Tume sasa yaukana ushindi wa Kibaki

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Tume sasa yaukana ushindi wa Kibaki

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima

WAKATI vurugu zinazoendelea nchini Kenya zikikaribia kufikia kiwango cha mapiganio ya kikabila, uhakika wa ushindi wa Rais Mwai Kibaki umeingia katika majaribu makubwa, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (ECK), Samuel Kivuitu, kusema kuwa hana uhakika iwapo Kibaki alishinda katika uchaguzi huo.
Kivuitu amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hana uhakika na matokeo aliyoyatangaza na kuwa aliyatangaza kutokana na shinikizo na kubanwa na wanasiasa kutoka vyama vikubwa viwili vya PNU cha Kibaki na ODM cha Odinga.

Kivuitu alizidi kubainisha maajabu aliyoyafanya alipoeleza kuwa alikipeleka cheti cha ushindi wa Kibaki Ikulu baada ya baadhi ya watu kutishia kuwa watakichukua na kukipeleka, wakati jukumu hilo ni lake.

"Nilipofika Ikulu wakati napeleka cheti, nilimkuta Jaji Mkuu akiwa tayari kumuapisha rais," Kivuitu alinukuliwa na vyombo vya habari akisema.

Alikiri kuwa wakati wote wa harakati za kujumlisha matokeo yaliyokuwa yakipokewa kutoka katika vituo mbali mbali, wanasiasa na viongozi wa PNU na ODM walikuwa wakimbana kwa kumpigia simu mara kwa mara wakimtaka atangaze matokeo hayo.

Alisema kwa upande mwingine, alikuwa pia akibanwa na baadhi ya mabalozi na wanadiplomasia pamoja na Maina Kiai wa Tume ya Haki za Binadamu, wakimtaka asiyatangaze matokeo hayo, mpaka matatizo yote yaliyojitokeza yatakapopatiwa ufumbuzi.

"Nilikuwa nimefikiria kujiuzulu, lakini nilighairi kwa sababu sikutaka watu wanione mwoga," alisema muda mfupi baada ya kikao chake na makamishna 22 wa tume hiyo.

Alisema kwa hali ilivyo, mpaka sasa hana uhakika iwapo mshindi wa nafasi ya urais katika uchaguzi huo ni Kibaki wa PNU au Raila Odinga wa ODM.

Kutokana na hali hiyo, alisema upo umuhimu wa suala hilo kufikishwa katika vyombo vya sheria, hususan mahakama na iwapo hilo litatokea, mahakama inapaswa kutoa maamuzi mapema iwapo mshindi ni Kibaki au Odinga, ili kukomesha vurugu zinazoendelea kusababisha mauaji ya mamia ya Wakenya.

Alikiri kuwa alifanya maamuzi ambayo yameiingiza nchi katika matatizo. Hata hivyo, alisema kuwa alilazimika kuyatangaza matokeo hayo kwa sababu tume yake haina mamlaka kuchunguza kasoro zilizoelezwa.

Alisema hivi sasa tume imeanza kuwasiliana na wanasheria ili washauri ni nini kifanywe ili kulimaliza tatizo lililojitokeza kisheria.

Alisema kama tume, wao pia ni watuhumiwa katika sakata lililoibuka na ingekuwa vema iwapo tume huru ingeachwa kuchunguza makosa yaliyojitokeza.

Katika kukabiliana na matatizo hayo, tume hiyo imewaalika wataalamu wa uchaguzi kutoka Afrika Kusini, ambao wanatarajiwa kuwasili nchini humo leo.

Wakati huo huo, dunia imeonyesha kushtushwa kwake na vurugu zinazoendelea nchini Kenya kutokana na kuonekana kuwa na mwelekeo wa kuingia katika hatua ya mapigano ya kikabila.

Mwendelezo wa vurugu hizo unaonyesha kuwa makabila makubwa mawili nchini humo, Waluo na Wakikuyu, yanawindana na kushambuliana.

"Sasa inaonekana kuwa haya ni mauaji ya kimbari yaliyopangwa ili kulimaliza kabila fulani, ambayo yamefadhiliwa na viongozi wa Orange Democratic Movement kabla ya uchaguzi mkuu," ilisema taarifa iliyosomwa na Waziri wa Ardhi, Kivutha Kibwana, kwa niaba ya wenzake.

Wakikuyu ni kabila kubwa kuliko yote nchini Kenya, ambalo Rais Kibaki, ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa hivi karibuni ndio ulianzisha vurugu hizo, anatokea. Waluo ni kabila la pili kwa ukubwa, na mgombea wa upinzani anayepinga ushindi wa Kibaki, Odinga, anatokea katika kabila hilo.

Wakati huo huo, wanajeshi wamesambazwa katika maeneo kadhaa yaliyokumbwa na vurugu, wakati kukiwa na wasiwasi wa kuibuka kwa mauaji ya kikabila.

Msemaji wa serikali, Dk. Alfred Mutua, alikiri kusambazwa kwa wanajeshi lakini akasema kuwa wanajeshi hao watakuwa na jukumu la kusambaza misaada ya kiutu katika maeneo yaliyoathiriwa na vurugu.

"Hii si mara ya kwanza kufanya hivi, mara nyingi jeshi limetusaidia katika masuala kama haya na hali ya sasa imetulazimisha tulitumie tena," alisema.

Katika kile kilichoonekana kama kikwazo kwa jitihada za kimataifa kutatua mgogoro ulioibuka, Dk. Mutua alisema kuwa Kenya haipo tayari kuwaita wasuluhishi wa kimataifa kama njia ya kumaliza mgogoro uliotokana na matokeo ya uchaguzi mkuu.

"Hatujafikia hatua kama ya Somalia, hivyo hatuhitaji wasuluhishi waje nchini mwetu," alisema na kubainisha kuwa Rais Kibaki yupo tayari kwa mazungumzo ili kumaliza tofauti zilizojitokeza.

Dk. Mutua alitoa kauli hiyo wakati taarifa zikionyesha kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Ghana, John Kufuor, alipanga kuwasili nchini humo jana, kusuluhisha mgogoro ulioibuka.

Wakati huo huo, makumi ya maelfu ya Wakenya wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vurugu hizo, ambazo zimesababisha vifo vya watu kadhaa.

Polisi jana walisema kuwa idadi ya watu waliokufa imefikia 178, wakati vyanzo vingine mbalimbali vinaeleza kuwa idadi ya vifo inazidi watu 300.

Hayo yanatokea wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice na yule wa Uingereza, David Miliband, wametoa taarifa ya pamoja wakiwataka wanasiasa nchini Kenya kukomesha vurugu zinazoendelea.

Waliwataka kufuata njia za kisheria kutatua matatizo yaliyojitokeza ili kumaliza vurugu kubwa kuwahi kutokea nchini humo tangu mapinduzi yaliyoshindwa ya mwaka 1982.

Nao maofisa uhamiaji wa Uganda walieleza kuwa mamia ya watu wa kabila la Kikuyu walikuwa wakivuka mpaka kuingia nchini humo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, naye aliungana na viongozi wengine wa kimataifa na kueleza masikitiko yake kutokana na vifo vya watu nchini humo.

Aliwataka wanasisa na viongozi wa vyama kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyojitokeza nchini humo ili kukomesha mauaji hayo.

Wakati huo huo, wizara ya elimu nchini Kenya ililazimika kusogeza mbele tarehe ya kufunguliwa kwa shule za sekondari hadi Januari 14 na 15.

Naye Rais Kibaki, aliwaalika wabunge wote wateule na kuwataka kufika Ikulu jana jioni kukutana naye.

Naye waziri wa sheria, aliwataka wanasiasa wa kambi ya upinzani ambao hawakubaliani na matokeo ya uchaguzi huo kwenda mahakamani, kwani ndiyo yenye mamlaka ya kutoa maamuzi kuhusu mabishano ya matokeo ya uchaguzi wa rais.
 
A recount should be conducted by an independent person transparently and with close supervision from both parties and ultimately a recount to be done.
 
A recount should be conducted by an independent person transparently and with close supervision from both parties and ultimately a recount to be done.
whatever the case. nadhani maji tayari yamemwagika,yana tabu kuzoleka. najiuliza je uchaguzi ukirejewa na odinga akatangazwa mshindi. hivi kweli watu wa kibaki si watakuwa wamesoma kitu.(ukichafua hali ya amani,uchaguzi unarudiwa) nilichokiweka kwenye mabano ndio wasiwasi wangu kwamba kitakuwa kigezo cha atakaeshindwa,pindipo uchaguzi ukirudiwa.la kufanya ni kuwaombea amani tu wenzetu wa kenya.naamini mungu atawasaidia katika kipindi hiki kizito kwao.
 
Back
Top Bottom