Jumakidogo
R I P
- Jul 16, 2009
- 1,851
- 417
Nimekuwa nikifuatilia kwa makini sana maoni ya wadau mbalimbali kuhusu ubora wa filamu zetu za kibongo. Wengi wamekuwa wakitoa changamoto badala ya kupongeza kazi za sanaa hiyo ya filamu kwa sababu ya kuchoshwa na kile ambacho kinaandaliwa na waigizaji hao hasa kwa upande wa hadithi za filamu hizo. Kwa bahati nzuri mimi ni mwandishi wa riwaya na simulizi za kusisimua hapa nchini. Binafsi nimekuwa nikifuatilia hadithi za filamu mbali mbali na kugundua kuwa waigizaji wetu wametawaliwa na tamaa ya kutaka sifa pamoja na ubinafsi wa kutaka kuonekana kuwa kila kitu kimefanywa na yeye. Matokeo kinachofanyika hakitokani na hadithi bali ubabaishaji wa maneno na mionekano yao ya kutaka kujiweka katika hali ya juu kwa kila filamu wanazoigiza. Ifahamike kuwa, msingi mkubwa wa filamu nzuri ni hadithi, hadithi ndiyo inayompa muigizaji muongozo wa nini kinachotakiwa katika muonekano wa filamu hiyo. Utunzi wa hadithi ni kipaji maalumu. Si kweli kwa sababu mtu anao uwezo mkubwa na kipaji cha kuigiza basi ajipe na kipaji cha utunzi wa hadithi. Hadithi ni kitu kingine na, uigizaji nao ni kitu kingine. Matokeo yake ndio haya, kila pembe ya nchi kumekuwa na malalamiko ya mashabiki wa filamu kuwa wanachoshwa na aina ya filamu zinazochezwa bongo. Napenda nikili tu kwamba, kwa sasa waandishi na watunzi wa hadithi hapa nchini wamebaki wachache sana. Lakini hilo lisiwe kikwazo kwa sababu waliopo wanafahamika na, kazi zao nzuri zinaonekana. Ikiwa ni lazima mwigizaji aonekane yeye ndiye mtunzi, ni kazi rahisi. Kwani si lazima mtunzi ajulikane, zungumza na mwandishi wa hadithi kisha mwisho wa kazi bandika jina lako. nani atajua? kuliko kuwalisha watu makapi. Nikiwa kama mwandishi na mtunzi wa riwaya hapa nchini, nawapa fursa waigizaji. Msiogope, leteni aidia zenu za kile mnachotaka kufanya. Si kazi kwa mtunzi mwenye kipaji kuandika hadithi za filamu. Acheni ukiritimba, sisi sote ni wasanii wenye jukumu la kuendeleza sanaa hapa nchini.