Tundu Lissu atema cheche kuhusu miradi inayoendelea Chato

PNC

JF-Expert Member
Feb 3, 2015
8,107
14,352
CHATO! CHATO! CHATO!

Tundu AM Lissu, MB
Tienen, Ubelgiji

Chato imetamalaki kwenye vichwa vya habari vya magazeti mengi ya Tanzania katika siku za karibuni. Chato imetawala mijadala katika mitandao ya kijamii ya Tanzania. Chato imo midomoni mwa watu wengi wanaofuatilia siasa za Tanzania na hata wasiofuatilia mambo ya siasa.

Chato inatembelewa na Marais na Wakuu wa Nchi; na shughuli za Ikulu, kama dhifa za kitaifa na magwaride ya heshima kwa ajili ya Wakuu hao, sasa zinafanyikia Chato.

Chato ina uwanja wa ndege wenye uwezo wa kutua na kurusha ndege kubwa sawa na viwanja vya ndege vya Dar Es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Mbeya.

Chato ina taa za kuongozea magari barabarani, mojawapo ya miji sita tu nchini yenye maendeleo hayo!!!

Chato ina mpaka Hifadhi yake ya Taifa ya wanyama pori waliobebwa kutoka hifadhi zingine kama Serengeti n.k. Na sasa tunasikia, hata wale tausi wazuri wa Ikulu aliowapewa Baba wa Taifa na marehemu Indira Gandhi, wamehamishiwa Chato na sasa wanagawiwa kama zawadi kwa Wakuu wa Nchi wanaotembelea Chato.

Pamoja na kwamba Chato na Mkoa mzima wa Geita hauna timu ya mpira wa miguu inayojulikana popote, Chato sasa ina mpango wa kujenga uwanja wa michezo wa pili kwa ukubwa nchini; na wa kwanza wa kisasa nchini.

Mabenki ya kibiashara ambayo Serikali ina hisa yanafungua matawi Chato; Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba Chato; Bohari Kuu ya Madawa inajenga bohari kubwa Chato, na Mamlaka ya Mapato Tanzania nayo inafungua ofisi kubwa Chato.

Chato kunani?

Mtandao wa kijamii wa Wikipedia una maelezo kidogo sana kuhusu Chato. Kwa mujibu wa mtandao huo, Chato "ni mji katika Mkoa wa Geita, uliyoko Kaskazini-Magharibi ya Tanzania. Ni kituo cha kiutawala cha Wilaya ya Chato."

Kuhusu Wilaya yenyewe ya Chato, Wikipedia inasema, Chato ni mojawapo ya wilaya tano za Mkoa wa Geita. Kiuchumi, Wikipedia inasema kwamba shughuli kubwa ya kiuchumi ya Wilaya hii ni "...kilimo cha kujikimu (subsistence farming) bila umwagiliaji, kinachotegemea mvua tu."

Juu ya utalii, tunaambiwa na mtandao huu kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo katika Ziwa Victoria ipo nje kidogo ya Wilaya ya Chato. Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1965 na, kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa, mwaka 2012 Hifadhi hiyo ilitembelewa na wageni 748 tu. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) haina takwimu zozote za miaka ya karibuni za wageni waliotembelea hifadhi hiyo.

Nimetumia taarifa za mtandao wa 'kibeberu' wa Wikipedia kwa sababu mitandao ya kizalendo ya Tanzania haina taarifa zozote za maana juu ya Chato. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Chato haina tovuti yake yenyewe. Tovuti iliyopo ni ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, na inazungumzia mambo ya Geita.

Kwa hiyo inabidi nirudi kwa mabeberu wa Wikipedia. Mabeberu hawa wanadai kwamba Wilaya ya Chato ilianzishwa mwaka 2005 kutoka iliyokuwa Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera. Mwaka 2012, Wilaya hiyo ilihamishiwa kwenye Mkoa mpya wa Geita.

Aidha, Wikipedia inaongeza, "John Magufuli aliyechaguliwa kama Rais wa Tanzania mwaka 2015, alizaliwa Chato mwaka 1959." Aha!!! Kumbe Chato ni nyumbani kwa Rais Magufuli!

Sio vibaya nyumbani kwa Rais wa nchi kuwa na maendeleo au mambo mazuri. Na wala sio sifa nyumbani kwa Mkuu wa Nchi kuwa pa hovyo hovyo au duni kimaendeleo.

Umaskini sio kitu cha kujivunia, bali ni mojawapo wa maadui watatu waliotangaziwa vita na Mwalimu Nyerere mara baada ya uhuru.

Suala hapa ni vipaumbele vya nchi na vipaumbele binafsi vya Rais wa nchi. Sio kila kipaumbele cha nchi ni kipaumbele binafsi cha Rais. Vivyo hivyo, sio kila kipaumbele cha Rais wa nchi kinapaswa kuwa kipaumbele cha nchi.

Ijapokuwa sio lazima, mara nyingi vipaumbele binafsi vya Rais vinaweza kuwa kinyume na vipaumbele vya Taifa au vya nchi. Ndio maana Katiba na Sheria hutungwa na mataifa ili kuweka mipaka na kudhibiti mamlaka ya Rais wa nchi. Hii ni katika kuzuia vipaumbele binafsi vya Rais kufanywa kuwa ndio vipaumbele vya Taifa.

Marehemu Samuel John Sitta, Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitumia fedha nyingi za Bunge kujijengea Ofisi ya Mbunge wa Jimbo lake la Urambo Mashariki, ambayo alidai inatakiwa kuwa na hadhi ya Spika wa Bunge.

Alipomwalika Rais Jakaya Kikwete kwenda Urambo kuizindua rasmi Ofisi hiyo, inasemekana Rais Kikwete alimuuliza Spika Sitta: "kama kila Spika ajaye ataamua kujijengea Ofisi kama hii jimboni kwake si nchi itafilisika?"

Kwa kidogo nilichoonyesha kuhusu Chato, ni wazi kwamba Wilaya hii sio yenye umuhimu mkubwa kiuchumi kama, kwa mfano, Wilaya jirani za Geita na Biharamulo. Geita ina Mgodi wa Dhahabu mkubwa kuliko yote katika Afrika nje ya Afrika Kusini na Ghana. Biharamulo ina mapori makubwa ya akiba ya wanyama pori matatu, yaani Burigi, Biharamulo na Kimisi.

Ni ukweli usiopingika kwamba mambo mengi na mazuri yanayofanywa Chato yanatokana na uhusiano wake na Rais Magufuli.

Mambo yote haya yameanza kutengenezwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliomwingiza Rais Magufuli madarakani. Hayakuwepo kwenye vipaumbele vya nchi yetu kabla ya Magufuli kuwa Rais. Ushahidi wa hili upo kwenye Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2011/12 -2016/17 uliotekelezwa chini ya Rais Kikwete.

Ni sawa, kwa hiyo, kuyaita mazuri haya kuwa ni vipaumbele binafsi vya Rais, ambavyo sasa vimefanywa kuwa vipaumbele vya Taifa. Ndio maana ya kelele zote juu ya Chato. Watu wanahusisha yanayofanyika Chato na Urais wa Magufuli. Hawajakosea.

Mwalimu Nyerere, Rais wetu wa kwanza, alikuwa madarakani mfululizo kwa miaka 24. Mwalimu hakuwahi kufanya haya tunayoyaona Chato nyumbani kwao Butiama.

Ali Hassan Mwinyi, Rais wetu wa pili, hakuwahi kufanya haya ya Chato nyumbani kwao Zanzibar au Rufiji alikozaliwa. Benjamin Mkapa, Rais wetu wa tatu, hakudiriki kufanya ya Chato nyumbani kwao Masasi, wala makazi yake mapya ya Lushoto.

Rais Kikwete anasemwasemwa sana juu ya Barabara ya Msata - Bagamoyo na Bandari (ambayo haikujengwa) ya Bagamoyo. Lakini hata yeye hakufanya haya tunayoyaona na kuyasikia Chato, kule nyumbani kwao Msoga katika miaka yote kumi ya Urais wake.

Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli yuko kwenye kundi la kipekee kabisa katika historia ya nchi yetu tangu uhuru. Amefanya mambo makubwa kwa kijiji chake kuliko watangulizi wake wote kwa ujumla wao.

Pili, amefanya mambo hayo makubwa ndani ya muhula wake wa kwanza. Kwa maneno mengine, hata kabla ya kufikisha miaka minne kati ya mitano ya muhula wake wa kwanza, Rais Magufuli amefanya mambo makubwa nyumbani kwao kuliko walivyofanya akina Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Kikwete katika miaka 54 waliyokuwa madarakani.

Tatu, Rais Magufuli amefanya yote haya katika mazingira ya kikatiba, kisheria na kisiasa ambayo ni magumu zaidi kuliko ya watangulizi wake wote. Nitafafanua hili kwa kirefu kidogo.

Tangu angalau tuwe Jamhuri mwaka 1962, Rais wa nchi yetu amekuwa na mamlaka makubwa sana kikatiba, kisheria na kisiasa. Kwenye hili, Mwalimu Nyerere mwenyewe aliwahi kusema, mwaka 1967 na akarudia tena mwaka 1978, kwamba alikuwa na mamlaka, kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu za wakati huo, ya kuwa dikteta.

Tanzania ya Mwalimu ilikuwa ni dola la kiimla la chama kimoja.
Haikuwa inatambua wala kulinda haki za binadamu kikatiba na kisheria. Hakukuwa na Uhuru wa Mahakama; na Bunge lilikuwa Kamati ya CCM kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Hakukuwa na uhuru wa vyombo vya habari na wala hakukuwa na vyombo vya habari zaidi ya RTD ya Serikali na magazeti mawili, Daily/Sunday News ya Serikali pia na Uhuru/Mzalendo ya CCM. Aidha, shughuli zote muhimu za kiuchumi zilikuwa zinamilikiwa au kuendeshwa na Serikali n.k.

Katika masuala ya maadili ya uongozi, hakukuwa na sheria wala taasisi mahsusi iliyoweka au kusimamia utaratibu wa maadili ya viongozi wa umma. Masuala haya yaliwekwa kwenye Katiba ya chama cha TANU na baadae CCM, sio katika Katiba na Sheria za nchi.

Katika mazingira haya, Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa wa kujilimbikizia mali yeye binafsi au watu wake wa karibu. Vile vile, alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya upendeleo kwa kijiji chake cha Butiama au Wilaya yake ya Musoma Vijijini, kwa kuipelekea miradi ya maendeleo kama tunayoiona Chato kwa Magufuli.

Lakini Mwalimu hakufanya hivyo. Aliogopa na kuheshimu macho na midomo ya wananchi wake. Hiki kimebakia, kwa maoni yangu, kuwa kielelezo kikuu cha ukuu (greatness) wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rais Mwinyi aliyepokea kijiti cha uongozi baada ya Mwalimu kung'atuka, alipokea kijiti hicho katika mazingira tofauti na ya Mwalimu.

Kwanza, kikatiba na kisheria, kulikuwa na mabadiliko makubwa yaliyoletwa na Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1984.

Mabadiliko hayo yalileta kanuni ya ukomo wa muda wa madaraka ya Rais; na pia yaliingiza Hati ya Haki za Binadamu kwenye Katiba yetu. Kwa mara ya kwanza tangu Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962, kuliwekwa udhibiti kiasi wa mamlaka makubwa ya Rais kwenye Katiba ya nchi yetu.

Kisiasa, Rais Mwinyi aliingia kwenye Urais wakati dola la kiimla la chama kimoja likiwa kwenye shinikizo kubwa. Hiki kilikuwa kipindi cha machipuko ya vikundi vya kijamii, ambavyo ndio vilikuja kutengeneza vyama vya siasa vya upinzani katika muhula wa pili wa Rais Mwinyi.

Hiki ni kipindi pia cha kuanza rasmi kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992; na kipindi cha kuibuka kwa vyombo vya habari visivyomilikiwa na Serikali. Aidha, ni kipindi cha Bunge letu kuanza kuamka kutoka usingizi mzito wa chama kushika hatamu.

Kwa maana nyingine, Mzee Mwinyi alikabiliwa na changamoto za kikatiba na kisiasa ambazo hazikuwepo wakati wa Mwalimu Nyerere.

Lakini pamoja na mazingira haya mapya ya kisiasa, bado Rais Mwinyi alikuwa na mamlaka makubwa sana kikatiba. Na kama angetaka, angeweza kujilimbikizia utajiri mkubwa yeye binafsi na wapambe wake. Aidha, Mwinyi angeweza kufanya upendeleo mkubwa wa kimaendeleo Rufiji alikozaliwa, au Zanzibar alikokulia.

Kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi nae aliogopa na kuheshimu macho na midomo ya wananchi wake. Hakufanya upendeleo tunaouona Chato kwa Magufuli.

Ben Mkapa na Jakaya Kikwete wao ni Marais wa zama za vyama vingi vya siasa na upinzani wenye nguvu. Ni Marais wa Tanzania iliyobadilika na kubadilishwa na teknolojia za kisasa za mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Ni Marais wa Bunge la vyama vingi lenye nguvu. Na, muhimu zaidi kwa mada yangu, ni Marais wa Tanzania yenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Sheria hii ilianza kutumika tarehe 1 Julai, 1995, wakati wa miezi ya mwisho ya utawala wa Rais Mwinyi.

Sheria hii imeweka masharti mengi kuhusu maadili ya viongozi wa umma na utaratibu wa kitaasisi wa kuyasimamia. Viongozi wa umma wamekatazwa kutumia dhamana zao za uongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Wameelekezwa kuepuka migongano kati ya maslahi yao binafsi na maslahi ya umma; na kwamba pale kunapokuwa na migongano hiyo, basi maslahi ya umma yanatakiwa kuwa juu ya maslahi yao binafsi.

Ukiachia Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sekretarieti yake ambavyo ni vyombo vya utendaji kwenye masuala haya, Sheria hii imempa Rais majukumu makubwa ya kuhamasisha viwango vya juu vya maadili ya viongozi wa umma.

Sehemu yote ya Pili ya Sheria hiyo inazungumzia wajibu mbali mbali wa Rais ambaye, kwa mfano, ana mamlaka ya kuweka viwango na kanuni za maadili ambazo zitafuatwa na viongozi wote wa umma.

Kwa hiyo, Rais Mkapa na Rais Kikwete waliongoza nchi katika mazingira magumu zaidi kikatiba, kisheria na kisiasa kuliko ilivyokuwa kwa Mzee Mwinyi na, kwa vyovyote vile, Baba wa Taifa.

Licha ya kukithiri kwa rushwa, ufisadi na uchafu mwingine mwingi katika Tanzania ya Mkapa na Kikwete, katika miaka yao ishirini ya uongozi, hawakufanya makwao haya ambayo Magufuli ameyafanya kwao Chato kwa miaka minne. Nao pia waliogopa na kuheshimu macho na midomo ya Watanzania.

Rais Magufuli alirithi mazingira haya magumu na zaidi yake. Katika zama hizi za vyama vingi, Magufuli ni Rais aliyeingia madarakani kwa kura chache kuliko watangulizi wake wawili, yaani Mkapa na Kikwete.

Aidha, Magufuli aliingia madarakani huku kukiwa na upinzani mkubwa zaidi Bungeni kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya nchi yetu.

Na nje ya vyama vya siasa vya upinzani, Magufuli alichukua madaraka katika Tanzania yenye mwamko mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Katika mazingira haya, Rais Magufuli ana rekodi ya kipekee ya kuweza kufanya mambo makubwa nyumbani kwao Chato katika mazingira yasiyokuwa rafiki kiasi hiki. Amewezaje kufanya hivyo ni mjadala mwingine wa siku nyingine.

Lakini aliyoyafanya Rais Magufuli nyumbani kwao Chato yanamuweka katika kundi la kipekee hata katika Bara zima la Afrika. Bara letu limekuwa na Marais wa aina hii wengi sana. Baadhi yao wameelezewa na mwandishi Peter Kenyon katika kitabu chake 'Dictatorland: The Men Who Stole Africa', kilichochapishwa Uingereza mwaka jana.

Sasa upekee wa Rais Magufuli ni upi miongoni mwa hawa 'Wanaume Walioiiba Afrika'???

Rais Mobutu Sese Seko wa Zaire, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alijenga hekalu la kifalme, mahoteli ya kifahari na uwanja wa ndege wenye uwezo wa kutumiwa na ndege ya aina ya Concorde na Boeing 747 Jumbo Jet, katika kijiji chake cha Gbadolite, katikati ya msitu wa Ikweta wa nchi hiyo.

Na alifanya kila aina ya upendeleo kwa familia yake, ndugu zake na kabila lake. Hata hivyo, Mobutu alifanya yote hayo katika kipindi cha takriban miaka 32 ya utawala wake. Magufuli wa Chato hajafikisha miaka minne bado.

Felix Houphouet-Boigny, Rais wa kwanza wa Cote d'Ivoire, alijenga Mji Mkuu mpya katika kijiji cha Yamoussoukro alikozaliwa. Hapo kijijini, Houphouet-Boigny alijenga kanisa ambalo, kwa mujibu wa Paul Kenyon, lina urefu wa ghorofa 35, nafasi ya kutosha viwanja vinne vya mpira na bustani zenye nafasi ya kutua ndege aina ya Boeing 747. Paa la kanisa hilo limetengenezwa kwa mfano wa paa la Kanisa la Mtakatifu Petro la Vatican City (Houphouet-Boigny alikuwa Mkatoliki).

Zaidi ya hayo, Rais huyo alijenga barabara zenye njia sita kuunganisha mji Mkuu wa Abidjan na Yamoussoukro. Hata hivyo, ilimchukua Felix Houphouet-Boigny miaka 33 ya Urais kuigeuza Yamoussoukro namna hiyo. John Pombe Magufuli hajakamilisha miaka minne kati ya mitano ya Urais wa Tanzania.

Ngwazi Dr. Hastings Kamuzu Banda, Rais wa kwanza wa Malawi, naye alihamishia Mji Mkuu wa nchi yake Blantyre kwenda kijijini kwao Lilongwe. Lakini ilimchukua miaka zaidi ya 30 kufanya hivyo. Magufuli hajamaliza muhula wake wa kwanza akiwa Rais wa nchi yetu.

Lakini mfano wa siku za karibuni wa ufisadi wa aina hii ni ule unaomhusu Jacob Zuma, aliyekuwa Rais wa tatu wa Afrika Kusini ya baada ya apartheid.

Mara baada ya kuingia madarakani kufuatia chama chake cha ANC kumwondoa mtangulizi wake Thabo Mbeki, Rais Zuma alianza kugeuza kijiji chake cha Nkandla kuwa kama ambavyo Magufuli anaigeuza Chato.

Vitendo hivyo, na vingine vya aina hiyo, vilizua kashfa kubwa inayojulikana kama 'State Capture', yaani 'Kutekwa kwa Dola' ya Afrika Kusini. Kashfa hiyo ilisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa katika nchi na ndani ya ANC yenyewe.

Hatimaye ANC ililazimika kumvua madaraka ya Urais wa chama na hivyo, kwa Katiba ya nchi hiyo, akapoteza madaraka ya Rais wa Afrika Kusini.

Leo Jacob Zuma amelazimishwa kurudisha fedha za umma alizotumia kujengea makazi yake kijijini Nkandla, na anakabiliwa na tuhuma kadhaa za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi mbele ya Tume ya Maadili ya nchi hiyo.

Huu ndio upekee wa Magufuli katika Tanzania na katika Bara la Afrika. Sio upekee wa kujivunia hata kidogo.

Lakini maendeleo yote haya yana maana gani kwetu??? Felix Houphouet-Boigny alipofariki December 1993, aliacha Cote d'Ivoire ikiwa imefilisika kiuchumi na ikiwa imegawanyika kisiasa kwa misingi ya ukabila na uzawa.

Haikuchukua muda kwa wapambe wake wa karibu, Alassane Ouattara aliyekuwa Waziri Mkuu na Henri Konan Bedie, Rais wa Bunge la nchi hiyo na mpwa wa Houphouet-Boigny, walianza kugombania madaraka. Mwishowe nchi hiyo iliingia katika machafuko ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo haikuisha mpaka miaka michache iliyopita.

Leo mji wa Yamoussoukro na Kanisa lake umebakia magofu na hakuna mtu anayetaka kuhusishwa na Felix Houphouet-Boigny na utapanyaji mali wake.

Kwa sababu ya utawala wake wa kidikteta na ufujaji mali za nchi yake, Mobutu Sese Seko alisababisha Zaire kuingia katika machafuko ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyomuondoa madarakani mwaka 1997.

Yeye mwenyewe alifia uhamishoni Morocco na hadi sasa imeshindikana kuurudisha mwili wake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya maziko katika nchi yake.

Gbadolite, 'the Versailles of the Jungle' kama alivyokuwa akijitapa kuhusu kijiji chake, imebakia magofu matupu. Na nchi yenyewe haijaweza kutulia hadi sasa, zaidi ya miaka ishirini baada ya Mobutu kuondolewa madarakani.

Angalau Lilongwe ya Kamuzu Banda imebakia Mji Mkuu wa Malawi. Lakini Malawi bado ni maskini kama alivyoiacha, baada ya kuitawala kimabavu kwa zaidi ya miongo mitatu.

Je, Chato ya Magufuli itakuwa tofauti baada ya Magufuli??? Na je, Tanzania yetu itakuwa salama kiasi gani baada ya Magufuli kuondoka madarakani???

Maswali yote mawili yanaweza kujibiwa na mifano niliyoitoa ya DRC, Cote d'Ivoire, Malawi na Afrika Kusini. Anayoyafanya Magufuli nyumbani kwao Chato ni classic case ya maslahi binafsi ya Rais kugeuzwa kuwa maslahi ya umma. Na kama ilivyotokea kwingineko, mazuri hayo yatageuka magofu na aibu ya taifa baada ya mpangaji wa sasa wa Ikulu kumpisha mpangaji mwingine.

Ili tuwe na wazo la nini kitatokea Chato baada ya Magufuli, inatosha tu kujiuliza hivi uwanja wa ndege wa Mpanda, uliojengwa wakati Mbunge wa Mpanda Mashariki, Mizengo Pinda, akiwa Waziri Mkuu unatumikaje kwa sasa???

Kama ilivyo kwa Chato hivi sasa, tuliambiwa wakati ule kwamba uwanja huo utahamasisha utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi na ukanda wa Ziwa Tanganyika. Leo hii, kama kuna ndege mbili zinatua kwenye uwanja huo kwa mwaka ni bahati.

Kuhusu swali la pili, kama alivyofanya Mobutu Sese Seko, Houphouet-Boigny na Kamuzu Banda, Rais Magufuli ataigawa nchi yetu vipande vipande kwa misingi ya ukabila, ukanda na aina nyingine za ubaguzi.

Ili watawale nchi wanavyotaka wao, watawala wa aina hii lazima wagawe watu mafungu mafungu na wafanye upendeleo haramu.

Ni lazima wawape ndugu zao, au marafiki zao, au watu wa makabila yao au dini zao upendeleo. Na lazima watenge, kukandamiza na kunyanyasa wengine. Lazima watumie mbinu chafu, mauaji, utekaji, utesaji na kila aina ya uovu na uonevu ili wahakikishe wanabaki madarakani na wanatekeleza agenda zao binafsi.

Vitendo hivyo huzaa chuki, visasi na upinzani mkubwa. Matokeo yake ni machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ya Chato na Magufuli sio madogo ya kupuuzia. Ni ya hatari kubwa kwa taifa letu. Tuna wajibu wa kuliokoa taifa letu kwa kumzuia Magufuli kufuata nyayo za Mobutu Sese Seko, Felix Houphouet-Boigny, Hastings Kamuzu Banda na Jacob Zuma.

Kwa bahati nzuri, hata ndani ya CCM kwenyewe hali sio shwari tena. Iliyokuwa minong'ono ya kichini chini sasa imeanza kuwa sauti za wazi wazi za kutokukubaliana na mambo ya Magufuli na watu wake.

Tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba sauti hizi hazizimwi kwa vitisho au kwa ukatili ambao hakuna mwenye shaka tena kwamba utawala wa Magufuli unaweza kuufanya.

Badala yake, tuna wajibu wa kuhakikisha sauti hizi zinakuwa nyingi na kubwa zaidi ili tuweze kuiokoa nchi yetu na janga hili la Tanzania ya Magufuli.
 
Mimi ninakumbuka kuna uwanja wa Mpira ulijengwa Singida wakati kulikuwa hakuna timu ya mpira ya Daraja la kwanza, ninakumbuka kuna reli ilijengwa na sisi wa Tanzania kutoka Dodoma/Manyoni kwenda Singida na watu hawakupiga kelele kama mkimbizi.

Sasa hivi Singida ina barabara mbili za lami kwenda Tabora na kwenda Arusha
 
Mimi ninakumbuka kuna uwanja wa Mpira ulijengwa Singida wakati kulikuwa hakuna time ya mpira ya Daraja la kwanza, ninakumbuka kuna reli ilijengwa na sisi wa Tanzania kutoka dodoma/manyoni kwenda singida na watu hawakupiga kelele kama mkimbizi.
Sasa hivi Singida ina barabara mbili za lami kwenda tabora , na kwenda Arusha
Endelea na kumbukumbu japo ni contrary na mada tajwa
 
LISSU AENDE ZAKE HUKO KAKAA UBUNGE MIAKA KIBAO JIMBONI KWAKE HAJAFANYA LOLOTE WALA KUWASEMEA WANANCHI WAKE WALIOMCHAGUA BUNGENI

Chadema hawaamini maendeleo ya vitu, shut up Lissu vitu havikuhusu it is non of your business

Utaongeleaje vitu wakati sera yenu ya CHADEMA haiamini kwenye maendeleo ya vitu?
 
Dubwana lenu la Chato lingekuwa na akili Kama ya Tundu Lissu nchi ingekuwa mbali sana kimaendeleo. Dubwana linaamini eti Chato tu ndio ina haki ya kuendelezwa
Ongeleeni maendeleo yenu ya watu ya vitu tuachieni CCM wenye sera hiyo ya vitu mbona mnahaha kudandia hoja za CCM? hAYO MAENDELEO YA WATU MKIAMBIWA ONYESHENI KWENYE MAJIMBO YENU NI YEPI MAENDELEO YA WATU MLIPELEKA ILI WATU WAONE KAMA MFANO HAMNA CHA KUONYESHA NI POROJO TU KWENDENI HUKO

DK MAGUFULI ONGEZA KASI pato la taifa asilimia kubwa linatoka GEITA kwenye migodi mikubwa ya dhahabu Afrika SIO SINGIDA KWA lisu kwenye VIDUMU VYA MAFUTA YA ALIZETI

GEITA lazima ibadilike iwe kama Dubai
 
Kwa mambo yanavyoendelea huko Chato hata kipofu atashtuka, haiwezekani kwa akili za kawaida kila mradi uende Chato tu, kwanini usipeleke hata mikoa au wilaya za jirani?

This Chato story is too much now.

Mtu wa aina hii ndio anaacha precedence mbovu kwa marais wajao nao wataona sifa kila kitu wapeleke kwao.
 
Mi nilikuwa nakerwa na Kodi za pembezoni kuijenga Dar pekeake! Ila kujenga nje ya Dar popote pale nchini ni sawa tu, hata Kikwete Kama alijenga kule kwao chochote (viwanda Pwani) ni sawa tu, angalau isiwe Dar tu, hata Majaliwa ukifika wakati wake akajenge Ruangwa Kama Chato, kama wabunge mmeshindwa kutunga sheria za makusanyo na mrejesho wa kimiradi hata maji tu! eneo zilikokusanywa basi wacha itumike mbinu hiyo tu.
 
ongeleeni maendeleo yenu ya watu ya vitu tuachieni CCM wenye sera hiyo ya vitu mbona mnahaha kudandia hoja za CCM? hAYO MAENDELEO YA WATU MKIAMBIWA ONYESHENI KWENYE MAJIMBO YENU NI YEPI MAENDELEO YA WATU MLIPELEKA ILI WATU WAONE KAMA MFANO HAMNA CHA KUONYESHA NI POROJO TU KWENDENI HUKO....
Mbunge wajibu wake ni upi? Nipe nukuu au chapisho la kazi zote za mbunge
 
Back
Top Bottom