Tumetupa maisha ya kijamii na madhara yake si muda mrefu tutayapata.

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Tumeumbwa katika taifa hili tuliangalie na kuliendeleza, lakini pia tupendane na kujaliana kama watu wa taifa moja. Hatuwezi kufanya hivi kama hatupendani, kama hatujaliani, na kama sio watu wamoja.

Na tujue kwamba kwenye ubinafsi na choyo hatuwezi kujenga vyote hivi. Kama tunataka kuendelea kama taifa ni lazima tubadilike kutoka ndani yetu kwenda nje.
Kama hatupendi vita ni lazima tuangalie haya mambo kwa umakini. Ni lazima tujenge mahusiano yetu na kutumikiana.

Katika taifa letu sifa isiwe kiasi gani umejilimbikizia mali, bali ni kiasi gani umeleta mabadiliiko kwenye jamii inayokuzunguka na taifa lako. Sifa iwe utumishi wako kwa taifa; sio mali. Sifa iwe uwepo wako unafaidisha nini taifa lako.

Vitu kama ufisadi na mambo mengine ni matokeo ya watu kuacha maisha ya kijamii na kujiangalia wao tu na kujilimbikizia mali, hasa kwa viongozi na watu wengine kwa njia ambazo si halali na kuacha kujali jamii ambazo wanatoka, na ambazo zinawategemea wao kuleta mabadiliko chanya. Huu ni uasi. Uasi dhidi ya jamii. Na uasi huu ukitendwa na viongozi jamii yote hukengeuka na kuwa ya kibinafsi. Hatuwezi kujenga nchi katika ubinafsi na nchi ikawa imara.

Ni wajibu wa serikali kusimamia maadili, sheria, usawa na haki. Serikali lazima iwekeze akili zote kwa wananchi na kuwa yenye maadili na nidhamu.

Kubomoka kwa maisha ya kijamii ni madhara makubwa yatokanayo na ubinafsi na choyo. Hatujali tena shule za serikali za pamoja ambazo ni muhimu, zinazopaswa kutoa elimu bora kwa wote. Kwakuwa uhai wa taifa lolote unakuwepo pale tu watu wake wote, wanapopata elimu bora ambayo haina matabaka na jamii inapoangaliwa kwa ukaribu katika ukuaji wake kiroho na kiakili, kwasababu binadamu si mali peke yake; lazima aangaliwe ukuaji wake wa kiroho na kiakili ambao humfanya kuwa na afya bora ya mwili.

Kwahiyo pamoja na matatizo tuliyonayo katika elimu yetu watu wanasomeshwa. Na lengo la kusomesha watu ni kufanya mapinduzi katika jamii zetu.

Tunahitaji watu wapate elimu ili wakafanye mapinduzi. Ili watumie elimu yao kutumikia nchi yao na jamii zao. Na wawasaidie wengine kupevuka kiakili ili tuwe na jamii pana iliyoelimika. Ili tulete mabadiliko. Elimu haipaswi kuchukuliwa kibinafsi.

Taifa linapo msomesha mtu na kuweka bajeti kwaajili ya elimu, malengo ni watu wanaosomeshwa waende na kuleta mapinduzi kwenye jamii zao. Sio kwa faida zao binafsi peke yake, ni kuleta mabadiliko katika taifa.

Tunachukulia elimu kama ni kitu cha kibinafsi; haitakiwi kuwa hivyo. Elimu yetu inatakiwa itengenezwe katika hali ile ambayo itafaidisha taifa kwa kiwango kikubwa. Na hii haitawezekana pasipo kujenga uzalendo wa watu wetu.

Ama sivyo tutajenga watu ambao wanafikiria tu kupata elimu na kuitumia elimu hiyo kwa maslahi binafsi pekee. Na hili sio lengo la taifa kusomesha watu wake. Malengo ya taifa kusomesha watu wake ni maendeleo ya pamoja kama nchi na kutatua changamoto zinazokabili maisha ya binadamu hasa maisha ya raia wa taifa hili. Ni kufanya watu au wasomi kitumia akili zao sio kutengeneza matatizo bali kutatua changamoto zinazotukabili. Sio kufanya ujanja ujanja na ulaghai.

Hii roho ya kujitolea tunawajibika kuijenga kwa watu wetu. Watu lazima wasome, na lengo lao liwe ni kuendeleza taifa lao, na sio kufikiria zaidi maslahi binafsi kuliko yale ya kitaifa. Ni jukumu letu kujenga taifa la watu wanaowajibika kwa nchi yao.

Tunaona tatizo hili pia kwenye siasa zetu, watu kujifikiria wenyewe kuliko maslahi mapana ya taifa. Na niaminini; tutaendelea zaidi kama tutaachana na ubinafsi, tukasikilizana kwa lengo la kuendeleza taifa letu. Sisi ni watu wamoja na tuna lengo moja maendeleo ya nchi yetu. Lakini ubinafsi ndio uliotugawa na kuturudisha nyuma kwenye maendeleo yetu.

Tunatakiwa kuwa wamoja, hakuna maendeleo kama sisi sio wamoja katika mawazo na matendo. Hakuna maendeleo kama hatutosikilizana na kutazamana kama watu wamoja ambao mwisho wao ni mmoja.

Tumegawanyika kimawazo sio kwasababu ya kutofautiana kifikra kuhusu njia bora za kuendeleza taifa hili, bali kwasababu za ubinafsi wa uchu wa mali na madaraka. Tunatakiwa tubadilishe mtizamo wetu na kulipa taifa hili kipaumbele kuliko matamanio yetu binafsi.

Tunatakiwa kuacha kutupa maisha ya kijamii ambayo ndio msingi wa uwepo wa taifa hili, na afya yetu kama taifa inategemea ubora wa maisha yetu ya kijamii, ambayo hayawezi kuwepo kama tutafuata ubinafsi.

Na furaha yetu kama taifa inategemea sana ubora wa maisha yetu ya kijamii. Na maisha yetu ya kijamii yataboreka pale tutakapokuwa na nidhamu na dira ya kujiongoza sisi wenyewe, ya kuangalia tabia zetu kwa ukaribu, na kujizuia kufanya matendo ambayo ni yenye madhara kwa uhai na umoja wa jamii zetu na taifa letu.

Na msingi wa uhai wa taifa lolote ni maadili ya watu wake, kinyume cha hapo hakuna taifa litakaloendelea kwa muda mrefu pasipo kuangalia kwa ukaribu maadili ya watu wake. Taifa watu wake wanapokengeuka haliwezi kusimama. Tunapoacha njia ambayo ni sahihi kama taifa tusahau kuhusu maendeleo. Kama makanisa na misikiti na elimu yetu, ikishindwa kujenga raia wema na bora, tusahau kuhusu uwepo wa taifa hili. Kutakuwa hakuna amani kama watu wetu watakuwa hawana uwezo wa kutenda mema.

Kama tunafikiri kwamba ubinafsi ni bora kuliko umoja na mshikamano wetu sisi ni wapumbavu. Kama tutaka kuendelea kama taifa hatuna budi kukubali kuwa wamoja na kuyapa kipaumbele maisha ya kijamii kuliko yale ya ubinafsi wetu.


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Well ..mkuu umetirilika vyema mpaka na kosa cha kuchangia hapo '. Hii elimu uliyoitoa hapa ingekuwa ni amri yangu basi nilitamani walau ipate kuwafikia watanzania walio wengi ili waweze kupata misingi nyoofu itakayo weza kuwakumbusha kurejea katika njia sahihi ambayo wengi wetu tumeelekea kuiacha ..

Ubinafsi" Udini " Ufisadi ni moja ya vitu vilivyoibuka ghafla kwa kasi ya mfanano wa mshale ulioruhusiwa kuruka na muwindaji mashuhuri na hatimae leo hii umefika kwenye mwili wa TANZANIA na kuuachia jeraha linalozidi kulitafuna taifa" tukiwa kama watu tunaotoka katika jamii ya taifa moja tunapaswa kuonyesha mshikamano " utakao weza kutusaidia kufanya kazi katika chumba chenye mtazamo wa aina moja nao sio mwingine bali nikulitumika taifa kwa moyo wote wa dhati' na kulitoa katika hatua moja hatarishi na kulipaisha katika hatua nyingine ambazo ni nufaishi

Asante

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Well ..mkuu umetirilika vyema mpaka na kosa cha kuchangia hapo '. Hii elimu uliyoitoa hapa ingekuwa ni amri yangu basi nilitamani walau ipate kuwafikia watanzania walio wengi ili waweze kupata misingi nyoofu itakayo weza kuwakumbusha kurejea katika njia sahihi ambayo wengi wetu tumeelekea kuiacha ..

Ubinafsi" Udini " Ufisadi ni moja ya vitu vilivyoibuka ghafla kwa kasi ya mfanano wa mshale ulioruhusiwa kuruka na muwindaji mashuhuri na hatimae leo hii umefika kwenye mwili wa TANZANIA na kuuachia jeraha linalozidi kulitafuna taifa" tukiwa kama watu tunaotoka katika jamii ya taifa moja tunapaswa kuonyesha mshikamano " utakao weza kutusaidia kufanya kazi katika chumba chenye mtazamo wa aina moja nao sio mwingine bali nikulitumika taifa kwa moyo wote wa dhati' na kulitoa katika hatua moja hatarishi na kulipaisha katika hatua nyingine ambazo ni nufaishi

Asante

Sent using Jamii Forums mobile app
Thanx mkuu. Tuko pamoja.


Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom