Tutumie mbinu hizi za kibunifu kuutangaza zaidi utalii wa Tanzania duniani ili utupe fedha za maendeleo

Elivius

Member
Sep 6, 2021
22
75
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa Nchi chache Duniani, zilizobarikiwa vivutio vingi vya utalii. Mbuga za wanyama, makumbusho ya kihistoria, uoto wa asili, milima na mabonde na vivutio vingine vya utalii, ni baadhi ya vivutio vya kitalii vilivyopo hapa Tanzania.

Sekta ya Utalii ni moja ya sekta mama, inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa na kuleta fedha nyingi za kigeni.

Mfano, mapato yaliyotokana na utalii, yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 2.2 mwaka 2017, ambapo ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

Sekta hii inachangia takribani asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni ~ Dkt. Hamis Kigwangalla.

Kwa takwimu hizo za Serikali, ni wazi kuwa sekta hii inachangia pato kubwa la Taifa, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutumia mbinu mbalimbali ili kuendelea kuutangaza zaidi Utalii wa Tanzania Duniani ili uendelee kutupa fedha nyingi zaidi, zitakazotumika katika miradi ya maendeleo.

ZIFUATAZO NI MBINU HIZO ZA KIBUNIFU, ZITAKAZOUTANGAZA ZAIDI UTALII WA TANZANIA DUNIANI.

1. Tutumie watu maarufu wa ndani kutangaza utalii wa Tanzania.
Licha ya Tanzania kubarikiwa vivutio vya kitalii, imebarikiwa kuwa na watu maarufu wenye ushawishi na wafuasi wengi ndani na nje ya Tanzania.

Nyota wa mziki kama vile Diamond, Harmonize, Ali Kiba na wengine chungu mzima, wanaweza kutumiwa na Serikali kuutangaza utalii wetu kupitia nyimbo zao na mitandao yao ya kijamii.

Nyota wa mpira wa miguu kama vile Samatta, Kelvin John na wengine wanaocheza soka la kulipwa nje, wanaweza kuutangaza utalii wetu pia.

Tunaweza kutangaza utalii wetu kupitia wasanii hawa kwa kuweka vipande vya utalii wetu mwanzoni mwa video zao za nyimbo ambazo zinatazamwa na mamilioni ya watu Duniani.

Hivyo, ni jukumu la Wizara husika kukaa meza moja na hawa wasanii na kupanga mikakati ya kufanikisha hili.

2. Tutangaze vivutio vyetu vya kitalii kwenye magazeti na tovuti kubwa Duniani.
Tunaweza kuandaa tangazo moja la kibunifu lenye sauti na michoro (graphics) likionyesha vivutio vyetu vya Tanzania kisha tukaingia makubaliono na wahusika wa tovuti na mitandao mikubwa Duniani kama vile "Amazon" ili kutangaza utalii wetu.

Lakini pia, tunaweza kuwasiliana na wahusika wa magazeti makubwa Duniani kama vile "NewYork Times", wakatangaza utalii wetu kwenye ukurasa wao.

Tukifanya hivi watalii watamiminika kama mvua za masika.

3. Kulipa fedha watu wenye ushawishi na wafuasi wengi Duniani kama vile Christian Ronaldo, Messi, The Rock na kadhalika, ili kutangaza utalii wa Tanzania kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Mfano, Christian Ronaldo ana zaidi ya wafuasi Milioni 300 kwenye ukurasa wake wa Instagram tu. Unadhani Ronaldo akiweka tangazo moja kutangaza utalii wetu, litatazamwa na watu wangapi Duniani? Hakika, litatazamwa na watu wengi.

Wala tusiogope gharama, kama Serikali ya Rwanda iliweza kuilipa timu nzima ya "Arsenal" kutangaza utalii wa Rwanda, sisi tutashindwa kumlipa mtu mmoja afanye hivyo?

Nakuhakikishia, Ronaldo akiweka tangazo la utalii wa Tanzania kwenye ukurasa wake, baada ya wiki moja Wazungu watajazana pale Uwanja wa Ndege. (Huyu jamaa ana ushawishi kupita maelezo).

Kama kitendo chake cha kutoa chupa ya Coca-cola mezani na kuhimiza watu kunywa maji, kiliitia hasara ya Matirilioni Kampuni ya Coco-cola ndani ya saa 24, huyu mtu ana ushawishi mkubwa.

Lazima tutumie fedha ili kupata fedha nyingi zaidi.

Kwa kufanya hayo, tutautangaza zaidi utalii wa Tanzania Duniani.

JE, TUKUZEJE UTALII WA NDANI?

Tuanze kupanda mbegu ya kupenda utalii kwa wanafunzi wa Shule za Misingi na Sekondari.

Wanafunzi hawa waanze kutembelea hifadhi na vivutio vyetu vingine vya utalii wakiwa shule japo mara mbili kwa mwaka.

Hii itajenga hamasa na mazoea kwa watoto kupenda utalii hata wakiwa wakubwa.

Watu wazima pia wahimizwe kutembelea utalii wetu.

Ni aibu kusubiri Wazungu tu kutembelea hifadhi zetu wakati Watanzania hatuungi mkono utalii wetu.

MWISHO. Serikali iendelee kudumisha amani ya Nchi na kupiga vita dalili zozote zile za machafuko ya kisiasa kwani utalii hushamiri sehemu iliyo na amani.

Mwisho wa makala haya.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom