Tundu Lissu rudi nyumbani, Rais Magufuli yupo tayari kutimiza ahadi yake

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,883
TUNDU LISU RUDI NYUMBANI, RAIS MAGUFULI ATIMIZE AHADI YAKE.

Na, Robert Heriel

Sisi wote ni wanadamu, kila mmoja anamapungufu yake ambayo anahangaika kuyaweka sawa ili tuwe wakamilifu. Hatuwezi kuwa na tabia zile zile mbaya zinazowaumiza wengine, ni lazima tuziondoe ili kulifanya taifa hili kuwa sehemu salama.

Hatuwezi kuendekeza jeuri na viburi vyetu vya uzima ambavyo kimsingi havitusaidii, ni wakati wa kujishusha, kujinyenyekeza kabla mwenye nguvu hajatunyenyekeza. Licha ya kuwa tuna sifa na hadhi tofauti, lakini haiondoi ukweli kuwa sisi ni sawa mbele za Mungu.

Nichukue nafasi hii kumuomba Lisu arudi nchini, nakuomba Tundu Lisu Rudi nchini tuijenge nchi yetu, pengine huenda tumekukosea, pengine huenda tumekuumiza, pengine huenda tumeufanya moyo wako umejawa na uchungu mwingi ndani ya nafsi yako. Sisi ni ndugu zako, haijalishi tumekosana kwa kiasi kipi, haijalishi tumejeruhiana mioyo yetu, akili zetu na miili yetu kwa kiasi kipi. Tunaomba utusamehe ikiwa ndivyo ilivyo.

Sisi ni binadamu, tunaweza kukosea kwa tamaa zetu, au kiburi chetu, au hata kujigeuza miungu.

Sisi kama ulitukosea, tumeshakusamehe, Rudi Nyumbani, huna haja ya kutanga tanga huko duniani.

Ikiwa wewe ni Mtu wa Dini, basi utafahamu kisa cha Nabii Yusufu na nduguze kumi na Moja, walivyotaka kumuua, lakini kwa nasibu na rehema za Mungu wakimuuza kwa Waishmael kisha baadaye akauzwa Misri kama Mtumwa, Baadaye Mungu akambariki na kumstawisha sana mpaka akawa sehemu ya watoa maamuzi wenye mamlaka katika nchi ya Misri, Mwishowe aliwasamehe ndugu zake licha ya kutaka kumuua na kumuuza.

Sasa huenda sisi ndugu zako watanzania tukawa mfano wa ndugu za Yusuph, nakusihi ufungue moyo wako kutusamehe Urudi Nyumbani tuijenge nchi. Kiukweli hatufurahii unayoyafanya huko, bila shaka nawe hufurahii mambo hayo.

Nawe Mhe. Rais, nakuomba uwe kama Baba kwa kijana wake, kwa vile wewe ni mtu wa dini pia, bila shaka unafahamu kisa cha Mwana Mpotevu katika kitabu cha Luka 15. Fungua moyo wako, haijalishi amekukosea au umemkosea, huo ni ubinadamu, lakini umungu ni kusameheana, mchukulie kama Mwana mpotevu.

Kwa bahati nzuri Mhe,. Rais kwenye kampeni zake alishasema kuwa yupo tayari kumpokea Tundu Lisu na kumpa kazi alitumikie taifa. Bila shaka Rais alikuwa anamaanisha kile alichokuwa akikisema. Sasa ni muda wa Lisu kurudi nyumbani, kumalizana katika yale anayoona tumemkosea nasi ametukosea.

Ninachoomba ni kuwa Tundu Lisu asiwe kama mwana Mkaidi akashupaza shingo kwa Kiburi cha Uzima. Arudi ajinyenyekeze kama Rais Magufuli alivyojinyenyekeza kwa kumuambia atampa kazi ndogo ya kufanya,

Rais Magufuli kusema hivyo sio kwamba hana watu wengine wa kuwapa cheo lakini ni dalili ya kuonyesha unyenyekevu kwa Tundu Lisu na kuhisi vile Lisu anavyohisi.

Nafahamu wapo watu watakaoumia na kurudi kwa Tundu Lissu na kupewa cheo na Mhe. Rais, wapo watakaokuwa kama yule mwana wa nyumbani aliyemuonea wivu mdogo wake(mwana mpotevu) kwa kufanyiwa sherehe ya kufa mtu na Baba yake.

Nafahamu wapo ambao watajisikia vibaya wakimuona Magufuli akimteua Lisu wakati wao wamekitumikia chama siku nenda Rudi. Hiyo haitaondoa ukweli kuwa, siku Lisu na Magufuli watakapo kutana na kuyajenga itakuwa siku kubwa sana ndani ya taifa hili.

Naomba Tundu Lisu, au watu wa karibu yake waanze mchakato wa kumsihi Lisu aache ukaidi, wamtafute Mhe. Rais wayamalize, kisha Lisu arudi nchini aendelee na ujenzi wa nchi.

Pia namuomba Mhe. Rais, awe kama yule Baba kwenye kisa cha mwana mpotevu ambaye kila ilipofika jioni alikuwa akisimama nje ya njia kuona kama mwanaye anarudi, au jinsi yule Baba alivyokuwa akituma watu kwenda miji ya mbali kumtafuta mwanaye.

Lisu acha ukaidi, Siasa za uchaguzi ulizifanya kwa kiwango chako na uelewa wako na uwezo wako. Uliyokosea tumekusamehe, waliyokukosea nawe wasamehe.

Samehe nafasi ikiwepo, usisubiri nafasi ikiwa haipo.

Tundu Lisu Rudi nchini, Mhe Rais Atimize ahadi yake. Ujeuri, kiburi na ukaidi havitasaidia.

Hata usipopewa cheo usije umia lakini tunakuhitaji nyumbani.

Nimalize kwa kusema, Heri waliowapatanishi kwa maana hao watamuona MUNGU.
Wale mnaopenda mifarakano mjue wazi kuwa haitasaidia kwa lolote lile.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar esa salaam
 
Nichukue nafasi hii kumuomba Lisu arudi nchini, nakuomba Tundu Lisu Rudi nchini tuijenge nchi yetu, pengine huenda tumekukosea, pengine huenda tumekuumiza, pengine huenda tumeufanya moyo wako umejawa na uchungu mwingi ndani ya nafsi yako. Sisi ni ndugu zako, haijalishi tumekosana kwa kiasi kipi, haijalishi tumejeruhiana mioyo yetu, akili zetu na miili yetu kwa kiasi kipi. Tunaomba utusamehe ikiwa ndivyo ilivyo.

Hii aya yako hii imebeba mengi sana ila hapo mwishoni uliposema "ikiwa ndivyo ilivyo" umeonyesha kiwango kikubwa sana cha unafiki. Ukweli unaujua ila unafiki umekufanya uone kama sio sehemu ya hayo yanayosemwa na yaliyotendwa.
 
Haa! Inawezekana kila mtu ana bei yake hivyo inaaminika.Lakini sidhani kwa Lissu its even near to possible kwa risasi zile na kutembea katika uvuli wa mauti kule, sijui

Akiwa na Roho wa Mungu anasamehe, kama walivyofanya kina Stefano waliopigwa mawe mpaka kufa, hapo ni ishu ya kiroho zaidi.
 
Muache mzee wa watu apumzike ana haki ya kuchagua kuwa raia wa nchi yoyote endapo itampendeza.
 
Mbona hiyo sentensi ipo sawa kabisa,
Sijasema haiko sawa kiongozi. Soma katikatibl ya hekima na maono. Umeonyesha hayo yanayolalamikiwa na Lissu ikiwa hata kuumizwa kwa risasi wewe unaona kama huna uhakika. Ndomaana ukaandika hivyo.
 
Sijasema haiko sawa kiongozi. Soma katikatibl ya hekima na maono. Umeonyesha hayo yanayolalamikiwa na Lissu ikiwa hata kuumizwa kwa risasi wewe unaona kama huna uhakika. Ndomaana ukaandika hivyo.

Sasa mimi nina uhakika?
Uhakika nilionao kila mtu anao, ambao ni kuwa Lisu kapigwa Risasi.
Lakini waliompiga ndio siwajui hata yeye mwenyewe hawajui labda kukisia tuu ambapo hata wewe na mimi tunaweza kukisia.
Sasa huoni uhalali wa sentensi hiyo?
 
Hata mtawala havimsaidii badala yake vinaongeza chuki, visasi na kufanya ile sifa tukufu ya upendo kwa watanzania ipukutike kama umande wa asubuhi katikati ya miale ya jua.
Wote wanahusika, iwe ni Lisu au Magufuli.

Utata ninaouona kwa Lisu ni kuona anataka kuleta ukaidi, kiburi na ujeuri wa uzima usio na maana yoyote.

Kipindi kile Magufuli alimwambia kuwa atampa kakazi kadogo, Lisu ulimsikia alijibuje?
 
Sasa mimi nina uhakika?
Uhakika nilionao kila mtu anao, ambao ni kuwa Lisu kapigwa Risasi.
Lakini waliompiga ndio siwajui hata yeye mwenyewe hawajui labda kukisia tuu ambapo hata wewe na mimi tunaweza kukisia.
Sasa huoni uhalali wa sentensi hiyo?
Robert Brother hii kitu umeandika mwenyewe. Baada ya kueleza hayo yoooote mwishoni ukaandika "Tunaomba Utusamehe ikiwa ndivyo ilivyo". Unamaananisha atusamehe kama hayo uliyosema kweli ndivyo yalivyo.

So kwamaaelezo yako nikwamba huna hata uhakika kama anapitia maumivu au alipigwa risasi. Broo shule yangu ndogo ila najua jua kuangalia angalia mambo.
 
Wote wanahusika, iwe ni Lisu au Magufuli
Utata ninaouona kwa Lisu ni kuona anataka kuleta ukaidi, kiburi na ujeuri wa uzima usio na maana yoyote.
Kipindi kile Magufuli alimwambia kuwa atampa kakazi kadogo, Lisu ulimsikia alijibuje?
Umeandika vyema. Ila umeonaje penye Lissu ujaribu kuweka Magufuli bila kuathiri maana ya maneno yako kwenye aya ya kwanza. Kisha vaa uhusika. Kuna tofauti kubwa sana kati ya Tanganyika na Zanzibar Robert.
 
Robert Brother hii kitu umeandika mwenyewe. Baada ya kueleza hayo yoooote mwishoni ukaandika "Tunaomba Utusamehe ikiwa ndivyo ilivyo". Unamaananisha atusamehe kama hayo uliyosema kweli ndivyo yalivyo. So kwamaaelezo yako nikwamba huna hata uhakika kama anapitia maumivu au alipigwa risasi. Broo shule yangu ndogo ila najua jua kuangalia angalia mambo.

Mkuu, wakati mwingine msamaha unaweza kuombwa hata kama hujui aliyefanya kosa, ili mradi kosa limefanyika katika mazingira yanayotuzunguka. Na ndio maana nikasema hayo
 
Back
Top Bottom