Tunduru: Asilimia 40 ya mazao yanaozea shambani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunduru: Asilimia 40 ya mazao yanaozea shambani

Discussion in 'Biashara, Uchumi na Ujasiriamali' started by kilimasera, Jan 7, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Jan 7, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  TUNDURU ni moja Wilaya nne za Mkoa wa Ruvuma, lakini yenyewe inasifika zaidi kwa shida ya usafiri na kwa uchache wa usikivu wa vyombo vya redio na televisheni.

  Wilaya hiyo imejaa eneo kubwa linalofaa kuishi, kilimo na hata kufanya biashara, lakini ni sehemu ndogo tu inayotumika. Kwa mfano, inalo eneo la hekta 914,030 zinazofaa kwa kilimo, lakini mpaka sasa zinazolimwa ni 101,214 tu na wala haina wawekezaji wakubwa wa kilimo. Wakazi wake kwa sasa wanafikia karibu 300,000 ambao asilimia 95 kati yao wanajishughulisha na kilimo.

  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ephraem Ole-Nguyaine anasema wilaya yake imesheheni utajiri wa ardhi, misitu, wanyamapori na hata maeneo ya kilimo cha umwagiliaji, lakini kero ni mawasiliano.

  “Usikivu wa redio huku ni matatizo kwani hata redio ya Taifa, TBC, haisikiki vizuri na mara nyingi redio ya nchi jirani ya Msumbiji ndiyo inayotuburudisha,” anasema.

  Nguyaine anasema Tunduru imesheheni kila aina ya neema, lakini kikwazo ni mawasiliano ya barabara na upatikanaji wa taarifa za habari za nchini na dunia kwa ujumla. “Gazeti la Mwananchi wanalipenda sana watu, lakini zinafika nakala tano baada ya siku mbili,” anasema na kuongeza: “Magezeti mengine hayafiki mpaka siku tano zipite.”

  Anasema wakazi wa wilaya yake ni wakulima wazuri wa korosho, ufuta, tumbaku na kwa msimu wa mwaka 2009/10 walivuka malengo ya uzalishaji hadi kufikia asilimia 131. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mazao hayo yanaishia kuoza.

  Anasema licha ya wakazi wake kuwa mstari wa mbele katika masuala ya maendeleo hususan ujenzi wa shule za msingi na sekondari, usafiri unasababisha walimu wengi kushindwa kufika huko hata baada ya kupangwa. Kwa sasa wilaya ina upungufu wa walimu 158 wa sekondari.

  “Mawasiliano mabaya yamesababisha wilaya iwe na upungufu wa wafanyakazi wa sekta afya hiyo 436 kati ya 606 wanaohitajika.” Mpaka sasa haina madaktari wa meno, mkemia na mfamasia jambo linalotia shaka jinsi wanavyotibiwa wenye matatizo hayo.

  Pia ina upungufu mkubwa wa wafanyakazi wa sekta ya afya kutokana na wengi wao kushindwa kufika huko kwa madai ya ugumu wa kufika huko. Wilaya ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,455.92 zikiwemo kilometa 398.3 za kiwango cha changarawe na nyingine zote ni za udongo.

  Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Madaha anasema Tunduru ni moja ya wilaya zenye utajiri wa asili, lakini imefunikwa na matatizo ya usafiri.

  “Wakazi wa wilaya, viongozi wa vyama vya siasa na serikali wilayani humu wote wanashirikiana vizuri kuhakikisha maendeleo yanapatikana, lakini kwa miaka mingi usafiri umekwamisha mafanikio ya wananchi,” anafafanua.

  Madaha anasema wananchi wanalima mazao mengi na karibu asilimia 40 yanaoza bila kutumiwa wala kuuzwa kutokana na kukosa soko kutokana na ubovu wa mawasiliano.
  Anasema kila msimu wa mvua unapofika wakazi wa Wilaya ya Tunduru wanapunguza safari zisizo za lazima kwenda mjini Songea ambako ni makao makuu ya mkoa wao kutokana na kero ya usafiri.

  Sababu za kupunguza safari ni kutokana na kero ya barabara ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikisababisha magari mengi kukwama. Tunduru ipo umbali wa zaidi ya Kilometa 200 kusini mashariki mwa mkoa huo. Barabara kubwa zinazoingia kwenye wilaya hiyo ni za kutoka Songea na nyingine Masasi.

  Hata hivyo, Madaha anatoa neno la matumaini, anasema baada ya kitambo kidogo wakazi wa wilaya yake wataona mwanga. Anasema serikali imetangaza neema ya kujenga barabara za lami kuanzia Namtumbo hadi Tunduru ambayo itapitiliza kwenda mkoani Mtwara.

  Anawaalika Watanzania kufika Tunduru kuwekeza katika kilimo, viwanda kutokana na ukweli kwamba ujenzi wa barabara za ukanda wa Mtwara hadi Mbambabay unaanza.
   
 2. M

  Malila JF-Expert Member

  #2
  Jan 7, 2011
  Joined: Dec 22, 2007
  Messages: 4,410
  Likes Received: 733
  Trophy Points: 280
  Mkuu asante sana kwa taarifa hii, je unaweza kutupa majina ya wanyama wa kufugwa waliopo Tunduru? Ktk orodha ya masuala ya kilimo,umetaja mazao tu na misitu. Hujataja kiwango cha mvua kwa mwaka, yaani kuna misimu mingapi ya kilimo kwa mwaka. Je hao wakuu wako tayari kutoa ushirikiano kwa wazawa ili wawekeze huko bila mizengwe?

  Asante, nitatembelea Tunduru,
   
Loading...