Tunauaga 2010 tukiwa na mengi ya kujifunza, tusirudie makosa

mzambia

JF-Expert Member
Dec 31, 2010
885
60
Send to a friend
werema.jpg
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema

Hassan Mohamed
WAHENGA walisema aliyeumwa na nyoka huogopa hata mjusi. Siku chache baada ya Serikali kutoa agizo kwa Mamlaka ya usafirishaji wa nchi kavu na majini nchini (Sumatra) kuvunja mkataba uliopo baina ya mamlaka hiyo na kampuni ya udalali ya Majembe kumekuwa na mjadala kuhusu hali itakavyokuwa baada ya kutekelezwa kwa agizo hilo Desemba 31 mwaka huu.

Hofu yenyewe inatokana na athari zinazoonekana sasa hivi baada ya serikali kuvunja mkataba kati ya Tanesco na Kampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans ambapo Mahakama ya Kimataifa ya migogoro ya Biashara iliiamuru Tanesco kuilipa Dowans Sh185 bilioni.

Awali Tanesco ilisema kuwa ingetoa tamko juu ya hukumu hiyo baada ya mwanasheria mkuu kulitolea tamko lakini Tanesco ilionyesha kuwa ina dhamira ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, hivi karibuni alitoa tamko kuwa hakuna haja suala hilo kukatiwa rufaa na hivyo kuishauri Tanesco ilipe gharama hizo.

Wakati hukumu hiyo ikiendelea kuitafuna Serikali, ‘kombora’ jingine linaonekana kuandaliwa baada ya kampuni ya udalali ya Majembe, maarufu kama Vijana wa Kazi kutangaza kuwa wanasubiri Desemba 31, Sumatra itekeleze agizo lililotolewa na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu la kuitaka mamlaka hiyo kuvunja mkataba na Majembe baada ya kusikiliza malalamiko ya wamiliki na madereva wa mabasi.

Agizo la Waziri Nundu la kuitaka Sumatra itumie kipindi cha wiki moja ili kuachana kistaarabu na majembe lilizusha mjadala miongoni mwa wadau wa usafirishaji.

Wamiliki wa mabasi na madereva walionyesha kufurahishwa na agizo hilo kwa kumpongeza Waziri kwa hatua hiyo kwa kuwa Majembe wamekuwa ‘wasumbufu’ kwao.
Kwa maana nyingine, mwaka mpya wa 2011 ukianza, zinazoitwa kero za majembe haziwezi kuwapo tena na kuwafanya madereva na makondakta kuwa huru zaidi.

Baadhi ya watumiaji wa huduma ya usafirishaji hasa wa mabasi pia wameungana na waendeshaji wa huduma hiyo wakiunga mkono kusitishwa kwa mkataba wa Majembe wakiwalaumu kuingilia kazi za askari wa usalama barabarani.
Hata hivyo wapo wengine wanaotilia mashaka matokeo ya kusitishwa kwa mkataba huo kwa pande zote wakisema kuwa japo kumekuwa na kasoro kadhaa za kiutendaji Majembe wamesaidia kuboresha hali ya usalama barabarani hapa jijini Dar es Salaam.

Siku moja nilimuuliza kondakta wa daladala ni kwanini wanawahofia majembe zaidi kuliko hata askari wa barabarani maarufu kama trafiki? Nilichoelezwa ni kwamba faini inayotolewa kwa kosa linalokamatwa na majembe ni kubwa kuliko trafiki na kwamba wakikukamata si rahisi kukuachia mpaka utoe faini.

“Kaka ni afadhali ukamatwe na trafiki kumi kuliko majembe mmoja, hawa jamaa hawana masihara” alisema konda huyo wa daladala inayofanya safari zake kati ya Mwenge na Posta jijini Dar es Salaam.
Hii inaashiria kuwa Vijana hao wa kazi wamekuwa makini zaidi katika kuhakikisha usalama barabarani unakuwepo ili kuwapa nguvu trafiki.

Lakini tujiulize, uwepo wa majembe kwa kipindi cha mwaka mmoja kumeleta mabadiliko yapi?Hivi ni kweli kasoro zilizoonekana zilishindwa kurekebishwa kwa njia nyingine zaidi ya kukatisha mkataba? Askari wa usalama

barabarani tayari wameshapewa meno ya kutafuna kama wafanyavyo majembe?
Kimsingi baadhi ya makosa ni pamoja na kukatisha ruti, kutovaa sare, kutovaa mikanda kwa madereva na abiria, kutowasumbua wanafunzi na kadhalika, mambo ambayo bila shaka tunajionea wenyewe kuwa kwa sasa hayo kwa kiasi kikubwa yanazingatiwa pengine kushinda kipindi cha kabla ya Majembe kuingia barabarani.

Ikiwa tunauaga mwaka kwa kuwaaga pia Majembe tutazame na mbadala wao kama sababu za msingi serikali kuipa kampuni hiyo udalali.
Suala la matokeo ya usalama barabarani ni moja lakini hili la kisheria la kuachana kistaarabu kwani tayari Majembe wamesema kuwa wanatazama taratibu za kisheria za kuhakikisha hawapati hasara, hii inamaanisha kuwa yale ya Dowans na Tanesco yanaweza pia kutokea kwa Sumatra na Majembe.

Tunajua serikali ilifanya uchunguzi kabla ya agizo lake lakini tukumbuke pia hata suala la Dowans ‘lilifanyiwa’ uchunguzi na hatima yake tumeiona ambapo imeleta hasara kubwa kwa Watanzania kutakiwa kuilipa kampuni hiyo mamilioni hayo ya fedha huku serikali ikiendelea kuwaomba wahisani kusaidia katika kuwatoa Watanzania katika lindi la umasikini.

Hivyo wakati tunauaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 tujifunze kutokana na changamoto zilizotufika na kujipanga sawa sawa ili kuhakikisha juhudi za kupambana na umaskini kweli zinaonekana zikitendeka kwa kuonyesha umakini katika masuala nyeti ya mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.
Kwaheri mwaka 2010 karibu 2011
 
Mwaka 2011

wahusika wa dowans kushitakiwa

katiba mpya
jk ajiuzulu urais
na mengineyo tutufurahi tukisikia hayo
 
Back
Top Bottom