Tunahitaji viongozi watanzania zaidi 2010 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunahitaji viongozi watanzania zaidi 2010

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by chuhila, Jul 28, 2010.

 1. c

  chuhila Member

  #1
  Jul 28, 2010
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 11
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  TUNAHITAJI VIONGOZI WALIO WATANZANIA ZAIDI.


  Utaratibu wa kuwa na dola haujaanza wakati wa enzi hizi za hivi karibuni, bali ni wa muda mrefu sana. Si rai yangu kutumia kalamu hii muda huu kuonesha ni namna gani dola ilianza lakini natamani angalau niseme umuhimu wa dola ulianza baada ya idadi ya watu kuwa inaongezeka kwa kasi, ongezeko ambalo lilisababisha watu kuanza kushindania kupata riziki zao ambazo pengine wasingeshindania endapo wasingeongezeka zaidi. Shindanio hilo la kutaka kupata mahitaji mbalimbali kutoka katika mazingira lilisababisha watu hawa kuanza kuingia katika migogoro mbalimbali. Kwa sababu binadamu huyu anahitaji maisha mazuri yasiyo na uhasama aliamua kuwa na utaratibu wa kuteuana miongoni mwao, nasema miongoni mwao viongozi watakaoshughulikia matatizo na migogoro yote itokanayo na jitihada za kila mtu kutaka kujipatia akitakacho kutoka katika mazingira asilia, hapa ndipo dhana nzima ya uongozi inapoasilia. Jamii zote duniani ikiwemo kule kunakosemekana kihistoria kwamba ndiko demokrasia ilikoanzia yaani Ugiriki ya kale zilianza kutengeneza uongozi au dola.
  Nieleweke mapema kwamba nimesema viongozi walitoka miongoni mwa wanajamii wenyewe; ndiyo, kwani wangetoka wapi? Jamii zilikuwa zinafanana na watu wake pia walikua wanafanana. Tokea enzi hizo, bila kuelezea vipindi tofauti tofauti vya kiuongozi tokea binadamu wa kale kila jamii duniani imejiwekea mifumo yao iliyoboreashwa (kwa mitazamo ya walioamua kuitumia) ya kupata viongozi.
  Tanzania kama sehemu tu ya jamii ya dunia hii hai pia ina mifumo kama siyo mfumo wa kuwapata viongozi wake. Nasema yapasa viongozi wa Tanzania wawe watanzania zaidi. Ndio, lakini simaanishi kuwa viongozi ndiyo wawe wanahaki ya uraia zaidi. Nini maana yangu basi? Tutaiona hivi punde.

  Nchi yetu kwa mujibu wa katiba, mwaka huu itafanya uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wakiwemo rais, wabunge na madiwani. Hawa ndio wanaopaswa kuwa watanzania zaidi. Tanzania yenye karibu asilimia 80% ya wananchi wanaoishi vijijini, asilimia 14% ya wanaopata umeme, yenye wazazi wengi wanaopata shida katika huduma za uzazi; walio na watoto wanaokutana kwenye majengo mfano wa vyumba vya madarasa lakini havina madawati kama pengine vimebahatika kusakafiwa, yule mtanzania anayelazimika kupanga foleni zaidi ya saa sita ili apate huduma ya hospitali na maji kwenye mabomba/vyanzo vilivyo umbali wa zaidi ya kilomita 15, foleni za magari ambayo nayo ni ya kugombania mno hasa katika jiji kama Dar es salaam.
  Mtanzania huyu anayeishi bila kujua walau baadae yake itakuaje, kwani hajui aamkapo asubuhi atakula nini, kama akibahatzika kupata uji uliotiwa chumvi kama mimi miaka kadhaa nyuma huko kijijini basi kwake ni furaha lakini hajui mchana na jioni zake zitakuaje. Mtanzania anayejua nini maana ya kutokuwa na chakula, malazi na nguo (si nguo nzuri bali nguo tu). Bila kuulizana maswali mengi, tunahitaji kiongozi aliye mtanzania zaidi. Sina hakika sana kama hawa wanaojitia kutangaza nia na kusema wameombwa na wananchi kugombea kama kweli ni watanzania zaidi. Sidhani kama huyu anayetangaza nia anaweza kuwa mtanzania zaidi kiasi cha kuwafanya wanajamii wenzake wamuombe awe kiongozi wao kama ilivyokuwa hapo kwa binadamu wa kale kama yeye hajawahi kuona jengo liitwalo darasa ambalo halina sakafu, madawati, viti na mambo yote hayo niliyokwisha yataja awali kwa sababu alipata huduma zote hizo kwa kiasi cha juu, asingeweza kuona watanzania wenyewe wanaishije na kusomaje.

  Tujiulize Je, huyu mwenzetu ameishi nasi? Amekula nasi? Tunafahamiana naye vizuri kama mwanajamii mwenzetu? Kuna jimbo moja lililopo wilayani Iringa ambako mmbunge wake huwa anashinda kwa urahisi sana kwa sbabu mpinzani wake ndani ya chama huwa anangÂ’aa eneo hilo wakati wa mchakato wa uchaguzi tu, na baada ya hapo huondoka kwenda kwake kwa kufikia Marekani. Siwezi kuthubutu hata kidogo kusema kwamba mbunge huyu anayemshinda mwenzie ni mtanzania zaidi kwani naogopa sioni akiwa na sifa nilizozitaja. Tumeshasoma sana na tutasoma zaidi (japo inakera macho na akili) kuwa mgombea mtarajiwa fulani au kiongozi fulani aliyeko madarakani na anatarajia kuiwania tena nafasi hiyo wakisemwa wametoa zawadi kwa kikundi cha akina mama, vijana, walemavu, SACOS n.k ili kusaidia hiki na kile kwa lengo la kujihalalishia kupendwa na kukubarika katika eneo tarajali la kugombea. Kama hawa wangekuwa watanzania zaidi walio miongoni mwetu, wanaoishi katika jamii inayomteua mwenzao kuwaongoza hakika wasingeweza kutoa zawadi kununua ushawishi wao kwa wananchi.
  Wale wote wenye adhma ya kuomba uongozi pamoja na kwamba kwa mahitaji ya jamii hampaswi bali jamii ndio inapaswa kuwaomba na kuwabembeleza muwe viongozi wao baada ya kujiridhisha kwamba mnafaa kuwaongoza, nasema sitii mchanga kitumbua chenu ila rai yangu kwenu ni kwamba ninyi ni watanzania zaidi? Kama si watanzania zaidi mtawezaje kuwatumikia wtanzania? Si kweli na wala sina nia ya kumaanisha kwamba wasio na sifa tajwa hapo juu si watanzania, Hapana, kwani kuwa mtanzania si mkosi bali ni baraka na furaha kubwa na kuwa na sifa hizo ni kudhihirisha utanzania wako zaidi kwa kuwa ndio kundi kubwa zaidi la wananchi (wenyenchi). Sina maana pia kwamba wtanzania wengi wamelaaniwa kwa kuwa na maisha ya kila siku ni aheli ya jana lakini huu ndio ukweli usiohitaji kualika wageni/wataalamu kutoka nje kuja kurudia kuusema, na pia sina maana kwamba kiongozi wa Tanzania ni lazima awe masikini, msisitizo wangu utabaki awe mtanzania zaidi.
  Hata wale ambao mama zao walipokaribia kujifungua walisafiri kwenda nje za nchi kupata huduma za uzazi salama (wakikwepa huduma za watanzania, ambazo sifa zake zinafahamika) na kurudi, walioishi/wanaoishi katika majumba yenye thamani ya kulisha kata kadhaa au hata mkoa kwa mwaka mzima, waliosoma vizuri (na pengine kutengenezewa vyeti bila kusoma). Hawa pia hapana haja ya mjadala, ni watanzania lakini nasikitika kwamba si watanzania zaidi. Na hawa ambao wanaandaliwa nafasi za uongozi kwa sababu majina yao yalikwishaingia kwenye mfumo wa uongozi wa nchi na wana watu fulani serikalini; hawa nao ni watanzania kwa maana ya uraia, lakini nasikitika wote hawawezi kuwa viongozi wazuri wa watanzania kwa kuwa wanakosa utanzania zaidi. Kwani kuna ubishi kwamba nafasi nyingi za siasa zinashikwa na majina yale yale yaliyozoeleka masikioni mwetu katika historia ya uongozi wa nchi yetu? Hapana ubishi. Kuna majina ambayo mimi binafsi toka nimepata akili ya kutambua mambo naendelea kuyasikia hadi kesho, hii inakera sana. Nchi hii si ya kifalme kuachiana madaraka kwa kufuata koo.
  Tazama historia fupi ya nchi hii huru, angalia viongozi wake waasisi, walikotoka, walivyoishi, walivyoongoza na walivyosema na kutenda. Kwa kiasi kikubwa walionesha kuguswa zaidi na hali za watu wao wanaowaongoza, walikuwa na sifa za kuombwa kuongoza. Huwezi kumuongoza mkulima wa mahindi namna ya kulima wakati wewe mwenyewe hujui jembe, mbegu na hatua zote kiujumla za uzalishaji wa mahindi. Huyu anatakiwa kuwa miongoni mwa wakulima wanaojua vizuri njia wazitumiazo kulima mahindi ambaye atawaongoza, huyu ndio watamuomba kwa dhati yao kabisa kuwa kiongozi wao. Kwa bahati mbaya kabisa viongozi waliopo sasa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hawatoki katika kundi hili lililo kubwa la watanzania zaidi. Wanatoka katika tabaka fulani la juu na la kati (kidogo). Kama hujabahatika (na kutobahatika si mkosi) kuzaliwa miongoni mwa matabaka haya sahau habari ya wewe kuwa kiongozi. Kama katika historia ya uongozi wa nchi jina lako linabahati mbaya ya kutowahi kutoa viongozi, sahau pia habari ya wewe kuwa kiongozi. Kwani utakuwa umekosa kutokea katika tabaka la juu ili moja kwa moja uingie uongozini na pia historia ya jina lako itakuwa haikupatii nafasi ya hata kupewa fadhila. Fadhila? Kwani babu yako au baba yako au hata mjomba wako walifanyia nini uongozi wa nchi yetu au chama chetu. Kama hakuna, huna nafasi ya fadhila.

  Tumeona wengi wakianza harakati zao za kusaka uongozi kwa udi na uvumba kwa kutafuta kwanza uongozi wa taasisi mbalimbali zikiwamo vyama vya michezo, vilabu vya soka, udhamini wa shughuli mbalimbali za vijana n.k ili wajiongezee sifa. Huhitaji kushika nafasi tofauti tofauti katika taasisi au kuwashawishi watu kwa nguvu kwenye dhana ya uongozi inayotaka miongoni mwa wanajamii ateuliwe mmoja wa kuwaongoza. Huyu wa kuteuliwa kutoka katika jamii ataonekana bila hata ya kupigiwa filimbi. Kwa hiyo basi wale wanaosema wameombwa wakagombee wakati jinsi walivyo hawafanani hata kidogo na wale wanaosema wamewaomba hawatendi haki kwani wanasema uongo. Ndiyo, kiongozi mzuri huombwa kuongoza, ifahamike pia kwamba kumuomba kiongozi mzuri agombee si kazi rahisi hata kidogo kwani mara nyingi hukataa kwa kuogopa jukumu zito la kushughulikia matatizo ya wanajamii wenzake. Mtu wa aina hii huwa anajiona hawezi kuongoza, lakini ikitokea anaikubali nafasi hiyo huongoza vizuri. Jiulizeni enyi vingozi wetu na viongozi wetu watarajiwa mliombwa/mmeombwa? Mlikataa baada ya kuombwa kuwa viongozi kwa kuwa mliogopa kupewa jukumu zito la kuwaongoza waliowatuma? Nini sasa mmekifanya kwa ajili ya wanajamii wenzenu? Majibu bila shaka ya maswali yote haya wanayo wenyewe. Tumeshuhudia wengi wakifurahia sana kuteuliwa kuwania nafasi za kisiasa/uongozi, jiulize kidogo tu wanafurahia nini wakati jukumu la uongozi ni zito? Wameshindwa hata kuchukua busara za waasisi wa nchi yetu kwamba uongozi ni mzigo mzito kwani wenye njaa, wasio na maji wasio na hospitali na wote watanzania wenye matatizo wakuangalia wewe, kweli utafurahia kuwa kiongozi kama lengo lako ni kuwaongoza wananchi wajikwamue na matatizo yao? Hutaweza kufurahia utahudhunika. Wanafurahi kwa sababu mbili hivi, mosi hawa si watanzania zaidi na hivyo hawajui kama watanzania wanashida kupindukia na wao kama viongozi watapaswa kuwaongoza kujikomboa, pili ni kwa sababu wanajua tayari wamepata ulaji zaidi, ulaji zaidi kwa sababu walio wengi kama sio wote tayari wana ulaji mzuri tu

  Kiongozi aliyemtanzania zaidi hawezi kutembelea waliompa ridhaa ya kuwaongoza akiwa ndani ya gari lililofungwa vioo vyake vyote huku wenzake hao wakiwa na hamu ya kumuona mpendwa wao huyo.

  Nihitimishe upesi basi, kwa kusema kwamba, ni dhahiri tunahitaji wenzetu ili watuongogoze katika mambo mbalimbali. Katika mchakato mzima unaoendelea wa kuwapata viongozi katika uchaguzi mkuu ulio mbele yetu, ili tuwe na uwakilishi mzuri wa mawazo yetu na hisia zetu inatubidi basi tujitahidi sana kuwateua (kuwaomba) miongoni mwetu kwenda kutuwakilisha. Wanaoomba nafasi za uongozi wajione wenye deni kubwa endapo watapata uongozi kwani jamii ya watanzania inahitaji kiongozi aliyejitoa kwa dhati kuitumikia na si kiongozi anayeingia uongozini kutumikia tumbo lake na la jamaa zake. Niwaombe watanzania wote tuwe makini sana, tuache kudanganyika na porojo hewa za viongozi watarajiwa. Tujitokeze kwa uwingi wetu kwenda kupiga kura na kuchagua wale walio wenzetu/watanzania zaidi (wanajamii) kama pengine watakuwa wamekubaliwa na vyama vyao kugombea nafasi hizo. Hawa ndiyo wataweza kutenda tutakayo watuma. Suala la wanajamii hawa walioonwa kuwa watanzania zaidi na kupewa ungozi na kisha kutenda ndivyo sivyo pengine litahitaji mjadala mwingine.

  Kwa Pamoja Tuijenge Tanzania Yetu.

  Mwandishi ni Mpembuzi wa siasa na mpenzi wa habari.

  Bw. Chuhila M.J

  Barua pepe:- chuhilamj@yahoo.com
   
Loading...