Tusipotoshe hoja ya Ngurumo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tusipotoshe hoja ya Ngurumo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Chacha Kisiri, Nov 25, 2008.

 1. C

  Chacha Kisiri Senior Member

  #1
  Nov 25, 2008
  Joined: Nov 1, 2008
  Messages: 156
  Likes Received: 20
  Trophy Points: 35
  Source: Tanzania daima Jumapili, 23 Novemba 2008

  Tusipotoshe hoja ya Ngurumo

  Na Chacha Kisiri

  Kwa heshima na taadhima naomba nijitose uwanjani katika malumbano ya kiuandishi yanayoonekena kutoa moshi huku wengine wakishindwa kupambana kihoja na kukimbilia propaganda za kuwachafua wenzao ilimradi tu wawasilishe kile wanachokitaka na kusahau kuwa wanaweza kuandika, kuchapa, kusambaza na kusomwa, wakasahau kwamba wanapuuzwa na wasomaji kwa sababu Makala aziendani na halihalisi na ikawa wanafanya kazi bure!. Itakumbukwa Jumapili Octoba 19, gazeti la Tanzania daima liliandika habari katika mtindo wa Makala ya “Maswali Magumu” kwamba ‘Wananchi wamechoka, watawala wamekwisha’ – Na Ansbert Ngurumo, Hull.

  Sitapenda kurudia yaliyokuwemo kwenye hiyo makala, ila kwa ufipi Ngurumo alichukua matukio manne yaliyojiri kwa kipindi cha wiki moja hadi Octoba 19 akayafanyia uchambuzi wa kisomi kutoa ujumbe mzito na tafsiri sahihi ya matukio kwa watawala wa sasa. Yalikua ni matukio ya Uchaguzi Jimbo la Tarime, Mgomo wa Walimu, Kisa cha Wazee wastaafu wa iliyokua Jumuia ya Afrika Mashariki kufanya vurugu Wizara ya fedha na mwisho Kisa cha Msafara wa Rais Kikwete Kupopolewa mawe mkoani Mbeya.

  Majid Mjengwa mmoja ya waandishi mahiri alijitokeza kukosoa kasoro kadhaa wa kadha kupitia gazeti la Raia Mwema kuhusiana na makala hiyo. Ngurumo alimsikia akamjibu. Huyu sitamjadili

  Said Awwal mtu ambaye amekua akijitambulisha kama msomi wa kutunukiwa shahada ya falsafa ya udaktari (kama sikosei) na yeye akatoa hoja na ‘vioja’ kumpinga Ngurumo. Tatizo huyu ameshindwa kujitambulisha vilivyo kutetea hoja zake, kwa maana nyingine amejificha katika giza wakati tupo katika dunia ya utandawazi tunaongea kwa uwazi bila kutii dhana ya woga au kutegemea kichaka cha giza kikusaidie kuwasilisha hoja zako. Huyu nae sitajadili hoja zake kwa sababu ameshindwa kujitokeza mbele ya kadamnasi tumjue yeye ni nani hasa.

  Lengo hasa la kuandika makala yangu ni kumkosoa Mtanzania mwenzangu Conges Mramba aliyeandika katika safu yake ya fikra pevu gazeti la Tazama Tanzania Novemba 4 na 11, makala aliyoipa kichwa kisemacho Ansbert Ngurumo “wakili wa waliokasirika” anapoungama nusu-nusu”. Kwanza naomba niwe wazi kwa wote wawili Mramba na Ngurumo kwamba nawajua kupitia makala zenu ila siwafahamu na hatufahamiani.

  Lakini kabla sijaendelea naomba nifikishe Kilio changu kwa waandishi wa gazeti la Tazama Tanzania badala ya kuendeleza mjadala juu ya tafsiri sahihi ya matukio hayo ndugu zetu mmejikita kumgeuza mwandishi wa ‘Maswali Magumu’ ndiye ajenda wa Makala zenu na kutufanya baadhi yetu kuanza kushuku madhumuni ya kusajili hilo gazeti katika kipindi hiki wananchi wa makundi mbalimbali wanapambana na serikali iliyoshindwa kuwahudumia ipasavyo kuboresha maisha yao.

  Mramba alijikita kuikosoa makala ya Ngurumo kwa kutoa hoja zake kadhaaa, lakini mimi nkiwa kama msomaji wa Safu ya Maswali magumu (Mwandishi Ansbert Ngurumo) na safu ya fikra pevu (Mwandishi Congres Mramba) nimegundua mapungufu kadhaa katika hoja za Mramba ambazo nimeona niwashirikishe wasomaji na watanzania wenzangu.

  Mosi, Mramba anataka Ngurumo awe wazi ni vipi serikali ya Kikwete inawawinda ili kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali ya awamu ya nne. Naomba atambue kunyamazishwa alikomaanisha Ngurumo kunajumuisha matendo yote yanayofanyika kuvidhoofisha vyombo vya habari visiweze kuandika habari kwa uhuru zaidi. Siyo lazima mwandishi auwawe ndio anyamazishwe.

  Mathalani, gazeti la MwanaHalisi limefungiwa na serikali bila sababu ya msingi ni hujuma tosha ya kuwanyamazisha baadhi ya waandishi. Wahariri wa MwanaHalisi wametoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya ufisadi na Mafisadi. Ndio walikua wa kwanza kuchapisha majina ya Mafisadi 11 mara baada ya kusomwa Septemba 15 mwaka jana. Itakumbukwa Orodha ya Wezi (Mafisadi) ilisomwa Jumamosi viwanja vya Mwembe Yanga – Temeke cha kushangaza hakuna gazeti lilodhubutu kuyaanika majina ya Mafisadi hadharani hadi Jumatano iliyofuata (kupitia MwanaHalisi). Si hilo tu, MwahaHalisi ndio waliobainisha hadharani majina ya vigogo waliolipwa fedha kupitia akaunti ya Tangold na Meremeta. Walitoa jina moja baada ya jingine. Haraka walidhubutu kutaja kashfa ya mkataba wa kinyonyaji wa Richmond.

  Ni MwanaHalisi ndio walioibua Ufisadi katika Ujenzi wa Jengo la Vijana (UVCCM) kwa kuchapisha nakala ya mkataba hadharani wakiainisha majina na sahihi za mafisadi waliohusika. Walikwenda mbali pia kuwapa taarifa wapenzi wa chama tawala kuhusu utafunwaji wa mishahara ya wafanyakazi wa Tanzania One Theatre (TOT) na kughushiwa nyaraka za malipo. Waliibua pia ufisadi katika shirika la Simu la Taifa-TTCL na sehemu nyinginezo serikalini na mashirika ya Umma. Lilifanya hivyo kwa nia moja; kutimiza wajibu wake kama mdomo wa umma.

  Kulifungua mwanahalisi ni sehemu ya mkakati kuwanyamazisha baadhi ya wakosoaji wa serikali ya awamu ya Nne. Leo hii Mramba aniambie ni lini gazeti la Tazama lilichapisha Orodha ya Mafisadi hadharani? Atuambie ufisadi uliowahi kuripotiwa na gazeti analolitumikia hasahasa ufisadi wa serikali ya awamu ya nne.

  Ajenda ya Ufisadi ni gumzo kila mahala hivi sasa kwani ndiyo sababu ya msingi serikali kushindwa kulipa hata mishahara midogo ya walimu wetu badala yake imejikita kuzuga na Igizo la kuhakiki majina ya walimu (Ilhali inawajua). Tangu serikali ilipolifungia MwanaHalisi “Maswali Magumu” ndiyo yamekua mbadala wake. Na kwa vile serikali haiwezi kuyafungia maswali magumu kwani yenyewe ndiyo inayatunga kwa vitendo vyake kandamizi dhidi ya wananchi, leo kina Mramba na wanzake wanaotumia majina bandia mnamsakama na kumchafua mwandishi wa maswali magumu badala kumsakama mtunzi ambae ni serikali. Hivyo naomba utambue kuandamwa na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari bila kosa la msingi ni sehemu ya mkakati wa kutaka kuwanyamazisha kina Ngurumo na wenzake.

  Pili, Mramba anadai “Mwandishi ama mtu yeyote atakaye jitangaza kwamba ni Kioo cha Jamii hapaswi kusherehekea, kufurahi au kushangilia wapumbavu wanapoamua kumtwanga mawe Rais huko Mbeya, kwa sababu usiku ule alishindwa kusimama ili kuwasikiliza”. Kwanza binafsi nampinga, nimesoma na kurudia rudia ‘maswali magumu” ya Octoba 19 sijaona sehemu Ngurumo amesheherekea, kufurahi au kushangilia Rais kopopolea mawe badala yake ametoa tafsiri ya upopoaji mawe kwa Rais na utawala wake - Kwamba wananchi wamechoka, watawala wamekwisha!.

  Mramba aelewe mara kwa mara watawala wa serikali wamekua wakirandaranda na magari ya kifahari maeneo yenye maisha magumu makiwamwagia vumbi wananchi walipa kodi bila sababu yoyote. Kule Mbeya baada ya wananchi kutaarifiwa ujio wa Rais kwamba angelisalimiana nao walitegemea kupata wakati mwafaka wa kumueleza Rais kuhusu matatizo yao, wananchi wakajitokeza kwa wingi!.

  Lakini kwa vile watawala walikosa nidhamu na kutaka kuwahi starehe mahotelini bila kufuata taratibu kwa kuwaomba radhi wananchi waliojipanga barabarani, wananchi wakajikuta wanabugizwa vumbi la misururu ya magari ya kifahari - Magari ambayo ni chanzo cha Maisha magumu kwao! Bila kujijua Serikali ikawapandishia hasira wananchi wa Mbeya, matokeo yake nao wakalipiza kisasi kujibu mapigo ya mavumbi ya msafara kana kwamba waliitwa kunyweshwa vumbi.

  Hapa watu wa itifaki msafara wa Rais lazima walaumiwe inaonekana si watu makini, vipaumbele vyao ni mahotelini badala ya wananchi. Ndiyo sababu ya kupopolewa mawe. Rais angesimama hata bila kushuka akawapungia mkono wasingepata ile kadhia. Dharau ya serikali dhidi ya wananchi na kuweka starehe za hoteleni mbele ndizo zilizoiponza. Kama ilishindikana kusimama kwa sababu ya muda wananchi wangetangaziwa mapema watawanyike waende makwao na sio kuwafanya “matoi” kushangaa magari yanayowatia umaskini.

  Tatu, Wakati flani Mramba anadai “Mwandishi hapaswi kuwa na hasiri kali dhidi ya anayedaiwa kuwa “mkosaji” Rais Kikwete. Hata hakimu mahakamani hapaswi kupandwa hasira kali dhidi ya mshitakiwa yaani Rais Kikwete”. Lakini Mramba asemi kama mkosaji anakosa nidhamu kuendana na kanuni na taratibu za kimahakama kiasi cha kuaribu mfumo mzima wa kusikiliza na kutoa hukumu afanyweje? Maswali magumu yamekua yakiandikwa mara kwa mara cha ajabu utawala wa Kikwete umekaidi kutoa majibu kwa kukaa kimya!. Kwa maana nyingine inakaidi utaratibu wa utoaji hukumu katika kesi inayoikabili. Kwa msingi huo hata kama Mramba angekua hakimu atapandwa na hasira, atamuhukumu mtuhumiwa kwenda jela kwa sababu ameshindwa kujitetea, si kwa sababu ametenda kosa.

  Lazima pia tukumbushane kwamba hasira ni matokeo ya kimaumbile ndani ya vinasaba vyetu. Wengine wameumbwa wana hasira nyingi, wengine za kawaida na wengine hawana hasira (Ila sijui kama wapo). Huwezi kumzuia mtu asiwe na hasira kwa sababu ni matokeo ya kimaumbile. Kufanya hivyo ni sawa na kulazimisha mtu asirefuke urefu wakati yeye hana mamlaka ya kujizuia.

  Ngurumo kama ana hasira ni matokeo ya kimaumbile aliyorithi toka kwa wazazi wake na muumba wake. Tusimlaumu yeye, tumlaumu muumba wake kwa nini alimuumba alivyo? Hivyo hatuwezi kumhurumia Rais Kikwete dhidi ya hukumu kali ya hakimu Ngurumo kwa sababu Maswali magumu yamekua yakiandikwa tokea mwaka 2002 katika gezeti la Mwananchi, hata kabla Kikwete hajawa rais. Mramba ameshindwa kuleta utetezi. Sasa hakimu afanyeje wakati mlalamikaji (Wananchi) wanataka hukumu? Jibu ni kwamba mtuhumiwa (Rais Kikwete) anaswagwa jela na kushindiliwa adhabu kali kwa kushindwa kujitetea. Hakimu habebi mtuhumiwa aliyeshindwa kujitetea.

  Nne, Kwa upande mwingine Mramba anadai “Ngurumo anamchukia Rais Kikwete kwa sababu utawala wake umejaa ufisadi anamshauri ingekuwa heri kama angechukia ufisadi bila kukasirika”. Naomba aelewe hivi kwa adui kama ufisadi huwezi kuuchukia bila kuukasirikia.

  Yeye Mramba kama hakasiriki juu ya vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na watawala basi si mwenzetu au naye anafaidika navyo au huenda yeye binafsi na famila yake wameshayaona maisha bora aliyoaidiwa na Rais Kikwete ndiyo maana haoni ufisadi kama ni kikwazo kwetu sisi tunaoumia na kusaga meno. Bila hasira dhidi ya ufisadi Mafisadi wataendelea kuchota hadi chakula cha “mbwa” kama wanavyotaka!. Ni hasira za wananchi (Ngurumo akiwamo) ndizo zitakazomaliza tatizo la ufisadi. Na kama yeye hana hasira dhidi ya Mafisadi basi ajue naye ni sehemu ya tatizo tulilonalo.

  Tano, Tunaarifiwa na Mramba kwamba “Ngurumo asipoacha hukumu za hasira namna hii, dunia itajaa wanadamu wenye chongo, vibogoyo na vilema watupu. Watapaje uhuru kamili? Watapataje haki na amani?” Labda nimuulize kitu kimoja, kama wananchi wa Afrika kusini wangendeleza nidhamu ya kinafiki kwa makaburu leo hii wangekua na uhuru? Ni kujitolea kafara kwa baadhi yao kupata hivyo vibogoyo na vilema ndivyo vimewawezesha kuliondoa genge dhalimu la makaburu.

  Hivyo hivyo wananchi wa Kenya wangendelea kumtii Kibaki aliyejiapisha Rais kwa njia bandia leo hii wasingekua na serikali ya mseto?, Serikali ambayo ni Tumaini Jipya hivi sasa nchini mwao. Vilema wa harakati za ukombozi siku zote hubaki kama mashujaa wa ukombozi na hatimaye huzaa jamii mpya inayoishi kwa amani na isiyo na vibogoyo wala vilema. Matumizi ya Nguvu ya Umma hayakwepeki pale tawala inapokaidi kusalimu amri au kutii matakwa ya wananchi. Vibogoyo, vilema na vifo ni sehemu tu ya matokeo yake na haviepukiki katika harakati za kujikomboa.


  Sita, Ndugu yangu Mramba anasema “Anachukia hatua ya vita kwa sababu anaye mama yake mzee anaitwa Nyasongorwa yeye vita ikianza lazima amezwe na ndimi za moto. Hawezi kukimbia kama wa Congo.” Kwanza nimpe hongera kwa kuishi na mama yake hadi leo. Binafsi nimempoteza Mama yangu miaka 5 iliyopita. Ila nimkumbushe kitu kimoja Mama yake ni kati ya Wazee walionyonywa na kudhulumiwa na tawala za CCM hivyo siku vuguvugu la Umoja wa Wazee likianza kudai mafao yao ya uzeeni asije shangaa akimwona akiungana na wazee wenzake kuupinga utawala anaonekana kuutetea. Ni jukumu la serikali kuhudumia jamii isiyojiweza (wazee wakiwamo). Mramba anadhulumiwa na serikali, siyo kazi yake kukaa na Mama yake mzee. Hata kama hakai naye siyo pia jukumu lake kutuma pesa za matumizi kugharimia gharama za Malezi ya Mama yake. Vita ikitokea serikali ndiyo inawajibika kuilinda jamii isiyojiweza na siyo jukumu la Mtoto, binamu, kaka, nk. Kama anawasiwasi na vita ikilipuka Mama yake atamezwa na ndimi za moto basi ni wakati wa kutumia kalamu yake kuihoji serikali ni vipi imejipanga kuwasaidia wazee mara kadhia ya vita itakapotokea?. Au aende wizara husika.

  Saba, Kuna aya moja Mramba ameandika hivi; Weusi wa Marekani walishauriwa na Martini Luther kutotenda baya kwa baya. Mimi nasema hivi anapaswa kukumbuka imeandikwa “Wema usizidi uwezo”. Wananchi hawawezi kuendelea kuitendea mema serikali wakati yenyewe kila kukicha inaitendea maovu kwa kuwambatia wanao wahujumu. Kutenda jema kwa jema unakikomo chake - Yani uwezo. Kuendelea kutenda mema zaidi ya uwezo ni upumbavu na ujinga. Hivyo huwezi kuwalazimisha wananchi waendelee kuitii na kuiheshimu tawala yao kama wameivumilia mpaka wamechoka! Ni wakati kwa upande wa pili wa sarafu kuchuku nafasi kufanya kile inapaswa kufanya kuokoa machafuko.

  Nane, Hoja ya kumtaka Ngurumo awakemee wanaovunja sheria za nchi haina nguvu kwani waliopambana na mamlaka (Walimu, Wazee wa EAC, Wananchi wa Tarime na Mbeya) wanahisi wanadhulumiwa na mamlaka. Serikali ndiyo ijikemee nafsi yake na siyo Ngurumo awakemee mateka wanaotaka kujinasua. Mtumwa anataka kuondoka makwapani afanyeje kama Mkoloni hataki?. Wananchi wafanyeje kama serikali haitaki kuwaheshimu? Jibu ni kwamba wanaitwanga na kuizomea barabarani inapopita(Kama Afrika kusini walivyowafanya makaburu).

  Mtoto kama amekua anataka kuachika kunyonya huwezi kumlazimisha kunyonya!. Ukilazimisha wewe kama mzazi utakua punguani. Sawa kuchukua sheria mkononi ni dhambi na kosa lakini Mramba ajamalizia kwamba si dhambi wala Kosa kwa Mamlaka Korofi.

  Tisa, Kwa upande mwingine Ngurumo anatuhumiwa na Congres Mramba kwamba “Ni wachache, wenye kujua Ngurumo anapandwa hasira na kukosa maneno ya staha anapokosoa utawala anaodai wa kifisadi wa Rais Kikwete”. Waandishi wenye mtamzamo wa Mramba lazima mkiri kwamba nidhamu na ustaarabu wenu wa kutumia maneno ya staha katika uandishi hususani katika tawala zilizopita ndio koleo lilolichimbia Tanzania katika kaburi la Mikataba ya kifisadi. Mfano Kulingana na maelezo yaliyomo katika Orodha ya Mafisadi inasomeka hivi; Nanukuu “Mnamo tarehe 5 Agosti 1994 Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete (Hivi sasa ni Rais) aliingia mkataba na kampuni ya madini Kahama Mining Corporation Ltd., kampuni tanzu ya kampuni ya Sutton Resources ya Canada. Ijapokuwa mkataba huu unaonyesha wazi kwamba ulikuwa unahusu eneo la Butobela Wilaya ya Geita Mkoani Mwanza, mwezi Agosti mwaka 1996 Kahama Mining Corporation wakisaidiwa na vikosi vya FFU walivamia eneo la Bulyanhulu, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na kuwaondosha kwa nguvu watu takriban laki nne waliokuwa wakiishi na kuchimba dhahabu katika eneo hilo. Baada ya kutwaa eneo hilo kwa nguvu za kijeshi, Sutton Resources iliiuza Kahama Mining Corporation na Bulyanhulu kwa Kampuni ya Dhahabu ya Barrick Gold Corporation ya Toronto Canada kwa dola za Marekani milioni 280. Leo hii Bulyanhulu ni moja ya migodi tajiri kwa dhahabu katika Bara la Afrika”. Mwisho wa kunukuu.
  Sasa tujiulize kama tokea zamani waandishi wote mngekua mnaandika kwa maneno makali ufisadi huu ungetokea?. Mafisadi wangetishika na wasingedhubutu kuliangamiza Taifa kwa mikataba ya hovyo. Maneno ya staha kwa watawala ndiyo yaliyowapa jeuri ya kuingia mikataba ya kifisadi kama wanavyotaka na kuvamia maeneo ya wananchi kwa nguvu za dola.
  Kumi, Kwa upande mwingine nimefurahi kuona Congres Mramba akiwaonya wananchi na kile alichoita kujikomba kwa watawala nyakati za kampeni wanapopewa pombe, khanga, kofia, fulana na kuimba nyimbo za kukienzi chama na wagombea na kuwarejesha madarakani huku wakinung’unika nyakati wakiwa madarakani. Nimefurahi pia alipotoa changamoto kwa watanzania kuiga nyayo za Wamerekani kupigia kura nafuu ya maisha na kamwe si kupopoa mawe mamlaka inayopandisha gharama za maisha. Hapa Kuna kitu Congres Mramba amesahau, kwa zaidi ya mara 3 wakazi visiwani Zanzibar wamepigia kura nafuu ya maisha lakini wahafidhina wanakataa kwa kutumia nguvu za dola huku wakiwapoza na mazungumzo yasiyokwisha. Tanzania bara hivyo hivyo, tumeshudia wizi wa kura Jimbo la Ubungo, Bukoba Mjini nk. Walau Karatu waligonga mwamba. Swali, wafanyeje? Jibu ni kwamba katika mazingira hayo Nguvu ya Umma lazima itumike. Na nguvu ya umma inahusisha upopoaji mawe na zomeazomea dhidi ya wezi wa kura.

  Kuna kitu kingine muhimu cha kujua pia, Tume zetu za Uchaguzi siyo kama za Wamarekani, wapinzani wanasakamwa na nguvu za dola nyakati za kampeni, chama tawala kinachota pesa za kampeni kwenye Hazina ya taifa huku vyama vya upinzani vikitegemea ruzuku ya kukinga kibakurini. Katiba ya nchi haitoi mazingira ya uchaguzi huru na haki. Na siku zote wanaharakati wamepigia kelele haya mambo watawala wameweka pamba masikioni. Swali kwa Mramba tufanyeje? Jibu linarudi kulekule, matumizi ya Nguvu ya umma (Upopoaji mawe ukiwemo) – Ni kwa sababu kura haina nguvu kumweka au kumwondo mtu madarakani Tanzania.

  Kumi na mosi, Congres Mramba katika makala yake amegusia hotoba ya Rais Kikwete ya mwisho mwezi uliopita. Ameipigia upatu kuwa imeweza kufafanua masuala anuwai huku Rais akiwa na utulivu mwingi wa kunyenyekea umma. Anadai hatujaona makeke na ubabe katika hotoba ile kwa sababu Rais anajua wapiga kura ni nani na wana nguvu gani? Binafsi naomba nimkumbushe kama tulivyoelimishwa siku za nyuma, kwamba ile hotoba haikua na hadhi ya kupewa jina la hotoba ya Rais bali ilipaswa kutolewa kama taarifa kwa vyomba vya habari kwa sababu imeacha maswali mengi miongoni mwa wananchi. Mfano, hotoba gani ya Rais inashindwa kuwataja wahujumu uchumi wakubwa hususani wa Deep Green Finance na Kagoda Agriculture Ltd? Hotuba gani inashindwa kusema mahala zilipo pesa zilizorejeshwa? Nk.

  Kitendo cha Rais kutoa hotoba (Kama mramba alivyoiita) huku akiwa na utulivu mwingi wa kunyenyekea umma ni ushahidi tosha kwamba Rais ana wasiwasi wa baadhi ya mambo anayowasilisha kwa wananchi labda hayako kamili, uongo, au ya kughushi!. Anakua makini ili kuteka akili za watanzania mbumbumbu wasiojua kinachoendelea na asije akajichanganya binafsi pia. Rais hakuwa na Makeke na ubabe katika kuwasilisha ile hotoba kwa sababu ilikua na mapungufu. Alijawa na huzuni.

  Kumi na mbili, Tunapewa somo la mwisho toka kwa Ndugu yetu Mramba kwamba “tuwaonye wenye madhambi siyo kuwabeza”. Hapa katuacha njia panda kidogo kwani hajawa wazi ni vipi tuwashughulikie wale wanaokaidi maono hususani wanaendeleza Ufisadi mathalani wananchi wanakosa huduma muhumu? Tuendelee kuwaonya huku tukifa au? Kisha Mramba anasema “tutende haki, kukosoa ni kutenda haki kama wanaokosolewa wamefanya kinyume cha haki”. Hapa sina cha kuongeza ila nadhani amelenga kuwapa shime wakosoaji wa utawala wa ari mpya waendelee na kazi ya kukosoa utawala wetu.

  Mwisho ningependa wapenzi, wafurukutwa na wasomaji wa Safu ya Maswali Magumu na ile ya Fikra Pevu tutambue tafsiri sahihi ya Maswali Magumu. Kwa mtazamo wangu Maswali magumu ni matokeo ya vitendo vinavyofanywa na serikali. Hivyo yanatungwa na serikali yenyewe. Ngurumo anachofanya ni kuyaandika tu.

  Kwa kweli kuna mapungufu mengi katika Makala ya Mramba, na inasikitisha kwa mwandishi mahiri kama yeye kuandika Makala na kuacha mashimo bila mfuniko. Kwa kifupi ni aibu. Kwa uandishi unaouegemea hakika utadumaza taaluma yake na hatimaye atakwisha.

  Mwandishi ni Kijana Mwanaharakati:-
  +255 715 866 522  Ifuatayo ni baadhi ya maoni niliyotumiwa kupitia simu yangu ya Mkononi, Sijaweka namba zao za simu kwa sababu sijaomba ridhaa yao kuanika maoni yao hapa

  1. Very good Chacha Kisiri kwa Makala yako ya leo “Tusipotoshe hoja ya Ngurumo”, umetoa ufafanuzi mzuri kiasi kwamba mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kuupinga. Mambo yako dhahiri ni wajinga wachache tu wanajifanya hamnazo, mamluki wakubwa. Umemsahau mwandishi mmoja wa Tazama anaitwa Julius Mapunda. Huyu Bwana kazi yake ni kusifu tu. Naitwa Abel Syliveste, Dsm. Keep it up! 23 November 2008, 09:41:09

  2. Safi umemrekebisha vizuri Mramba na Mwenzake Mjengwa. Ila mjomba JK Nchi imemshinda mapema nashauri asigombee tena apishe kina Shibuda. Ngurumo ni Mwanaharakati bora anafundisha na kuonya huyu ni mtetezi wetu sie raia wa chini. 2010 nashauri Dr.Slaa agombee Urais atashinda huyu ni bonge la Kiongozi bora. Mwanaharakati Bukoba. 23 November 2008, 10:40:41

  3. Je kumfukuza Odong ndo mwisho wa migomo? Je Odong ndo amesababisha kufungwa kwa vyuo saba? Je Odong kuwa na kadi ya CCM mzembe ni nani? Je Odong kukosa Urais Daruso inahusiano gani na serikali? Je si Odong aliyemfanyia kampeni Machibia? Tafakari Chukua hatua Ngo! Haki mgomo. Tunajenga taifa ambalo halitakuwa na watatuzi wa matatizo bali visingizio. Ndo haya tunayoyaona. Kila mtu kumshutumu mwenzake badala kiini. 23 November 2008, 12:50:12

  4. Nakupongeza kwa Makala yako yenye mantiki! Watu kama Mramba ni wa kupuuzwa! Ni mafisadi wa taaluma ya uandishi!. 23 November 2008, 13:11:41

  5. Nakupongeza kwa makala yako yenye mantiki! Watu kama Mramba ni wa kupuzwa! Ni mafisadi wa taaluma ya uandishi!!! 23 November 2008, 13:11:41

  6. Habari yako! Hakika nimefurahishwa mno na makala yako leo kwenye Tanzania daima. God bless you Ndugu. Mi Munishi msomaja. 23 November 2008, 14:05:08

  7. Sawa Kaka endeleza mapigano. 23 November 2008, 14:06:23

  8. Kwa kweli Mramba Kachemsha hongera Kaka. 23 November 2008, 14:45:00

  9. Ni kweli kabisa hawana hoja wakianikwa upuuzi wao kwa raia, jazba inawatawala kuliko busara. Harakati zenu hakika Mungu atawalinda. Watu kama wewe mnati *some text missing* 23 November 2008, 15:27:23

  10. Hakika nakupongeza kwa Makala yako nzuri Tanzania daima leo. Mtu mwingine gazeti la Tazama ni huyu Mapunda huyo yupo pale kwa kupinga makala za wenzake kwa kujipendekeza nililazimika kuacha kulisoma, waandishi wawazi kama ninyi mmbarikiwa sana endeleeni kukosoa serikali mnaisaidia sana. Bibi Keath ni wa EAC. 23 November 2008, 15:50:46

  11. Hongera kwa Makal yako ya leo Tanzania daima imejaa ukweli mtupu, nakuunga mkono 100% uchambuzi wa mwenye akili na kwa maslahi ya taifa. keep it up. 23 November 2008, 16:33:07

  12. Ndugu Chacha Kisiri napenda kukupa hongera kwa nakala yako “Tusipotoshe hoja ya Ngurumo” Majid kaongea utumbo hana hoja kwa wananchi, tisa kumi ni huyu Congres ndo mlemavu na mpofu kisiasa wa hoja. Hoja za Ngurumo ni nzito na makini. Rais alitumia kauli ya upole akijua alidanganya. Ngurumo ni Mwanaharakati. 23 November 2008, 16:51:02

  13. Kweli umenena Mramba sikutarajia aandike Makala ya kipuuzi namna hiyo, TAZAMA gazeti la kina waandishi kama Mapunda. Kuna namna mpaka abadilishe uandishi wake kwenye kigazeti uchwara. Ngurumo Uzi ule ule. 23 November 2008, 17:03:01

  14. Ni kweli na wala tusichoke kukemea na kupayuka na ikibidi nguvu tunazo tumechoka kufanywa wajinga na ukondoo huu wa watanzania ndo utaangamiza hadi vizazi vyetu wakati wao wananemeeka na familia zao sisi tunawapigia makofi na wimbo wa kipumbafu maisha bora mara kasi mpya nk huu ni ujinga kupumbaza watu wakati nchi ni yetu wote wengine wanakula kivulini wengine tunalia juani na mateso yasiyostahili tusikubali. Nitatafuta siku tuonane tuongee tuelimishe jamii. 23 November 2008, 17:09:59

  15. Makala ya leo kali kaza buti kamanda tuko nyuma ya kalamu yako mwanaharakati. God be with you. 23 November 2008, 17:18:14
  16. Habari za Jumapili nimesoma Makala yako kwenye Gazeti la Tanzania daima la leo uliyokuwa ukimjibu Ndugu Mramba kwa kweli nakupongeza sana kwa makala hiyo nafikiri huyo Bwana Mramba atakapoisoma atajua kabisa kuwa wananchi wamechoka na hizo bla blaa zao kuitetea hii serikali inayowakumbatia mafisadi uku wananchi tukitaabika kwa hali ngumu ya maisha. Nakutakia Jumapili Njema. 23 November 2008, 17:28:49

  17. Ni kweli kabisa Ansbert ameandika leo kuwa Salva alikua Mkali kipindi cha Mkapa leo kapewa ulaji na JK kawa Mpuuzi. 23 November 2008, 17:47:48

  18. Kama ulivyosema lazima kafara ya watu ili kuikomboa nchi shida watawala wanalindana kwenye maozo wanayoyatenda. Kila la heri kaka. 23 November 2008, 17:58:49

  19. Makala yako ya Ngurumo naipenda sana inaeleza ukweli inagusa hisia za wengi, mimi ni mfanyakazi wa Bandari njoo huku pia ufisadi upo mwingi. Mungu akubariki. 23 November 2008, 18:41:27

  20. Bravo! Umekamua mkuu! Maswali magumu yanajitetea kuliko takataka za wachumia tumbi na waganga njaa, Umesema kweli tupu! Keep up good job. 23 November 2008, 19:23:16

  21. Kaka kaza buti kazi yako tuna ikubali. Bomoa mafisadi na vibaraka wao wanao walinda. Tumia fani yako kuusema umma. Mungu akuongeze katika hilo. Mwenzio kwenye harakati. 23 November 2008, 19:23:49

  22. Ndio hivyo! Habari ndo hiyo. Ila laana ya Watanzania Makabwela itawatafuna. Hata ubinadamu wameishiwa. I liked ur article! 23 November 2008, 19:27:41

  23. Laiti kama Tanzania ingekuwa na wapiganaji kama wewe tungekuwa na mafanikio kama Baba yetu aliyetuacha. Makala ya leo ya Tanzania daima ina point ya Taifa. 23 November 2008, 20:53:42

  24. Machoni naona kiza, kiubish nimekusoma kaka. Makala yenye uzito wa dunia na machungu ya msalaba na wingi wa mateso. Na ufisadi umekua wimbo wa taifa, pia ni mtandao wenye nguvu sana na vibaraka kama vile Majid, Awwal na Mramba. Sio siri matumbo yanauma kwa wingi wa ngojangoja, kesho ya jana ipo wapi? Taifa la kesho michosho, mirisho isiyo na mwisho. Ila tukiandamana hawataweza kuchukua ushindi. Tukuja kwa mawe, mapanga makundi kwa makundi. Sikiliza wimbo wa taifa-KALA. 23 November 2008, 21:12:18

  25. Ongera kwa Uwanaharakati usiye na nidhamu ya uwoga, unayekubali lawama na chuki kwa ajili ya taifa la kesho. Endelea hivyohivyo na usiogope kufungwa au kudondoshewa vitasa coz huu mziki tushauchoka. 24 November 2008, 21:22:18

  26. Tanzania bila CCM yawezekana. Ichukie CCM, kama ukoma. 24 November 2008, 00:02:20

  27. Nimesoma makala yako “Tusipotoshe hoja ya Ngurumo” hongera sana, washambulieni hao vibaraka nasi wananchi tuko nyumba yenu! Naamini tutafika siku moja. Gud lucky. 24 November 2008, 10:39:01

  28. Though sikujaliwa kusoma Makala ya huyo mtu anayejiita Mramba but nimevutiwa sana na mtiririko wa hoja zako katika kuonesha namna jamii yetu inavyopaswa kujihadhari na watu type ya Mramba, he is rather non-patriot, we should question his citizenship too?! I realy hate politics bro 4 million of reasons too. Kikwete akiwa ni moja ya Sababu. Mimi ni Kijana nliemaliza kidato cha sita mwaka huu Ndanda High School. 24 November 2008, 10:52:30

  29. Keep it up bro, I wish pngeanzishwa gazeti maalum katika kipindi hiki special kwa habari zinazohusu EPA na kila ishu inayohusu ufisadi, hao wanakerwa na magazeti yanayoandika ufisadi beta pangeanzishwa tume kuwachunguza bro. 24 November 2008, 11:03:23

  30. Msihofu, watanzania wanaamka kwa kasi sana! Wapambe wa Kikwete hawakujua kama Ujiko wanaompa utageuka KITANZI. Mi naona jamaa ana akili za kawaida mno kuwa kawaida mno kuwa Rais. 24 November 2008, 12:34:53

  31. Akina Congres Mramba ni wasaliti. Usaliti ndio umetufiksha katika hali tete tuliyomo. Nadhani tuki-eleminate usaliti kwanza Maswali Magumu ya Ngurumo Automatically yatakuwa mepesi. Tunasumbuliwa na Usaliti. 24 November 2008, 12:44:31

  32. Ndugu Chacha, asante kwa mawazo yako Mazuri. Makala za Ukombozi wa kifikra zina upinzani sana! Nawaombea endelea mbele. 24 November 2008, 15:09:57

  33. Ongera kwa Makala yako katika Tanzania Daima, nami niko upande wa Maswali Magumu. 24 November 2008, 16:17:32

  34. Naishi Mwanza namfaham vizuri mramba ni CCM kwa hiyo usishangae anachoandika ni kuwatetea wanachama wenzake mafisadi 24 November 2008, 20:31:01


  Sasa ni zamu yenu wanaJF, Tujadiliane, uwanja kwenu.
   
Loading...