Makala hii imetoka RAIA MWEMA-28/11/2007 na imeandikwa na P-Karugendo. Ilikuwa ndefu lakini nimeweka kipande tu ambacho tunaweza kufanya comparison kati ya TZ na Rwanda.
Mambo mengi yalinishangaza Rwanda kinyume na nilivyotarajia. Kutoka mpakani hadi Kigali, sikuona askari mwenye bunduki. Ina maana kwa muda mfupi, wameweza kujenga amani na utulivu.
Lakini la kushanga zaidi ni uchumi wao. Pale mpakani nilipotoa shilingi 10,000 za Tanzania, nilipewa 3,500 za Rwanda. Ni wazi niliibiwa kidogo, lakini ukweli ni kwamba pesa ya Rwanda ina nguvu zaidi ya Tanzania. Wenyewe wanasema ni shilingi 10,000 kwa shilingi 5,000 za Rwanda lakini kwa maisha ya kawaida ya mpakani ni 3,500 hadi 4,000.
Swali ambalo bila shaka linaweza kujibiwa na wanauchumi, ni inakuwa vipi, Rwanda, nchi iliyokuwa vitani, nchi ambayo haina rasilmali nyingi kama Tanzania, iwe na pesa yenye nguvu kuliko Tanzania?
Mfano, Mkoa wa Kagera, ni mkubwa zaidi ya Rwanda. Mkoa wa Kagera, una rasilmali nyingi, una ardhi ya kutosha, mazao mengi ya biashara yanastawi, una misitu, una madini, una ziwa lenye samaki wengi, una watu milioni mbili. Ukilinganisha watu wa Mkoa wa Kagera na rasilmali zilizopo, kila mtu angekuwa na maisha mazuri. Rwanda ina watu milioni tisa na rasilimali kidogo ukilinganisha na Kagera, lakini Rwanda imeendelea kwa mbali ukilinganisha na Mkoa wa Kagera.
Wanyarwanda, wanasema maendeleo yao yanatokana na rasilmali watu na uongozi bora. Ni kwamba Rais Paul Kagame na viongozi wenzake wana vision na mikakati ya kuendeleza taifa lao. Wana mipango mingi na wamefanya mengi, hapa ninataja yale tu niliyoelezwa kwa muda mfupi niliokaa Kigali: Mpango wa kufuta magari ya serikali, umepokewa na kukubaliwa na wengi. Leo hii kila Mnyarwanda, anatambua jinsi pesa nyingi za serikali zilivyokuwa zikipotea kwa kuyashughulikia na kuyatunza magari ya serikali.
Mpango wa kuwajibishana, umewavutia walio wengi. Hakuna kulindana katika serikali ya Rwanda, hakuna urafiki wala kulindana; anayeshindwa kuwajibika, anafukuzwa bila kujali cheo chake au mchango wake wakati wa vita ya ukombozi. Kinachotangulia na kujenga taifa, na wala si urafiki, undugu au chama. Mpango wa kuwasikiliza wananchi na kutambua kwamba serikali ipo kuwahudumia wao, umewavutia wengi. Nimeambiwa kwamba Rais Kagame, anapotembelea wilayani, viongozi wanakuwa matumbo joto, maana akijitokeza mwananchi akalalamika na malalamiko yakawa ni ya kweli, mkuu wa wilaya anaweza kupoteza kazi hapo hapo!
Mpango wa kujenga utaifa na kufukia tofauti za makabila , umepokewa kwa shangwe kubwa na wote. Ingawa ni vigumu kuangalia kwenye mioyo ya watu, yale yanayoonekana kwa nje yanaleta matumaini makubwa. Mpango wa kufuta uongozi wa mikoa, na kupeleka madaraka yote wilayani , umewavutia watu wengi na umepunguza gharama zilizokuwa zikitumika kufanya mambo yale yale kwenye ngazi ya mkoa na ngazi ya wilaya.
Mfano Mganga Mkuu wa Mkoa na Mganga Mkuu wa Wilaya. Watu hawa walikuwa na kazi zinazofanana, matumizi yalikuwa yakiongezeka bure. Hivyo kwa ngazi zote, ni kutoka wizarani na kwenda wilayani. Pesa nyingi zilizokuwa zikitumika kwa mishahara ya watumishi wa mikoa, zinatumika kwa mambo mengine, na mambo haya yanaonekana!
Mpango wa kujenga shule nzuri na vyuo vizuri, umewavutia Wanyarwanda wengi. Watoto wa Rais Kagame, wanasoma Kigali. Watoto wa viongozi na matajiri wanasoma Kigali. Hivyo wakiongea juu ya kujenga shule, watu wanawaamini.
Maendeleo ya Rwanda, yanaonekana kwa macho. Si lazima uwe mtaalam wa uchumi kutambua kwamba Rwanda, inapiga kasi ya kutisha ya maendeleo. Jiji linavyojengeka, barabara zilivyopangiliwa, usafi, huduma muhimu kama ubora wa hospitali, vijiji vilivyopangiliwa, ubora wa mashamba ni ishara tosha kuonyesha maendeleo ya nchi.
Serikali ya Rwanda inapambana na rushwa na inaelekea kufanikiwa. Juzi, walifukuzwa askari zaidi ya sitini, baada ya kubainika wamepokea rushwa, walikamatwa baada ya mama mmoja askari wa cheo cha juu kujibadilisha na kujifanya dereva wa lori la mkaa. Wana mbinu nyingi za kuwakamata wala rushwa.
Linaloshangaza zaidi ni uzalendo wa Wanyarwanda. Watu hawa wanalipenda taifa lao. Inaonekana wazi kwamba kila mmoja anafanya kazi kufa na kupona ili kulijenga taifa lake. Na wanaposema juu ya taifa lao, wanasema kwa majivuno.
Kuna rafiki yangu mmoja, aliyeniambia kamba ili Tanzania iendelee ni lazima Watanzania wabadilike, wawe na moyo wa uzalendo na walipende taifa lao. Huyu ni Mnyarwanda, aliyeishi Tanzania kwa miaka mingi. Bila shaka alikuwa na maana yake kusema hivyo.
Lengo la makala hii ni kutaka kutoa ujumbe kwa Watanzania kwamba tuna mengi ya kujifunza kutoka Rwanda. Ni nchi ndogo yenye mambo makubwa. Badala ya kusema uchumi wetu unapaa wakati shilingi 10,000 za Tanzania ni sawa na shilingi 3,500 za Rwanda; badala ya kuendelea kuyahudumia magari ya serikali wakati tunachangisha wananchi kujenga sekondari za kata; badala ya kuendelea kuwahudumia watumishi wa mikoa na wilaya, wakati hatujajenga hospitali za kutosha; badala ya kuendeleza urafiki na utamaduni wa kulindana wakati mambo yanakwenda vibaya serikalini, ni bora kukubali kwenda kujifunza kwa jirani zetu wa Rwanda.
Ninaamini Weusi tuna akili nzuri. Tatizo ni kwamba tunateleza na kuanguka, na wakati mwingine tukianguka, ni mwereka wa mende, tunashindwa kuamka na kuendelea na safari. Tanzania, tumeteleza na kuanguka, anayekataa, si mkweli!
Juzijuzi tuliwafukuza maelfu ya Wanyarwanda kutoka Karagwe. Watu hawa walikuwa wamelima mashamba makubwa na kuzalisha chakula kingi, walikuwa wafugaji. Kukaa kwao kwenye maeneo ya Bushangaro na kwingineko, kuliwafukuza wanyama. Walipoondoka, mashamba yao yamegeuka mapori na wanyama kama Tembo wameanza kusogea tena na kutishia maisha ya wakazi wa Karagwe.
Mbunge wa Karagwe Brandes Begumisa, alilalama bungeni, kwamba watu wake wa Karagwe, wanashambuliwa na wanyama pori. Hakumbuki kwamba hayo ni matokeo ya kuwafukuzwa Wanyarwanda. Tuliwafukuza bila kuangalia mbele, tuliwafukuza bila mipango inayoeleweka. Tungewaacha, wakalima, wakafuga, tukawatoza ushuru, ingechangia kiasi kikubwa maendeleo yetu. Tumewafukuza na sasa tunapiga kelele kwamba tunashambuliwa na wanyamapori.
Wakati umefika wa kujihoji na kutafuta tulipoteleza. Wakati umefika wa kujiuliza ni mawaziri wangapi ambao watoto wao wanasoma kwenye sekondari za kata; hakuna waziri asiyetoka kwenye kata; ni mawaziri wangapi ambao watoto wao wanasoma sekondari za Tanzania.
Wakati umefika wa kukubali kujifunza hata kama ni kutoka kwenye nchi ndogo kama Rwanda. Tusipokubali kujifunza, majuto ni mjukuu!