Tume kuchunguza kutupwa maiti za vichanga Mwananyamala | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tume kuchunguza kutupwa maiti za vichanga Mwananyamala

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Rutashubanyuma, Feb 2, 2011.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Feb 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,592
  Trophy Points: 280
  Tume kuchunguza kutupwa maiti za vichanga Mwananyamala

  Gedius Rwiza

  KUFUATIA vifo vya vichanga 10 vilivyokutwa vimefukiwa katika shimo jirani na Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, jopo la wataalam mbalimbali limeundwa kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.

  Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema Serikali imeunda tume ya watu watano (5) kufanya uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo ambayo itakamilisha uchunguzi huo ndani ya siku saba.

  Alisema juzi jioni alipopata taarifa hizo alifika katika eneo la tukio na kukuta vichanga kumi vikiwa vimefukiwa katika shimo na kwamba walizaliwa wakiwa wamekufa.

  “Ni kweli taarifa za awali tulizozipata ni kwamba watoto saba walikuwa hawajafikia hatua ya kuzaliwa na wengine watatu walikuwa wamefikisha wakati wa kuzaliwa na sasa tayari uchunguzi unaendelea, kubaini aliyesababisha kufukiwa kwa watoto hao katika shimo,”alisema Rugimbana.

  “Hata kama viumbe hivyo vimekufa, ni lazima taratibu zifuatwe sio kufanya kitendo kile. Kweli kinasikitisha, kwa hiyo uchunguzi unaendelea muda sio mrefu jamii itapata majibu sahihi, tunaiomba jamii ivumilie wakati uchunguzi ukiendelea,”alisema Rugimbana.

  Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Nduguru alisema kwa mazingira ya tukio hilo lazima uongozi wa Halmashauri ujiridhishe kwa kufanya uchunguzi wa kutosha na kubaini chanzo cha tukio hilo na kwamba kama kuna uzembe ulifanywa na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Mwananyamala watachukuliwa hatua za kisheria.

  “Kwa kawaida kuna taratibu za kumzika mtu mara baada ya kufariki sio kama ilivyotokea, hili ni tukio la kusikitisha kwa hiyo tunawaomba wananchi wawe na subira ili uchunguzi ufanyike na ukweli utajulikana,”alisema Ndunguru.

  Hata hivyo, tayari wanaharakati wamepinga tume hiyo wakitaka isishirikishe mfanyakazi yeyote wa Manispaa ya Kinondoni.

  Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na utawala bora na afya la Sikika, Irenei Kirio alisema kuwa tume hiyo ni batili na kwamba isithubutu kufanya kazi yoyote.

  "Tume iliyoundwa ni kiini macho kwa sababu ni watendaji wa manispaa hivyo watakuwa wanajichunguza wenyewe, ni walewale. Tunaomba tume huru isiyomhusisha mtendaji hata mmoja wa manispaa hiyo au hospitali ya Mwananyamala,"alisema Kirio.

  Akizungumza katika mkutano uliowahusisha viongozi wa Manispaa ya Kinondoni na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema mtu mmoja ametiwa mbaroni akidaiwa kuhusika na tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo chake.

  Alisema kuwa kwa sasa upelelezi unaendelea kubaini watu wengine waliohusika katika tukio hilo.

  “Kwa sasa tayari kuna mtu mmoja amekamatwa, anaendelea kuhojiwa na polisi wakati upelelezi wa kuwakamata wengine ukiendelea na baada ya hapo tutatoa taarifa za chanzo cha tukio hilo,”alisema Kenyela.

  Alisema kuwa katika hatua ya uchunguzi zipo taarifa za wote waliojifungua watoto hao, ambapo alisema wataitwa na tume hiyo ili kuhojiwa na kujua ukweli.

  "Kwa bahati nzuri anuani za wale wazazi wa vile vichanga tunazo, kwa hiyo tutawatafuta na watahojiwa ili kupata ukweli wa mambo yalivyokuwa," alisema Kenyela.

  Hata hivyo, malumbano yalizuka baina ya wanahabari walioshuhudia tukio hilo awali na uongozi wa manispaa kuhusu watoto hao kufikia au kutofikia hatua ya kuzaliwa.

  Kuzuka kwa malumbano hayo kulitokana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sofinias Ngonyani kudai kuwa watoto saba kati ya kumi waliofukiwa walikuwa hawajafikia muda wa kuzaliwa bali mimba zilizotoka (abortion) na watatu pekee ndio waliofikia hatua ya kuzaliwa.

  Kauli hiyo ilipingwa vikali na wanahabari walioshuhudia tukio hilo juzi na jana kuhudhuria mkutano huo wakisema mganga huyo anajaribu kuuhadaa umma.

  “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kati ya waandishi walioshuhudia tukio hilo na kupiga picha, mimi ni miongoni mwa hao. Kama kuna ubishi tunaweza kuwaonyesha picha za watoto hao ili kupata uhakika wa suala hili maana walikuwa wamefikia muda wa kuzaliwa,” alisema mwanahabari Sam Mahela wa ITV mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Feb 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,592
  Trophy Points: 280
  Ukatili Mwananyamala wafichua siri nzito

  Maiti za watoto huuzwa kwa matumizi ya ushirikina

  na Waandishi wetu

  SAKATA la kukutwa kwa maiti za watoto wachanga 10 katika shimo moja fupi eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam juzi, limezua utata mkubwa baada ya madaktari wa hospitali hiyo kutoa maelezo ya kujikanganya, yanayotia shaka na kuacha maswali mengi bila kujibiwa.

  Jana madaktari wa hospitali hiyo pamoja na mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, walifanya mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa manispaa hiyo, kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo la kikatili na la kusikitisha lililogusa hisia za watu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

  Madaktari hao kwa nyakati tofauti walisema miili ya vichanga hao ilikabidhiwa kwa wazazi wao baada ya kupoteza maisha na kati ya vichanga hao, walizaliwa wakiwa hawajatimiza muda (njiti) wakati watatu walitimiza miezi ya kuzaliwa.

  Dk. Sophinias Ngonyani ambaye alikuwa wa kwanza kutoa ufafanuzi huo, alisema maiti za vichanga watatu waliookotwa juzi katika eneo la makaburi ya Mwananyamala, walizaliwa majumbani mwao wakiwa wametimiza muda, lakini walifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.

  "Mtoto wa pili kati ya hao watatu, alikuwa wa ajabu kwani viungo vyake havikutimia na wa tatu alikuwa na tumbo kubwa na miguu iliyopinda," alisema Dk. Ngonyani.

  Alisema maiti ya vichanga saba, vifo vyao vilitokana na mimba za mama zao kuharibika na vichanga hivyo vilikuwa na umri wa kati ya wiki sita na saba.

  Alipobanwa na wanahabari kutaka ufafanuzi wa kichanga cha wiki sita kuonekana na viungo kamili, daktari huyo alibadilisha kauli na kusema walikuwa na umri wa kati ya miezi mitatu, minne, mitano hadi sita.

  "Katika uchunguzi uliofanywa, watoto hao watatu, ilionekana walipishana kwa siku mbili ambao pia maiti zao zilikabidhiwa kwa wazazi wao," alisema Ngonyani.

  Hata hivyo daktari huyo alishindwa kujibu swali la maiti za vichanga hivyo kukutwa kwenye shimo moja na shuka la Hospitali ya Mwananyamala.

  Pia alishindwa kufafanua kwa vipi maiti hizo ziliruhusiwa kutoka hospitalini hapo na kukabidhiwa kwa wazazi wao bila kibali, huku zingine zikiwa na plasta zenye majina ya mama zao.

  Akijibu utata huo, Dk. Rugimbana alisema si vibaya watoto kuzikwa na shuka lenye nembo ya hospitali kwani kuna baadhi ya wazazi wasio na uwezo wa kununua sanda, hivyo shuka hizo hutolewa kama sehemu ya msaada kwao.

  Kuhusu vichanga hivyo kuzikwa kwenye kaburi moja, Dk. Rugimbana alisema mazishi ya watoto hao yalifanyika kinyume na taratibu kwani walipaswa kuzikwa kwa heshima kama binadamu wengine.

  Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema jeshi la polisi linamshikilia mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo, pia wanamsaka mtuhumiwa mwingine anayedaiwa kuhusika na utata wa maiti za vichanga hivyo.

  Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Raphael Ndunguru amesema kuwa amelazimika kuunda tume ya watu watano ndani na nje ya hospitali hiyo ili ifanye uchunguzi wa kina kubaini jinsi miili ya ya vichanga hivyo ilivyotoka wodini, mochwari na kufikishwa katika eneo la mazishi.

  Aliwataka walioteuliwa kuwa wanatakiwa wafanye kazi hiyo ndani ya siku saba. walioteuliwa ni pamoja na Nduguru.

  Wengine ni Dk. Charles Kalumbo, Gaudance Nyanihusha, Zuhura Majapa, Dk. Sophinias Ngonyani na Mwanasheria wa Manispaa ya Kinondoni.

  Wakati viongozi wa serikali wakitoa taarifa hizo habari za kuaminika ambazo Tanzania Daima Jumatano ilizipata zinadai kuwa baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo hasa kitengo cha kuhifadhi maiti, wamekuwa wakiendesha biashara za kuuza miili ya watoto wachanga kwa wafanyabiashara kwa imani za kishirikina.

  Chanzo hicho kilieleza kuwa maiti za watoto hao zimekuwa zikiuzwa kulingana na umri wa mtoto kuanzia sh elfu 50 na zaidi.

  Habari hizo zilidai kuwa kuna vitendo vya kushangaza vinavyofanywa ndani ya hospitali ambapo vichanga vinavyopoteza maisha na wazazi wao kushindwa kuwarejesha nyumbani kwa ajili ya mazishi, huuzwa kwa imani za kishirikina.

  "Huwezi kuamini lakini mimi nimeshuhudia mambo ya ajabu yanayofanyika katika upande wa kuhifadhi maiti kwani maiti za watoto hao zinauzwa kama njugu na huu ukatili wa juzi ni Mungu kataka kuwaumbua," kilisema chanzo hicho.

  Kwa mujibu wa habari hizo, viungo vinavyohitajika katika viungo hivyo ni pamoja na ulimi, viungo vya siri, kucha na nywele.

  Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Sikika na utawala bora katika sekta ya afya ya Irene Kiria alisema, hakubaliani na tume ilioundwa kwa ajili ya uchunguzi wa vichanga hivyo.

  Akizungumza kwa njia ya simu Kiria alibainisha kwamba mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Kinondoni, alitakiwa kuunda tume huru badala ya hiyo itakayohusisha sekta ya afya.

  Hata hivyo alisema tume zinazoundwa na serikali, hazitaweza kutoa majibu sahihi kwa madai kuwa siyo mara ya kwanza kutokea katika hospitali hiyo kwani miaka mitatu iliyopita, kilitokea kifo cha utata cha mtoto Salome na serikali ilishindwa kutolea ufafanuzi licha ya kuundwa tume.

  Amewataka wazazi wenye vichanga hivyo kujitokeza ili kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kubaini ukweli wa sakata hili.
   
 3. RayB

  RayB JF-Expert Member

  #3
  Feb 2, 2011
  Joined: Nov 27, 2009
  Messages: 2,754
  Likes Received: 88
  Trophy Points: 145
  Tume Bingo bana hasa kwa Bongo kila siku wati wanaombea tume zitokee wachaguliwe
   
 4. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #4
  Feb 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,592
  Trophy Points: 280
  Hivi tangia tupate uhuru ni Tume ngapi zimeundwa na zimetatua matatizo yepi nionavyo ni wafilisika kifrika bado wazitarijia Tume zitoe ufumbuzi wa matatizo ya kitaalamu kupitia mlolongo wa kisiasa.
   
 5. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #5
  Feb 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,592
  Trophy Points: 280
  Kigugumizi Mwananyamala


  *Maelezo ya madaktari, DC yatofautiana

  Na Waandishi Wetu

  MADAKTARI wamepatwa na wakati mgumu baada ya kubanwa walipokuwa wakijichanganya kutoa maelezo ya awali kuhusu
  watoto 10 waliokutwa wamezikwa katika shimo moja Mwananyamala kwa Kopa Dar es Salaam.

  Tukio hilo lilitokea jana katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Rugimbana katika mkutano wa waandishi wa habari na madaktari, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Kamanda wa Polisi Kinondoni na watendaji wengine wa wilaya hiyo.

  Taarifa iliyotolewa na Bw. Rugimbana ilikuwa ikieleza kuwa watoto watatu walizaliwa wakiwa wafu, watoto saba walizaliwa kabla ya wakati na wote walikabidhiwa kwa wazazi kwa ajili ya maziko.

  Lakini Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dkt. Sofinius Ngonyani alisema watoto watatu walizaliwa wafu na wengine saba ni mimba zilizoharibika kati ya wiki 4-6.

  Kauli hiyo ilizua utata kwani walioshuhudia walisema watoto wote 10 walikuwa wakubwa na si mimba za wiki, kwani mimba zilizoharibika zenye ukubwa huo huwa haijafikia kuwa kiumbe bali huwa ni damu.

  Daktari alishindwa kuendelea kutoa maelezo baada ya waandishi wa habari kuonesha dhahiri kuwa hawakuamini hadi Mkuu wa Wilaya aliamua kuingilia kati na kuinuka kutoa ufafanuzi kwa mara nyingine.

  "Tusikilizane, nilivyoona mimi ni vitoto vichanga, naomba tutumie lugha za wataalamu," alisema na kuongeza kwamba wataalamu wanajua aina za watoto hao.

  Hata hivyo, alisema kwa mazingira yoyote iwe mimba zilizoharibika au watoto waliokufa utaratibu uliotumika kuwazika sio unaostahili, hivyo watafanya uchunguzi kuanzia kwa wazazi wa watoto hao kumjua aliyehusika.

  Aliendelea kufafanua kwamba eneo walilofukiwa watoto hao ni sehemu ya makazi na si eneo rasmi lililotengwa kwa ajili hiyo, hivyo inaonesha wazi kwamba makubaliano yalikuwa kati ya wazazi na huyo aliyekwenda kuzika watoto hao.

  Alitoa mwito kwa wananchi wanaotaka kusaidiwa kuzika watoto wao kufuata mamlaka inayohusika na endepo wangefuata taratibu za hospitali badala ya njia za panya hali hiyo isingetokea.

  Waandishi wa habari pia walihoji ni vipi shuka la hospitali likutwe katika shimo hilo na isijulikane nani aliyefanya hivyo.

  Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Raphael Ndunguru alisema kutokana na mazingira yasiyoeleweka, aliamua kuunda tume ya watu watano kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.

  Alisema tume hiyo itachunguza kuona kanuni na utaratibu wa hospitali zinasemaje, katika kesi ya watoto hao inakuwaje, namna maiti zilivyotoka wodini, shuka lilivyotoka chumba cha kuhifadhia maiti na kufikishwa katika shimo hilo.

  "Tunatoa siku saba kuanzia leo, uchunguzi ufanyike na ripoti itolewe," alisema.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema kazi yao ni kuchunguza waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria, ambapo wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano na mwingine bado wanamsaka kwa sababu ya kuhusika na uzembe huo.

  Alisema uchunguzi utakapokamilika na watuhumiwa wote kupatikana watafikishwa mahakamani na katika kufanikisha hilo wanawatafuta wenye watoto, kwani namba zao za simu zipo, ili wasaidie kumtambua aliyehusika.

  Kwa upande wa wauguzi katika Hospitali ya Mwananyamala walipohojiwa kuhusiana na tukio hilo walizungumza kwa woga kwamba hali hiyo imewanyima raha na kuwafanya wanashindwe kufanya kazi.

  "Kila unapopita unasikia Mwananyamala wauaji, inasikitisha sana, hospitali ilishafikia katika hali nzuri kwenye utoaji huduma lakini imeingia doa," alisema kwa unyonge na kuomba asitajwe jina gazetini sababu si msemaji.

  Maiti za watoto hao zilikutwa juzi kwenye shimo katika eneo lililopembezoni mwa makaburi ya Mwanyamala kwa Msisiri B yalipo makazi ya wananchi zikiwa zimezungushiwa shuka jeupe lenye nembo ya Hospitali ya Mwananyamala.

  Majina katika kanga

  Majina ya wazazi wa watoto waliofukuliwa katika shimo la taka jirani na makaburi ya Mwananyamala kwa Kopa yamekutwa katika kanga zilizoviringishiwa katika miili ya watoto hao.

  Kamanda Kenyela alisema majina ya wazazi hao Furaha Rajab mkazi wa Manzese, ambaye alijifungua mtoto wa kiume Januari 23, mwaka huu na kuwa na maumbile yasiyo ya kawaida

  Alisema vitabu vya hospitali hiyo vinaonesha kuwa alichuliwa na baba yake aitwae Bw. Idrisa Zuberi Januari 24.

  Alisema mzazi wa pili alijulikana kwa jina la Ruth Mtanga na kumbukumbu zinaonesha alijifungua mtoto wa kiume akiwa njiani kwenda hospitalini Januari 27 saa 12:00 asubuhi

  Alisema kichanga hicho kilifariki baada ya kufikishwa hospitalini na kumbukumbu za chumba cha kuhifadhiwa maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.

  Alimtaja mzazi mwengine ni Bi. Regina Samwel mkazi wa Kimara na kumbukumbu za hospitali hiyo zinaonesha alijifungua mtoto wa kike akiwa amekufa pia kumbukumbu za chumba za kuhifadhia maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.

  Kamanda kenyela aliongeza kuwa vichanga vingine saba vilikua vimefungwa kwenye shuka yenye mandishi ya hospitali hiyo wodi namba IA lakini hazina kumbukumbu zozozote zinazoonesha kuwa wamezaliwa na kufa katika hospitali hiyo.

  Aliongeza kuwa polisi na madaktari walifika eneo la tukio na kuchunguza vichanga hivyo na kungundua vimezaliwa vikiwa na miezi saba hadi tisa, maiti zimehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi.

  Imeandaliwa na Gladness Mboma, Kulwa Mzee na Nassra Abdulla

  [​IMG]


  6 Maoni:

  [​IMG]
  Anonymous said... Hii hospitali ya Mwananyamala mbona ina visa vingi? Vifo vya akina mama wajawazito vimetisha, na sasa haya. Hivi hiyo Wizara ya Afya na serikali yenyewe imeshindwa kabisa kudhibiti hii hali? Tanzania tunapelekwa wapi na huu utawala wa CCM? Nchi yetu imekuwa kama nyumba ya wahuni!
  February 2, 2011 12:16 AM [​IMG] [​IMG]
  Anonymous said... Mh! NO COMMENT
  February 2, 2011 12:37 AM [​IMG] [​IMG]
  Anonymous said... Wanaharakati hasa wakina mama mko wapi katika suala hili? Mashehe na Maaskofu ambao wajibu wenu ni kulinda uhai na utu wa kila mwanadamu aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu mko wapi? Hata kama walikua wamekufa, maiti za wanadamu zinapaswa kuheshimiwa, hawa si ayawani! Nilitegemea protests kuzunguka hospitali ya Mwananyamala mpaka ukweli ujulikane!
  February 2, 2011 2:46 AM [​IMG] [​IMG]
  Anonymous said... Protest kutoka wapi wakati mama wa hawa watoto ndio waliokubali kuzikiwa vichanga vyao! wako wapi mbona kimya hadi hii leo? hii kashfa in siku ya nne! kama kweli wangekuwa hawakuhusika basi wangekua vifua mbele kuongoza maandamano hayo unayoulizia! lakini kimyaaaaaa! bado tu hujapata jibu? ukitaka zaidi kafukue fukue kila suspicious shimo karibu na spitali uone mambo! kisingizio "Umasikini!"
  February 2, 2011 3:32 AM [​IMG] [​IMG]
  Anonymous said... This is strange joke! una uwezo wa kustarehe na kuzaa lakini but when it comes kuhusu kuzika unakuwa masikini ghafla?!!! hata inabidi kusaidiwa wa walinzi wa hospitali?!! angekuwa hai huyo mtoto angukulelea nani?!! this is funny!
  February 2, 2011 3:38 AM [​IMG] [​IMG]
  Anonymous said... Politics addicted people mnaboa sana kila linapotokea tukio mnaliongelea na kuchombeza political affiliations zenu!mnatuboa tafuteni jukwaa sahihi la utashi wenu wa kisiasa.Jadilini matukio ya kijamii kwa mtazamo wa kuijenga jamii na si kupenyeza agenda zenu za kisiasa.Case hii ya mwananyamala inafichua maovu ambayo yamekuwa yakitendwa na Wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji.Madada wanatupa watoto hai sembuse hao walofariki.Nawashauri Wanzania wote tumrejee Muumba wetu na tuepuke maovu.MUngu anatuona ati!Iweje ubebe ujauzito then usijali mtoto wako.Hata kama ni mfu bado ni mtoto wako mbele za Mungu na anastahili haki zote za Ubinadamu.
  February 2, 2011 5:13 AM
   
 6. RayB

  RayB JF-Expert Member

  #6
  Feb 2, 2011
  Joined: Nov 27, 2009
  Messages: 2,754
  Likes Received: 88
  Trophy Points: 145
  Ukishaangalia idadi yake then unachek matokeo yake then na implementation, outcome, na impact almost ni sifuri tu
   
Loading...