Tumepotea kwa kuwaabudu wawekezaji wa nje

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
bul2.gif
Hivi kweli ni chachu ya maendeleo yetu?


Lula wa Ndali-Mwananzela
Raia Mwema
Septemba 30, 2009


SIKU za hivi karibuni nimeanza kuhoji kama Rais Kikwete ana sababu yoyote ya kugombea awamu nyingine ya pili; ukiondoa sababu ya kijima inayotolewa na baadhi ya wana CCM wakidai ni utamaduni "wao" kuachiana awamu zote mbili.

Kwa kadri mambo yanavyokwenda, ndivyo naanza kuamini pole pole kwamba yawezekana Rais Kikwete amefikia mahali ambapo tunajua kuwa hawezi kwenda zaidi na hivyo atalifanyia taifa letu hisani kubwa kama hatogombea 2010.

Mawazo yangu haya yameanza kunijia tena hivi karibuni baada ya kusoma katika gazeti moja kuwa Rais Kikwete ameamua kuongeza kitu cha tano katika vile vitu vinne tunavyovihitaji ili tuendelee. Mwanzoni tuliambiwa kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora.

Lakini hivi karibuni Rais Kikwete aliripotiwa na baadhi ya magazeti akisema kuwa ili Tanzania ipige hatua mbele ya maendeleo, tunahitaji pia “wawekezaji”, na kadri nilivyomuelewa; siyo wawekezaji wa aina yoyote ile bali ni wale wa kutoka nje.

Kauli yake iliyonukuliwa kuwa “Lazima tuwe na haraka katika kuvuta wawekezaji badala ya kuwa wazuiaji wa uwekezaji katika nchi yetu, nchi yetu inayo bahati kubwa ya Kijiografia na lazima tutumie fursa hiyo kuvuta watu kuja na kuwekeza katika uchumi wetu”, inanifanya niamini pasipo shaka yoyote ile kuwa Rais Kikwete anapozungumzia “wawekezaji”, anawafikiria wageni kutoka ng’ambo.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuuza hili wazo la maendeleo yetu yanategemea wawekezaji wa kigeni. Ni wazo ambalo lina lengo la kuendeleza utegemezi wa watu wa nje katika kuleta maendeleo yetu na mifano iko mingi.

Kuna mambo ambayo sisi wenyewe tungeweza kabisa kuwekeza na kuleta mabadiliko ya watu wetu sisi wenyewe kwa kiasi kikubwa na wawekezaji wa nje wanachangia tu sehemu ile ndogo au katika maeneo yale ambayo aidha yanahitaji utaalamu wa hali ya juu au yanahitaji uingizaji wa mitaji mikubwa na miundo mbinu mikubwa ambayo kwa sasa hatuna uwezo nayo.

Tuangalie mifano michache ya uwekezaji anaoupigia debe Kikwete na kama sisi wenyewe hatuwezi kuufanya.

Ardhi kuazimishwa kwa Wasaudi kwa miaka 99 kwa kilimo
Mwezi wa Aprili ilitolewa ripoti kuwa Tanzania imetoa ahadi kwa Saudi Arabia kuwa wakitaka kuwekeza nchini katika kilimo, basi, wasiwe na wasiwasi kuna eneo kubwa tu ambalo linaweza kuazimwa kwao kwa shughuli za kilimo.

Iliripotiwa kuwa msaidizi wa Rais Kikwete, Bw. January Makamba aliwaambia maafisa wa Saudia kuwa wanaweza kupewa ardhi kwa kuiazima kwa miaka 99 na wao Saudia walisema wako tayari kufanya hivyo na walikuwa wanajiandaa kutuma ujumbe.

Mpango huo wa Saudia unaendana na mpango wao wa kutafuta mahali pa kuzalisha chakula cha kulisha watu wa ufalme huo; hasa mazao ya mpunga na mtama. Sasa mimi ninajiuliza; kama kweli Wasaudia wanazo hizo fedha za kuweza kuazima ardhi na kuwekeza katika kilimo kwa muda huo wote, kwanini basi tusiwatake watupatie sisi hizo fedha (kwa makubaliano) ili sisi wenyewe tuwekeze kwenye ardhi yetu wenyewe (bila kumpa mtu mwingine) na kuzalisha mazao ambayo tayari tuna uzoefu, utaalamu na uwezo wa kuyazalisha? Kwa nini tuwaache wageni wawekeze kwenye kilimo cha vitu ambavyo sisi wenyewe tuna uwezo wa kuvifanya?

Lakini zaidi, kwanini wataalamu wetu wasiende huko Saudia, wajifunze mahitaji yao na kuwaambia sisi tuna uwezo gani wa kutimiza mahitaji hayo na hivyo badala ya wao kukodisha mashamba wanajikuta tunawauzia chakula moja kwa moja kutoka katika kilimo chetu?
Hivi kwa mfano Wasaudia wakisema wanahitaji ngano tani elfu 20 kutoka Tanzania, hatuna uwezo wa kutumia mitaji yetu sisi wenyewe na wakulima wetu (wawekezaji wa ndani) kuanzisha kilimo hicho huku tukiwa na uhakika wa soko?

Lakini kwa sababu watawala wetu hawaamini uwezo wetu katika kujiletea maendeleo, hilo haliwezi kutokea.

Kati ya sisi kulima na kuwauzia mazao na wao kuja kukodi, kulima na kutuuzia baadhi ya mazao sisi wenyewe, ni ipi hasa njia rahisi ya kujenga kujitegemea na kujiletea maendeleo? Rais Kikwete anaamini hiyo njia ya pili!

Mfano wa Shirika la Reli

Mawazo haya ya kutukuza uwekezaji wa kigeni yalionekana zaidi kwenye masuala mbalimbali hasa lile la Shirika la Reli la Tanzania (TRC) ambalo kwa sababu ambayo serikali inajua, ilishindwa kuliendesha kwa mafanikio.

Katika fikra za kutegemea “wawekezaji kutoka nje”, serikali yetu ikaamua kuwaalika kampuni ya “Rites Consortium” ya India ambayo tuliahidiwa kuwa, chini yake, shirika la reli litabadilishwa na kufanya vizuri zaidi.

Kampuni hiyo iliingia ikisifiwa kwa uzoefu wake wa biashara ya reli sehemu mbalimbali duniani. Tukaingia nao mkataba wa miaka 25 ambao leo tunaambiwa hatuwezi kuuvunja. Licha ya mambo mabaya kuendelea ndani ya shirika hilo, bado tunawategemea kufanya vizuri.

Mawazo haya ya kutegemea wawekezaji wa nje yanadumaza kabisa uwezo wetu kama taifa kuweza kutafuta suluhisho la matatizo yetu.
Ni kiasi gani cha fedha kilikuwa kinahitajika kuiokoa TRC? Hivi, tunashindwa kuiendesha TRC kwa kulifanya kuwa shirika la umma linaloendeshwa kwa hisa? Kwanini tusianzishe shirika jipya kwa fedha za hisa na kuziuza kwa wananchi na makampuni ya ndani na kuwafanya watumishi wa shirika hilo na Watanzania wengine, na hata vyombo binafsi vya Tanzania, kuwa ni wadau?

Hivi kweli katika serikali yetu hakuna mtu aliyefikiria kuanzisha kampuni ya hisa, kununua mabehewa mapya, kuweka mtandao mpya wa kompyuta na kuweka vyombo vya uelekezaji vya GPS (global positioning system) ambavyo vingesaidia sana katika usalama wa reli na kusababisha uwepo wa matreni kadhaa yaendayo kasi kama ilivyo katika TAZARA?

Mfano mwingine wa ATCL

Ni yale yale tunayoyaona pia kwenye ATCL. Katika fikra za kutegemea wawekezaji, tuliombea kuwa wawekezaji toka Afrika ya Kusini wataliokoa shirika letu la ndege na kama vile tusiojifunza katika makosa yetu, tukajikuta tukiachiwa shirika lililo katika hali mbaya.

Badala ya kufikiria ni jinsi gani tunaweza kuboresha ATCL na hata kama ingebidi kuingia ushirika na Precision Air au shirika jingine la Watanzania, tukakimbilia tena kwa wawekezaji wa kigeni. Lakini ni kwanini sisi hatujiamini kuwa tuna uwezo wa kuendesha haya mashirika sisi wenyewe, tukitumia mbinu mpya na hata ikibidi kutengeneza taratibu mpya za uendeshaji?

Nauliza hivyo kwa sababu; hata baada ya Waafrika Kusini kushindwa, wakubwa bado wanajiuliza ni “wawekezaji” gani wengine kutoka nje wanaweza kutuendeshea shirika letu? Wameanza hata kuwafikiria Wachina!

Hivi katika Tanzania nzima hakuna watu wenye akili, utaalamu, uwezo, vipaji, na uzalendo wa kutosha kuweza kuiendesha ATCL ukiondoa wale ambao ni marafiki wa wanasiasa wanaotafuta kazi kwa kutumia undugunization?

Kwanini wasitangaze ili kampuni zishindanishwe wazi katika mchujo ambao utasimamiwa na kampuni huru kuweza kupata walio bora kati ya walio bora na kuwawekea kipimo kinachoeleweka cha utendaji wao? Najua hilo ni kazi kubwa. Ni rahisi zaidi kwa serikali yetu kualika “wawekezaji” kutoka nje!

Mikataba ya nishati
Hata kwenye ile mikataba ya kashfa ya nishati ya Richmond na Dowans fikra zilizowaongoza kina Kikwete ni zile zile kuwa wawekezaji kutoka nje ndio watakaotuokoa na matatizo yetu.

Tumefika mahali hadi tumealika makampuni hewa huku tukioneana aibu kwanini tumeumbuliwa. Kwamba tufikiria upya utendaji wa sekta ya nishati, tuboreshe miundo mbinu yetu na kujenga mabwawa ya uhakika zaidi huku tukiboresha usimamizi wa umeme na njia zake, tunaona hilo gumu kweli.

Tunaaona kuwa ni rahisi kuwaleta watu wale wale waliopora wanyama wetu kupitia Loliondo tuwape tena na Dowans! Tukisema “hatudanganyiki tena” tunaambiwa tuna malengo ya kupotosha watu!
Ninachojaribu kuhoji hapa ni kwamba sisi Watanzania tuna uwezo wa kufanya kitu gani kwa ufanisi sisi wenyewe na tukakifanya vizuri na tukajivunia matokeo yake?

Ni mradi gani mkubwa ambao sisi wenyewe tunaweza kuubuni, kuusimamia na kuufanikisha bila kuwapigia magoti wawekezaji wa nje?
Nadhani tukikubali sana mawazo ya Rais Kikwete na chama chake cha CCM kuwa wawekezaji wa kigeni ndio njia ya haraka ya kutuletea maendeleo, tutakuwa tumeingia kwenye mtego wa akili ambapo tunawarithisha watoto wetu na watoto wa watoto wetu mawazo ya kutetgemea wafadhili wa nje kwa vitu ambavyo wao wenyewe wanaweza kuvifanya.

Kama Kikwete yu sahihi. Hata hivyo, kama Rais Kikwete kweli anaamini kuwa maendeleo yetu yanategemea sana wawekezaji wa kigeni namna hiyo, na ya kuwa ili tuendelee tunahitaji kufanya kila jitihada ya kurahisisha ujio wao, basi, nina pendekezo jepesi.

Kama kweli wawekezaji ndio suluhisho letu, basi Rais Kikwete kama atashinda tena mwakani, basi, kati ya zile nafasi kumi za wabunge wa kuteuliwa ateua “wawekezaji” ili awape uwaziri ili watuletee maendeleo ya haraka; kwani sisi wenyewe hatuwezi bila ya wawekezaji!

Kwa ufupi, Watanzania tunahitaji Rais anayeamini katika uwezo wetu wenyewe. Tunahitaji Rais anayetutia moyo katika tuyafanyayo na ambaye anaamini kuwa tunaweza kubadilisha maisha yetu sisi wenyewe na kutusaidia kujenga mazingira ya kufanya hivyo.

Hao wawekezaji wa kigeni yafaa wawe ni kama limau na ndimu tu ya kukoleza mapishi yetu sisi wenyewe!

Vinginevyo, tutabakia kuwa walaji wa mapishi yanayopikwa jikoni mwetu, kwa chakula chetu wenyewe, kwa mafuta yetu na kwa masufuria yetu; halafu tuambiwe tulipie. Kisa na mkasa, eti waliopika ni wataalamu toka nje! Jamani hata ugali unauhitaji mwekezaji?
 
Mzee wa Motown,

Kikwete yuko sawa katika kutaka wawekezaji, haya ni mambo ya basic Economics a la "The Wealth of Nations".

Tatizo la kimsingi si katika kutaka wawekezaji, hasha.Kama kuna tatizo basi ni ridiculous terms tunazopata katika hizi deals. Kutaka wawekezaji si kuabudu wawekezaji, kuabudu huku kunakuja pale kwenye negotiating table.Mpaka sasa nashindwa kuamini kwamba huku ni kuabudu tu na hakuna mlungula unaotembea.
 
Mzee wa Motown,

Kikwete yuko sawa katika kutaka wawekezaji, haya ni mambo ya basic Economics a la "The Wealth of Nations".

Tatizo la kimsingi si katika kutaka wawekezaji, hasha.Kama kuna tatizo basi ni ridiculous terms tunazopata katika hizi deals. Kutaka wawekezaji si kuabudu wawekezaji, kuabudu huku kunakuja pale kwenye negotiating table.Mpaka sasa nashindwa kuamini kwamba huku ni kuabudu tu na hakuna mlungula unaotembea.

Naamini tatizo haliko kwenye terms; tatizo liko kwenye aina ya uwekezaji tunaotafuta. Unapoenda kutafuta mwekezaji wa kulima mpunga au wa kutujengea choo kwenye shule fulani ya msingi basi ina maana kuna tatizo. Kuna uwekezaji ambao hautafutwi bali huja wenyewe kutokana na mazingira ambayo sisi tumeyatengeneza; katika hali hiyo wawekezaji hutubembeleza waje kuwekeza; angalia mabadiliko yaliyofanyika Malaysia, Costa Rica, Korea ya Kusini n.k
 
Naamini tatizo haliko kwenye terms; tatizo liko kwenye aina ya uwekezaji tunaotafuta. Unapoenda kutafuta mwekezaji wa kulima mpunga au wa kutujengea choo kwenye shule fulani ya msingi basi ina maana kuna tatizo. Kuna uwekezaji ambao hautafutwi bali huja wenyewe kutokana na mazingira ambayo sisi tumeyatengeneza; katika hali hiyo wawekezaji hutubembeleza waje kuwekeza; angalia mabadiliko yaliyofanyika Malaysia, Costa Rica, Korea ya Kusini n.k

I don't know about "kutujengea choo kwenye shule" (hii wapi mazee?).Ila kwenye kulima mpunga sawa tu, unawapa terms tu, wakitaka tuwalimie tutawalimia, wakitaka kuja kulima wenyewe waje ila terms zitakuwa za juu zaidi kwa sababu tunawapa control, mwisho wa mchezo tuna reserve right ya ku rescind the whole thing.

Kwishne. Nilikuwa nasoma kitabu kipya cha Memoirs za Zhao Ziyang wa China (aliefariki 2005 baada ya kukaa katika house arrest after a power struggle culminating in the Tiananmen Square uprising), alikuwa anaeleza hatua zilizofanya China iwe successful economically. Moja ya compelling point aliyoimake - not verbatim- ni kwamba kuwa na unused land in some ways ni sawasawa na kuwa na an unoccupied house, hii haimsaidii landlord ila inamrudisha nyuma tu.

Kinachotakiwa kufanywa ni kuhakikisha kama alivyosema January kwamba "hatuendi kuwa kama Nigeria" i.e,. exporter wa mafuta ambaye nchi yake haina mafuta. Tunaweza kabisa kuwa dynamic na kutumia funds zitakazotoka katika hii program kuendeleza wananchi.

Tatizo langu si soundness ya investment model, bali commitment na competency ya uongozi.
 
Tangu watanzania tuiponde tena kwa fujo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, basi ndo ukawa mwisho wa viongozi wengi kufikiri.
Siasa ile haikuwa mbaya kama inavyofikiriwa , ingawaje ujamaa si siasa endelevu.
Badala ya kujitegemea tukajiwekea malengo ya KUTEGEMEA. na mara zote ni kutegemea misaada toka nchi za nje.
Haya ndio mawazo yaliyotawala vichwa vya viongozi wetu tena karibu wote.
Wengi hatuja sahau miradi mikubwa sana iliyotekelezwa na wananchi kama vile Nyamagana,Uwanja wa Sokoine Mbeya,Mtaro wa Umwagiliaji wa Ntomoko.
Mbaya zaidi kwa viongozi wengi UTEGEMEAJI huu unachochewa na RUSHWA kubwa kubwa.
Hoj nzito hujengwa za kuombea misaada ili ule ufadhili upate kuchotwa.
Ni kweli kuna miradi mingi sana inayoweza kutekelezwa kwa msaada wa nchi za kigeni lakini kuna miradi mikubwa sana iliyoweza kutekelezwa na sisi wenyewe bila kutegemea wajomba.
Barabara za Dodoma- Singida,kivuko cha Kigamboni na uboreshaji wa miundo mbinu mingi.
Twaweza sana kujitegemea lakini mwamko wa kujitegemea haupo.
 
Back
Top Bottom