Ubora wa Maudhui: JamiiForums yaongoza kwa maoni yanayokosoa Serikali na kujumuisha mitazamo mbalimbali

Ubora wa Maudhui: JamiiForums yaongoza kwa maoni yanayokosoa Serikali na kujumuisha mitazamo mbalimbali

UBORA WA MAUDHUI YA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA 2018
UTANGULIZI
Wanataaluma wa tasnia ya habari, wanahabari, na jamii kwa ujumla wana matarajio sawa kuhusu ubora wa vyombo vya habari. Matarajio haya yanajumuisha kuandika/kurusha habari zenye maslahi kwa jamii, kuzingatia ukweli, kutoa habari sio tu za matukio ya kila siku, bali kwenda mbali zaidi na kuchambua masuala mbalimbali. Uandishi wa namna hii utaweza kujenga ajenda za kisiasa, utazalisha majukwaa ya midajala na kuhamasisha mitazamo mbalimbali, na kuwawajibisha walio na mamlaka.

Utafiti huu unaangazia ubora wa vyombo vya habari kwa kutumia vigezo maalumu vya ubora wa habari. Utafiti huu umefaidika sana na utafiti wa awali wa mwaka 2017 na umeongeza idadi ya vyombo vya habari kutoka 12 kwa mwaka 2017 mpaka 25. Pia, umejumuisha vyombo vya habari kama redio za kijamii, redio za mikoani, blogu, mitandao, vyombo vya habari vya mitandaoni na vyombo vya habari kutoka Zanzibar.

Mazingira ya Kibiashara
Mazingira ya kibiashara yametawaliwa na kushuka kwa mapato yatokanayo na matangazo kwa redio, magazeti na televisheni, watangazaji kuhamishia matangazo yao kwenye vyombo vya habari vya mtandaoni, na kuhama kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji kutoka vyombo vya habari vya jadi kwenda vyombo vya habari vya mtandaoni. Kushuka kwa matangazo kwa sehemu fulani kumechangiwa na maamuzi ya Serikali kupunguza bajeti yake ya matangazo ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza matumizi. Kabla ya uamuzi huu, Serikali ilikuwa ndio mtangazaji mkuu kwenye vyombo vya habari nchini.

MBINU ZA UTAFITI
Moja ya mbinu za kitafiti za kupima namna vyombo vya habari vinavyoripoti habari zao, ni kwa kuchambua maudhui yanayotolewa (habari, makala, na vipindi) kwa kutumia vigezo vinavyofanana.

Utafiti huu umetumia vigezo maalumu vya kupima ubora wa maudhui ambavyo vilijadiliwa na kukubaliwa na wahariri na wadau wa sekta ya habari . Vigezo hivi vimekuwa vikitumika kupima ubora wa maudhui nchini . Vigezo hivi vimegawanyika katika maeneo manne kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini

Mwaka 2017, jumla ya vyombo vya habari 12 vilijumuishwa kwenye utafiti wa majaribio. Wakati wa kujadili matokeo ya awali ya mwaka 2017, ilipendekezwa kwamba utafiti wa mwaka 2018 ujumuishe vyombo vya habari vingine kutoka Tanzania Bara na Zanziabar, na hususani redio za mikoani. Baada ya majadiliano na wadau mbalimbali, jumla ya vyombo vya habari 25 vilijumuishwa kwenye utafiti huu

MATOKEO YA UTAFITI
Sampuli ya utafiti huu umejumuisha habari, makala, vipindi na posti 1,886 kutoka magazeti 7, redio 12, televisheni 4, blogu 1, na mtandao 1. Uwasilishaji wa matokeo unatenganisha redio za mikoani na redio za kitaifa kutokana na tofauti zao.

1. Mada zilizoripotiwa na vyombo vya habari
Masuala yanayoangaziwa na vyombo vya habari ni pamoja na uchumi(29%) hii ikijumuisha miundombinu, mafuta na gesi, usafirishaji, biashara; masuala na maendeleo(28%) ikiwemo afya, elimu, kilimo na mazingira. Masuala yenye mvutano kama matatizo ya kijamii, migogoro, haki za binadamu, masuala ya jinsia, utawala bora nakadhalika yamechukuwa asilimia 16.

Ajali na uhalifu/kesi za mahakamani zimeripotiwa kwa asilimia 12. Kuripotiwa kwa masuala ya kisiasa kuko chini (11%), hii ikijumuisha maudhui ya sera, uchaguzi, usalama wa taifa, na majadiliano ya kisiasa. Masuala ya utamaduni, vyombo vya habari na tafiti vimeguswa kwa kiasi kidogo

Hata hivyo, kila kundi la vyombo vya habari lina namna lilivyoangazia mada hizi kama inavyoonekana kwenye chati hapa chini.
Jedwali hapo juu linaonesha kuwa Magazeti yanaongoza kuripoti masuala ya kisiasa, lakini yako katikati (wastani) katika kuripoti masuala ya kiuchumi, maendeleo, na ajali/uhalifu. Redio za kitaifa zinaripoti habari za maendeleo zaidi, na kwa uchache habari za kisiasa. Redio za mikoani zinaongoza kuripoti habari zenye utata pamoja na (JamiiForums) na zile za maendeleo, ikifuatiwa na habari za kisiasa. Zinatoa nafasi kidogo kwa habari za uchumi na ajali/uhalifu.

Televisheni zinaongoza kuripoti habari za kiuchumi na ajali/uhalifu, huku zikitoa nafasi kidogo kwa habari za maendeleo na kisiasa. Michuzi blog ina idadi kubwa ya habari zenye maudhui ya ajali/uhalifu, na maendeleo na uchumi, lakini idadi ndogo sana ya habari za kisiasa na zenye utata. JamiiForums inaongoza kutoa taarifa za kisiasa (kama magazeti), na idadi kubwa ya habari zenye utata (kama redio za mikoani).

2. Habari za kitaifa na za mikoani
Redio za mikoani zinaripoti zaidi habari za mikoani (71%, ukilinganisha na wastani wa 60%). Michuzi Blog ina habari nyingi zaidi zenye taswira ya mikoani, wakati JamiiForums imejikita kwenye masuala yenye taswira ya kitaifa.


3. Sababu za kuripotiwa kwa habari
Matokeo yanaonyesha kwamba magazeti yanaweka sababu za kuripotiwa kwa habari fulani (ikipimwa kwa kuwa na paragrafu mbili au zaidi ambazo zinatoa maelezo ya sababu husika) kwa 37%, wakati redio za kitaifa zinafanya hivyo kwa 15%.

Idadi kubwa ya habari zisizokuwa na sababu ya kuripotiwa kwa habari husika ni za redio za kitaifa na Michuzi Blog. Mlengo wa JamiiForums ni wa kujenga mijadala na kubadilishana mitazamo, na sio sana katika kuchimba na kupata sababu za kwanini jambo fulani limetokea. Hii inaonekana kuwa ni wajibu wa magazeti au TV.


4. Ujumuishaji wa mitazamo mbalimbali kwenye habari
Uwepo wa mitazamo mbalimbali kwenye habari/kipindi ni njia nzuri ya kuwajuza wananchi. Inatoa fursa ya kuonyesha kwamba watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti na hivyo kuifanya habari iwe kamili na yenye mizania. Mada zinapaswa kuripotiwa kwa kutumia lensi tofauti, ambayo inaongeza ukamilifu wa habari.

Magazeti yanaongoza kwa kuripoti habari kwa kutumia angalau lensi mbili kwa 24% ya habari zote, yakifuatiwa na redio za mikoani(12%), redio za kitaifa (10%), na TV (10%). Kwenye Michuzi blog na JamiiForums, hali sio nzuri kwani kuna mtazamo zaidi ya mmoja kwa asilimia 1 na 3, mutawalia.


4.1 Ujumuishaji wa maoni kwenye habari
Chati namba 9 inaonyesha kwamba magazeti (32%) na JamiiForums (38%) ndio yanajumuisha maoni mbalimbali kwenye habari/taarifa zao, yakifuatiwa na redio za mikoani (29%). Redio za kitaifa zinafanya hivyo kwa 17%. Michuzi Blog inafanya hivyo kwa 1%.

4.2 Ujumuishaji wa maoni kinzani kwenye habari
Kuweka mizania katika habari ni msingi mkuu wa uandishi wa habari kwa kuhakikisha kwamba maoni kinzani yanapewa nafasi. Hili linaonekana kufanywa zaidi na JamiiForums na sio vyombo vya habari.

5. Habari zenye kukosoa Serikali
Ni nadra kwa vyombo vya habari kutoa habari zenye kuikosoa Serikali. Ni JamiiForums pekee ambayo ina maudhui yenye mlengo huo kwa 35%, ikifuatiwa na redio za mikoani na magazeti ambazo zina 4% kila moja. Tayari mwaka 2017 wahariri walishabainisha kwamba vyanzo vya habari vyenye mawazo kinzani na serikali haviko tayari kuzungumza hadharani.

6. Muundo wa habari
Muundo mzuri wa habari unamwongoza msomaji au msikilizaji kuanzia mwanzo hadi mwisho wa habari husika. Redio za kitaifa ziko chini kidogo ya wastani (56% ya muundo mzuri wa uandishi), ikiwakilishwa na magazeti na redio za mikoani. Vituo vya televisheni na JamiiForums vinafanya vizuri, ingawa tofauti sio kubwa kama inavyoonekana kwenye chati namba 11.


Imeandaliwa na
Baraza la Habari Tanzania likishirikiana na Spurk Media Consulting Ltd., Bern, Switzerland

Watafiti
Christoph Spurk, Bern, Switzerland,
Abdallah Katunzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania
Nakubaliana na uchambuzi uliofanyika. Papo hapo kuna uwezekano wa JF kufanya vizuri zaidi kama tutaondokana na uchangiaji usio na maana kwa kudhani kufanya hivyo ni kuikosoa serikali. Pamoja na kwamba mtu una uhuru wa kusema upendavyo, fanya hivyo kibusara, kwa heshima, bila matusi, ukijikita kwenye hoja inayozungumziwa na kutoa pendekezo mbadala la hoja yako. Baadhi ya Wana-JF wanaishia kumdhihaki Rais kwa kila kitu kinachoonekana vibaya, au kuikejeli serikali kwa ujumla. Kwa mfano polisi wa trafiki amenaswa akipokea hongo. Mchangiaji anasema "Hiyo ndiyo serikali ya CCM". Mtu mwingine anaanzisha uzi kuzungumzia umeme wa Stieglers Gorge. Mwingine anachangia kwa kuuliza "Vipi zile korosho za Mtwara?" Mwingine anaanzisha uzi kuhusu reli ya 'Standard gauge'. Mchangiaji mwingine anakuja na swali 'tuelezeni zile trilioni 2.4 ziko wapi?'. Hizi ndiyo dosari ninazoziona kwenye jukwaa hili ambazo tukiziondoa hadhi ya JF itapanda sana. Hususan Rais Magufuli amekuwa mtu wa kutukanwa tu kila kukicha kama vile hakuna jema alilotenda. Huku ni kukosa adabu. Hata baba yako akifanya kitu ambacho unaona siyo sahihi hutoki na kuanza kumzomea kwa majirani zako. Badala yake tafuta namna ya kumuelimisha kuhusu kosa alilofanya ndani nyumbani mwenu au kwa kuwaita ndugu wengine, hasa wa rika lake, n.k. Hivi sivyo inavyofanyika kwa Rais Magufuli na serikali yake. Sikatazi kumkosoa Rais au serikali yake. Lakini tufanye hivyo kwa adabu na kupendekeza kitu mbadala.
 
Mungu ibariki Jf na member wote walioko humu,waelimishao watu na wasema ukweli na wabishi pia maana nao wapo kwa kutupa changamoto, Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki waliokaa na kubuni chombo kizuri kama hiki ila wanafiki msiokipenda mfe mapema kabla chombo hiki na imani yangu kitadumu milele na milele AMEEN!
 
Rais Magufuli amekuwa mtu wa kutukanwa tu kila kukicha kama vile hakuna jema alilotenda. Huku ni kukosa adabu. Hata baba yako akifanya kitu ambacho unaona siyo sahihi hutoki na kuanza kumzomea kwa majirani zako. Badala yake tafuta namna ya kumuelimisha kuhusu kosa alilofanya ndani nyumbani mwenu au kwa kuwaita ndugu wengine, hasa wa rika lake, n.k. Hivi sivyo inavyofanyika kwa Rais Magufuli na serikali yake. Sikatazi kumkosoa Rais au serikali yake. Lakini tufanye hivyo kwa adabu na kupendekeza kitu mbadala.
Naunga mkono hoja, hili hata mimi nilishauri
Wito Kwa wana JamiiForums kuhusu ukosoaji wa Rais Magufuli - JamiiForums
P.
 
Hongereni sana wamiliki wa JF, Maxence Mello na Mike Mushi, kwa kuhimili mikikimikiki yote iliyowakabili kwa kuwa na mtandao bora kabisa na mtandao pendwa kuliko wowote nchini Tanzania!

Kumbukeni usemi wa hekima unaosea mti wenye matunda mazuri, hauishi "kupopolewa" mawe kila kukicha!

Lakini vile vile tusijisahau kujipigia makofi wachangiaji wote humu JF, bila kujali itikadi zeru za kisiasa......

Unajua humu JF wachangiaji wake naweza wafananisha na watani wa jadi wa Simba na Yanga.....

Na humu JF kadhalika kuna timu mbili zinazotoana jasho kwelikweli nazo ni za wale wa Kambi ya Lumumba VS Ufipa

Uzuri humu JF TUNAPINGANA bila KUPIGANA!
 
Sijutii kuwepo humu mjengoni, saa hizi saa nane usiku sijalala nipo Jamii forum najifunza mengi na nimejifunza mengi sana humu.

Mungu ibariki JAMII FORUM, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
 
NAWAKARIBISHA MPATE MURO KAMIRI JAMANI MSIONEANE HAYA ILA MJE NA MICHANGO
 
Back
Top Bottom