SoC01 Tunao akina 'Chama na Miquissone' wengi tatizo hatuwekezi kwenye michezo

Stories of Change - 2021 Competition

JS Farms

Member
Oct 17, 2011
71
131
Habari ya wachezaji wa Simba Clatous Chota Chama raia wa Zambia ambaye amenunuliwa na klabu RS Berkane ya Morocco na Jose Luis Miquissone raia wa Msumbiji ambaye amenunuliwa na Klabu bingwa ya Afrika AL Ahly ambao wamenunuliwa kwa mabilioni ya fedha inatukumbusha umuhimu wa kuwaanda wachezaji wa Kitanzania.Tatizo kubwa la wachezaji wa Kitanzania ni kutokuandaliwa kuwa wachezaji wa kitaaluma.

Tanzania imebahatika kuwa na wachezaji kama Mrisho Ngasa, Haruna Moshi Boban, Shomari Kapombe, Feisal Salum, Ibrahim Ajibu na wengineo ambao kama wangepata mafunzo mazuri ya soka leo hii wangekuwa wamecheza kwa mafanikio Ulaya au wangekuwa bado wanacheza Ulaya.

Huu mshahara wa milioni 95 kwa mwezi ambao atalipwa Luis hata vijana wa Kitanzania wangeweza kuupata kwani viwango vya akina Luis na Chama havijatofautiana sana na akina Ajibu na wenzake tatizo la Ajibu ni kutokupata mafunzo sahihi ya soka akiwa tangu mtoto ndiyo maana leo hii unaweza ukauona udhaifu wa Ajibu kirahisi kuliko ule wa Chama, ukimuuliza Ajibu alianza kukutana na mwalimu mwenye cheti cha ukocha akiwa na umri gani atakuambia akiwa na zaidi ya miaka 17 na wakati huo alikuwa anakula cha aina gani atakujibu chakula hiki hiki tunachokula Watanzania kila siku.Ukimuuliza alikutana lini na mtalam wa viungo, mshauri wa kisaikolojia, mshauri wa wachezaji, mshauri wa biashara za wachezaji, mtaalam wa vyakula,daktari wa michezo atakujibu baada ya kujiunga klabu ya soka ya Simba.

Hakuna miujiza kwenye mafanikio ya michezo Lionel Messi mchezaji bora wa soka alijiunga na kituo cha kufundisha soka cha La Masia mwaka 2000 akiwa na miaka 13 na Cristian Ronaldo mchezaji mpya wa Manchester United alijiunga na kituo cha kufundishia soka cha Sporting CP Youth academy mwaka 1997 akiwa na miaka 12. Dunia ya sasa wachezaji ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine wanatakiwa waandaliwe kitaalamu na wachezaji wanaandaliwa kwenye vituo vya kufundisha michezo huko ndiko wanakofundishwa jinsi ya kucheza kitaalamu, jinsi ya kukimbia,jinsi ya kutoa pasi, jinsi ya kupokea mpira,jinsi ya kuishi kiuna michezo na jinsi ya kufanikiwa kwenye michezo na kuvuna fedha.

Alipokuwa Mwanza kwenye mkutano na vijana Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kwa wizara ya michezo kuanzisha vituo vya kufundisha michezo kila mkoa nchi nzima na Waziri mhusika akatangaza kila mkoa watatenga shule mbili moja ya msingi na nyingine ya sekondari kwa ajili ya kufundishia michezo.

Hii ni siasa ambayo haiwezekani kwa sababu hivi vituo ni gharama, vinahitaji uwekezaji mkubwa,vituo vinahitaji viwanja bora vya kuchezea,vifaa vya mazoezi,sare za kuchezea,watoto wanatakiwa kupata chakula bora ambavyo vitaruhusu miili yao kukua na kuwa na nguvu,kituo kinahitaji walimu wabobezi na wataalam waliojifunza kufundisha watoto,kituo pia kinahitaji majengo mazuri kwa ajili ya watoto kulala na ofisi,kituo kinahitaji madaktari na wataalam wa viungo na mambo mengine muhimu.

Kwa uchumi wetu haiwezekani kukawa na vituo viwili kila mkoa labda kama ni kutaka tuwe na vituo vyenye viwanja vya vumbi,vituo ambavyo watoto watakula kila siku ugali na maharage na mwisho kudumaa,vituo ambavyo vitafundishwa na walimu ambao hawana ujuzi na vituo ambavyo watoto hawatakutana na wataalamu wengine muhimu.Tuandae watoto watakaokuja kushindana kimataifa,kituo lazima kiwe na kiwango cha kimataifa.

Hivyo basi angalau Serikali ianze kwa kujenga vitu kwenye kanda.

Karibuni kwa mjadala na kupiga kura.
 
Back
Top Bottom