Tunamkumbuka Edward Sokoine - Mtu wa Watu

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,462
39,928
Leo ni miaka 23 tangu Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine atutoke ghafla na kuacha simanzi na wingu la huzuni. Siku ile ya machozi na majonzi imebakia katika kumbukumbu za Watanzania wengi kama vile jana. Mfano wake ni kumbukumbu ya Wamarekani waliposikia habari za kuuawa kwa Rais John F. Kennedy.

Kila mtu aliyekuwa mtu mzima wakati ule anakumbuka vizuri siku hiyo alikuwa wapi na alikuwa anafanya nini. Je pengo aliloliacha marehemu limeanza kuzibwa?

Je, kuna kiongozi yoyote ambaye anakaribia sifa na utendaji kazi wa Marehemu Sokoine? Leo tunamkumbuka Edward Sokoine.

Pata kidogo chini hapa toka kwa mkuu Kyoma:

Wazee, heshima yenu kwanza,

Mimi natofautiana na nadhalia ya kumfananisha Moringe Sokoine na Ngonyani Lowasa au Lyatonga Mrema. Sokoine alikuwa na sifa ya Uongozi, kwa maana ya kudhamilia kuonyesha njia. Pia, alikuwa ni mfanyakazi mwenye juhudi na maarifa. Dhamila ya Sokoine ilikuwa haimsuti katika utendaji wake wa kazi, ndio maana alifanikiwa kuthubutu kupunguza kero zilizowasibu watanzania. Mrema na Lowasa hawana sifa ya Uongozi, bali wana sifa ya kutawala. Pia, Mrema na Lowasa hawana sifa ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, bali wana sifa ya kushughulika. Dhamila zao wote wawili zinawasuta katika utendaji wao wa kazi, ndio maana hawawezi kufanikiwa, sio tu kupunguza, bali hata kugusa kero zinazowasumbua watanzania.

Lowasa na Sokoine wanafanana katika mantiki ya kuwa wote wameshika cheo cha uwaziri mkuu, lakini tofauti ni kuwa Sokoine alikitumia hicho cheo kuongoza watanzania, na Lowasa anakitumia hicho cheo kutawala watanzania. Katika michango yangu ya nyuma, nilikwisha elezea kwa kinaga ubaga tofauti kati ya cheo na uongozi, kwa maana ya kuwa uongozi si cheo, na cheo si uongozi. Hii ndio tofauti ya msingi kati ya ndugu yetu marehemu Moringe Sokoine ambaye aliunganisha cheo na uongozi katika nafsi yake, na kiongozi wetu mheshimiwa Ngonyani Lowasa ambaye amepata cheo cha uwaziri mkuu. Ili tuwajue hawa viongozi watatu, lazima pia tufahamu tofauti kati ya shughuli na kazi. Shughuli si kazi, na wala kazi si shughuli.

Kwa sababu nina mengi ya kuongea kuhusu Lowasa, naona nimuweke kiporo kwa leo, na nianze na tofauti kati ya Mrema na Sokoine. Mwaka 1973, nchi yetu ilikumbwa (off-guard) na ongezeko la bei ya mafuta ya petroli duniani. Hii iliathili ubadilishaji wa fedha ya kigeni. Mwaka huo huo mpaka 1974, tulikumbwa na ukame usio na kikomo, hivyo kusababisha upungufu wa chakula. Sukari, Mahindi, Unga wa ngano, na vifaa vya ujenzi ka simenti, na mabati vilikuwa hadimu. Serikali ililazimika kuingilia mgao wa chakula pamoja na mafuta ya Petroli kwa kutoa vibali kwa wale waliotaka kununua ili kulinda wananchi waliokuwa hawana uwezo wa kuchuana.

Tulichechemea mpaka mwaka 1977 wakati jumuia ya nchi za Afrika ya Mashariki ilipovunjika. Serikali ililazimika kutumia fedha ili kugharamia huduma ambazo mwanzoni zilikuwa zinatolewa na jumuia. Kumwaga tindikali kwenye kidonda, mwaka 1978 tukajiingiza kwenye vita dhidi ya Idi Amin. Kwa kiasi kikubwa, ile vita tuliigharamia sisi wenyewe bila ya fedha za mikopo. Resources zote zilienda kwenye vita, hivyo, uhaba wa kweli wa bidhaa ukaifadhaisha nchi yetu (kumbuka Sembe ya njano kwa foreni).

Tatizo kubwa lililozaliwa ni baadhi ya maafisa watendaji wa serikali katika ngazi za mikoa na wilaya, kutumia udhaifu wa uhaba wa bidhaa kwa kujilimbikizia mali. Mtindo waliotumia ulikuwa ni rushwa, kwa maana ya watendaji kuongwa na wafanya biashara ili wapewe vibali vya kulangua bidhaa zote hadimu katika bei ya serikali, na kuzificha hizo bidhaa mpaka kipindi fulani, alafu wanakuja kuziuza kwa bei ya magendo na kupata faida maradufu, wakati wananchi wakiteseka. Wafanyabiashara walipata faida isiyo kifani, na watendaji wa serikali walipata hongo kutokana na kuwauzia vibali walanguzi. Sokoine alikuwa kiongozi wa kwanza kustukia hiyo janja ya watendaji wa serikali walioshirikiana na walanguzi.

Sokoine alitoa matamko kuwa katika hali ya uchumi tuliokuwa nayo, mkate wa umasikini ilibidi ugawanywe kwa wote. Alisema, watu wanaolangua bidhaa zote na kuzificha kwapani, alafu wananchi wakiuliza tatizo ni nini wenyewe wanasema eti hali ya uchumi ni mbaya, lazima wasakwe mijini na vijijini. Akaimarisha jeshi la polisi ili liweze kupambana na hiyo tabia. Ili watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wapate adhabu kali, akaliomba bunge kupitisha muswada kwamba wale wanaouza vibali na kulangua bidhaa hadimu wapatikane na hatia ya kuhujumu uchumi badala ya kosa la kula rushwa. Akaifanya iwe kampeni ya kitaifa.

Niliwahi kusoma paper ya Maliyamkono T. na Bagachwa, M.S.D (1990) ambayo haikumuongelea Sokoine lakini iliyoonyesha dhamila ya serikali ya kupambana na wahujumu uchumi. Inaonyesha idadi ya watu toka mwaka 1980 mpaka 1983 waliokamatwa, fikishwa mahakamani, na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia. Kwa Sokoine, hii haikuwa shughuli, bali ilikuwa ni kazi, kwa maana kuwa aliona kero, akaimarisha taasisi ya jeshi la polisi kwa kuiwekea mazingira ya kisheria baada ya kupata kibali kutoka katika taasisi ya bunge.

Kazi ya waziri au waziri mkuu ni kuimarisha taasisi zote anazoziongoza. Mwalimu aliwahi kusema kuwa, nchi inaongozwa na sheria. Watu lazima wajue kuwa sheria zimebadilika ili waweze kuzitii. Nchi haiongozwi na akili za mtu. Mambo ya kuona kiongozi anatoka kwenye vilabu vya pombe, au anaamka usingizini na kuanza kutoa hamri, au kufungia taasisi mbalimbali bila mpangilio, ni mishughuliko sio kazi.

Kifo cha Sokoine, kilikatisha watu huondo wa mechi kati yake na Msuya, ambapo mwamuzi alikuwa Nyerere na Kawawa. Sheria ya kuhujumu uchumi ilikuwa ni msumeno, na yeye hakuwa na hitilafu ya kuhofia. Inasemekana vijana wenye Land lover zilizokuwa ma matunubali walionekana nje ya nyumba ya Msuya. Waliulizwa wamepata wapi mamlaka ya kumpekua waziri, lakini vijana walimuonyesha kibali cha kufanya upekuzi. Inadaiwa Kawawa ndiye aliwaondoa vijana nyumbani kwa Msuya, kitendo kilichomuhudhi Sokoine. Nyerere alimwambia Moringe kuwa mambo mengine yanahiyaji tuyafanye taratibu, na Moringe akamjibu kuwa sheria lazima zichukuwe mkondo wake. Alisema kama tunaamua kuwa wajamaa, basi iwe hivyo, vinginevyo tufatute sera zingine.

Sokoine hakutumia vyombo vya habari kutangaza aliyokuwa akifanya. Tena mambo yake mengi yalikuwa hayatangazwi mpaka alipokufa.

Mrema alipokuwa waziri wa mambo ya ndani aliongoza vyombo vilivyopashwa kusimamia haki, sheria, usalama wa raia na mali zao. Hata hivyo, kipindi cha uangalizi wake, tulishuhudia utawala uliokiuka misingi ya sheria, usio tenda haki, na ulioshindwa kusimamia usalama wa raia. Badala ya kuimarisha taasisi ya jeshi la polisi, alitoa amri za kuwalazimisha raia kulala nje wakiliwa na mbu eti wanajilinda pamoja na mali zao kwa mtindo wa jadi wa Sungusungu. Polisi walibaki maofisini wakila rushwa, kulinda wahalifu waliohujumu nchi yetu, na kuota vitambi. Raia walikuwa na nondo, majembe, mapanga, visu vya jikoni, uma na vijiko, bila hata kupata mafunzo ya aina yoyote, wakingoja usiku kucha kupambana na majangiri yenye bunduki za SMG. Kwa Mrema, eti huo ndio ulikuwa usalama wa raia na mali zao. Watu wanasema huko ndiko kuchapa kazi kwa Waziri wa mambo ya ndani.

Mwaka 1993, chini ya uangalizi wake, Paspoti mpya za Tanzania 10,000 zilipotea wakati zinakabidhiwa wizara ya mambo ya nje kutoka uhamiaji (gazeti la Uhuru januari , 14 1993). Hapakuwepo na uzembe, bali vilikuwa ni vitendo vya rushwa ambavyo vilipelekea taifa kupata fedhea kwani hizo paspoti ziliangukia mikononi mwa raia wa Somalia na wale wabeba madawa ya kulevya. Hakuna aliyekamatwa. Packets 2,000 za madawa ya kulevya ‘Mandrax" ziliyeyuka zikiwa chini ya uangalizi wa polisi (Uhuru Januari 7 1994), Kilometa za mraba 4666 ziliuzwa kwa msukumo wa rushwa (Mfanyakazi januari 20 1993). Kila siku ya Mungu, magazeti yalikuwa yakiandika wizi upolaji wa mali ya Umma, na vitendo vya rushwa, huku Mrema akinguruma kutisha raia wasiokuwa na hatia kwa kutumia vyombo vya dola. Matukio yote makubwa yaliandikwa na kupita bila kumkamata mtu.

Sasa hivi mambo ya kuhujumu uchumi ni ya kawaida, lakini kipindi cha uwaziri wa mambo ya ndani wa Mrema, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, uchumi wa nchi ulikuwa unahujumiwa chini ya uangalizi wake. Yeye ndiye alipalilia msamiati wa vigogo, alipojifanya polisi pale airport kwa kuingilia mali za wakubwa zikiwa zinatoloshwa nje ya nchi. Kwake yeye, sheria zilibagua vigogo na hazikutakiwa kuchukua mkondo wake. Hata wakati sheria zilipobadilishwa ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi, aliongoza vyombo vya dola kuwapiga mabomu ya machozi viongozi wote wa vyama vya upinzani. Aliwanyima haki ya msingi ya kuhutubia wananchi kwa kuwakatalia vibali vya mikutano. Majuzi wakati anahojiwa na Radio Butiama, akasema alifanya hivyo kwasababu alikuwa akimtumikia kafili, lakini hakusema mradi wake alioupata ulikuwa ni upi? Sokoine alikuwa hamtumikii kafili, bali aliwatumikia wananchi.

Aliyavalia njuga matokeo ya uhalifu kwa kujenga vituo vya polisi kila kona ya nchi, ili kuzuia vibaka na kuwaacha ‘vigogo' ambao ni wezi wa kweli wakipeta. Badala ya kufanya kazi ya kuliwezesha jeshi la polisi kuwa na uwezo wa kuwakamata wahalifu wote ili wafikishwe mahakamani, akaanzisha utaratibu wa kutoa siku kumi kumi. Aligeuza ofisi na nyumbani kwake kilalacha kuwa kituo cha polisi, mahakama, na jela. Hakuna mhalifu hata mmoja aliyeitwa nyumbani au ofisini kwake, alafu akafikishwa mahakamani. Wizara zina miongozo, sheria pamoja na taratibu ambazo zinatakiwa kuheshimiwa na kiongozi yeyote. Alizinyamazisha taasisi za Mahakama na Polisi, badala yake hizi taasisi zikaanza kuwa mapango ya wala rushwa. Wahalifu walitakiwa kupelekwa polisi sio nyumbani kwa Waziri. Eti watu wanasema huku ndiko kuchapa kazi.

Akaanzisha tabia mbaya ya kulala uvunguni mwa vitanda vya wanandoa. Hizi ni busara alizokopa kutoka kwa mabibi wa kijadi waliokuwa wanataka kuhakikisha kama mke aliyeolewa na mjukuu wao ana bikira au la!. Waziri unamwita mke wa mtu ofisini kwako, tena kupitia kwenye vyombo vya habari? Kwa nini Waziri anaingilia ndoa za watu? Kwa nini asiimalishe taasisi zinazoshughulika na mambo ya jamii? Nchi inaporwa, vyombo vya dola vimewekwa kibindoni, Waziri anayeongoza taasisi zote hizo yuko ofisini na mke wa mtu akisuluhisha ugomvi wa makonde yatokanayo na wanandoa kunyimana uroda, au kufumaniana. Hizi zote ni shughuli na sio kazi.
Kwa nini Mrema alipata umaarufu wakati ule na sio sasa hivi?

Kila Mrema alipokwenda, alilakiwa na ‘umati mkubwa" wa watu ukiongozwa na kitengo cha umoja wa vijana, huku wakijivinjari na mapikipiki, bendera, pamoja na jezi zao za kijani na nyeusi. Ikasadikikika kuwa Mrema alikuwa na ‘mvuto wa watu". Yote haya yalitangazwa kila siku na vyombo vya habari. Alipojiengua CCM, na kuamua kugombea uraisi mwaka 1995, matangazo ya Radio Tanzania na magazeti ya chama yalienguliwa pia. Mrema aliendeleza matangazo yake ya kuwa na mvuto wa watu kupitia kitengo cha vijana wa NCCR –Mageuzi.

Walitueleza kuwa Mrema alikuwa na mvuto wa watu kiasi cha kubebwa kila anapotokeza. Wengine walimlilia Mrema kama wafanyavyo wapenzi wa Michael Jackson. Matangazo mengine yalisema Mrema alikuwa njiani kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, lakini wakazi wa Dodoma wametembea kwa miguu kutoka Dodoma mpaka Chalinze ili kumpokea. Matangazo hayo yalionekana kuishawishi serikali kutumia vyombo vya dola ili kuzuia watu wasiende kupokea kipenzi chao. Hata hivyo, kinara wa mizengwe, Mwalimu Kambarage, aliona hiyo janja ya nyani na wakati akifungua kampeni za Mkapa pale Jangwani 1995, aliwaambia viongozi wa Serikali kuwa ‘Muacheni". ‘Kama mtu anapenda sana kubebwa, na watu wa kumbeba wapo, hata wakipokezana maili kumi kumi kama jeneza, waacheni".

Baadae Mrema alianza kuona haya, na mambo ya kubebwa bebwa yakayeyuka. Hakuwa na fedha wala ujanja wa kuendeleza matangazo yaliyokuwa yanavutia watu. Yeye hakuwa na sifa ambayo ingeendelea kuwapendeza, kuwashikilia na kuwavutia watu.

Kama mtu ana sifa fulani, mvuto wa watu unakuwepo hata kama matangazo yanakoma. Ni vema kutofautisha kati ya mvuto wa matangazo na mvuto wa sifa ambapo vyote viwili vinajenga mvuto wa watu. Matangazo yaligunduliwa ili kujaribu kuchukuwa nafasi ya sifa ambacho ni kiini katika mvuto wa watu. Hivyo basi, mvuto wa watu halisi sio sifa ya msimu kama ilivyo Kiangazi na Kipupwe, bali ni sifa ambayo mtu anakufa nayo kama Sokoine. Lakini hiyo sifa ikiwa ni matokeo ya kilemba cha ukoka kama ilivyokuwa kwa Mrema, ndipo inakuwa na tabia za msimu. Ndio maana amedolola kwa sasa.
 
Ndugu Mwanakijiji shukrani kwa kutuwekea Kumbukumbu ya Bwana Edward Moringe Sokoine,Ambao waliwahi kufanya kazi na huyu mtu watakubaliana nami kwamba alikuwa mtu wa watu na asiyependa makuu.

Siku ya Msiba wa Mzee Sokoine naikumbuka vizuri!,wengine tulikuwa ndio tunaanza utumishi serikalini, tulikuwa tupo Dodoma kwenye vikao vya Bunge ambapo Mzee Sokoine aliondoka mchana kuwahi majukumu mengine Dar, baada ya vikao vya Bunge.

Kwa maelezo ya wasaidizi wa Marehemu walipofika Dumila wilayani kilosa ndipo lilipotokea gari lililokuwa linaendeshwa na Mkimbizi Dumisani Dube na kuligonga gari la Marehemu.

Habari za ajali ya Waziri Mkuu zilifika Dodoma mapema,na watu wote waliondoka Dodoma kuwahi Morogoro ambako Marehemu Sokoine alikimbizwa kwenye Hospitali ya Mkoa.Nakumbuka majira ya saa mbili za Usiku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (Mama Anna Abdalah), akifuatana na Spika wa Bunge Chifu Sapi Mkwawa (marehemu) na Daktari wa Mkoa Dr Msimbe (Marehemu) walidokeza viongozi wa Mkoa kwamba PM amefariki.

Mwalimu JK alilihutubia Taifa usiku huo huo, na kutangaza wiki moja ya maombolezo! Jamani nakumbuka ilikuwa siku ya Hudhuni mkubwa, Nchi nzima ilizizima kwa kuondokewa na kipenzi cha watu.

Tumkumbuke Marehemu Sokoine kwa kuimarisha Uongozi Bora na kujali Matakwa ya wengi! Tufuate nyayo zake kwa kuwajibika kwa Dhati na kuwa Watumishi wa kweli wa Umma wa wa-Tanzania.
 
Tunapaswa kumkumbuka kwa kutekeleza yale yote aliyoyapigania kwa nguvu zake zote hasa haki sawa kwa watanzania wote na kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.
 
Mzee Mwanakijiji,

Heshima yako kwanza,

Nakumbuka mwaka 1995, katika hotel ya Kirimanjaro, Eda Sanga, aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania, alishauri umuhimu wa kuwa na utaratibu wa kuwaandaa viongozi wa kitaifa. Alimkumbusha Mwalimu Nyerere jinsi alivyokuwa "akim-groom" Moringe Sokoine kuliongoza taifa baada ya yeye kung’atuka, lakini mauti yakamkuta. Mwalimu hakuwa mtu wa kutoa machozi hadharani, lakini Eda Sanga aliwakumbusha waandishi wa habari jinsi kifo cha Sokoine kilivyomliza Mwalimu. Alimuuliza Mwalimu kuwa, kwa nini tusiwe na utaratibu wa "kuwa-groom" viongozi wa kitaifa?

Mwalimu alijibu kwamba yeye hakuwahi "kum-groom” Sokoine ili achukue nafasi yake aking'atuka. "Sokoine alikuwa kiongozi chini yangu, lakini kama mambo yalikuwa hayaendi vizuri, ananiambia kuwa Mwalimu mambo hayaendi vizuri”. Kulikuwepo ukimya wa dakika kama mbili, alafu aliendelea kusema kuwa Sokoine hakuwa na sababu ya kutokumwambia mkubwa wake wa kazi kuwa mambo hayaendi vizuri”.

Katika tukio lingine mwaka 1995, nyumba ya mwalimu ya msasani ilikuwa inafanyiwa matengenezo, hivyo, akawa anaishi kwa muda kwenye nyumba ya Waziri Mkuu karibu na St. Peter, Osterbay. Aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuongelea sakata la kumchuja mgombea uraisi ndani ya CCM. Nakumbuka Lowasa na Kikwete walikuwa na mtandao ambao ulikuwa umepenyaza hata kwenye vyombo vya habari. Pia ilikuwepo minong'ono ndani ya vyombo vya habari kuwa Mwalimu alikuwa anampinga Lowasa.

Katika mkutano huo, mwandishi mmoja wa habari ambaye hakutumia utaratibu wa kunyoosha mkono kuuliza swali, na alikuwa nyuma, aliamua kupaza sauti gafla, na kusema kuwa, miongoni mwa wagombea wa CCM kuna anayefaa kuongoza kwasababu ni mchapa kazi, kijana, na ni Mmasai kama alivyokuwa Sokoine. Ingawa hakutaka kumtaja jina, lakini ilijulikana bayana kuwa kambi iliyokuwa inataka kujulikana kwa hizo sifa ni ile ya Kikwete na Lowasa. Nyongeza ya Mmasai, iliashiria kuwa mlengwa alikuwa Lowasa.

Ulikuwepo ukimya wa muda mfupi. Hilo halikuwa swali, bali maelezo katika mtindo wa ulopokaji, na aliyeyatoa hayo maelezo hakujitambulisha anatoka chombo gani cha habari. Katika hali ya kawaida, mwalimu alikuwa hajibu maelezo ya namna hiyo. Kwa mshangao, Mwalimu hakuuliza jina la mtu mwenye hizo sifa, bali aliamua kutoa maelezo mafupi yaliyoashiria kuwa alimfahamu mlengwa, na hakutaka hata kutaja jina lake katika hayo maelezo. Alisema Watanzania watafanya makosa kudhani kuwa wamasai wote ni kama Sokoine. Pamoja na madaraka aliyokuwa nayo, Sokoine alikufa na pair mbili za viatu.

Baada ya mwalimu kutoa hayo maelezo, mwandishi mwingine alinyoosha mkono na kutoa maelezo kuwa watanzania sasa hivi wamechoka kuongozwa na wazee, na wako tayari kuongozwa na vijana. Aliongeza kuwa miongoni mwa wagombea ndani ya CCM, wapo wenye sifa hizo na sura nzuri zenye mvuto wa watu zitakazo irahisishia CCM ushindi dhidi ya tishio la Mrema. Mwalimu alimkatisha huyo mwandishi na kumwambia kuwa hatufanyi posa, bali tunamtafuta Raisi wa nchi. Kama unaona kuna mmojawapo wa wagombea ndani ya CCM ana sura nzuri, basi kanywe naye chai.

Bahati mbaya, mtu kama mimi na wengine ambao ni kizazi chetu, hatukupata nafasi ya kushuhudia kwa macho yetu utendaji kazi wa Sokoine kwa sababu ya umri tuliokuwa nao wakati huo. Ningefurahi kama tungekuwa na vitabu vingi vinavyoelezea maamuzi aliyokuwa akiyafanya Sokoine na mazingira yaliyosukuma hayo maamuzi. Ingekuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vijavyo, kama watu waliofanya kazi na Sokoine wangetuandikia vitabu vinavyoonyesha sifa zilizomfanya awe tofauti na viongozi wenzake kwa wakati huo. Kuna kitabu kimoja tu cha maana kuhusu maisha ya Sokoine ambacho kwa mawazo yangu hakitoshi.

Kuna manabii wa uongo wanaotaka kujifananisha na Sokoine ili kukoga nyoyo za watanzania, na kutulaghai sisi ambao hatukubahatika kuona matendo yake. Wasiwasi wangu ni kuwa hawa manabii wataendelea kujitokeza hata siku za usoni. Maneno ya mwalimu katika mikutano miwili na waandishi wa habari niliyoielezea juu, yalikuwa ni bakora ya kuwashushuwa hawa manabii. Ningefurahi kuyaona haya maneno kwenye vitabu vya historia ya nchi yetu.

Kutokana na simulizi za watu waliomjua Sokoine, na kwa kusikia maneno ya Mwalimu ambaye alikuwa mkuu wa Sokoine kikazi, naamini kuwa Sokoine alikuwa miongoni mwa watu wachache waliounganisha cheo, busara, na uongozi katika nafsi ya mtu mmoja. Watu mithiri yake, ni kama Kakakuona, kwa maana kwamba, wanazaliwa mara moja katika miongo kadhaa.
 
Jamani ukweli kuhusu kifo cha Sokoine usemwe maana walioshuhudia wengine wanazeeka na kufa. Tuweke sawa historia, after all hata kama kuna siri kwenye secret files miaka zaidi ya 20 imepita tayari.

Ule uvumi kuwa alikuwa na majeraha ya risasi kifuani uwekwe wazi ,kwa nini dube hakuchukuliwa hatua? kuna tetesi kuwa maelezo ya Dube yalikuwa mwiba kuendelea kuwepo nchini, wanadai yeye alisema baada ya ajali alishuhudia mtu mrefu mweusi akiongozwa na askari ku-escape akitembea mwenyewe na alishangaa kusikia huyo mtu alikufa. Je, waliomuhamisha kwenye gari lingine walifanyaje?

Ni wakati wa kusafisha hali iliyokuwepo, na kama hizi ni imani potofu ziondoke masikioni mwa watu..kwa nini isiundwe tume ili ukweli ujulikane na kama kuna waliotuhumiwa waweze kusafishika if possible?

Nawasilisha!
 
Kama huna sababu mhimu sana inayokuzuia kukusanya habari za marehemu Sokoine na kuziweka kwenye kitabu, basi inafaa ufikirie kuifanya kazi hiyo.

Sababu ya wewe kuwa mdogo wakati huo sio ya msingi. Si lazima uandike peke yako, lakini unaweza kuwa chachu na mshiriki imara kati ya kundi la watu kama akina Mawado mnaoweza kuendesha na kuifanikisha shughuli mhimu kama hiyo.

Baadhi ya matatizo yetu mara nyingi ni haya ya kutegeana. Kumsubiri mtu mwingine afanye.
 
Mwendapole na wengine, mkumbuke kuwa katika Tanzania hakuna kiongozi au mtu anayekufa kwa kifo cha kawaida! Vifo vingi kama siyo vyote hutafutiwa maelezo ya kishirikina au njama!

Wakati Sokoine anakufa kuna watu waliodai kuwa amechukuliwa msukule, na kuna watu hata walidai ati "alionekana" mahali fulani! Hili si kwa viongozi tu hata watu wengi wanapopoteza ndugu zao kitu cha kwanza wanajaribu kutafuta "nini kilimuua". Hapa imani za kishirikina hutana, watu watatafuta nani kalogwa na nani? Nani aliapizwa na nani kabla hajafa na nani alinyoshewa kidole na nani!!

Vifo katika Tanzania ni vitu ambavyo vinatokea kwa sababu ya watu wengine hata kama mtu atakufa kwa Ukimwi watu watasema labda kalogwa! Ukweli wa mambo ni kuwa ajali hutokea na watu hufa hata wawe wamependwa vipi.

Suala la njama za vifo vya viongozi siyo geni kwani tunatarajia kuwa viongozi wana utaratibu mzuri wa kuhakikisha usalama wao. Kwa wale mnaokumbuka maelezo ya jinsi ajali ilivyotokea utaona kwamba ilionekana kuwa kana kwamba Dumisane Dube "alilenga" gari la Waziri Mkuu baada ya kuyapita magari ya usalama yaliyotangulia hadi kulifikia la Waziri Mkuu!
 
Mzee Mwanakijiji,

Nipo mjini hapa nayaona yote LIVE. Na kwa mara ya kwanza nimegundua kuwa pamoja na kwamba Watanzania walio wengi hawafahamu maana halisi ya neno UHURU na matumizi yake, sasa nimekuja gundua kuwa - pia wengi hawafahamu maana halisi ya neno la kibiashara SOKO HURU. Na hii inawafanya wengi kuamini ama kukubali mfumo mzima wa uongozi huu wa -CHUKUA CHAKO MAPEMA - unaoendelea. Brother, sasa hivi ni kweli chukua chako mapema sii CCM, Chadema wala mjomba wake. Lawana hazina nafasi tena maanake Tatanic ndio imeisha jaa maji!...uzalendo ni kuokoa abiria ama kujiokoa mwenyewe lakini sii meli tena. Tanzania hakuna tena Politician ila ni viongozi wafanya biashara.

Kwa mtazamo wa haraka haraka nadiriki kusema kwamba leo hii Tanzania wakulima ni aslimia chini ya 20, wababaishaji 40, Wajasiriamali 10 kati yao asilimia 90 ni ndugu ama jamaa za viongozi ktk taasisi mbali mbali. Kila kampuni kubwa ina mkono wa kiongozi na kila jengo kubwa mijini ama kiwanja kikubwa kina mkono wa kiongozi. Yaani kuna kiongozi ana redio kila mkoa na TV, bob pima mwenyewe!

Sasa Bi. Asha hiii habari sijui anaipokea vipi....

Lakini pamoja na yote hayo jamani TZ ni nchi ya kuchuma....purchasing power ni ndogo sana kwa mtazamo wa kiuhumi lakini bob watu wanafanya matusi ktk matumizi ya anasa....damn nimechokaa!

Watu wana hela kama vile hakuna kesho yaani huwezi kuzungunzia 2/m USd kama ni deal mbele ya wanaume (wenye nazo).

Wanabodi, tutazungumza zaidi nikirudi huko kwenye nyenzo za uhakika ili nikamilishe lile hoja nililoacha kiporo na kifupi nitasema kwamba SIDHANI kama TZ itakuja kujikwamua kiuchumi kama nchi hivi karibuni... Gonjwa hili limeisha kuwa sugu halina dawa tena. Siii kisayansi, Kisiasa wala kwa kupitia kamati za ufundi.

Join the Club!
 
Family friend wangu mmoja ambaye alikuwa waziri ktk awamu ya kwanza na ya pili amenisimulia visa vifuatavyo kuhusu Marehemu Sokoine;

Anasema Marehemu Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia kuna siku akifanya kazi sana asubuhi mchana akienda lunch huwa analala kidogo kabla hajarudi Ikulu kuendelea na kazi. Kuna siku ilitokea dharura ya kikazi na Marehemu Sokoine akiwa ni PM alitaka maelekezo ya Mwalimu. Akapiga siku akaambiwa Mwalimu kapumzika kidogo, akasema muamsheni, Mwalimu akaamshwa tatizo likatatuliwa.

Anaendelea kusema huyu Bwana alikuwa mfuatiliaji SANA ktk utendaji wa kazi, alinipa mfano Sokoine alipokuwa PM alimwita waziri wa ulinzi ampe update ya silaha zilizopo katika makambi mbalimbali ya jeshi. Siku ya pili bila waziri kujua, Sokoine akawa anapiga simu kwa wakuu wa vikosi mwenyewe wampe data kazi ambayo imemchukua siku moja tu. Baada ya wiki 2 waziri anakuja na "update" yake na anakuta tayari mwenzie anayo na la kushangaza iliyo sahihi zaidi!

He was true leader, big loss to the nation.
 
Ukweli wa mambo kuhusu kifo cha Sokoine,haujulikani,lakini kuna Tetesi ambazo sikudhani kama ilikuwa muhimu kupuuzwa kwamba Sokoine ameuwawa.Katika msafara wake kulikuwa na magari matatu yaliyotangulia,yalivukwa magari mawili na lile la tatu lilijaribu kulikinga gari la marehemu bila mafanikio,sasa kwa hesabu za haraka haraka ni rahisi kupata wazo kwamba kulikuwa na mkono wa Mtu! na ukizingatia kipindi hichi ndio kile cha kuwabana Wahujumu Uchumi.

Tetesi za kwamba Sokoine ameuwawa zilienea na kulikuwa na uvumi pia kwamba wakati wa jioni alikuwa anaonekana ktk viwanja vya Bunge la zamani Karimjee Hall (Dar).Mwalimu alihutubia Taifa mahsusi kuhusu tetesi hizo,na alitoa maelezo kwamba "Mpendwa Sokoine amekufa kwa amri ya Mwenyezi Mungu" na hataki kusikia uvumi wowote kuhusu kifo chake! na atakayebainika kuvumisha mambo hayo atamfunga!Huo ndio ulikuwa mwisho wa Tetesi hizo!.

Kwa wale wenye wazo la kuandika kitabu ni vyema,kwani ndio itakuwa njia sahihi ya kumuenzi Mzee Sokoine vinginevyo Historia itamsahau mapema!.Katika uandishi wako jaribu kumtafuta Mzee Philemon Mgaya na Hans Kitine wana hadithi nzuri itakayorutubisha kitabu hicho.

Dada Asha naomba uondoe maneno yako ya kumfananisha Moringe na Ngoyayi ni watu tofauti.Kumbuka maneno ya Mwalimu kwamba "wamasai wote sio kama Sokoine"!Kiona mbali cha Mwalimu kilikuwa kinafanya kazi vizuri,kwani Lowasa aliyekuwa anamzungumzia wakati huo alikuwa msafi! Sio huyu wa leo aliyejaa tope mwili mzima!!Namkumbuka Mwalimu kwani aliwahi kusema kuwa "angalieni sana vijana wenye sura za Mama zao,wanapendeka/za lakini ni wajanja wajanja na wahuni tu!,hawana cha maana cha kutueleza",alisema hayo alipowafukuza viongozi walioanzisha mgomo kule Sokoine University - Morogoro.Leo hii naona tena kigezo cha Sura kinatumiwa kuwapa watu Uongozi wa Nchi!!
 
18 Reactions
Reply
Back
Top Bottom