Azizi Mussa
JF-Expert Member
- May 9, 2012
- 9,172
- 7,428
Utaratibu wa kuwakamata viongozi hao unaonekana kutokuwa na faida kwa CCM, hauna faida kwa viongozi wanaokamatwa, hauna faida kwa viongozi ambao hawajakamatwa, hauna faida kwa viongozi wa upinzani, hauna faida kwa wananchi na hauna faida kwa taifa kwa ujumla.
Sana sana una mfululizo wa madhara ya hatari ambayo katika hatua fulani yanaweza kumuangukia yoyote. Yaani unazalisha tatizo kama ugonjwa wa kuambukiza ambapo haifahamiki atakayeambukizwa ni nani na mwisho wake ni nini. Nitataja madhara yake kwa uchache kwa minajili ya kufanya hoja yangu iwe na nguvu.
Kwanza, Kwa upande wa wanaokamatwa mara kwa mara wanakuwa na hisia za kudhulumiwa. Hisia hizo zikijenga mizizi, watu hao wanaandaliwa kuwa watu wabaya na hatari. Wanaandaliwa kuwa watu wa visasi, roho mbaya na dhuluma na haifahamiki madhara yatakayotokana na kujenga tabia hizo yatakuwa ni ya kiasi gani na kwa nani. Je! kama nchi, hii ndio aina ya watu ambao tungependa kuzalisha? Ikumbuke tabia ya binadamu (njema au mbaya ) hujengwa na mambo anayopitia “Experience”. Kwa maoni yangu, uamuzi wa kuamua kuzalisha watu kama hawa ni hatari kwetu sote kama taifa, hivyo ni vizuri kulitizama kwa umakini jambo hili.
Pili, Kwa upande wa vyama vya upinzani ambao kwa maoni yangu hawana hoja za maana kwenye mambo mengi, wanapata hoja ya bwerere, “Unaona sisi tunavyoonewa?” kwa hiyo wanavutia huruma badala ya kuegemea kwenye mambo ya msingi ‘Appeal for sympathy”, kwa hiyo matukio hayo yanatengeneza shida ambayo haikuwa na ulazima.
Tatu, Kwa upande wa CCM, wanapata madhara makubwa ya aina mbili. Kwanza kwa wapenzi wa CCM wanapata wakati mgumu kidogo kukitetea chama kwa hoja kwa sababu ya swali moja tu “kama mna hoja, kwa nini mnawakamata wapinzani badala ya kuwashughulikia kwa hoja?”Nje ya swali hilo, CCM wana mengi mazuri sana ya kujivunia. Pili, hali hiyo inaweza kuwapa wana CCM shida ya ndani ya kisaikolojia na kuwapelekea kupunguza kiwango cha kujiamini katika ujengaji hoja na kuzisimamia.
Nne, kwa upande wa jamii matukio ya namna hiyo yanasababisha taharuki isiyo lazima kwa jamii. Na ,
Tano, matukio ya namna hiyo huivuta jamii ya kimataifa kutuangalia kwa jicho lisilopendeza. Ikumbukwe, hata kama tuko vizuri kiasi gani, kwa kadiri tunavyokuwa na uhusiano mzuri zaidi na kuaminika kwenye jumuia za kimataifa ndivyo tunavyoweka mazingira ya kufanikiwa zaidi na kinyume chake tunajiweka kwenye changamoto ambazo pengine zingeepukika.
Kwa mantiki hiyo basi, nashauri yafuatayo;-
Kwanza, Pamoja na matatizo yote waliyonayo viongozi wa upinzani, bado ni watu, ni watanzania na binadamu huwa wana matatizo mbalimbali na tunapoamua kuwa viongozi, maana yake tunakuwa tumeamua kuongoza watu wenye matatizo. Kwa hiyo ni muhimu kuwa na namna bora ya kujadiliana na kwekeana misingi kwenye mambo muhimu.
Pili, ikiwa viongozi wa vyama vya upinzani wanaokamatwa wanakuwa wanakosea mahali fulani; basi vyama husika vikutane vikubaliane juu ya utaratibu unaokubalika kwa wote na utaratibu huo uwe wazi, ili anayeuvunja kila mtu aone. Hili ni la maana zaidi na lina faida kwa watu wote ikiwemo CCM na vyama mbadala.
Tatu, ikiwa wanaokamatwa wanakuwa hawajavunja utaratibu, basi ni bora utaratibu huo ukafikiriwa upya kwa kuwa ni wazi kwamba una hasara nyingi kuliko faida, na hasara hizo katika hatua flani zinaweza kuathiri aliyekuwemo na asiyekuwemo. na,
Mwisho,Kwa mazingira ya Tanzania, CCM bado imevizidi vyama vingine kwenye mambo mbalimbali tena kwa mbali sana. CCM imefanya mambo mengi mazuri, kwa hiyo inaweza kujitangaza kwa mambo hayo na kueleweka. CCM ina rasilimali watu ya kutosha; inaweza kujibu hoja zote za vyama mbadala kiraia.
CCM ina karibu nguvu zote za msingi ili kujenga ushawishi na kukubalika kisiasa kwa mbinu za kiraia; kwa hiyo inaweza kushida kwenye uchaguzi huru na haki. Kwa hiyo ni vizuri kuhakikisha uwanja sawa wa kisiasa na kisha hawa jamaa tukawakabili kwa hoja ambazo kimsingi tunazo. Hiyo itakuwa na faida kwa Taifa, kwa CCM kwa vyama mbadala na kwa kila raia.
Ndugu zangu, tunapotathmini jambo na kubaini kuwa halina faida kwa yoyote, bila shaka si busara sana kuliendeleza, au ni nani anayedhani ipo haja ya kuendeleza jambo lisilomsaidia yeye mwenyewe wala kumsaidia yeyote? vinginevyo labda ajitokeze mtu na kuthibitisha kwamba yeye linamsaidia. Kama sivyo, ni vyema kuangalia njia bora zaidi ya kufanya siasa kwa maslahi ya wote na Taifa kwa ujumla, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua kwa busara na hatutajuta kwa uamuzi huo.