Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,110
- 15,375
Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande
Siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025 kuliripotiwa kutokea kwa maandamano, vurugu na taharuki na siku chache baadaye, taarifa za vifo vya Watu, majeruhi na uharibifu wa mali zilianza kuripotiwa mitandaoni.
Tume hiyo ilianza kazi zake Novemba 20, 2025 ikiwa na lengo la kukamilisha majukumu ndani ya siku 90. Hata hivyo, muda wake uliongezwa hadi Aprili 3, 2026 kabla ya kuomba nyongeza nyingine, na hatimaye ripoti hiyo kuwasilishwa leo.
Inaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, tume hiyo pia inaundwa na wajumbe saba ambao ni Profesa Ibrahim Juma, Balozi Ombeni Sefue, Balozi Radhia Msuya, Luteni Jenerali Paul Meela, Said Mwema, Balozi David Kapya, pamoja na Dkt. Stergomena Tax.
Rais Samia aliunda tume hiyo Novemba 18, 2025 kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi (Sura ya 32).
Wewe unatarajia ripoti hii ilete majibu au mwelekeo gani?
Tume imejielekeza katika kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha ghasia zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na siku chache zilizofuata. Jukumu la pili lilikuwa ni kuchunguza lengo kuu lililokusudiwa na waliohusika katika kupanga na kutekeleza vitendo hivyo vya ghasia na uvunjifu wa amani. Aidha, Tume ilichunguza na kubaini madhara yaliyojitokeza kutokana na ghasia hizo, ikiwemo vifo, majeraha, uharibifu wa mali na miundombinu, pamoja na madhara ya kiuchumi na kijamii.
Katika hatua nyingine, Tume ilichunguza mazingira na hatua zilizochukuliwa katika kubaini na kukabiliana na ghasia hizo. Hii ilijumuisha kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia katika kulinda amani, utawala wa sheria, haki za binadamu, utawala bora, na mifumo madhubuti ya majadiliano ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi. Lengo ni kufikia maridhiano ya kitaifa na kuhakikisha kuwa vurugu kama hizo hazitokei tena.
Uchunguzi huu ulihusisha maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 na mikoa 11, ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Mwanza, Geita, Arusha, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Mara, na Ruvuma.
Tume imechambua jumla ya picha mnato 450 na picha mjongeo (video) 880 kwa lengo la kubaini chanzo halisi cha ghasia zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 na siku chache zilizofuata. Uchunguzi huu umelenga kuelewa madhara ya kibinadamu, ikiwemo vifo na majeraha, pamoja na kutofautisha taarifa halisi na zile zilizochezewa kwa kutumia akili munde ili kupotosha umma. Hatua hizi ni muhimu katika kufikia maridhiano ya kitaifa na kuhakikisha kuwa vurugu kama hizo hazitokei tena nchini.
Tume imebaini kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi kama fursa ya kuwashawishi na kuwachochea kushiriki katika ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Hili lilifanyika kwa kutumia kaulimbiu na matamko mbalimbali yenye lengo la kuamsha ari ya vurugu.
Vichochoo hivi vimegawanywa katika makundi makuu matatu, huku mitandao ya kijamii ikitajwa kuwa kichocheo kikubwa zaidi;
- Matumizi ya Mitandao: Mitandao ya kijamii ilitumiwa kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyowahi kutokea nchini hapo awali.
- Wabunifu wa Maudhui (Content Creators): Walibuni mada maalumu za kuhamasisha wananchi kutoshiriki uchaguzi au kuhakikisha haufanyiki.
- Majukwaa ya Majadiliano: Mitandao ilitumiwa kupanga mbinu za kuzuia uchaguzi na kuelekeza namna ya kutekeleza vurugu hizo
- Zana za Kazi: Washiriki walipewa simu maalumu za mkononi.
- Maelekezo: Walipewa kazi ya kupiga picha na video za matukio ya majeraha, vifo, na harakati za vyombo vya ulinzi (kama magari ya jeshi).
- Usambazaj: Picha na video hizo zilirushwa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuibua hasira kwa wananchi.
Tatu, washiriki wa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi mkuu walibeba silaha za aina mbalimbali zikiwemo mawe, nondo, mkuki, sururu, fimbo, marungu, visu, vibiriti, vipulizi, bunduki, manati, kombeo, rato, mapanga jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika maandamano ya amani.
Hii ni kinyume cha sheria na taratibu za kimataifa ibara ya 21 ya mkataba wa haki za binadamu na raia na kisiasa mwaka 1966, wa kikanda ibara ya 11 ya mkataba wa Afrika wa haki za binadamu wa watu na binadamu mwaka 1981 na ibara ya 10 na 11 ya mkataba wa Ulaya wa haki za binadamu mwaka 50 na kitaifa ibara ya 18 na 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haviruhusu maandamano ya watu waliobeba silaha.
Na nne sheria na taratibu za kimataifa kikanda na kitaifa haziruhusu maandamano yanayosababisha taharuki katika jamii, kuhatarisha usalama wa taifa, kusababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na kuhatarisha maisha ya watu wengine.
Mambo hayo yalifanyika na yanakua ni kinyume cha sheria na tafsiri ya maandamano ya amani. Kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizotajwa, maandamano ya amani ya kimataifa, kikanda na kitaifa na ushahidi uliowasilishwa mbele ya tume ni maoni ya tume kuwa kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu haikuwa maandamano ya amani na hivyo kuwa nje ya kinga ya sheria na kanuni hizo.
Ghasia ya tarehe 29 Oktoba yalipangwa, yaliratibiwa, yalifadhiliwa na kutekelezwa na watu waliopata mafunzo. Waratibu walitumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuwatumia watu wasio na ufahamu wa kina na vijana waliokata tamaa huku wakihakikisha kuwa vitendo vya ghasia vinafanyika kwa wakati mmoja kufika maeneo tofauti ili kuwachanganya na kuwatawanya jeshi la polisi.
Mheshimiwa Rais taarifa na ushahidi unathibitisha kuwa watu waliokuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali kama vile mitaani, vyuoni, kwenye masoko na stendi za mabasi wakishawishi na kuwaandikisha watu mbalimbali kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
Mfano, watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki na wajasiriamali wadogo walieleza kuwa walipewa fedha kati ya shilingi 10,000 hadi shilingi 50,000 na waliahidiwa ajira na maisha bora. Imeelezwa zaidi kuwa kuanzia tarehe 12 Oktoba mwaka 2025 hadi tarehe 28 Oktoba waliwekwa pamoja kupewa mafunzo, kuandaliwa na kuhamasishwa kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki ghasia siku hiyo.
Aidha, ilibainika kuwa makundi yaliyoshawishiwa ndio wahusika zaidi katika ghasia wakati wahusika wakuu wa ghasia na waratibu hawakuwepo kwenye maeneo ya matukio. Hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kutokamatwa kwao huku wengi wa waliokamatwa wakiwa ni wananchi wa kawaida wakiwemo wafuata mkumbo au kushawishiwa kwa malipo kidogo au hadi ya kunufaika na mabadiliko yaliyopangwa bali kuwa na uelewa bila kuwa na uelewa wa malengo halisi ya wahusika wa maandamano.
Kuna kijana mmoja Usa River wa Arusha wa miaka 16 alishawishiwa, alipewa shilingi 50,000 ashiriki na walimuahidi, kwa maneno yake walimuahidi watampa shilingi milioni tano akishiriki na kwa ushahidi wake anasema walinipa mchongo utakaonitoa kwenye umaskini. Huyo ni mmoja tu katika mashahidi ambao wamekuja mbele ya tume kueleza namna walivyorubuniwa ili kushiriki kwenye ghasia.
Ikitokana na ushahidi na taarifa na maoni yaliyopatikana tume inabainisha na kuainisha, imeainisha kwenye ripoti yake mheshimiwa Rais mbinu 16 zilizotumika na wahusika wakuu na waratibu kufanikisha ghasia za wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Baadhi ya mbinu hizo ni kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto mali mbalimbali, matumizi na ishara mbalimbali ya kutambuana, matumizi ya pikipiki kuanzisha ghasia, uanzishaji wa ghasia sehemu nyingi na kwa wakati mmoja.
Lengo mheshimiwa Rais kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa kwenye tume na maelezo tulioyapata ni kwamba matukio yale yalikuwa na malengo makuu yafuatayo...
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa kwenye Tume na maelezo tuliyoipata ni kwamba matukio yale yalikuwa na malengo makuu yafuatayo:
La kwanza ni kuzuia na kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 20, 2025. Kutokana na ushahidi uliotolewa mbele ya Tume, lengo kuu la ghasia za Oktoba 25 lilikuwa ni kuzuia na kuvuruga uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba. Lengo hili linajidhihirisha kupitia vitendo mbalimbali vya wafanya ghasia, ikiwemo kuharibu vituo vya kupiga kura, kushambulia askari kwenye vituo, mawakala na wasimamizi wa uchaguzi, kuharibu mali za wasimamizi wa uchaguzi, vitisho, madhara na mashambulizi dhidi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura, kupora mali za wasimamizi wa kupiga kura. Na pia kuna ushahidi kwa wale waliopiga kura na bado walikuwa na vidole vyenye alama ya wino, kukatwa vidole vyao au kujaribiwa kukatwa vidole vyao, na wengi wao walilipa fedha ili wajinusuru kufanyiwa hivyo.
Pili ni kufikisha ujumbe kwa serikali. Kupitia ushahidi, taarifa na maoni, imekuwemo majadiliano na wataalamu wa uchumi, inaonekana kuwa kupitia ghasia za uchaguzi mkuu, vijana walioshiriki walipata mwanya wa kufikisha ujumbe kwa serikali kuwa wanataka kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao zinazowakabili. Ilibainika kuwa waratibu wa ghasia walitumia malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali wakati wanawashawishi kushiriki kwenye ghasia.
Lengo la tatu kwa walioshiriki ni wizi na uporaji. Kwa ajili ya ushahidi, taarifa na maoni, miongoni mwa wafanya ghasia, yalichokeza makundi makubwa yalikuwa na lengo la kuiba na kupora mali. Ushahidi wa moja kwa moja wa waathirika waliopora mali zao au kuibiwa, pamoja na picha za kidijitali na kupitia picha mnato na picha mjongeo, unaonyesha namna vitendo vya wizi na uporaji vilivyofanywa na makundi hayo. Kwa mfano, wizi na uporaji uliotokea katika maduka na maeneo mengine ya biashara kwenye mikoa iliyotembelewa na Tume. Vitendo hivi vimethibitishwa pia na baadhi ya wamiliki wa mali na biashara waliofika mbele ya Tume kutoa ushahidi.
Madhara ya kiuchumi;
Madhara makubwa ya kiuchumi yaliyotokea ni yale yanahusu mali za watu binafsi na mali za serikali kuharibiwa. Tume imebaini kutoka vyanzo mbalimbali kuwa mali iliyoharibiwa ina thamani ya Tsh. Bilioni 125.
Kati ya mali hizo, mali za sekta binafsi ambazo ni watu binafsi, vituo vya mafuta, CCM na benki, zina thamani ya Tsh. Bilioni 89 sawa na 71.2%. Na mali za umma ambazo ni mali za serikali na taasisi kama zile shule, TRA, mahakama, polisi, DART, TANROADS, TANESCO, TTCL, zina thamani ya Tsh. Bilioni 36 sawa na 28.8%.
Lakini sekta binafsi ndio imepata madhara makubwa kuliko sekta ya umma. Ushahidi na waathirika wengi waliopoteza mali binafsi unaonyesha machungu waliopata na wanaendelea kuwa nayo. Mfano mmoja ni mstaafu...
Kuzuia na kudhibiti ghasia;
Kuhusu kubaini, viashiria vya kuelekea kwa ghasia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, vyenye lengo la kuzuia na kuvuruga uchaguzi vilianza kujitokeza kupitia mitandao ya kijamii takribani miezi sita kabla ya uchaguzi.
Kwenye nyakati tofauti kuanzia mwezi wa Aprili hadi Oktoba 25, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikuwa ikiwasilisha taarifa zinazoonyesha viashiria vya ghasia kwa mamlaka na vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine ili zichukue hatua. Tarehe 27 Oktoba 2025, TCRA ilibaini bango mtandaoni lililokuwa na maudhui yanayohamasisha ghasia na kuzuia uchaguzi mkuu. Bango hili lilionyesha malengo ya maandamano yaliyooandaliwa kuwa ni ya kitaifa, kuwa ni ya kuzuia na kuvuruga uchaguzi mkuu uliopangwa tarehe 29 Oktoba.
Katika taarifa yake ya 26 Oktoba, TCRA pia ilibaini kuwepo kwa mjadala katika mmoja ya mitandao ya kijamii kuhusu namna watakavyotekeleza ghasia siku ya uchaguzi. Majadiliano hayo yalionyesha kuwa siku ya uchaguzi wangeharibu mifumo ya umeme ili kuingiza nchi gizani, kuchoma moto vituo vya mafuta na kuchoma moto vituo vya kupiga kura kwa lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu.
Licha ya viashiria vya mtandaoni vilivyowekwa wazi zaidi, kulikuwa pia na viashiria ambavyo Tume ilivigundua kupitia mashahidi waliofika mbele ya Tume. Mfano ni kuwepo kwa vijana wasiopungua 500 katika majengo, misitu na makambi katika maeneo mbalimbali nchini kwa takribani siku 28 ambapo walihifadhiwa na kupatiwa mafunzo kwa ajili ya kufanya ghasia siku ya uchaguzi mkuu.
Tume kupitia uchunguzi wake ilibaini kuwa moja ya nyumba hizo iliyopo Dar es Salaam ilikuwa umbali wa takribani mita kumi kutoka kituo cha polisi. Pamoja na Tume kupokea ushahidi unaoonyesha kuwepo kwa baadhi ya viashiria vya mipango ya vurugu siku ya uchaguzi mkuu, hakuna ushahidi unaoonyesha kubainika kwa vitu hivyo vichache ambavyo nimeviongelea au hatua stahiki kuchukuliwa kikamilifu kama ilivyo kabla ya matukio ya uvunjifu wa amani.
Sehemu ya Hotuba ya Rais Samia Suluhu
"Tume zote hizi matokeo yake hayakuwa bayana. Lakini Awamu ya Sita, kama mnavyojua, tuliunda Tume ya kuangalia mfumo wa haki za jinai na haki za wananchi... Lakini pia Tume hii ambayo imechunguza matokeo ya vurugu kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025 ya Jaji Othman Chande. Na Tume hii tuliitangaza bayana na leo imetupa matokeo ya uchunguzi bayana."
"Kwa vyovyote vile, walioumizwa na tukio lile ni sisi Watanzania. Ni sisi tuliopoteza watoto wetu. Ni sisi tuliopoteza ndugu zetu, jamaa na marafiki zetu... Haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania awe na uchungu zaidi kuliko sisi Watanzania, haiwezekani."
"Wakati tunapata uhuru, tulichoachiwa na wakoloni halikuwa taifa, bali mkusanyiko wa makabila. Lakini kwa dhamira na utashi wa waasisi wetu, waliamua kujenga taifa moja imara lisiloendeshwa kwa misingi ya kidini, kikabila au hadhi ya mtu... lugha yetu adhimu ya Kiswahili inatumika kama nyenzo ya kutuunganisha pamoja na kudumisha na kuimarisha utaifa wetu."
"Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na nchi yenyewe... sasa nasi kama nchi tuachwe tujenge demokrasia yetu kwa misingi yetu, mila na desturi zetu."
"Kupitia falsafa ya R4—yaani Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya—nilichukua hatua kadhaa ikiwemo kuundwa kwa kikosi kazi... bado kuna mambo kadhaa ya kufanyiwa kazi katika nyanja za siasa, ikiwemo swala la mabadiliko ya Katiba. Kama mnavyofahamu na kama nilivyoahidi, tumepanga kukamilisha mchakato huu katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Sita."
"Hii ni ripoti ya Rais. Aliyeunda tume ni Rais na ripoti yote hii ni ya Rais. Kwa hiyo wasitokee watu wengine wakadai ownership ya ripoti hii, ni ripoti ya Rais. Nilisema tume za huko nyuma zilikuwa zinabanwa kimyakimya, mimi nimeamua tuambizane, lakini ripoti ni mali ya Rais."
"Mimi ni Samia yule yule wa 4R. Ni yule yule wa 4R. Ninachoomba ni ushirikiano wenu katika kutekeleza hizo 4R. Wanasema kidole kimoja hakivunji chawa, au 'it takes two to tango'. Kwa hiyo mkimtegemea Samia peke yake afanye, hayaendi. Lakini mkinipa ushirikiano mkubwa ndugu zangu, tutafika tunakoenda."
"Hatima ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe. Nguvu ya ushawishi ya makundi ya nje inasaidia kuvunja amani, kuvuruga usalama na kubomoa nchi. Lakini kurudisha amani na usalama na kuijenga upya nchi yetu, hufanyika kwa misaada yenye masharti magumu ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara."
"Ni rahisi kupoteza amani, lakini si rahisi kuirejesha. Ni rahisi kuibomoa nchi, lakini ni vigumu kuijenga upya. Tanzania ndipo kwetu, hatuna pengine katu, hatuna. Hatuna pengine. Kwa hiyo tukijenga nchi yetu tutakaa kwa raha, tukivuruga nchi yetu tutaendelea kukaa jinsi tunavyokwenda. Tutakuwa na matatizo yasiyoisha."
"Katika kuhakikisha mapendekezo ya taarifa ya tume, serikali itachukua hatua za haraka zifuatazo: Kwanza, katika muda mfupi ujao itaundwa tume ya maridhiano... Pili, baada ya tume ya maridhiano kuwasilisha ripoti yake, maoni na mapendekezo yatakayowasilishwa ndiyo yatakayoongoza kwenye mchakato wa kurekebisha Katiba ya nchi. Tatu, kwa kuwa ripoti imebainisha kuwepo kwa viashiria vya jinai... tutaunda chombo maalum cha upelelezi 'criminal investigation' kwa ajili ya kufanya kazi iliyopendekezwa na tume."