Tume ilivyotimiza sheria uteuzi Wabunge wa CUF

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni ilifanya uteuzi wa Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), uteuzi uliopokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wadau.

Baadhi ya wafuasi wa CUF, viongozi wa chama hicho na gazeti moja la Kiswahili ni miongoni mwa wadau walioshambulia Tume kwa madai kwamba kulikuwa na njama kati ya Tume na Spika wa Bunge, katika kulishughulikia suala la wabunge wanawake wa CUF waliofukuzwa uanachama na kusababisha uteuzi wa wabunge wengine kujaza nafasi zao.

Suala hili liliibua mjadala miongoni mwa wanajamii na Tume ikalaziamika kutoa ufafanuzi kwa ajili ya kuielimisha jamii ili kuziba mwanya wa ufahamu ambao umesababishwa na upotoshaji pamoja na ukosefu wa uelewa juu ya namna ambavyo Tume inafanya kazi zake.

“Nadhani tatizo hapa ni ukosefu wa uelewa wa watu kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine kuna upotoshaji wa makusudi kabisa, pia inaonekana kuna watu hawajui na hawataki kujua,” anasema Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani.

Anasema NEC imezingatia matakwa yote ya kisheria yanayohusiana na viti maalumu vya wabunge wanawake kwa kuzingatia kwamba sheria zinazoiongoza Tume zinatambua chaguzi za aina mbili, ule wa kupiga kura na ule wa wabunge wa kuteuliwa.

“Ifahamike kwamba viti maalumu vya wanawake ni aina ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria, wabunge wanapatikana kwa njia mbili, ile ya kupiga kura na hii ya viti maalumu ambayo inatokana na uwiano wa kura kwa kila chama,” anasema.

Kailima anasema kwa bahati mbaya baadhi ya wapotoshaji ni viongozi wa CUF ambao kwa nafasi zao wanajua vizuri kanuni na taratibu ambazo zilifuatwa na tume kwenye mchakato huo. “Labda nianze kwa kuelezea viti maalumu vya wanawake vinatoka wapi?

Kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 78 (1) na taratibu zilizowekwa, vyama vya siasa ambavyo vimeshiriki uchaguzi mkuu na kupata angalau asilimia tano ya kura za wabunge vinakuwa na sifa ya kupata wabunge wa viti maalumu vya wanawake ambavyo ni asilimia 40 ya wabunge wote,” anafafanua Kailima.

Ibara ya 78 (1) ya Katiba inasema “Kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge wanawake waliotajwa katika ibara ya 66 (1)(b), vyama vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za wabunge, vitapendekeza kwa Tume ya Uchaguzi majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa wabunge”.

Kifungu namba 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinavipa vyama vya siasa nafasi ya kuwasilisha kwa tume ya uchaguzi majina yanayopendekezwa kuteuliwa kwenye viti maalumu vya wanawake. “Chama cha siasa kinachogombea katika uchaguzi wa ubunge utakaofanyika baada ya kuvunjwa kwa Bunge kinaweza kupendekeza kwa tume majina ya wagombea wanawake wenye sifa kwa uteuzi wa viti maalumu kwa wanawake,” kinasomeka Kifungu 86A (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

Kailima anasema ili kutimiza matakwa ya kisheria, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Tume iliviandikia vyama vya siasa kuwaomba watume orodha ya majina wanayopendekeza kwa ajili ya viti maalumu vya wanawake bungeni.

Anasema kwenye mchakato wa kujaza nafasi za wabunge wanawake wa viti maalumu, Tume imekuwa ikivigawa viti kwa vyama ambavyo vimefanikiwa kupata asilimia tano ya kura za wabunge na katika uchaguzi wa mwaka 2015 vyama vilivyofanikiwa kuwa na sifa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kifungu namba 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinasema: “Endapo mbunge anajiuzulu, kufariki au anaachia ofi si yake kwa sababu nyingine tofauti na zile zilizopo chini ya kifungu cha 133 (kuhusu kesi inayosubiria maamuzi ya mahakama), Spika, kwa maandishi kwa mwenyekiti wa tume na kwa taarifa itakayochapishwa katika gazeti la serikali, atatangaza kwamba kuna nafasi katika kiti cha ubunge”.

Kailima anazidi kufafanua kwamba baada ya NEC kupokea barua kutoka kwa Spika, hatua inayofuata inatekelezwa kwa mujibu wa Ibara ya 74 (4) ya Katiba ambayo inaelekeza kwamba orodha iliyowasilishwa tume awali na chama husika cha siasa wakati wa uchaguzi mkuu itumike kujaza nafasi iliyopo wazi au nafasi zilizo wazi. Anasema ujazaji huo wa nafasi unafanyika baada ya kushauriana na chama husika cha siasa.

“Orodha ya majina ya wagombea wanawake iliyowasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi na kila chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu ndiyo itakayotumiwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kushauriana na chama kinachohusika, kwa madhumuni ya kujaza nafasi yoyote na mbunge wa aina hii inapotokea wakati wowote katika maisha ya bunge,” inasomeka Ibara ya 78 (4) ya Katiba.

Kailima anasema kutokana na matakwa ya sheria kwa kawaida tume inaviandikia vyama vya siasa barua kuwauliza ni yupi miongoni mwa wale walioko kwenye orodha anafaa kuteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi.

Anasema vyama hivyo vinatakiwa kujibu barua ya Tume kwa kujaza Fomu Namba 8E, na baada ya kuipokea hiyo fomu Tume huendelea na taratibu nyingine za kiutawala kujiridhisha kwamba mhusika au wahusika wana sifa stahiki na kupitisha jina au majina yao.

Anasema vigezo vya kuwa na sifa vinatokana na matakwa yaliyowekwa na sheria kuhusu sifa za mtu anayefaa kuwa mbunge lakini ni lazima kwanza jina linalopendekezwa liwe kwenye orodha iliyowasilishwa Tume wakati wa uchaguzi mkuu na kwamba Tume haipokei majina mapya.

“Bila ya kuathri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo; ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza; ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa,” inasomeka sehemu ya Ibara ya 67 (1) ya Katiba.

Kailima anafafanua zaidi: “Baada ya kukamilisha utaratibu wa kupitia na kujiridhisha juu ya vigezo vya jina la mwanachama anayependekezwa, tunamwandikia Spika wa Bunge kumfahamisha kwamba tumeshafanya uteuzi, barua pia inatumwa kwa chama cha siasa kwa kunukuu barua yao ya maombi kuwafahamisha kwamba maombi yao yamepokelewa na yameshughulikiwa na wakati mwingine huwa tunawaandikia wahusika wenyewe (wabunge walioteuliwa).”

Akizungumzia suala mahususi la CUF, Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi anasisitiza kwamba taratibu zilifuatwa. Kwamba Julai 26 Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika kumfahamisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwamba kuna viti maalumu viko wazi Bungeni vya CUF.

Anasema siku iliyofuatia, Julai 27 Tume ilimwandikia katibu mkuu wa CUF. Kwa taratibu za tume, barua ikiandikwa na mwenyekiti wa tume inatumwa kwa mwenyekiti wa chama cha siasa na nikiiandika mimi (Mkurugenzi wa Uchaguzi) naituma kwa katibu mkuu wa chama husika”.

Anasema wakati wa kutuma barua, NEC imekuwa ikitumia anuani zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa sababu Tume haishughuliki na mambo ya usajili wa vyama na badala yake inapokea taarifa zote kuhusu majina ya vyama, majina ya viongozi, namba za usajili na anuani kutoka kwa Msajili.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo anakiri kwamba kuna vyama vina anuani zaidi ya moja kama CCM ambacho kina anuani ya Dodoma na Dar es Salaam na CUF ambacho kina anuani ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Kailima anasema kwamba katika suala la CUF la hivi karibuni lililohusisha wabunge wanane waliotenguliwa na hatimaye Tume kuteua wabunge wengine, utaratibu ulifuatwa na barua kwa chama ilitumwa kwa anuani ya Dar es Salaam kwa kuwa barua iliyotumwa Tume ilitoka Dar es Salaam.

Akifafanua zaidi juu ya madai kwamba majina ya wabunge walioteuliwa hayakuwa kwenye orodha iliyotumwa awali na CUF, Kailima anasema matamshi au tuhuma kama hizo ni mfano tosha kabisa kwamba kuna watu, hasa wanasiasa ambao walijipanga kupotosha umma kwa makusudi kabisa kwa sababu za kisiasa wanazozijua wenyewe.

“Inashangaza kwa sababu Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ambaye anadai kwamba majina ya wateule hayakuwa kwenye orodha, yeye ndiye aliyesaini karatasi yenye orodha hiyo ambayo iliwasilishwa hapa Tume mwaka 2015,” anasema.

Akifafanua juu ya madai kwamba ni kwa nini tume ililishughulikia suala la CUF kwa haraka, Kailima anasema kwamba sheria ambazo zinaisimamia Tume kwenye mchakato wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu hazijaweka masharti ya muda kwenye uteuzi na kwa hiyo Tume ipo huru kufanya maamuzi haraka kadri iwezekanavyo na ni jambo linalopaswa kupongezwa na siyo vinginevyo.

Habari Leo
 
Back
Top Bottom