Tundu Lissu: Niliposhambuliwa walisema nimeshambuliwa na waliotumwa na Mbowe sababu ya kugombea madaraka ya chama

KAULI YA MAKAMU MWENYEKITI WA CHADEMA, MH. TUNDU AM LISSU, KUHUSU KUSHAMBULIWA KWA MWENYEKITI WA CHADEMA, MH. FREEMAN AIKAELI MBOWE

Usiku wa kuamkia jana tarehe 9 Juni 2020, majira ya saa saba usiku, watu watatu wasiojulikana walimvamia, kumshambulia na kumuumiza vibaya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Aikaeli Mbowe, nyumbani kwake katika eneo la Sengia, Area D, Dodoma. Taarifa za awali zinaonyesha kwamba Mh. Mbowe amevunjwa sehemu ya kifundo cha mguu wake wa kulia na kuumizwa sehemu nyingine za mwili. Watu waliomshambulia walikimbia na kutokomea gizani.

Shambulio hili ni mfululizo wa mashambulizi dhidi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA ambayo yamekithiri sana katika utawala wa Rais John Pombe Magufuli. Ni shambulio la pili dhidi ya kiongozi wa juu wa CHADEMA kufanywa katika mazingira yanayofanana. Tarehe 7 Septemba, 2017, mimi mwenyewe nilishambuliwa kwa risasi nyingi katika eneo hilo hilo la Area D. Kama ilivyokuwa kwangu, Mwenyekiti Mbowe naye ameshambuliwa nje ya makazi yake ndani ya eneo la nyumba za viongozi mjini Dodoma. Kama ilivyokuwa kwangu, eneo hilo pia lina ulinzi mkali na wa muda wote. Na kama ilivyokuwa kwangu, walinzi wote waliondolewa kwenye lindo lao, mara hii kwa kisingizio cha kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kwa mara nyingine tena, Serikali ya Rais Magufuli na vyombo vyake vya usalama, hasa Jeshi la Polisi, inatuasa tuwe watulivu wakati vyombo vya usalama vinafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti Mbowe. Hatuwezi kuwa watulivu tena. Kwa sababu, sasa umekuwa ni utamaduni wa kawaida wa Tanzania ya Magufuli, wa kuwafanyia wapinzani wa serikali vitendo vibaya vya kihalifu, halafu kuwazuga na kuwatuliza wananchi na dunia kwa ahadi za vyombo vya usalama kufanya uchunguzi.

Ndivyo tulivyoambiwa mwaka 2017 kufuatia kushambuliwa kwangu. Wakati ule, Jeshi la Polisi liliahidi kuchunguza kwa kina mazingira yote ya kushambuliwa kwangu. Hadi leo Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote ya uchunguzi wake huo, kama kweli ulifanyika. Hadi leo Jeshi la Polisi halina mshukiwa, mtuhumiwa wala mshitakiwa wa shambulio lile. Wakati ule, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Job Yustino Ndugai aliielekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake Mh. Adadi Rajabu, kufanya uchunguzi wa kina wa mazingira yote ya kushambuliwa kwangu. Kamati hiyo haijawahi kutoa taarifa yoyote ya uchunguzi wake, kama kweli ulifanyika, au kusema kwa nini taarifa hiyo haijatolewa hadi leo.

Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliposhambuliwa kwa risasi katikati ya Mkutano wa kawaida wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza, katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Azam, kwamba tukio la aina hiyo lilikuwa la kipekee na halitarudia tena kwa sababu taratibu zote za kiusalama zimekwishachukuliwa kuhakikisha halitokei tena. Sasa, katika Mkutano wa Bunge la Bajeti na kuelekea mwisho wa maisha ya Bunge la 11, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ameshambuliwa na kuvunjwa mguu.

Hatuwezi kuwa watulivu tena kwa sababu nyingine. Kauli za kuwadharau na kuwakejeli waliofanyiwa uhalifu, kwa lengo la kuhamisha mjadala wa matukio haya ya kihalifu na kuyafanya yaonekane kama matukio ya uhalifu wa kawaida, au yasiyostahili kupewa uzito wowote, zimeanza kutolewa tena. Niliposhambuliwa mimi tulisikia kauli za viongozi na watendaji wa serikali kwamba nilijishambulia mwenyewe ; au nilishambuliwa na watu waliotumwa na Mh. Mbowe kwa sababu ya kugombania madaraka ndani ya chama. Baadae viongozi na watendaji hawa walihamisha mjadala na ikawa uchunguzi hauwezi kufanyika kwa sababu CHADEMA imemtorosha dereva wangu na mimi mwenyewe nimekimbia kesi, n.k.

Lakini sio kesi ya kushambuliwa kwangu tu. Serikali ya Rais Magufuli na vyombo vyake vya usalama imeingiza utamaduni mbaya na wa hatari wa kuwalaumu wahanga wa vitendo vyake vya kihalifu.

Ben Saanane alipotekwa nyara na kupotezwa mwezi Novemba mwaka 2016, viongozi na watendaji wa serikali walisema hadharani kwamba amejiteka nyara mwenyewe au amekimbilia nchi jirani. Hadi sasa hivi Ben Saanane hajulikani alipo na serikali hii na vyombo vyake vya usalama havijawahi kutoa taarifa yoyote ya uchunguzi wa tukio hilo la utekaji nyara. Na Jeshi la Polisi halina mshukiwa, mtuhumiwa wala mshitakiwa katika suala hili.

Mwandishi habari Azory Gwanda alipotekwa nyara na kupotezwa miezi michache baadae viongozi na watendaji wa serikali walisema hadharani kwamba amejiteka nyara mwenyewe au amehamia nchi jirani. Baadae Waziri wa Katiba na Sheria akakiri kwenye mahojiano na BBC kwamba ameuawa kama walivyouawa mamia ya wananchi wengine wa maeneo ya Kibiti, Mkuranga, Kilwa na Rufiji. Hadi leo hii Azory Gwanda hajulikani alipo, na wala hakuna taarifa yoyote ya uchunguzi ambayo imewahi kutolewa na serikali na Jeshi la Polisi juu ya kupotea kwake. Na Jeshi la Polisi halina mshukiwa, wala mtuhumiwa wala mshitakiwa katika kutekwa nyara na kupotezwa kwa Azory Gwanda.

Kiongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Abdul Nondo alipotekwa nyara, kuteswa na baadae kutupwa maeneo ya Mafinga mkoani Iringa, hadithi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Magufuli ilikuwa ile ile ya Ben Saanane na Azory Gwanda: amejiteka nyara mwenyewe na kujipeleka hadi kwa mchumba wake. Na Jeshi la Polisi sio tu lilimshtaki mahakamani kwa kutoa taarifa ya uongo polisi, bali pia lilitafuta hata mwanamke wa kuja kutoa ushahidi mahakamani kwamba Abdul Nondo alikuwa amejipeleka mwenyewe Mafinga. Baadae Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Iringa ilitupilia mbali madai hayo ya Abdul Nondo kujiteka mwenyewe. Hata hivyo, hadi leo hii Jeshi la Polisi halina jina la mshukiwa, wala mtuhumiwa wala mshitakiwa katika utekaji nyara wa Abdul Nondo.

Sasa, Mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini ameshambuliwa na kuumizwa vibaya nyumbani kwake, na kauli zile zile za kudharau, kukejeli na kufifisha uzito wa kitendo hicho cha kihalifu vimeanza kutolewa tena. Sasa tunawasikia viongozi na watendaji wa serikali na wapambe wao ndani na nje ya Bunge wakitoa kauli kwamba Mh. Mbowe hakushambuliwa bali ameanguka mwenyewe kwa sababu alikuwa amelewa. Mara wanahoji kwamba alikuwa wapi na anafanya nini usiku wa manane hadi ashambuliwe. Mara kwa nini alikuwa anatembea peke yake bila kuwa na mlinzi binafsi.

Kunywa pombe ama kulewa sio kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania na wala halihalalishi mashambulizi dhidi ya mtu yeyote. Aidha, hakuna tangazo lolote la hali ya hatari linalokataza mtu yeyote kutembea usiku. Kauli hizi ni maandalizi ya kuhalalisha vitendo hivi vya kihalifu ; au kuvififisha uzito wake. Haya ni maandalizi ya kuhalalisha Jeshi la Polisi kutofanya uchunguzi wowote wa tukio hilo. Tukinyamaza na kusubiri uchunguzi ufanyike hakutakuwa na uchunguzi wowote. Kama kawaida yake, Jeshi la Polisi halina halitakuwa na mshukiwa, wala mtuhumiwa wala mshitakiwa.

Hatuwezi kukaa kimya na kusubiri uchunguzi wa Jeshi la Polisi, ambao tunajua hautafanyika, kwa sababu kumshambuliwa Mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini sio kitendo cha uhalifu wa kigaidi. Kama walivyosema viongozi wa kidini katika tamko lao la kulaani shambulio hili, Mh. Mbowe ameshambuliwa kwa sababu za kisiasa. Kama ilivyosema taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini, hili ni ‘... tukio la hivi karibuni katika mlolongo mrefu wa matukio ya kusikitisha ya utumiaji wa nguvu na unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani.’

Mashambulizi ya kihalifu yanayofanywa dhidi ya raia au viongozi wa kisiasa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ndio tafsiri halisi ya vitendo vya kigaidi kwa mujibu wa sheria zetu zinazohusu mapambano dhidi ya ugaidi. Haijalishi yamefanywa na serikali au mojawapo ya taasisi zake ; au yamefanywa na mtu binafsi au na kikundi cha watu. Ni ugaidi.

Na kama walivyosema wawakilishi wa kibalozi wa nchi 27 wanachama wa Jumuiya ya Ulaya katika taarifa yao ya pamoja kuhusu shambulio hili, ‘kila shambulio dhidi ya mwakilishi wa taasisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kujali msimamo wake wa kisiasa, ni shambulio dhidi ya demokrasia.’

Na hatuwezi kukaa kimya na kusubiri uchunguzi wa Jeshi la Polisi kwa sababu washukiwa wa kwanza na wa wazi wa tukio hili hawajatajwa na, kwa uzoefu wa matukio ya aina hii ya siku za nyuma, hawatatajwa wala kuhojiwa wala hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi yao. Mapema mwezi Februari ya mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya miaka 43 ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mwenyekiti wake, Heri James, aliwahamasisha vijana wa CCM kuwashambulia na kuwadhuru viongozi wa vyama vya upinzani. Mwenyekiti huyo wa UVCCM aliwataja kwa majina yao Mh. Mbowe na Mh. Zitto Kabwe, Mbunge na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo.

Siku hiyo hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Kenan Kihongosi alisema hadharani kwamba eti ‘wale wanaochafua taifa letu wanapaswa kuuawa.’ Kauli za aina hii zilitolewa pia kabla ya jaribio la mauaji dhidi yangu. Lakini, kama ilivyokuwa katika jaribio hilo dhidi yangu, wamasishaji hawa wa uhalifu wa hawatachunguzwa wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria kwa sababu ni viongozi wa CCM.

Vitendo vya aina hii haviwezi kwisha kwa kunyamaziwa na kusubiri muda upite na wananchi wasahau. Hivi ni vitendo ambavyo hujenga chuki na mwisho kusababisha machafuko na mauaji makubwa ya watu wasiokuwa na hatia. Hivi ni vitendo vya kupingwa na kila mtu mwenye nia njema na nchi yetu. Ni vitendo vya kukemewa na kupigiwa kelele

kila mahali dunia nzima ili wale wote wanaovifanya au wanaowatuma kuvifanya wasipate mahali popote pa kujificha. Hii ndio namna pekee ya kuhakikisha havitokei tena.

Kwa hiyo tunawaomba wananchi wote wanaochukizwa na vitendo hivi kuvipigia kelele kila mahali. Tunaziomba taasisi na mashirika ya kiraia na ya kidini kutokunyamaza kimya na kusubiri uchunguzi ambao kila mmoja wetu anajua moyoni mwake kwamba hautafanyika.

Tunatiwa moyo na ukweli kwamba mashirika mbali mbali ya kiraia, taasisi za kidini na wawakilishi wa kidiplomasia wa nchi za nje, wamejitokeza hadharani na kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa Mwenyekiti Mbowe. Tunawaomba waendelee kufanya hivyo.

Tundu AM Lissu (MB) MAKAMU MWENYEKITI Tienen, Ubelgiji
10 Juni 2020
 
Huo msemo wao wanaupenda sana; tuwe watulivu, serikali na bunge wanaungana kuwalaumu waathirika wa matukio ya kihalifu, badala ya kuwatafuta wahalifu wawapeleke mahakamani.

Hii tabia yao ya kujaribu kutunga visababu ili kudhoofisha uhalifu wanaofanyiwa viongozi wa upinzani inaonesha jinsi wasivyojali uhai, utu, na heshima za wanadamu wenzao; kwa kifupi ni wabinafsi kupitiliza.
 
Sasa huyu tindu lissu anatuambie tupige makelele anafikiri sisi tunaakili km zake

Yaani nipige kelele tu huyu lissu amekuwa comedy ya Taifa sasa
 
Jeshi LA polisi mpaka Leo halijazungumza nani waliompiga lisu ,kwa mbowe tutawaaminiji
 
🙄 yaani kabisa MBOWE akatega mguu, piga, vunja kabisa, vunjavunja kabosa kifunda hiki....
Kamwe haiiingii akilini.
Polisi waseme ukweli
Unauhakika kavunjika mgu
Yawezekana kafunga kitambaa cheupe tu.
Msigizo ya futuhi
 
7 Reactions
Reply
Back
Top Bottom