‘Tumwache Rais Magufuli awabane wakwepa kodi’

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
WATANZANIA wamehadharishwa kuendeleza siasa za majukwaani badala yake, wametakiwa kumwacha Rais John Magufuli afanye kazi yake na wamuunge mkono katika kuwabana wakwepa kodi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo alitoa angalizo hilo jana wakati akizungumzia madai ya kuwapo kwa uonevu, vitisho na kuongezewa kodi kwa wafanyabiashara walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani.

Madai hayo yalitolewa na aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa. “Wakati wa siasa za majukwaani umeisha. Rais amepatikana aachwe afanye kazi, na ili afanya kazi yake vizuri ni lazima akusanye kodi na tusianze kudhoofisha kasi na utendaji wake kwa maneno kama haya,” alisema Bulembo.

Lowassa anadaiwa kusema hayo wakati wa ibada maalumu ya kukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli alipopewa nafasi ya kutoa neno la shukrani na kutoa salamu za mwaka mpya.

Alikaririwa akidai kuwa serikali imekuwa ikiwaandama wafanyabiashara na wananchi waliokuwa wakiunga mkono upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita na kuwaambia wafuasi wake kwamba kazi ya kutafuta mabadiliko ndiyo kwanza imeanza.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Bulembo alimtaka mwanasiasa huyo kujitokeza hadharani na kutaja kwa majina, wafanyabiashara wanaodai kuongezewa kodi kutokana na kuwa wafadhili wa Chadema.

Alisema haitoshi kwa Lowassa kutoa malalamiko hayo kiujumla bila kubainisha watu hao kwani kwa kufanya hivyo, kutachangia mgongano kati ya Serikali na wafanyabiashara. Bulembo alisema kauli ya Lowassa pia imelenga kudhoofisa kasi na jitihada za Rais John Magufuli za kukusanya kodi na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi iliyokuwapo.

“Suala la kulipa kodi ni la wote wanaotakiwa kulipa kodi, bila kujali kama mtu huyo alisaidia au kufadhili CCM, CUF (Chama cha Wananchi) au Chadema. Kama unatakiwa kulipa kodi wewe lipa tu na suala la kukwepa kodi katika uongozi wa awamu ya tano halipo,” alisema.

Alisema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani, Sh bilioni 850 zilikuwa zikikusanywa kwa mwezi na kwa muda mfupi wa kuwapo madarakani zaidi ya Sh trilioni moja zimekusanywa. Alisisitiza kuwa juhudi hizo ni lazima ziungwe mkono na Watanzania wanaopenda maendeleo ya nchi.

“Tunamtaka ajitokeze na kuwataja kwa majina watu wanaoonewa na kuongezewa kodi kubwa eti kwa sababu ni wafadhili wa Chadema, kauli kama hizi sio nzuri, zinalenga kuibua mgongano kati ya serikali na wafanyabiashara ambao ndio walipakodi,” alisema Bulembo.

Wakati Jumuiya ya Wazazi kupitia kwa Bulembo ikielezwa kukerwa na wanaoendeleza siasa za majukwaani, kutoka mkoani Arusha, inaripotiwa kuwa viongozi wa kimila wa kabila la Kimasai maarufu kwa jina la Laigwanani wa wilayani Monduli, wamemtaka Lowassa kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita ya kupambana na ufisadi nchini.

Walisema hayo mjini Monduli mwishoni mwa wiki kwa waandishi wa habari baada ya mkutano wao uliolenga kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwamo ya kimila. Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya viongozi hao wapatao 50 waliotajwa kutoka kwenye kata zote za Wilaya ya Monduli, Lota Sanare alisema viongozi hao wa kimila wamemtaka Lowassa aliyekuwa mbunge wao, kuunga mkono mkakati wa Magufuli wa ‘kutumbua majipu’ .

“Kama yeye Lowassa hawezi au hataki kumuunga mkono Rais Magufuli katika kutumbua majipu ya wakwepa kodi, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma na mafisadi, basi akae kimya amwache mwenzake (Rais Magufuli) awatumikie Watanzania kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na si kulalamika ,”alisema Sanare.

Sanare alisema, “anachofanya Rais Magufuli na serikali ni kuwashughulikia wafanyabiashara wanaokwepa kodi, wawe CCM au Ukawa (umoja wa vyama vinne), sasa anapotokea mwanasiasa anapinga vita hiyo maana yake anaunga mkono ukwepaji kodi na huyo ni fisadi na adui mkubwa wa Watanzania.”

Alisema kodi na ushuru wa serikali ndiyo nguzo ya maendeleo ya nchi. Alisisitiza wanaokwepa kulipa kodi washughulikiwe bila kujali ni akina nani. “Lazima washughulikiwe hata awe nani, kwa mujibu wa sheria na sisi tunaunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na serikali na tuko tayari kusaidiana nayo kuyatumbua yale majipu yaliyojificha huku kwetu,” alisisitiza Sanare.

Kauli ya viongozi hao wa kimila imekuja siku chache baada ya Lowassa kunukuliwa hivi karibuni akilalamika kanisani Monduli kwamba serikali inawaandama wafanyabiashara waliokuwa wakiunga mkono Ukawa.
 
Back
Top Bottom