SoC01 Tutumie ubunifu wa vijana kupunguza tatizo la ajira

Stories of Change - 2021 Competition
Jul 15, 2021
15
45
AJIRA kwa vijana inaendelea kuwa tatizo kubwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla. Kila kukicha idadi ya vijana inaendelea kukua na mahitaji ya namna bora ya kupata ajira yanazidi kupungua.

Ni imani yangu ya kuwa hakuna suluhisho la moja kwa moja la kutatua tatizo la ajira kwa vijana Tanzania ila ni vyema tukaanzia mahali na kupata suluhisho la kudumu hapo mbeleni.

Takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2014 zinaonyesha idadi ya vijana Tanzania kuwa asilimia 34.7 ambayo inazidi kuongezeka kila kukicha. Takwimu hizo zinaonyesha zaidi ya kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana Tanzania ni asilimia 13.7.

Kumekuwa na mbinu mbalimbali zinazotumika na serikali na mashirika binafsi ili kuhakikisha vijana wanapata fursa za kuajiriwa ama kujiajiri. Jitihada zote hizi ni kuahakikisha vijana wanapata fursa ya kutumia ujuzi wao kupata ajira ili kuboresha maisha yao na ya jamii nzima kwa ujumla.

Makala hii inapendekeza njia nyingine ambayo inaweza kuongeza fursa ya vijana kupunguza tatizo la ajira nchini na Afrika kwa ujumla.

Nipende kusisitiza ya kuwa, vijana wengi katika karne hii ya 21 wanatumia bongo zao kuja na ubunifu wa aina mbalimbali kwa nia ya kusaidia jamii zao na pia kujisaidia wenyewe. Mara nyingi changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na kukosa fursa ya kukua zaidi katika kuboresha ubunifu wao ili uendane na taratibu sahihi za nchi.

Ubunifu mwingi unaofanywa na vijana umekuwa ukipata msaada kidogo sana ama kutokupata kabisa na hivyo kuwakatisha vijana tamaa ya kuendelea kuwa wabunifu. Kuna mifano mingi, kwa miaka mingi tumeona vijana wakija na gunduzi zao za kutengeneza magari, helicopter, mitambo ya redio na nyingine nyingi. Ila vijana hawa hawajaweza kupata kipaumbele kikubwa na kuishia na vipaji vyao na kukata tamaa tu.

Upande mwingine wa ugunduzi ni kwa wale vijana watengeneza gongo. Ndio gongo, najua fika ni kinywaji haramu kutokana na taratibu za nchi. Ila ifike mahali tuangalie uharamu wake uko kwenye nini hasa, maana ukiangalia ni ugunduzi mkubwa unaofanywa na watengenezaji hawa japo ni kwa mitambo dhaifu ila wanaweza kutengeneza kilevi kama vile makampuni yaliyopewa kibali cha kufanya hivyo.

Yamkini, hapa ni kuboresha utengenezaji gongo huu na kuwa na viwango vinavyohitajika na mamlaka husika za serikali kama vile mitambo maalumu, sehemu maalumu, viwango vya kilevi vinavyokubalika, kuweka katika vifungashio maalumu, kuweka bei kikomo na kutumia bidhaa sahihi za utengenezaji. Nadhani haya yakifanyika itaifanya gongo kuwa kilevi sahihi kama vile tunavyoona vilevi vingine. Badala ya kupiga teke ubunifu huu na kuuita ubunifu haramu na kuwanyima fursa vijana wenye ujuzi huo ni bora kuufanya kuwa bora zaidi.

Tunapoongelea ubunifu ni muhimu kuelewa hutokana na uwezo wa watu husika katika kufanya jambo, unaweza kuchagizwa kwa kuwa na elimu rasmi ama bila elimu rasmi ila kwa kupitia ujuzi na mambo kama hayo.

Njia tunayoweza kupata na kutumia ubunifu wa vijana wetu wa kitanzania ni pamoja na kuwaweka katika makundi mbalimbali kutokana na uwezo wao na ujuzi wao kama vile vijana watakavyochagua.

Makundi haya yanaweza kuwekwa katika kambi maalumu ambazo zitawapa fursa vijana hawa kufikiria kwa pamoja na kuja na gunduzi mbalimbali zitakazowawezesha kupata vitu tunavyohitaji kama nchi. Makambi haya yawekewe miundombinu yote muhimu na mitaji kwa ajili ya ugunduzi ili vijana wetu waweze kuleta katika uhai ubunifu wao kisha utumike na viwanda vyetu kuzalisha kwa wingi vitu vinavyogudiliwa na vijana hawa.

Kwa maoni yangu hii ni fursa ambayo vijana tunakosa kwani mara nyingi vijana wanauwezo mkubwa ila wanakosa fursa za kuwakutanisha pamoja na kuwapatia vitendea kazi vitakavyoweza kuwafanya walete katika uhai ubunifu walionao.

Katika karne hii ya 21 nchi yetu inaweza kubuni na kutengeneza karibu kila kitu tunachoagiza kutoka nje nya nchi kwa matumizi mbalimbali. Kitu pekee tunachoweza kufanya ni kuweka mazingira sahihi ambayo yatawafanya vijana wakihitimu mafunzo mbalimbali waende katika kambi zilizotengwa kwa ajili ya kufanya uwezo na ubunifu wao kutumika kuzalisha kile tunachohitaji. Kambi hizi zitafanya vijana wasiwe na sababu za kukaa nyumbani na kusubiri fursa za ajira wasizojua zinapatikana wapi.

Tunaweza kuanza na kambi chache ili kuweza kuangalia namna zitakavyonufaisha jamii na nchi kwa ujumla. Kambi hizi zinaweza kuwa katika kila wizara ili kuweza kuzalisha ubunifu katika kila sekta hapa nchini na hii itafanya Tanzania ya viwanda kufikiwa kirahisi kutokana na ubunifu na technolojia kutoka ndani ya nchi tena isiyo na masharti.

Ni imani yangu serikali italitizama hili kwa njia bora zaidi na kulifanya wazo hili kuwa la faida zaidi kwani vijana wa kitanzania watasidiwa na nchi yao tu na sio jitihada zingine kutoka nje.

Nihitimishe kwa kusema, vijana wote wanauwezo wa kusukuma taifa mbele pindi fursa sahihi zikipatikana. Vijana hawahitaji ajira wanahitaji fursa za kuonyesha uwezo wao na kubuni mambo yatakayoweza kuzalisha mitaji mikubwa zaidi.
 
Back
Top Bottom