Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid amefunga maduka matatu ya rejareja na kusimamisha magari ya abiria kati ya Wete na Mtambwe kwa madai ya kutoa huduma kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa.
Wafanyabiashara waliofungiwa ni Said Juma Seif, Titi Juma Othman wa Mtambwe na Hamad Haji wa Mchangamdogo. Alisema wafanyabiashara hao wamelalamikiwa na wafuasi wa CCM, wakiwatuhumu kukataa kuwahudumia kutokana na itikadi zao za vyama.
Rashid alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kuwa wafanyabiashara hao wanawabagua wanaCCM.
"Tumelazimika kuyafungia maduka hayo matatu baada ya Serikali ya Wilaya kujiridhisha kwamba yanawabagua wanachama wa CCM," alisema.
Akizungumzia hatua hiyo, Haji aliitaka Serikali kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kuchukua hatua akisema hahusiki na masuala ya kisiasa. Alisema hizo ni chokochoko za wabaya wake.
*Usafiri wasitishwa*
Mkuu huyo wa wilaya, aliagiza kuzuiwa kwa magari yote ya kubeba abiria kwenye Barabara ya Wete-Mtambwe kwa madai hayohayo ya kuwabagua wanaCCM. Alisema mbali ya hatua hiyo, atawasiliana na wizara husika ili kuchukua hatua kwa wahusika kwa kukiuka leseni.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama zuio hilo alilosema ni la muda usiojulikana litayahusu magari ya Ruti B ambayo leo ndiyo yaliyotarajiwa kutoa huduma kwani yaliyozuiwa jana kwenda Mtambwe, nyumbani kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif ni ya Ruti A.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wete, Mmanga Juma Ali alisema katika utekelezaji wa agizo hilo hakutakuwa na huruma:
"Hatutaishia hapo wanaofanya ubaguzi huo watafikishwa mahakamani."
Hata hivyo, baadhi wa wahuduma wa vyombo vya usafiri walisema si wao wanaowashusha, bali ni wananchi na kwamba dereva na konda hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa lengo lao ni kutafuta faida.
Source: Mwwananchi