Tume kusikiliza maoni yote, hata ya kuvunja muungano

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1]
salimu%2Bna%2Bwarioba.JPG
[/h]Written by administrator // 19/06/2012 // Habari // 9 Comments


TUME ya Mabadiliko ya Katiba iko tayari kupokea maoni kuhusu masuala yoyote yanayohusu nchi ikiwa ni pamoja na yanayotaka Muungano uvunjwe na hata ya kuundwa kwa Serikali tatu au mbili na mengineyo.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa shughuli za Tume hiyo ambapo alifafanua, kwamba kwa kuwa inatakiwa Katiba mpya ni lazima kujadili mambo yaliyo kwenye Katiba ya sasa ikiwa ni pamoja na Muungano.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, wanatarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, wawe wamemaliza kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na mapema mwakani waanze kukusanya mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wajumbe wote wa Tume akiwamo Makamu Mwenyekiti, Jaji Augustino Ramadhani na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid na waandishi wa habari.
Alisema watapokea maoni ya wananchi kama wanataka idadi yoyote ya Serikali katika Muungano, kurekebishwa kwa mipaka ya nchi na mengineyo, kwani suala hilo lipo katika mambo tisa ya msingi yaliyo katika sheria.
“Kwa kufuata sheria tunapokea maoni ya kila aina ikiwa ni pamoja na suala la Muungano, hata ikiwa wapo watakaotaka uvunjwe nasi tutayachambua, ninawahakikishia wananchi kuwa Tume hii itafanya kazi kwa uwazi na maoni yote yatakayosikilizwa yatafanyiwa kazi ipasavyo,” alisema.
Alisisitiza kuwa kwa kutumia busara ya kutosha wasiposikiliza maoni ya wananchi, watakuja kukwama katika kura za maoni baadaye, baada ya kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba Akizungumzia ufanyaji wao wa kazi, Jaji Warioba alisema hivi karibuni Tume itaanza safari mikoani na wamejigawa makundi saba ambapo kila moja litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho wa mwaka.
Warioba alisema kila kundi litafanya kazi kwa wastani wa mwezi mmoja kila mkoa isipokuwa kwenye mikoa midogo kwa eneo ambako Tume itatumia muda mfupi. Jaji Warioba alitangaza kuanza kusikiliza maoni ya mikoa minane ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kwa uwazi bila hofu na kwa utulivu, tunaomba wawe wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza maoni ya wengine hata kama hawakubaliani nayo,” alisema.
Alisema lengo la Tume ni kuhakikisha Watanzania wanatoa maoni lakini kwa kuzingatia ukubwa wa nchi na mazingira halisi, hawataweza kuonana na kila mtu ingawa wanataka kupata maoni ya wote kwa njia mbalimbali.
Alisema pamoja na mikutano mbalimbali katika mikoa yote, pia kutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa ndani na nje ya nchi kwa kutumia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii kama Face book, twitter, blogu pamoja na Posta.
Jaji Warioba alisema katika mikutano hiyo maoni yatakuwa yakichukuliwa kwa kuandikwa, kurekodiwa kwa kamera za video ili iwe rahisi kuchambuliwa, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwenye kumbukumbu rasmi za mijadala na katika maktaba kwa ajili ya kumbukumbu.
Aliomba wananchi kutoa hoja badala ya malalamiko pekee na mapendekezo ya kuingia kwenye Katiba yatasaidia. Katiba 500,000 Alisema kwa mwezi mmoja na nusu tangu waanze kazi, walikuwa wakijiandaa na kutambua umuhimu wa elimu kwa umma, kuhusu yatakayozingatiwa kwenye Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, wameandaa nakala 500,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na nakala 500,000 za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012.
Jaji Warioba alisema kwa kutambua kuwa nyaraka hizo hazitoshi na hata kama zikipatikana kwa wingi, ni vigumu wananchi kuzisoma na kuzielewa kirahisi, pia wameandaa nyaraka rahisi kuzisoma na kuzielewa. Alizitaja nyaraka hizo rahisi kuwa ni Katiba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Lugha Nyepesi, Hadidu za Rejea, Programu ya Elimu kwa Umma na Utekelezaji wa Kazi za Tume ambavyo tayari vimeanza kusambazwa.
Alisema mwelekeo wa kubaini maeneo ya kufanyia kazi umeanza kuonekana hasa kuhusu taasisi za Dola kama Serikali na vyombo vyake na madaraka ya viongozi na taasisi zao.
Alisema Tume inaomba maeneo mengine muhimu nayo yapewe uzito, hasa yaliyo katika sura ya kwanza ya Katiba ya mwaka 1977ambayo ndiyo moyo wa Katiba.
Alitaja maeneo manne muhimu ambayo Tume itapenda kupata maoni kuwa ni linalohusu misingi ya Taifa iliyotajwa kuwa ni uhuru, haki, udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote, ingawa wananchi wana uhuru wa kuabudu.
Alisema ingawa misingi hiyo ndiyo nguzo ya mshikamano na utulivu wa wananchi, baadhi ya watu wanasema ama misingi hiyo haitoshi au imetelekezwa, huku wengine wakidai inatosha, Tume ingetaka maoni kutoka kwa wananchi.
Warioba alisema eneo la pili ni kuhusu mamlaka ya wananchi, kwani wapo wanaodai mamlaka hayo lakini hayakufafanuliwa kama maeneo mengine na hakuna utaratibu wa kuyatumia kwani yameporwa na kutumiwa kisiasa. Eneo la tatu kwa mujibu wa Jaji Warioba ni mlengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali.
Alisema Tume ingependa kupata maoni kuhusu malengo muhimu ya Taifa na jinsi ya kuyalinda, kuyaendeleza na kuyatumia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Alisema pia Tume yake ingependa kusikia ndoto za wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wafanyabiashara wakubwa na wadogo na wengineo.
Na eneo la nne ni haki za binadamu na wajibu wa jamii ambapo sura ya kwanza ya Katiba ya mwaka 1977 ina orodha ndefu ya haki na wajibu kwa raia, lakini wapo wanaosema hazitoshi au zinadhulumiwa na kuminywa.
Warioba alisema awamu ya pili ya uratibu na ukusanyaji maoni itafanyika kupitia mabaraza ya Katiba, huku akisihi wananchi kuwa makini katika utoaji maoni, ili isitokee kama ilivyo kwa nchi nyingine, zilizodai mabadiliko kabla ya awali hayajaanza kufanya kazi.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei mosi, baada ya wajumbe wake kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, inaongozwa na Mwenyekiti, Jaji Warioba akisaidiwa na Makamu wake Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhan na wajumbe 30, ikiwa ni wajumbe 15 kutoka kila upande wa Muungano wa Tanzania.
Kutoka Bara ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Mngwali, Dk Sengodo Mvungi, Richard Lyimo, John Nkolo, Alhaji Saidi El Maamry na Jesca Mkuchu.
Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Malale na Joseph Butiku. Kutoka Visiwani ni Dk Salim Ahmed Salim, Fatma Saidi Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Saidi, Ussi Khamis Haji na Salma Maoulidi.
Wengine ni Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh. Shughuli za Tume hiyo zinaratibiwa na Sekretarieti ambayo Katibu wake ni Assaa Ahmad Rashid na Naibu ni Casmir Kyuki.
chanzo;habarileo
 
Back
Top Bottom