Tundu Lissu apongeza kufutwa kwa kesi, atamani kauli ya Serikali ya Rais Samia

Sep 17, 2021
39
84
Imefahamika kwamba kesi tano zilizokuwa zikimkabili Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu zimefutwa tangu Rais Samia aingie madarakani.

Gazeti la Mwananchi, limezungumza na Tundu Lissu aliyepongeza kufutw akwa kesi hizo kwa kusema ni JAMBO JEMA. Licha ya kwamba hakuna mahali ambapo Serikali imemtaka Lissu kurudi Tanzania, Lissu amedai kwamba, ili arudi nyumbani ni lazima asikie kauli kutoka kwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ikimhakikishia usalama wake .

“Ni jambo jema kwa sababu hazikupaswa kuwapo. Kama wameona hazina sababu ni jambo jema. Ni hatua nzuri, lakini jambo la pili wanatakiwa wanihakikishie usalama wangu. Hilo linahitaji kauli yao. Wakitoa kauli sina sababu ya kuendelea kuishi huku.

“Mimi sikukimbia nchi kwa sababu ya kesi za kubumba kama hizo walizonifungulia. Nilikimbia nchi kwa sababu ya jaribio la mauaji dhidi yangu. Serikali inatakiwa kunihakikishia usalama wangu ili niweze kurudi nyumbani nikijua nitakuwa salama. Hilo likifanyika nitarudi nyumbani,” alisema Lissu.

Lissu ambaye hivi sasa anaishi nchini Ubelgiji alikuwa akikabiliwa na kesi tano za uchochezi katika mahakama ya Kisutu zilizodumu kwa miaka kati ya minne na mitano.

Kesi zilizofutwa na DPP ni pamoja na ile ya jinai namba 208/2016 iliyokuwa inamkabili Lissu, mwandishi wa habari wa gazeti la Mawio, Jabir Idrisa, mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob. Walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano yaliyotokana na habari iliyoandikwa na gazeti hilo, iliyokuwa ikidaiwa ya uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati Januari 12 na 14, 2016, jijini Dar es Salaam, Lissu na washtakiwa wengine waliandika na kuchapisha katika gazeti hilo taarifa yenye kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’ kwa nia ya kuleta chuki kwa wananchi.

Katika kesi nyingine ya jinai namba 233 ya mwaka 2016, Lissu alishtakiwa kwa uchochezi baada ya kusema mamlaka ya Serikali ni mbovu na ya kidikteta, maneno ambayo Jamhuri ilidai yaliyolenga kuleta chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali yao. Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Rashid Chaungu, ilipangwa kutolewa uamuzi wa kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la Oktoba 4, 2017.

Kesi nyingine tatu zilizofutwa na mahakama chini ya kifungu cha 225 (5) cha CPA ni pamoja na kesi ya jinai namba 123/2017 ambayo Lissu alikuwa akikabiliwa na mashtaka matano ya uchochezi baada ya kutoa kauli isemayo: “Tangu mwaka 1964 Tanganyika ndiyo inayoamua nani atawale Zanzibar” Alitoa kauli hiyo akiwa Zanzibar.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele na tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka alishatoa ushahidi.

Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa na mahakama baada ya kukaa muda mrefu bila kusikilizwa kutokana na mshtakiwa kutokufika mahakamani.

Lissu alikuwa akikabiliwa pia na kesi ya jinai namba 236 ya mwaka 2017 baada ya kutoa maneno akiwa katika makao makuu ya Chadema kuwa Serikali ya Hayati Rais John Magufuli ni ya kibaguzi na kikabila.

Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando, ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa awali baada ya upelelezi kukamilika, lakini ilifutwa Agosti mwaka huu.

Kesi ya mwisho ilikuwa kesi ya jinai namba 279 ya mwaka 2016 iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya ilihusiana na kauli nyingine ya Lissu kumwita hayati Rais John Magufuli dikteta uchwara.

Katika kesi hiyo, Lissu alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi, kuleta chuki dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na kuidharau mahakama, Agosti 2, 2016. Kesi hiyo ilifutwa Julai 2021.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom