Ubovu wa majengo Chuo Kikuu Dodoma; tatizo linalohitaji kumulikwa haraka

Colgate

Member
Dec 30, 2010
16
1
Thursday, 11 August 2011 20:47
0digg
Na Habel Chidawali
KUNA wakati wa kulia, na wakati wa kucheka, kuna wakati wa kufurahi na wakati wa kununa, lakini pia kuna wakati wa furaha na wakati wa huzuni.Yawezekana wakati tulionao kwa sasa hauko katika maeneo hayo niliyoyataja awali na kama hivyo ndivyo je huu ni wakati gani basi?

Wakati mwingine Watanzania tumekuwa tukifanya mambo bila ya umakini jambo linalotugharimu mbele ya safari na kuonekana tuliyoyafanya si mali kitu jambo linalotufanya tujibatize majina ya ufisadi au uchakachuaji.

Inawezekana pia, tunafanya tusichokijua ama tunafanya tunachokijua, lakini kwa makusudi mazima tunaamua kulazimisha kwa kutumia msemo wa liwalo na liwe bila ya kujali athari inayoweza kutupata mbele ya safari.

Ni hivi karibuni ilishangaza kusikia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), eti yanavuja. Yanavuja! lilikuwa ni swali ambalo nilijiuliza kabla sijathibitisha kauli hiyo na ilikuwa ni vigumu kwangu kuamini kile kilichokuwa kikizungumzwa.Tumezoea kuona hata nyumba za nyasi zinazojengwa zinakuwa na kipindi maalumu cha kudumu katika uhai wake ama matumizi yake kabla ya kuhitaji matengenezo ama kubomolewa kabisa.

Na hatujasikia muda maalumu uliowekwa kwa ajili ya kudumu au uhai wa majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ni muda gani hasa, lakini wananchi wa Dodoma na vitongoji vyake watakubaliana nami kuwa kwa mtazamo wa nje tulitegemea majengo hayo angalau yafikishe miaka 50 kama si 100.
Kwa wageni ambao hawajafika Dodoma inapendeza waamini kuwa hakuna mahali palipojengwa vizuri na kwa ustaarabu kama ilivyo kwa UDOM. Ama hakika kizuri hakikosi kasoro!

Inawezekana yaliyokuwa yamefichwa ndani ya chuo hicho yana maana kwa watu wengine, lakini kwa upande wa pili yalikuwa na hasara pia ndio maana watawala wa eneo hilo walikuwa wakitumia muda wao mwingi kwa ajili ya kukanusha.Ukweli wa mambo ulithibitika Aprili 9 mwaka huu pale mawaziri wawili na naibu mawaziri walipotembelea chuo hicho kikubwa kuliko vyote katika Ukanda wa Afrika Mashariki kilichopo eneo la Chimwaga, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Awali, viongozi wa chuo chini ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula walikuwa wakipinga maneno yaliyokuwa yamezagaa mitaani kuwa majengo ya UDOM ni mabovu na yamejengwa kwa kulipuliwa.

Prof. Kikula huenda kwa kutokujua ama kuziba pamba masikio ili kusafisha kikombe kwa nje, alilazimika kutumia maneno ya ukali wakati mwingine kwa watu waliojaribu kukosoa jambo lolote lililohusu chuo kile na hakuwahi kuwa rafiki na mtu wa aina hiyo.
Siku hiyo mambo yalikuwa hadharani na msomi huyo (Prof Kikula), safari hii alishindwa kupinga mbele ya wakuu wake akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya aliyeibua uozo huo.

Hapa sasa ni mahali pa kujiuliza, je, huu ni wakati gani ndani ya UDOM? Bila shaka huu ni wakati wa kuamini kuwa kumbe ni rahisi kwa Watanzania kudanganywa na kuendelea kuamini uongo huo kwa ajili tu ya kuwabeba baadhi ya watu.
Mambo mawili yalijitokeza katika ziara hiyo, kwanza ni ubovu wa majengo ambayo yamefikisha umri wa miaka mitatu tu tangu yajengwe, lakini yanavuja na pili ni fedha zaidi ya Sh 800 bilioni zilizotumika kukijenga chuo hicho kutumika bila ya kuwa na mkataba.

“Sipati picha hapa, nimekuwa nasikia, lakini leo nimejionea mwenyewe kwamba majengo hapa UDOM yanavuja kama si ubadhirifu ni nini? Yaani, jengo limejengwa miaka miwili au mitatu iliyopita, lakini linavuja hivi usimamizi ukoje hapa,” alifoka Prof Mwandosya.
Mbali na kauli ya ukali aliyoitoa katika kikao cha uongozi kilichodumu hadi saa moja usiku, profesa huyo alimtaka profesa mwenzake kueleza ni hatua zipi zimechukuliwa kwa watu walijenga majengo hayo ikiwa ni pamoja na kusimamisha malipo yao.
Mbali na hiyo, Prof Mwandosya alihoji pia ni njia zipi zinatumika kunusu majengo hayo ambayo yameigharimu Serikali ya Tanzania mabilioni ya Shilingi tena zikiwa ni fedha za ndani.

Tofauti na siku zote, safari hii, Prof Kikula hakuuma maneno na badala yake akasema kuwa uongozi wa UDOM umekuwa ukitumia muda wa wanachuo kuwa nje ya chuo (likizo) kwa ajili ya kufanya ukarabati mdogomdogo jambo lililoonyesha kuwa hata uongozi unalijua suala la kuvuja kwa majengo hayo.
Kwa maneno mengine, kunafanyika ukarabati tu lakini ujenzi ulishapita na hatujui ukatarabati huo ni wa kiwangogani, lakini pia msomi huyo alishindwa kueleza hatua stahiki zinazochukuwa ama zilizochukuliwa kwa watu waliojenga majengo mabovu. Hapa kuna jambo.
Hii ni wazi kuwa kipande cha kiraka ndani ya nguo mpya hakiwezi kuongeza sifa au ubora wa nguo hiyo na badala yake kinaharibu kabisa ubora wa nguo husika na kuiondolea heshima, lakini pia genge haliwezi kuzidi sifa ya soko.
Hapa tukubali kuwa ndani ya miaka mitatu tayari majengo yake yameshawekewa vilaka, je tutakapofika miaka 50 kama ilivyo kwa majengo mengine ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hali itakuwaje?
Watu wanajiuliza kama UDSM kilichoanzishwa Julai Mosi 1961 kama kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha London bado majengo yake hadi leo hii yanakuwa na mvuto na ni imara sijui kuna kidudu mtu gani kilichovamia UDOM na hatujaambiwa chuo hiki kinatazamiwa kudumu kwa muda gani au ni cha mpito tu.

Lakini, pia kuna jambo la kuhoji ama ni ndani ya uongozi wa UDOM au Serikalini kwamba mifuko inayotoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho hadi leo bado hakuna mikataba maalumu waliyowekeana na menejimenti ya chuo?
Na hilo lilithibitishwa na wawakilishi wa mifuko hiyo mbele ya Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa ambao walisema kuwa licha ya kutakiwa kuendelea na ujenzi bila ya kusimama lakini wanajenga bila ya kuwa na mikataba jambo linalotishia upotevu wa mabilioni hayo ya wavuja jasho.
Uthibitisho huo pia ulitolewa na Profesa Shaaban Mlacha ambaye anasimamia kitengo cha fedha chuoni hapo aliyekiri ujenzi huo kuendelea bila ya kuwa na mikataba na mifuko inayotoa fedha hizo katika kipindi chote.

Kwa maneno ya Mlacha, wamekuwa wakikwamishwa na Hazina (Wizara ya Fedha) kila walipojaribu kusaini mikataba hiyo, lakini cha ajabu hakuna mahali paliposemekana kuwa palikwamisha utoaji wa fedha hili nalo ni jambo la kujiuliza juu ya uhalali wa uchukuaji wa fedha hizo na namna ya kuzirudisha.
Bila shaka kupitia machache haya ambayo yalianikwa hadharani mbele ya vyombo vya habari, yatakuwa ni ushahidi tosha kwamba ndani ya utawala wa chuo hicho kuna mengi ambayo yamejificha na ambayo yakimulikwa kwa kurunzi yanaweza kustia wengi.

Haiwezekani kwa kiongozi makini kuruhusu malipo ya mabilioni ya fedha kwa kampuni ambazo zinajenga majengo yanayothibitishwa kuwa ni mabovu ilihali majengo hayo yanapaswa kutumiwa na vizazi vijavyo hivi hii kama si dhambi tunaweza kuitaje.
Kuna nini ndani ya chuo hicho ambako pia kumekuwa na migogoro ya kila siku, maandamano yasiyokwisha pamoja na migogoro ya ndani ya uongozi mbali na malalamiko ya kudhurumiwa fedha kwa wafanyakazi.

Tunaambiwa Shilingi bilioni 800 zimetumika katika ujenzi wa UDOM pamoja na miundombinu yote na ni jambo la kujivunia kuwa fedha hizo zote zimetoka katika mifuko ya Watanzania wenyewe ikiwamo PPF,NSSF na mifuko mingine, lakini kwa nini tuweze kutafuta fedha. Kwanini tushindwe kusimamia kwa ubora kile tunachokiumba?

Kwa sasa chuo hicho kinasifika kwa kuwafanya polisi waone kuwa ni uwanja wao wa mazoezi kwa mabomu ya machozi pamoja na namna ya kurusha virungu ingawa sasa ndani ya chuo hicho kumeibuka tabia ya fukuza fukuza. Ipo haja ya kulitazama suala hilo kwa makini yawezekana kuna chanzo au mzizi ambao bila ya kung’olewa kila kitu kitakuwa cha kulaumiana.
UDOM kimejitangaza kwa kutumia fedha nyingi ikwamo katika majukwaa ya wanasiasa hasa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, umefika wakati sasa kikatafutiwa tiba mbadala ili kiweze kuendana na sifa yenyewe kiliyopewa vingine sifa zimezidi ubora halisi uliopo pale.



Chanzo:
Ubovu wa majengo Chuo Kikuu Dodoma; tatizo linalohitaji kumulikwa haraka
 
Inadhihirisha kuwa kila penye mkono wa ccm uchakachuaji na ufisadi vipo nyuma yake kama mamba na kenge TZ ndo changamoto kubwa tuliyobakinayo
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom