SoC01 Ubepari ulivyochangia kushuka kwa malezi na anguko la uwajibikaji. Nini suluhisho?

Stories of Change - 2021 Competition

Ushirombomoya

Member
May 11, 2021
61
101
Habari! wanajukwaa, nimekuwa msomaji wa bandiko mbalimbali za wanajukwaa hili kwa kipindi kirefu hata kabla sijajiunga rasmi humu bandiko hizo zimeniongezea maarifa na kunihabarisha kwa kiasi kikubwa. Leo nami napenda nitoe mchango wangu kuhusu uhusiano kati ya ubepari na athari zake kwenye mfumo mzima wa malezi na kuanguka kwa uwajibikaji nchini. Lakini kabla sijaendelea zaidi naona ni vyema nikaelezea kidogo maana ya maneno ubepari, malezi na uwajibikaji ambayo ndiyo yamebeba dhima kubwa ya andiko langu hili.

Ubepari ni mfumo wa kiuchumi ambao utoa fursa kwa watu binafsi kutawala vyanzo vya uzalishaji mali kwa kiwango kikubwa, katika mfumo huu serikali uwapa fursa wawekezaji au watu binafsi kuzalisha mali au kufanya biashara, jukumu kubwa la serikali ni kuhakikisha kuwa watu au wawekezaji wanalipa kodi stahiki na kufuata matakwa ya sheria kila wazalishapo au wafanyapo biashara.

Malezi ni hatua au maandalizi ambayo familia au jamii kwa ujumla uchukua au kufanya ili kumkuza mtoto vyema ili baadae aweze kuwa na mchango chanya katika jamii, malezi uhusisha mambo mengi mfano elimu, maonyo na mafundisho mbalimbali kutegemea na mahitaji ya jamii husika. Dhana ya malezi mema imeongelewa na kutiliwa mkazo katika vitabu mbalimbali ila kwa kuwa jamii yetu ya watanzania imegawanyika katika imani kuu mbili yaani Ukristo na Uislamu, nitatumia vipengele vichache kutoka katika vitabu tukufu vya dini hizo mbili, lengo langu ni kuonyesha umuhimu wa malezi na sio vinginevyo.

Biblia takatifu imeelezea sana suala hili ila mimi napenda kutumia Mithali 22:6 "mlee mtoto katika njia impasayo naye hatoaicha hata atakapokuwa mzee" lakini Quran tukufu kupitia Surat Luqman inaelezea kuwa mzazi ana wajibu wa mzazi kumwonya mtoto juu ya adhabu amabazo atazipata endapo atakuwa na tabia mbaya. Japo nimeeleza kwa uchache lakini vitabu hivyo vimeeleza kwa kina juu ya umuhimu wa malezi mema.

Uwajibikaji ni" hali ya kiongozi au mtendaji wa jambo kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyofanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa"- Policy Forum( utawala bora), nchini Tanzania dhana ya uwajibikaji imetabanaishwa kupitia Ibara ya 8(1) ambayo inasisitiza kuwa mamlaka yote ya serikali yanatoka kwa wananchi.
Ibara hiyohiyo hususani kwenye kipengele (c) inasema serikali itawajibika kwa raia, kwa maana nyingine ni kwamba viongozi wote wa serikali bila kujali vyeo vyao wote kwa ujumla wanawajibika kwa wananchi ambao wamewapa mamlaka ya kuwatumikia. kiongozi ambaye anawajibika ufanya kazi kwa ufanisi na kwa maslahi mapana ya wananchi wake waliomchagua.

Tofauti ya Malezi kabla ya Ubepari na Baada ya Ubepari
katika kichwa cha uzi huu nimesema kuwa mfumo wa ubepari umechangia kushuka kwa malezi yanayotolewa kwa watoto katika jamii yetu hivyo mwishowe tumeshuhudia anguko kubwa sana la uwajibikaji nchini husasani kwa viongozi ambao wamepewa mamlaka ya kuwakilisha wengine na kufanya maamuzi kwa niaba yao.

Lakini naamini kuwa ninaweza nisieleweke vyema endapo nitaelezea athari ya ubepari dhidi ya malezi na hatimaye anguko la uwajibikaji endapo nitagusia mfumo huu wa ubepari bila kulinganisha na mfumo wa uzalishaji mali uliopita yaani ujamaa. siku zote hauwezi ukasema kitu hiki ni bora kuliko kile bila ya kukilinganisha kitu hicho na kitu kingine. Kwa mantiki hiyo basi hapa chini nitaelezea hali ya malezi katika vipindi tofauti.

Malezi kabla ya mfumo wa ubepari
Baada ya uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961 tunaona juhudi mbalimbali zilifanywa na serikali hili kuweza kujikwamua kiuchumi ambao uliathiriwa na ukoloni, mnamo mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzaa nchi inayoitwa Tanzania hadi sasa. Japokuwa katiba yetu iliyotungwa mwaka 1977 inatutambulisha watanzania kama wajamaa hususani kupitia Ibara ya 9 lakini ni ukweli kuwa tumeshaachana na mfumio huo wa uchumi, lakini ningependa kuelezea hali ya malezi ya watoto katika kipindi cha ujamaa na kabla ya kipindi hicho.

kabla ya ujamaa na kipindi cha ujamaa jukumu la malezi lilikuwa linabebwa na jamii yote, nyakati hizo mtu mzima yoyote katika jamii aliweza kumwonya, kumfundisha na hata kumuadhibu mtoto yoyote yule aliyefanya jambo lisilofaa au lisilo la kiungwana. katika vipindi hivyo malezi mema kwa watoto yalitiliwa mkazo, yaani naweza kusema kuwa ule msemo wa samaki mkunje yu ngali mbichi ulitendewa kazi ile ipasavyo na jukumu la kufanya hivyo lilikuwa ni mikononi mwa wanajamii wote, malezi mema ya watoto yalijidhirisha katika mienendo na tabia njema zilizoonyeshwa na watoto wa kipindi hicho, pia viongozi wengi waliokuwa zao na mfumo huu walikuwa ni waadilifu na wawajibikaji.

Katika kipindi hicho viongozi waliwajibika kwa kuwashirikisha wananchi na pale walipofanya makosa waliomba radhi na kujirekebisha lakini wengine walienda mbali zaidi na kujing'atua katika nafasi zao ili kuwapa nafasi watu wengine walio na uwezo zaidi kuweza kuendelea pale walipoishia. Ubadhirifu wa mali za umma na matendo ya matumizi mabaya ya ofisi yalikuwa kwa nadra sana. Kwa kifupi naweza kusema ile hali ya juu ya malezi iliwatengeneza vijana kuwa viongozi wazuri na wenye kutimiza wajibu wao.

Malezi baada ya Ubepari
Kuanguka kwa mfumo wa uchumi wa kijana kulifungua mlango kwa mfumo huria yaani ubepari, katika mfumo huu nchi yetu imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa yameleta athari kwenye malezi ya watoto, katika mfumo huu ambao ndio tunao hadi sasa pesa au umiliki wa mali umetiliwa mkazo sana, wanajamii tumetawanyika na kupangaranyika, maisha sio kama ilivyokuwa zamani ambapo wanajamii tulikuwa na ushirikiano katika mambo kadha wa kadha ikiwemo malezi ya watoto na kuwafunza maadili mema.

Jukumu la malezi ya watoto limebaki kuwa la wazazi wenyewe, ambao nao katika mfumo huu imekuwa nadra sana kutimiza jukumu hilo maana utumia muda mwingi kutafuta fedha, hivyo hivi sasa jukumu la malezi wameaachiwa watu wanaofanya kazi hiyo wa ajira kama vile wajakazi wa ndani na vituo vya kulelea watoto" day care" ambavyo hivi sasa vimejaa kila pande ya nchi hii.

Hivyo kwa kuwa wazazi wanakimbizana mbio na fedha na kuwaachia jukumu la malezi watu wengine, imekuwa vigumu kwa wao kugundua mienendo mibovu ya watoto wao kabla hali haijawa mbaya, lakini kwa kuwa watu waliopewa jukumu la malezi ya watoto utekeleza jukumu hilo kwa sababu ya ujira tu ambao nao ni kiduchu ukilinganisha na jukumu wanalofanya, mara nyingi watu hao wamekuwa hawatekelezi jukumu hilo sawa. Kipindi ambacho wazazi wanatambua tabia mbovu ya mtoto wao wanakuwa wamechelewa na kutatua tatizo hilo linakuwa vigumu kama ule msemo wa wahenga kuwa Mbwa mzee hafunzwi mbinu mpya, na ukijaribu kufanya hivyo hakika hatoelewa. hivyo wazazi wengine wamejikuta wakishindwa la kufanya tena zaidi ya kuomba kudra za Mungu.

Tabia zilizojitokeza kipindi cha Ubepari na athari zake katika uwajibikaji
kama nilivyoeleza hapo juu kwa mfumo huu wa uzalishaji mali unawanyima wazazi fursa ya kuwalea watoto wao na wanajamii wengine kwa ujumla wamekuwa wakikwepa jukumu hilo kwani nao wana matatizo mengine mengi, mfumo huu umetufanya watu kuwa watumwa wa fedha hivyo tumekuwa tukitumia muda mwingi kutafuta fedha na kusahau au kushindwa kabisa kupata muda wa kukaa na watoto wetu na kuwafunza tabia njema, pia kuangalia mienendo ya yao na kukemea zile tabia mbaya na zilizo kinyume na maadili, kwa sababu hiyo watoto kwa kiasi kikubwa sana wamekuwa na maadili mabovu.

Lakini naamini kuwa utakubaliana na mimi kwamba mtoto ambaye amekuwa katika mazingira yasiyo na malezi mema pindi akuapo na kupewa mamlaka mtoto huyo hawezi kuwa wajibikaji kamwe, hivyi karibuni tumeshuhudia tabia mbalimbali ambazo zimeletwa na mfumo huu wa ubepari na pia kuathiri hali ya uwajibikaji. Tabia hizo ni:

1. Ubinafsi
Ubinafsi hili hali ya kufanya jambo pasipo kujali maslahi ya wengine, kipindi hiki cha Ubepari tumeshuhudia ubinafsi wa hali ya juu watu hawajali mahitaji ya watu wengine kabisa kila mmoja yupo mbio mbio kujilimbkizia mali kwa njia ya halai au isiyo ya halali. Jamii sasa hivi inathamini kitu na sio utu, mwnenye pesa ndiye anayesifiwa na kuonekana kuwa bora zaidi ya wengine.

Watu ambao wengine ni viongozi wetu tukumbuke kuwa wamelelewa katika mfumo huu, wao nao pia wapo mstari wa mbele kujilimbikizia mali na hawana aibu tena kuonyesha ukwasi wao hadharani na mbaya zaidi hawawajibiki kabisa kwa wananchi ambao ndio wamewapa mamlaka ya kuwakilisha, viongozi ambao wengi wao malezi yao yaliathiriwa na mfumo huu, baada ya kuwakilisha wananchi na kuwapa matumaini wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuwapoka wananchi hata kile kidogo walichobaki nacho.
Kipindi hiki tumeshuhudia viongozi wakija na sheria kandamizi zenye kuleta maumivu yasiyostahimilika. Wananchi wanaumia na kupiga mayowe lakini watafanya nini mbele ya viongozi wasio na maadili na wasiowajibika?

2. Kushuka kwa maadili
Changamoto ya malezi katika kipindi imesababisha kwa kiwango kikubwa kushuka kwa maadili, hii ni kwa sababu malezi yasiyo sahihi hayawezi kujenga jamii yenye maadili tumeona hapo juu kwamba wazazi wengi katika mfumo huu wamejikita katika kusaka fedha na kupuuzi suala la malezi bora kwa sababu hiyo maadili ndani ya jamii yameshuka kwa kiasi kikubwa, kushuka huko hakuishii tu kw wananchi na jamii bali kunaenda hadi kwa viongozi ambao ndio wamepewa dhamana ya kuwakilisha mahitaji ya wananchi wao, katika kipindi hiki haishangazi tena kusikia kuwa kiongozi fulani amefanya ubadhirifu mkubwa.

Tupo kwenye mfumo ambao viongozi wabadhirifu wanaonekana mashujaa na wale ambao hawana kitu lakini wanaitumikia au wameitumikia serikali kwa uaminifu uonekana ni wazembe na waliojisahau, inasikitisha kweli maana na vijana ambao hawapo kwenye madaraka kwa sasa wanafikiri ni lini wakati wao utafika ili nao wakwapue kama walivyofanya waliotangulia, uwajibikaji kwao sasa ni neno lisilo na mashiko tena na hata wakilisema wanakuwa hawamaanishi hivyo.

3. Matendo ya Ukatili
Pukurushani za kutafuta fedha katika mfumo wa ubepari sio kwamba tu zimefanya wazazi kushindwa kuwapa watoto malezi sahihi lakini zinasababisha msongo wa mawazo ambao pia ufanya mawasiliano baina ya wazazi ya mke na mme kuwa ya nadra na mara nyingine ugomvi kutokea baina yao, katika hali kama hii wanaothiriwa sana ni watoto maana upata matatizo ya kisaikolojia na pindi wanapokuwa na pengine kushika madaraka makubwa wengi wao uwa wakatili na uwatendea watu vitendo visivyofaa na ambavyo si vya kiungwana.
UKATILI.jpeg

Picha kutoka mtandaoni: Pichani mtoto anaonekana akiathiriwa na migogoro ya wazazi.

Kiongozi alikiyekua na kulelema katika mazingira ya ukatili mara nyingi hawezi kuwa mwajibikaji hata kidogo. Naamini wengi tumesikia unyama mbalimbali ambao umekuwa ukifanywa na viongozi au watu waliopewa madaraka ya kuwaongoza wengine, pia mara nyingi viongozi hao uwa hawajutii kile walichokifanya.

Nini kifanyike kutunasua katika hali hii?
Nakubali kuwa suala la malezi hasa katika kipindi linagubikwa na changamoto nyingi maana tunaishi kwenye kipindi ambacho vitu vinathaminiwa kuliko utu, kipindi ambacho jamii imekuwa ikilalamikia tabia mbovu lakini jamii hiyo hiyo haipo tayari kujitoa katika kuwalea na kuwakuza watoto ili wawe viongozi wazuri na wajibikaji. Jamii imekuwa ikiimba wimbo wa uzalendo lakini yenyewe imeshindwa kuonyesha kwa vitendo.

Licha ya changamoto hizo binafsi naamini kuteleza sio kuanguka na hata ukianguka haina maana utabaki hapo hapo chini, swala la msingi la kujiuliza mbona mataifa mengine yanatumia mfumo huu lakini yana uwajibikaji wa hali ya juu unaonyeshwa na viongozi wao, je sisi tunashindwa nini na kwa nini!

Binafsi naona ni muhimu kwa wazazi licha ya majukumu waliyonayo inabidi watenge muda wa kufuatilia mienendo ya watot wao na suala ma malezi wasiwaachie wajakazi tu maana wao ni watu wa ajira ni ngumu wao kuvaa viatu vy a mzazi, siwadharau wajakazi lakini licha ya huduma zao muhimu nina uhakika wao pekee hawawezi, hivi sasa kumekuwa na tabia ya watu wenye kipato kuwadekeza watoto wao wakidai eti wanawalea kizungu, bila kujali kuna utofauti mkubwa wa kiutamaduni kati ya jamii mbili hizo yaani jamii yetu na jamii za mataifa mengine.

Pia naaamini jamii nzima ikitimiza majukumu yake na kulibeba jukumu la malezi kwa pamoja kama ilivyokuwa wazamani ambapo kila mwanajamii alimwona mtoto wa mwenzie kama wake, kinyume na siku hizi ambapo mtoto wa mwenzio na mkubwa mwenzio. Ninawakilisha na ninawakaribisha kutoa michango yenu maana maneno yangu sio msaafu nilipokosea mnaweza kunikosoa.

Aksanteni.
 
Nilikuwa sijui...kumbe Tanzania ilipopata uhuru ilifuata mfumo wa kibepari! Ngoja nifanye utafiti kwanza.
 
Nilikuwa sijui...kumbe Tanzania ilipopata uhuru ilifuata mfumo wa kibepari! Ngoja nifanye utafiti k

Nilikuwa sijui...kumbe Tanzania ilipopata uhuru ilifuata mfumo wa kibepari! Ngoja nifanye utafiti kwanza.
Nimesikitika kuona kuwa umetoa mchango wako bila kusoma vizuri, ila siwezi kutoa lawama hili utokea mara nyingi kwa watu wengi, kwenye uzi wangu nimeelezea bayana utofauti uliopo kati ya mfumo wa ubepari na mfumo uliopita yaani ujamaa, pia nimeeleza zaidi kuwa japo kuwa katiba hadi sasa inatutambua kuwa sisi ni wajamaa lakini ukweli ni kwamba mfumo huo wa uchumi haupo tena. katika uzi wangu nimeongelea ubepari kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ndio umebeba dhima kuu. Natumaini sasa utaweza kunielewa.
 
Back
Top Bottom