Tunataka wabunge wanaoona mateso ya wapiga kura wao | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunataka wabunge wanaoona mateso ya wapiga kura wao

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ngalikivembu, Feb 14, 2011.

 1. Ngalikivembu

  Ngalikivembu JF-Expert Member

  #1
  Feb 14, 2011
  Joined: Oct 6, 2010
  Messages: 1,908
  Likes Received: 355
  Trophy Points: 180
  MWAKA jana wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiongeza majimbo ya uchaguzi na kwa maana hiyo kuongeza idadi ya wabunge, niliandika makala kuhoji umuhimu wa wabunge wengi.
  Kwa maoni yangu, katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia, wingi wa wabunge si hoja, bali uwezo wa wabunge. Kwa maoni yangu hata kila wilaya inaweza kuwa na mbunge mmoja.
  Wabunge si walimu ambao unaweza kusema wanahitajika walimu kadhaa kwa wanafunzi.
  Wabunge si mahakimu au majaji ambao unaweza kusema kwa wingi wa kesi wanahitajika mahakimu kadhaa.
  Wabunge si madakatari ambao unasema kwa kila wagonjwa wanahitajika madaktari kadhaa. Wabunge si polisi ambao ungesema uwiano wa polisi kwa raia ni huu au ule.
  Taja taaluma nyingine yoyote utakayo. Sioni mantiki ya kuongeza utitiri wa wabunge ambao nao wanaongeza gharama tunazobeba kwa kodi zetu.
  Nimelazimika kukumbuka maandiko yangu hayo baada ya kufuatilia hapa na pale kile kinachoendelea katika bunge letu hivi sasa. Nimepata bahati ya kufuatilia sehemu chache lakini sijaridhika bado.
  Swali la msingi sasa kwangu ni ikiwa wabunge wanawakilisha wananchi au vyama vyao? Kwa mtazamo wa haraka tayari inaonekana kinachofanyika sasa ni kulinda kwanza masilahi ya vyama halafu ya wananchi yanafuata.
  Tumesikiliza wakati fulani utadhani bungeni ni “Waswahili” wanasutana. Mjadala kama ule wa kutolea ufafanuzi kuhusu kanuni zinazohusu kambi rasmi ya upinzani bungeni umetufanya tuhoji staha ya wabunge wetu.
  Wakati fulani nikalazimika kufikiri kumbe idadi ya wabunge inahitajika zaidi ya uzito wa hoja za wabunge? Hii inatokana na watu badala ya kujadili hoja za msingi watu wanatumia zaidi kejeli na maneno mengine ya kusutana.
  Hata baada ya wabunge wa CHADEMA kuamua kutoka nje wakati wa kupiga kura nilisikia maneno ambayo ukiyatafsiri unaweza kushindwa kujua hasa wawakilishi wetu hao wanafikiri nini katika vichwa vyao.
  Wanawafikiria wananchi au wanajifikiria wao? Tulikuwa tukifuatilia mjadala ule kupitia katika runinga. Wakati wabunge wale wa CHADEMA wakitoka nje, tulisikia mmoja wa wabunge waliobaki akisema “hata kwenye posho msije”.
  Ukiichukulia kienyeji kauli hii unaweza kuiona ya kawaida au hata ya busara. Lakini ukiitafakari unapata shaka na mawazo ya aliyetoa kauli hiyo.
  Wazo lililomjia la kwanza huyo aliyetamka mawazo hayo ni “posho”. Katika hali ya kawaida ungedhani kwamba angejiuliza, je, wakitoka nje wananchi wanaopaswa kuwakilishwa na wabunge hao watakuwa wametendewa haki?
  Unapoanza kufikiria hoja ya waliotoka nje kama wamelipwa posho au la, ni kiwango cha ubinafsi. Je, yeye alikuwa kule bungeni ili apokee posho? Kupokea posho kwake ndio wajibu wake wa kwanza?
  Ndiyo hoja yake ya kwanza? Ana bahati hatukumtambua mbunge huyo aliyetamka hayo. Tungemshitaki kwa wapiga kura wake.
  Lakini hoja yangu ya wingi wa wabunge na ustawi wa watu wetu bado unaonekana katika aina ya uchangiaji. Karibu kila mbunge wa chama tawala akipata nafasi ya kuchangia hoja anaanza na sifa, pongezi na vibwagizo vingine.
  Nitafurahi kama atatokea mtafiti akatuambia ni muda wa kiwango gani unatumika kumsifia na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushindi wa kishindo. Hapo hawajamshukuru Muumba wao kwa kuwawezesha kuingia bungeni.
  Hapo bado hawajaanza kusifia amani na utulivu. Tunapoteza muda mwingi kujadili mambo ambayo hayatabadili chochote katika maisha ya Mtanzania.
  Nimeambiwa hotuba ya rais inajadiliwa kwa siku tano. Hapa naungana na wengine tunaohitaji ufafanuzi kuhusu hasa mantiki ya kuijadili hotuba ya rais. Nafahamu huu ndio umekuwa utaratibu katika Bunge letu.
  Sijui katika mabunge mengine. Lakini tutazame chetu kwanza. Hivi ile hotuba au hotuba nyingine yoyote ya rais inajadiliwa kusudi iweje? Nasema tunahitaji mwongozo hapa. Maana rais alizungumza akamaliza, akaondoka.
  Tunatarajia utekelezaji wa kile alichosema. Sasa wabunge wanapoijadili huwa wanamwongezea maneno? Wanambadilisha fikra? Na mchango huo wa wabunge unafanyiwa nini wakishazungumza?
  Kuna utekelezaji wa kile wabunge wanachosema? Tofauti na pale wanapochangia kwenye bajeti walau tunajua mawaziri husika hutilia maanani maoni ya wabunge kwenye utekelezaji.
  Hili la kuijadili hotuba ya rais kwa siku tano, tunahitaji kuelezwa matokeo yake katika maisha ya kawaida ya mwananchi ni yapi?
  Hoja ya wingi wa wabunge bado inakuja kwenye hili la kujadili hotuba. Hivi wingi wa wachangiaji ndio utaleta ufanisi au akili na uzito wa hoja za wachangiaji?
  Unaweza kuwa na wabunge mia wanaochangia lakini nusu yao wakaishia kumshukuru Mungu kwa ushindi wa kishindo, kusifu amani na utulivu, kuunga mkono asilimia mia kwa mia yale yote aliyosema rais halafu mwisho ndipo anapachika ka-hoja ka kuomba zahanati yao itupiwe macho.
  Hotuba kama ile ya rais ingeweza kuchangiwa na wabunge kumi tu wakaiangalia na kuweka mkakati wa namna ya kuwezesha hayo yaliyoahidiwa kama yapo yatekelezeke.
  Wingi wa wabunge hapa haupo. Alichozungumza rais kinajulikana na muhimu kwetu ni kuona hali yetu ya maisha inabadilika.
  Mabadiliko yetu ya maisha hayataletwa kwa wingi wa wabunge wanaochangia, wanaosutana, wanaokejeliana au wanaotetea vyama vyao.
  Nakumbuka niliwahi kuandika kwamba ni afadhali tuwe na wabunge wachache na fedha itakayookolewa kwa kupunguza wabunge ipelekwe kwa wataalamu wetu kama walimu, madaktari, mahakimu, majaji, mabwana shamba na watu kama hao.
  Kwa kupeleka fedha kwa watendaji, tutakuwa tumepeleka maendeleo ya moja kwa moja. Wabunge si watendaji wa moja kwa moja, hivyo wingi wao si lazima uwe na tija.
  Katika muda mfupi wa Bunge hili tayari tumeanza kuona kama wabunge wanakuwa watu wa kujali zaidi maslahi ya vyama vyao badala ya maslahi ya wapiga kura. Kile ambacho Watanzania wengi tunalalamika kukikosa kinaweza pia kikawa kimelikumba Bunge hili.
  Kila mbunge anapaswa kusema na kuamini kwamba tunahitaji “Tanzania kwanza” ndipo yaje haya ya vyama na mengineyo. Tunaona hatari ya kushindwa kufikia suluhu ya kweli ya matatizo yetu kwa sababu za kutetea kwanza vyama.
  Bahati mbaya nyingine ni kwamba si wote wanaotetea kwanza vyama wanafanya hivyo kwa maana ya vyama vyao kweli bali kulinda masilahi yao ambayo yanalindwa na vyama. Kwa hakika mtu anaweza kusema kama wabunge hawatakuwa wakiangalia masilahi ya umma kwanza, basi maana yake wanaangalia masilahi yao kwanza. Tumefika mahali ambapo tuwaambie hatutaki wabunge wanaofikiria posho kwanza. Tunataka wabunge wanaoona mateso na dhiki za wanachi wetu kabla ya kuona ushindi wa kishindo wa chama chao.

  source Tanzania daima


  [​IMG]


  juu[​IMG] [​IMG]
  [​IMG][​IMG]Habari Mpya | Matangazo | Bei zetu | Wasiliana nasi | Tuma habari | Webmaster
  Copyright 2011 © FreeMedia Ltd. Wasomaji
  [​IMG] [​IMG] hit counter


  © free
   
 2. G

  Gad ONEYA JF-Expert Member

  #2
  Feb 14, 2011
  Joined: Oct 26, 2010
  Messages: 2,641
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Very few MPs will carter for that! Mateso ya wapiga kura mara nyingi wabunge wanayaona wakati wa kampeni tu. baada ya hapo...
   
Loading...