U wapi ewe tabibu?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,391
39,484
Na. M. M. Mwanakijiji

Laputopu nimeshika, na dodosa wa porini,
Sina budi kuandika, niliseme la rohoni,
Mwenzenu nafadhaika, namngoja wa ubani,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Najilaza kitandani, homa imenizidia,
Na maumivu mwilini, nyongani yameshikia,
Na sasa ni mashakani, ugonjwa umevamia,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Yalianza kunisibu, kwanza nilipokuona,
Ukawa mwanzo wa tabu, na sasa nataka pona,
Namtaka mahabubu, mganga wa kiaina,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Ukaniteka mateka, ulo teka moyo wangu,
Ukanitoa mashaka, kuuliza jina langu,
Mtima ukashituka, nikaapa uwe wangu,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Namkiri Subihana, yeye kakupendelea,
Umbile lako mwanana, kama chezo waelea,
Wenzako wakikuona, gele wanakuonea,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Ewe tabibu wa ndani, mganga uloumbika,
Wewe binti wa nyumbani, ni lini utajafika,
Wa tabasamu la shani, na umbo la malaika,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu.

Ahadi tukapeana, tarehe tuje kutana,
Tuzidi fahamiana, na kuzidi kujuana,
Na hata tulipoachana, na busu tukapeana,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Siku sasa zinapita, nakusibiri ufike,
Na homa nimeshapata, natetema niko pweke,
Nakaa najikunyata, nangoja giza litoke,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

Michuzi nimetamka, kalamu naweka chini,
Imenipanda mizuka, namuwaza wa ubani,
Betti nimeziandika, usizabane mtani,
U wapi ewe tabibu, fanya hima kunitibu!

M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
Mwanakijiji@klhnews.com
 
Tabibu mtoa jibu, asoweza kuharibu
Wa roho kupoza sibu, kama maji ya zabibu
Sikivu aso na zibu, chambicho bila ghilibu
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu


Tabibu angaza tele, sherehe isije shere
Kuzunguka tangu Bwire, mpaka pande za Ukwere
Patapo patika kile, chambua kama mchele
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Kuna wezi na wakwezi, laazizi na wapenzi
Wengine wapenda Mbezi, na kujimwaga mabenzi
Wana waso utetezi, watapiao malezi
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Mwenye kushikwa haoni, upofu huita chongo
Hatosikia maoni, hatohofu bwia dongo
Atakaa ubaoni, kucheza pasi ubongo
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Mzee nakuamini, kwa uturi na yamini
Hata kwa mdalasini, au kwa nzuri jibini
Misahafu yazo dini, tamthiliya makini
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Sema naye kwa kituo, hata kama kijapani
Usitake mkupuo, pole siyo hayawani
Bila hata mshituo, tamuweka kiganjani
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Omba unachokitaka, sichotaka kitazame
Usije kutapatapa, maridadi akazame
Kisha ukishakipata, acha wanga wakabane
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu

Kaditama nimefika,nane zangu hizi beti
Namtumia edita, gazetini aziseti
Mzee nimekuita, chini kukuweka keti
Sifa zote za muhibu?, makini sije aibu
 
Wa ubani nyonda wangu,nakusubiri kwa hamu
Unitibu donda langu, nipate kuwa muhamu
Sininyime haki yangu, kunipa penzi la hamu
Nitibie nyonda wangu, nakusubiri kwa hamu

Kitandani sibanduki, sijenifika madhila
Si mkuki si bunduki, maumivu ninakula
hata waje mamluki, sinyanyuki nimelala
Nitibie nyonda wangu, nakusubir kwa hamu
 
nimekubali vijana,kawajalia maulana,
namimi nimeyaona,usihofu utapona,
wakwangu alinuna,kimsalimia anaguna,
mimi bado sijapona,langu donda nimeshona.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom