Tusijisahau Ukimwi bado unamaliza kizazi

DustBin

JF-Expert Member
Jun 3, 2021
544
558
Historia inatuonesha kuwa ugonjwa wa UKIMWI uliingia katika nchi yetu mnamo mwishoni mwa miaka ya themanini na kushamiri mwanzoni mwa miaka ya tisini. Kipindi hicho ugonjwa huo ulikua ni hatari sana na tishio kubwa, ulipukutisha watu wengi mno ndani ya nchi yetu na dunia kwa ujumla. Ukimwi ni ugojwa unaosababishwa na virusi, mpaka hivi sasa ugonjwa huo hauna dawa, tiba wala chanjo. Zaidi ni njia tu za kujikinga zinapendekezwa ili mtu aweze kujiepusha na kupatwa na virusi hivyo.

Kadri miaka ilivyozidi kuyoyoma wataalamu wa mambo ya tiba kimataifa wakawa wanajaribu kupata ufumbuzi wa ugonjwa huo hatari ambao njia kuu inayotajwa ya maambukizi ni kitendo cha kujamiiana. Ingawa kuna njia zingine za maambukizi kama vile kuchangia vifaa vya kutogea, maambukizi ya mama mjamzito kwa mtoto aliye tumboni, mtu kupewa damu ya mtu aliyeathirika nk, lakini kwa kiasi kikubwa waathirika wengi wa ugonjwa huu wameupata kwa njia ya ngono/kujamiiana. Hali iliyopelekea watu kukata shauri kwa kila aliyepata Ukimwi basi kaupata kwa njia hiyo na si vinginevyo.

Miongoni mwa mambo ambayo wanatiba wetu wamefanikiwa katika tafiti zao ni kuvumbua dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV’s), wengine huziita dawa za kuongeza siku. Tangu dawa hizo zimevumbuliwa taharuki na ile hali ya kutisha kwa ugonjwa huu imepungua. Watu hawana hofu tena hasa wakiona watu ambao wanatumia dawa hizo wanaendelea kuishi kwa miaka mingi tu pasi na kutetereka. Leo hii idadi ya waathirika tunaoishi nao ni wengi mno kwa sababu watu hawaogopi tena. Ingawa tunaweza kusema hayo ni mafanikio, kwani tungeweza kupoteza nguvu kazi kubwa ya taifa kama hizo dawa zisingepatikana lakini kwa upande mwingine dawa hizi zimeongeza tatizo kwa kuzidisha idadi ya waathirika.

Hali ilivyo hivi sasa watu wamejisahau na kujisahaulisha kwa hiyari kana kwamba ugonjwa huo haupo. Watu hawajali na wala hawana mpango wa kuchukua tahadhari. Kujisahaulisha huku kumeongeza wimbi la waathirika. Kuna siku niliwahi kupita kwenye hospitali moja ya Wilaya, pasi na kutegemea nikapitishwa kwenye idara inayosimamia masuala ya ugawaji wa dawa hizo. Nilistaajabu kuona kundi kubwa la watu wakiwa wanasubiri kugaiwa dawa zao, wengi wao wakiwa wanawake. Hao ni wale waliojiandikisha kwenye vituo maalumu, lakini wapo ambao hawajajiandikisha wapo tu mtaani na wanazidi kuueneza kwa wengine.

Vifo vingi vya ghafla tunavyovisikia baadhi ya vifo hivyo hutokana na waathirika wa Ukimwi ambao hawafuati kanuni za matumizi sahihi ya dawa au hawaendi kliniki kupata huduma ya matumizi ya dawa hizo. Bali wataalamu wa maswala ya tiba wanatueleza kwamba hata huu ugonjwa mgeni ambao ni tishio kwa dunia nzima hivi sasa, ugonjwa wa Covid19, una athari kubwa sana kwa waathirika wa Ukimwi. Kwani mwathirika wa Ukimwi hana kinga mwilini dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Hitimisho:
Sio kama nawatisha, au naleta taharuki hapana! Nawaeleza ukweli kwamba Ukimwi bado upo na unaendelea kuua watu wazee kwa vijana, hivyo tusijisahau tukadharau kujikinga na kuchukua tahadhari. Dunia bado ipo kwenye vita dhidi ya Ukimwi, na mapambano yanaendelea. Wakati tukihangaika na shuguli zetu za kila siku tukae tukijua juwa Ukimwi bado upon a waathirika wa Ukimwi wapo wengi lakini hatuwezi kuwatambua kwa kuwaangali kwa macho. Kinga dhidi ya Ukimwi inaanza na wewe mwenyewe, chukua hatua okoa kizazi.

DustBin
 
Duh... Kweli UKIMWI haina deal sikuhizi, baada ya miezi 8 toka Uzi ubandikwe ndo watu wanacomment.
 
Siwezi kwenda field kwenye hili nautuliza tu mdudu wangu sitaki mengi..😂
Ukimwi ungekuwepo tungeona gari za WHO zikirandaranda mtaani zikiwa na mabango makubwa ya HIV/AIDS..

Umewahi kuona sehemu zenye ebora mambo yanavyochukuliwa serious?
 
Nyie mnaopinga kutowepo UKIMWI endeleeni. Tutakuja kusema "Kosa la marehemu........"
 
Back
Top Bottom