji mtu mmoja tu.
  Kwa hesabu watu waliohojiwa walikuwa 2000 katika wilaya 63. Tuone katika kila wilaya walihojiwa watu wangapi, tunachukua watu 2000 na kugawanya kwa idadi ya wilaya 63, jibu tunapata watu 31.7 hii ni sawa na watu 32 walihojiwa katika kila wilaya.
  Tuchukulie kwa wastani kuwa kila wilaya ina tarafa 5, watu 32 tugawanye kwa 5 tunapata watu 6.
  Kwa maana hiyo katika kila tarafa walihojiwa watu 6. Katika tarafa tuchukulie kuwa kwa wastani kuna kata 5, sasa tugawanye watu hao 6 kwa kata hizo 5.
  Kwa maana hiyo 5 tunaigawanya kwa 6.Jibu tunapata 0.83, wanatuambia kuwa idadi ya watu wengi waliohojiwa ni wale wa vijijini, lakini kwa mchanganuo huo hapo juu inamaanisha kuwa hakuna mtu wa kijijini aliyehojiwa.
  Hivi kweli hilo ni suala linaloingia akilini kuwa kati ya watanzania zaidi ya milioni kumi waliojiandikisha kupiga kura jamaa hawa walifanikiwa kuwapata watu wa kuwahoji 2000 tu?
  Tasisi hizi zinatakiwa kubadilika sasa na kufanya kazi ambayo kila mtanzania akiisikia ataamini kuwa hakuna usanii wowote uliofanyika kuliko kurufaa akili za watu.


  Umefika wakati kwa taasisi hizi kuacha kupangia mipango yao kwenye vilabu vya komoni na kangala na badala yake wafanye tafiti kutokana na kuwahoji watanzania kwa wingi wa idadi ili kuleta matokeo yatakayokuwa yanakaribiana na ukweli halisi. Ukifanya utafiti wa papo kwa papo kwa kutumia akili yako timamu utagundua kuwa kati ya wagombea watatu wanaovuma sana katika kinyang’anyiro hicho cha uraisi,utabaini kuwa Dk Slaa yupo juu akifuatiwa kwa karibu na Kikwete na anayeshika nafasi ya tatu ni Profesa Lipumba.
  Kwa mtazamo wa watanzania wngi kuwa Dk Slaa anafaa ni kutokana kuwa ndiye mgombea pekee ambaye ameonyesha kuwa ndiye mwanamapinduzi wa kweli katika mapambano dhidi ya ufisadi, ufisadi ambao umetokea kuwa kero kubwa sana kwa watanzania hivi sasa.
  Huyu ndiye pekee ameonyesha uthubutu kuwa anaweza. Hilo limewafanya watanzania waamini kuwa kwa msimamo wake huo pia anao uwezo wa kusimamia sera,ilani na,mambo mengine yanayohusu maendeleo kwa ujumla ukiacha hilo la ufisadi. Watanzania wameonyesha mabadiliko makubwa katika kujitambua tangu kuingia kwa mfumo huu wa vyama vingi mwaka 1992.
  Dalili za ushabiki wa kweli wa kisiasa zimekuwa zikijionyesha dhahili hasa kwenye mikutano ya kampeni. Wakati wa ugeni wa vyama hivi tulikuwa tukishuhudia watu wakiogopa kuzungumza hata na wagombea wa vyama vya upinzani kwa kuogopa jicho la Serikali.
  Wafanyabiashara wakubwa walikuwa wakiogopa kushirikiana na vyama vya upinzani kwa kuogopa kuhujumiwa biashara zao. Walimu walikuwa wakiogopa kugombea ungozi kwa hofu ya kufukuzwa kazi.
  Hali ni tofauti hivi sasa ambapo tunashuhudia watu maarufu nao wakijiunga upande wa upinzani bila woga, haya yanaonyesha kuwa hata taasisi hizi ambazo zinaingia katika dhambi ya uongo kwa kuwadangaya watanzania kwa kufanya mahojiano na watu maalumu ambao wamewalenga wao.
  Ikiwa Dk Slaa atashindwa katika uchaguzi huu, basi atakuwa ameshindwa kutokana na mambo makubwa mawili au matatu.
  Jambo kubwa la kwanza ni kama atakuwa anashabikiwa na mashabiki ambao hawajajiandikisha kama ilivyokuwa kwa Mrema katka uchaguzi wa mwaka 1995.
  Hii ni kawaida ya mashabiki wengi na wanachama wa vyama vya upinzani.Huwa ni wazito sana katika kujiandikisha pamoja na kwenda kupiga kura.
  Mafanikio ya Chama Cha Mapinduzi yanatokana pia na kuwatumia makada wao walioko kata ngazi za chini za chama kwa kuwahamasisha wanachama wao kwenda kujiandikisha katika daftari la wapiga kura hivyo kufanya wawe na wapiga kura wenye uhakika wakati wa chaguzi mbalimbali zinapotokea.
  Jambo lingine kubwa litakaloghalimu ushindi wa Dk Slaa ni upinzani usio wa kweli kwa vyama vya siasa nchini mwetu, wapinzani wangeamua kuacha tamaa ya madaraka na kwa makusudi wangeamua kumuunga mkono mgombea mmoja anayekubalika basi katika uchaguzi wa mwaka huu ni dhahili bila ubishi ungekuwa na mafanikio makubwa sana kwa upande wao.
  Vyama vya upinzani vya Tanzania vinahitaji umoja na si kujitenga, wahenga walisema umoja ni nguvu,utengano ni udhaifu. Msemo huo, huu ndio ulikuwa wakati wake hasa.
  Suala la mwisho ni wizi wa kura, ni mashaka yangu makubwa kuwa vyama hivi havina uwezo wa kuweka mawakala katka vituo vyote vya kupigia kura nchi nzima mpaka vijini hivyo kutoa nafasi na mwanya wa kupangiwa matokeo ya bandia.
  Kwa kutambua hilo tayari taasisi za ulanguzi wa kura zimeanza kutoa matokea ya kuwasingizia wanavijiji kuwa ndio watakuwa wengi zaidi kati ya wapiga kura wote baada ya kutambua kuwa vyama hivi masikini havina uwezo wa kuweka mawakala nchi nzima hasa maeneo ya vijijini. Watambue kuwa watanzania wa sasa siyo wadanganyika tena na hawadanganyiki kwa utafiti wenu huo wa kukisia usio na tija wala manufaa kwa wanachi.


  Mwandishi wa makala haya ni mtunzi wa hadithi na mwandishi wa makala katika magazeti mabali mbali pia ni msomaji mkubwa wa tovuti hii. 0764 561078 jumakidogo@yahoo.com
   
 2. lufunyo

  lufunyo Member

  #2
  Oct 29, 2010
  Joined: Oct 29, 2010
  Messages: 70
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hiyo ni fact na kila fisadi atakasirika kuisoma..mbaya zaidi mchanganuo wa utafiti wa hawa siyowatu (synnovate) halafu ni madokta lakini hawajui maana ya utafiti na umuhimu wa uwakilishi wa watu katika utafiti yaani sample. Lakini mtu yeyote anayefanya kazi kwa kulazimishwa na fedha za mafisadi hupoteza asili yake hata kama ni msomi vipi kama hawa wa redet na siyowatu. Big up aluta continua:smile-big:
   
Loading...