Masanilo
Platinum Member
- Oct 2, 2007
- 22,286
- 4,493
KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa kila mtu ana haki ya kuishi mahali popote pale anapotaka ili mradi havunji sheria, haki ambayo ombaomba maarufu hapa nchini, mzee Anthony Matonya, pia anastahili kuwa nayo. Kwa haki hiyo hiyo, mzee Matonya aliyejijengea umaarufu mkubwa hapa nchini kwa staili yake ya kuomba, umaarufu wake ulianzia jijini Dar es Salaam na amekuwa akizunguka katika mikoa mingine ya Dodoma na Morogoro akiendelea na kazi hiyo inayomuingizia riziki kutoka kwa wasamaria wema.
Wengi wanamuona mzee huyo kama binadamu mwenye ulemavu wa macho anayeishi kwa vituko, baadhi wamtaja kuwa ni tajiri mkubwa wa mifugo na hakustahili kuomba kwa kuwa ana mali nyingi hususani katika ukoo aliotoka.
Sijui zaidi kwa undani maisha ya mzee huyo pamoja na utajiri wake wote unaoelezwa, lakini inashangaza kwa nini mzee huyo na umri wake mkubwa aamue kuomba badala ya kusimamia mifugo yake huko Dodoma.
Hicho ni kitendawili kikubwa ambacho mzee huyo mwenyewe ndiye anayeweza kukitegua na pengine anataka aingizwe kwenye kitabu cha Guiness ambacho kinaweza kumtoa Mtanzania wa kwanza aliyefanikiwa kuomba kwa muda mrefu na akiwa na umri mkubwa kuliko wote waliowahi kuomba duniani.
Simshangai mzee Matonya na siwalaumu wale wanaofuatilia maisha ya mzee huyo kwa karibu kila kukicha kwa kuwa tayari amekwisha jijengea umaarufu mkubwa wa kuomba, kazi ambayo hawezi kuiacha hadi mauti yatakapo mkuta.
Lakini kwa mfano huo wa mzee Matonya Watanzania wanapaswa kujiuliza kuwa wapo akina Matonya wangapi wanaoshindwa kuishi kwa dola moja kwa siku kutokana na kipato duni na hawawezi kuendesha maisha yao bila kuomba.
Zipo aina mbalimbali za kuomba na si tu aina hiyo ambayo mzee wetu Matonya anaitumia, wapo waombaji wakubwa waliovuka viwango hadi wakajitokeza kuwa waombaji wa mbinu za juu za ulaghai wanaoitwa ‘matapeli'.
Kama watu wanavyodai kuwa mzee huyo ana mali nyingi na mwanzo wake umetokana na fedha anazopewa kidogo kidogo na akizipeleka kwao kununulia mifugo iliyoendelea kuzaliana kazi hiyo.
Tukimsema Matonya tusisahau kuwa haitakuwa vigumu kujisema wenyewe na serikali yetu kwa kuwa wote tumekuwa omba omba na zaidi pale tunapoomba kila kitu kwa nchi wahisani ili waweze kuendesha bajeti yetu ya nchi.
Nchi wahisani sasa zinainyooshea mkono Serikali ya Tanzania kuwa licha ya kuomba na kupatiwa misaada mingi bado wahisani hao hawaridhishwi namna fedha zao zinavyotumika katika shughuli za maendeleo.
Wahisani wameshituka wameamua kupunguza misaada yao na hali inazidi kuwa ngumu upande wa serikali, ikitarajia kuwa na bajeti ya sh trilioni 11.1 kwa mwaka 2010/2011 fedha ambazo haziwezi kupatikana moja kwa moja kutoka vyanzo vya ndani.
Nchi kama Sweden inahoji namna serikali ya Tanzania inavyoendelea kuwa masikini na watu wake huku kukiwa na rasilimali za kila aina, wanashangaa huu umaskini tulionao unatoka wapi?
Ni majuzi tu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alinukuriwa na vyombo vya habari akiushangaa umasiki wa Watanzania, kuwa nchi hii ni ya neema imejaliwa rasilimali tele, ardhi kubwa, wasomi na wataalamu wa kila aina lakini mambo hayaendi.
Waziri Mkuu Pinda anashangaa umasikini wa nchi hii na hawezi kushangaa leo kwa kuwa yupo kwenye mfumo wa serikali tangu awamu ya kwanza na ana miaka zaidi ya 35 katika utumishi wa umma hivyo anaifahamu zaidi nchi na serikali zote zilizotangulia na hii ya awamu ya nne akiwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za serikali.
Umaskini wa Watanzania ndio maajabu ya leo tunayoyaona na yanayowashangaza wahisani na waziri mkuu, kuwa inatia aibu nchi inapokuwa omba omba huku ikiwa na rasilimali tele, huko nje si bure kuwa tunaitwa kina ‘Matonya'.
Kama ilivyo kwa mzee Matonya alivyojibebea umaarufu mkubwa kwa kuomba, Watanzania tutaepukaje aibu ya kuomba kila siku nje, leo hii Pinda anahoji, hivi Watanzania nani kawaroga, mbona tuna kila kitu nchi hainyanyuki ?
Tukimshangaa mzee Matonya kumbe wote tunaomba na serikali yetu inaomba, sasa katika waombaji wote hii aibu ya kuendelea kuomba, kutegemea wahisani katika bajeti yetu itakwisha lini? Tumekosa nini?
Hii aibu ya kuomba inayofanywa na mzee Matonya na aibu ya nchi yenye neema kuendelea kuomba itatufikisha wapi ambako wenzetu wanazidi kwenda mbele kiuchumi sisi tunategemea kuomba?
Yupi bora, Matonya au Serikali na kama adha ya kuomba inawakera wananchi wanapomuona mzee huyo akihama huku na kule kufanya shughuli hiyo ni namna gani nchi wahisani zinavyoisema vibaya Tanzania inayoshindwa kutumia vyema rasilimali zake?
Umefika wakati ambao inatisha kusikia kuwa serikali ipo tayari kukopa benki na hilo halijalishi nchi wahisani zinapopunguza misaada kwenye bajeti ya serikali ya mwaka 2010/2011 na maneno yanayotolewa na serikali huko ni kujikaza kiume.
Muda wa kuendelea kumshangaa mzee Matonya umechukua miaka mingi huku tukishuhudia raslimali za nchi kama zingetumika vizuri watu kama akina Matonya wasingekuwepo kwa wingi.
Malalamiko kutoka kwa wafanyakazi yasingekuwepo kwa kuwa kila mtu angeweza kupata kipato cha kutosha kutokana na rasilimali zetu, wakulima na wafugaji wasingeweza kuzuiwa kuuza mazao yao, sasa wanalia kila mtu anaomba.
Kama kuomba ni aibu, basi tusimsakame vibaya mzee Matonya kwa kuwa hata serikali nayo inajiendesha kwa kuomba fedha kwenye mabenki na nchi wahisani.
Ili tuweze kuondokana na aibu hii, tujibu maswali ya Waziri Mkuu Pinda, hivi ni nani kawaroga Watanzania? Tumelaaniwa na nani, nchi haiendi, rasilimali tele, tumekosa nini ?