Tunduma: Madiwani wamwomba DC msamaha, watengua kauli na msimamo wa kutoshirikiana na naye

Hivi punde

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
2,554
8,551
madiwani.jpg

Baada ya miezi takriban saba ya mgogoro wa kimamlaka na kiutendaji kati ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando, madiwani hao wameomba radhi na kutengua kauli na msimamo wa kutoshirikiana na kiongozi huyo.

Mgogoro huo uliibuka Agosti mwaka jana baada ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Mwafongo (Chadema) kutangaza msimamo wa madiwani wote katika mkutano wa hadhara kuondoa ushirikiano na Irando kwa kile walichodai hawana imani naye.

Irando alijibu mapigo kwa kufuta vikao vyote vya madiwani na alitoa amri kwa watumishi wa Serikali katika mji huo kuanzia maofisa watendaji wa mitaa, kata na halmashauri kutopokea amri yoyote kutoka kwa madiwani hao.

Kutokana na hilo, madiwani walianza harakati za kutafuta suluhu kwa kuupeleka mgogoro huo Serikali Kuu ambako Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo aliwataka kumwomba radhi mkuu huyo wa wilaya.

Ingawa Waziri Jafo hakupatika alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, juzi katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwaka mjini Tunduma, Mwafongo alisema baada ya kupeleka mgogoro huo kwa waziri mwenye dhamana ili kutafuta suluhu, waliamriwa kurudi kwa wananchi kumuomba radhi mkuu wa wilaya kupitia mkutano wa hadhara kama walivyofanya wakati wakitangaza kuondoa ushirikiano wao kwake.

“Mtakumbuka sisi madiwani wa Mji wa Tunduma hatuna ushirikiano na mkuu wa wilaya, lakini pia na watumishi wa halmashauri yetu. Kwa kutafakari na kwa ushauri wa mheshimiwa waziri (Jafo) na kwa kuliona hili kwamba si la msingi… pia linawaathiri wananchi wa mji wa Tunduma, hawapati huduma za kimaendeleo kwa sababu tu wachaguliwa wao tupo pembeni, hatushirikiani na watumishi wa halmashauri.

Kauli yangu si zaidi ya maendeleo ya wananchi wa Tunduma, si zaidi ya wananchi walionichagua. Hivyo basi narudia kauli yangu ambayo nimekuwa nikiisema kwenye mikutano ya hadhara kwamba natengua kauli yangu niliyoisema hapa mwaka jana ya kutompa ushirikiano mkuu wa Wilaya ya Momba na kuanzia leo tutampa ushirikiano wa kutosha mheshimiwa DC kama mkuu wa wilaya lakini kama Serikali Kuu na nikiri pale nilipomkwaza basi anisamehe na aelewe nilimkwaza kwa misingi ya utendaji wa kazi,” alisema Mwafongo.

Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka aliwaambia wananchi kuwa hakuna kazi yoyote ya maendeleo inayoweza kutekelezeka bila ya viongozi wa kisiasa kwa maana ya wenyeviti wa Serikali za mitaa, madiwani na wabunge hawatakuwepo na kufanya kazi, hivyo ni lazima washirikiane baina yao na mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na Rais John John Magufuli.

Alisema, “Siku zote tunasema mji wa Tunduma ni zaidi ya kitu chochote kile, mimi mbunge na madiwani wote tumewaita mahali hapa ili tuseme, na tunasema kwa sababu tuliyasema sisi wenyewe, lakini tuliyasema kwenu na ndio maana tumekuja kuyasema tena kwenu, hivyo tunaomba mtuelewe nini tunachomaanisha kwa masilahi mapana ya mji wa Tunduma. Tunasema kwenu lakini tukitoka hapa litaitishwa baraza la madiwani ambako pia tutatoa kauli hii ya kuomba radhi.”

Mwakajoka alisema wataendelea kumheshimu Irando kama mkuu wa wilaya ambaye yupo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, huku akisisitiza kwamba jambo la msingi ni kila mmoja kufanya kazi kwa kufuata misingi na kuzingatia mipaka yake ya kiutendaji.

Alisema kwa muda ambao madiwani wamekuwa nje bila kushirikiana na watumishi wa Serikali na mkuu huyo wa wilaya, wananchi wamekuwa katika wakati mgumu kwa kuwa mambo mengi yalikwama.

Mwakajoka alisema wameona ni busara kufuata ushauri wa Waziri Jafo kurudi kwao na kuwatangazia kwamba wametengua kauli dhidi ya Irando ili waweze kusukuma gurudumu la maendeleo.

Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Irando alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa hana taarifa kamili kutoka kwa vyanzo vyake kujua walichozungumza madiwani.

“Nimesikia wamefanya mkutano wakilenga kuzungumzia suala hilo, lakini kimsingi siwezi kuwa na kauli yoyote kwa sababu bado sijajua walichozungumza, hivyo nisubiri hadi nitakapopata kauli zao kutoka kwa vyanzo vyangu nilivyovituma kufuatilia mkutano ule ndipo nitakapokuwa na cha kusema,” alisema Irando.

Chanzo: Mwananchi
 
Utawala wa kibabe hautatufanya sisi wananchi kuipenda ccm bali ndiyo tunazidi kuichukia pamoja na Serikali yake
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom