Tundu Lissu: Napasha

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,238
Na Ahmed Rajab

TUNDU Lissu, kama wasemavyo baadhi, ni mfano wa kuigwa. Kadri siku zinavyoendelea ndivyo anavyozidi kuwa alama ya upinzani dhidi ya utawala wa Rais John Magufuli. Amekuwa alama ya upinzani, na kipenzi cha umma, kwa sababu yuko safu ya mbele ya wale wenye kuwakabili watawala bila ya woga kutetea haki na demokrasia.

Lissu ni mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na rais wa zamani wa Tanganyika Law Society (Chama cha Wanasheria Tanganyika). Anajulikana kwa mengi mengine ndani na nje ya Tanzania. Yote ni mazuri kwa wapenda demokrasia, utawala bora, haki na uwajibikaji katika ngazi zote za utawala.

Anasifika kwa ujasiri wake, umahiri wake wa kuwasilisha hoja kuhusu mada mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kimazingira au kisheria. Kwenye sheria ndiko alikobobea.

Masaibu yaliyomfika Lissu katika utawala huu wa awamu ya tano si masaibu ya kawaida kuwakuta wanasiasa wa Tanzania, hasa walio Tanganyika. Ni mepya kabisa na yanawapa nguvu wale wasemao kwamba Tanzania inatawaliwa kimabavu.

Mmojawao ni yeye Tundu Lissu. Ni wazi kwamba mwanasiasa huyo aliyevuliwa ubunge wa Singida Mashariki na Spika Job Ndugai wiki iliyopita amekuwa mwiba wenye kuichoma serikali ya Rais Magufuli na Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala.

Ni wazi pia kwamba serikali na chama chake hawamwezi juu ya mabavu yanayotumiwa dhidi yake. Anawashinda kwa kutumia nguvu ya hoja.

Lissu amekuwa akikamatwa mara kwa mara akituhumiwa, miongoni mwa mingine, kumtukana rais na kuchafua amani. Kamatakamata hiyo haikumyumbisha wala kumyamazisha. Agosti 23, 2017 baada ya nyumba yake kupekuliwa na polisi alikamatwa na akasailiwa kuhusu tuhuma za usaliti na za kumtukana Rais Magufuli kwa kumwita “dikteta uchwara”.

Ilikuwa dhahiri kwamba watawala waliamua kumtia adabu kwani alikamatwa baada ya kufichua siri hadharani ya kwamba ndege moja iliyonunuliwa na Shirika la Ndege la Air Tanzania ilizuiwa Canada kwa sababu ya madeni ya serikali ya Tanzania ambayo hayakuwa yamelipwa.

Maafa makubwa yaliyomfika ni lile shambulio lililodhamiria kumuua alasiri ya Septemba 7, 2017. Wakati huo na siku hiyo “watu wasiojulikana” walimtwanga kwa risasi zilizommiminikia na kumjeruhi vibaya sana akiwa ndani ya gari yake huko Dodoma.


Wiki chache kabla ya shambulio hilo, Lissu alitangaza hadharani kwamba kulikuwa watu waliokuwa wakimfuata kwa wiki kadhaa. Aliwashutumu Inspekta Mkuu wa Polisi Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) Dkt. Modestus Kipilimba ndio waliowatuma watu hao wafanye hivyo.

Mara tu baaada ya kushambuliwa Lissu alipelekwa Hospitali Kuu ya Dodoma na baada ya saa kadhaa alisafirishwa kwa ndege hadi Nairobi, Kenya, alikotibiwa kwa miezi katika Hospitali ya Aga Khan. Baadaye alisafirishwa hadi Ubelgiji kwa matibabu zaidi na ambako alifanyiwa upasuaji si chini ya mara 19.

Hivi sasa sifa za Lissu zimevuka mipaka ya Tanzania. Na hii hatua ya juzi dhidi ya ubunge wake imezidi kumzidishia umaarufu na kumjenga katika serikali na taasisi za nchi kadhaa za Ulaya na Marekani alizoziruru baada ya kupata nafuu.

Katika ziara zake zote hizo amekuwa akizieleza serikali na taasisi zinazohusika juu ya nakisi ya demokrasia nchini Tanzania. Pia amekuwa akihojiwa na vyombo vikuu vya habari vya kimataifa. Kila alipohojiwa alikuwa akiueleza ulimwengu kuhusu kasoro anazoziona katika serikali ya sasa ya Tanzania.

Kampeni hiyo ya Lissu imekuwa ikifua dafu kiasi cha kuwafanya watawala wazidi kukereka naye na wamzushiye mambo yasiyopo. Shutuma moja kubwa anayotuhumiwa nayo ni kwamba yeye ni msaliti, kibaraka wa nchi za Magharibi na yuko kibaruani kuiuza Tanzania.

Shutuma nyingine, tena ya kitoto, ni ile ya wiki iliyopita ya kumkashifu kwa kumhusisha na vitendo ya kishoga alipokuwa uwanja wa ndege wa London. Picha aliyopiga hapo akiwa na Salim Amar, mwenyekiti wa tawi la Chadema la Uingereza, ilifanyiwa usanii kwa kuyaingiza kwenye picha maandishi yaliyoonesha kana kwamba Lissu na mwenzake walikuwa wakihudhuria mkutano wa haki za mashoga.

Tuhuma zote hizo hazikuufanya msimamo wake Lissu uregee. Ukikutana naye unakuwa kama unayekutana na nishati ya aina fulani licha ya kwamba bado anatembea kwa magongo na anachuchumia, ikiwa athari ya zile risasi alizopigwa na “watu wasiojulikana”.

Anapozungumza huchoki kumsikiliza licha ya kwamba anaweza akazungumza kama bomba. Wakati wote unavutiwa na adabu na heshima zake.

Moja ya mambo unayoyatambua baada ya kuwa naye kwa muda mfupi ni kwamba Lissu anazielewa vilivyo siasa za Tanzania na anawaelewa vyema pia mahasimu zake wa kisiasa na njama zao.

Jambo jengine unaloling’amua ni kwamba si wakubwa wote walio upande wa serikali ambao ni maadui zake. Ana marafiki wengi serikalini na ndani ya chama kinachotawala. Sitokuwa natia chumvi nikisema kwamba Lissu ni mwanasiasa anayekubalika hata na baadhi ya wanachama wa CCM wanaopendelea utawala wa kisheria.

Nadhani hiyo ni moja ya sababu zilizomshajiisha afikirie kugombea urais 2020. Lakini amesema kwamba atafanya hivyo pale tu atapopata ridhaa ya chama chake na ya mwenyekiti wao Freeman Mbowe. Lissu anamstahi sana Mbowe na haielekei, kutokana na mazungumzo yake, kwamba ataweza kumkiuka kumgeuka au kumwendea kinyume.

Jumapili iliyopita tulimsaka Lissu jijini Brussels, Ubelgiji, na tulipomnasa tulimuuliza iwapo alishtushwa au kushangazwa na hatua ya Ndugai ya kumtangaza kuwa si mbunge tena.

Tundu Lissu: “Uamuzi wa Spika Ndugai haujanishangaza wala kunishtua hata kidogo. Alikwishatangaza hadharani kwamba atanifutia ubunge wangu. Kati ya Desemba mwaka jana na Machi mwaka huu alinisimamishia mshahara na posho za kibunge na alitangaza hivyo hadharani.

Nilipopiga kelele hadharani kwamba hawezi kusimamisha mshahara na posho zangu wakati mimi ni mbunge akaurudisha mshahara na posho hizo. Baada ya hapo, hakuwa na njia nyingine ya kutokea isipokuwa kunifutia ubunge. Kwa hiyo hakukuwa na siri yoyote kuhusu maamuzi haya.”

Raia Mwema: Kwanini unasema Ndugai ametumwa? Na nani au una ushahidi gani?

Tundu Lissu: “Uamuzi wa Spika Ndugai ni utekelezaji wa maagizo. Wala hakuna siri kwenye jambo hili. Ilikwishazungumzwa hadharani kuhusu sisi wabunge wa upinzani: wafukuze bungeni ili wakose kinga ya kibunge, halafu tutawashughulikia huku nje. Kilichofuata kwa wabunge wa upinzani, hasa sisi wa Chadema, kinajulikana na dunia nzima. Kuhusu mimi binafsi, Spika Ndugai mwenyewe amesema hadharani, na kwa maandishi kwa wakili wangu, kwamba siwezi kulipiwa gharama za matibabu yangu kwa sababu idhini kwa ajili hiyo haijatolewa.”

Raia Mwema: Wiki iliyopita ulikuwa London ukionana na ninaoweza kuwaelezea tu hapa kuwa ni “watu wazito”. Unadhani Ndugai kuchukua hatua hiyo kwa wakati huu ili kukutia adabu na kulipiza kisasi kwa kampeni unayoendelea kuifanya kimataifa dhidi ya watawala ?

Tundu Lissu: “Ni wazi kwamba uamuzi wa Spika Ndugai ni kulipiza kisasi kwa kampeni ya kimataifa ambayo nimeifanya na ninaendelea kuifanya. Kabla ya ziara yangu ya Uingereza, Makao Makuu ya Muungano wa Ulaya (EU) Brussels, Ujerumani na Marekani kati ya Januari na Februari mwaka huu, Spika Ndugai alikuwa hajawahi kunitishia hadharani kunifutia ubunge wangu.

Hawakuwa na shida na mimi wakati nahangaika kujiuguza na kujitunza. Hata hivyo, nilipoanza kuwakabili kwenye uwanja wa kidiplomasia walijawa hofu na kuanza kunitukana kila aina ya tusi na kutishia kunivua ubunge. Juzi ilikuwa ni hitimisho la vitisho vyao.”

Raia Mwema: Unasema unakwenda mahakamani kuipinga hatua ya Ndugai. Una imani hivyo na mahakama na mfumo mzima wa sheria na haki wa Tanzania ya leo?

Tundu Lissu: “Mahakama ya Tanzania imekuwa na rekodi mbaya ya kusimamia haki za binadamu, hasa katika kipindi hiki. Hata hivyo, bado tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi, kama sio kutendewa haki basi ili kuonyesha jinsi ambavyo, katika Tanzania ya leo, hata Mahakama zetu zimeingiliwa na kuvurugwa.

Raia Mwema: Mara kadha wa kadha umeahidi kwamba utarudi nyumbani Septemba mwaka huu. Tukujuavyo, ukirudi hutokaa kimya. Pengine wale “watu wasiojulikana” huenda wasijaribu tena kukuua lakini kuna wengine wenye kujulikana (kama hao waliokuvua ubunge) ambao watakubana usiweze kufurukuta. Pana salama hapo?

Tundu Lissu: “Nitarudi nyumbani September 7, 2019, si kama mfungwa au mhalifu, bali kama raia huru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama raia huru, sitakaa kimya kwenye masuala yote ya nchi yanayohitaji kusemwa hadharani. Nitazungumza kama ambavyo nimezungumza.

Kama 'watu wasiojulikana' na wale wanaojulikana watakubaliana na nitakachosema sijui. Kama watanizuia au la sijui. Siwezi kuwaamulia au kuwasemea. Hilo ni la kwao, si langu.”


Baruapepe: aamahmedrajab@iloud.com; Twitter: @ahmedrajab



IMG-20190703-WA0020.jpeg
IMG-20190703-WA0019.jpeg
 
Tundu lisu Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania 2020-2025 watanzania tunamuombea awe na afya njema jembe letu ili aje apige kazi.
 
Haki haipo hapa duniani.
Pamoja na kwamba misaafu inasema "tuwatii viongozi wa kiserikali" lakini hao viongozi bado itihali ya uongozi na hofu kwa watawaliwa haina ijali kabisa.

Sasa hapa ndg Lissu anarejea na anasema atakomaa kuongea ukweli bila hofu kwa kutegemea 'constitution security' mmmh sidhani, hii ni Africa siyo ubeligiji.

Kama asipowekwa rokapu ya miezi kumi na kitu basi safari yake sijui itakuwaje...

KARIBU BONGOLAND.
 
Tundu Lissu ameshachokwa na wananchi wa Singida hawamtaki, amechakaa , na wanasema asikanyage Singida aishie Dar, hawana haja naye wanasubir ridhaa ya Tume ya uchaguzi wakabidhi jimbo kwa mwingine haraka iwezekanavyo.
 
Kume_pambazuka. .Mambo Yana taradadi

Kila ninapo jaribu kuyaangalia matendo ya wanasiasa.. haswa wa CCM na kuyatazama matendo yangu''

Nina Hakika kabisa Mimi peponi lazima Niingie. Tena muda Malaika watakuwa wametoka kuni safishia Palace Langu
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom