Twaweza: 88% wana imani na elimu bure

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
UTAFITI uliofanywa na asasi ya Twaweza unaonesha kuwa asilimia 88 ya watu waliohojiwa, wana imani kubwa na Serikali katika utoaji wa elimu bure, lakini wameshauri mazingira ya utoaji wa elimu yaboreshwe zaidi.

Akiwasilisha utafiti uliowahusisha watu 1,894, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwenye utafiti huo asilimia 97 ya waliohojiwa wana ufahamu wa ahadi ya Rais John Magufuli ya kutoa elimu bure.

Matokeo ya utafiti huo yalifanywa na Shirika la Twaweza kati ya Desemba 10, 2015 na Januari 2, 2016 kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.

Profesa Mkumbo alisema Dar es Salaam jana kuwa wananchi hao wakijibu swali kama wana matumaini na ahadi ya elimu bure, walisema wana imani kubwa kuwa ahadi hiyo itatekelezwa.

“Asilimia 76 ya wananchi wanaamini kuwa utolewaji wa elimu bure utaongeza ubora wa elimu kwa kuboresha mazingira ya kufundishia, pamoja na wananchi wengi kuwa na mtazamo chanya, asilimia 15 wanaamini elimu ya bure haitaboresha elimu. Hii ni kutokana na ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi ambao utatumia rasilimali nyingi,” alieleza Profesa Mkumbo.

Profesa Mkumbo alisema asilimia 49 ya wananchi walisema wanafunzi hawatafanya vizuri kutokana na kukatazwa kwa masomo ya ziada ambayo walimu waliyatumia kuwasaidia wanafunzi wasiofanya vizuri huku wakijipatia kipato cha ziada na asilimia 22 wana hofu na upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya kufundishia.

Kuhusu michango shuleni, Profesa Mkumbo alisema wazazi wengi walikuwa wanaelemewa na michango kwani asilimia 89 ya wazazi walikiri kuchangia fedha kwenye shule za umma huku asilimia 80 wamechangia hadi Sh 50,000 wakati asilimia 8 wakichangia zaidi ya 100,000.

“Kwa mujibu wa wazazi, michango hutumika kulipia ulinzi (asilimia 66), mitihani ya majaribio asilimia 57, madawati asilimia tatu, huku kiwango kidogo kikielekezwa kwenye mahafali (asilimia nne) na safari za kishule asilimia nne. “Shule zinapaswa kuwa makini na kiwango cha fedha kinachopatikana, kwani vitu vingi ambavyo wazazi huchangia havijajumuishwa kwenye ruzuku,” alisema mhadhiri huyo.

Kuhusu ubora wa elimu, Profesa Mkumbo alisema asilimia 49 ya wananchi wanasema ubora wa elimu umeongezeka, lakini asilimia 36 wanasema elimu imezorota na asilimia 14 wanasema hakuna mabadiliko yoyote.

Alisema asilimia 37 ya wananchi wanaamini kuwa uhusiano wa karibu kati ya jitihada za mwalimu na matokeo ya darasa la saba, asilimia 93 wanaamini kuwa walimu ndio msingi wa maendeleo ya nchi.
 
Back
Top Bottom