SoC01 Tukipeleka umeme vijijini, tutaua ndege wawili kwa jiwe moja kwa kupata nishati ya umeme na tutatengeneza fursa nyingi zitokanazo na umeme

Stories of Change - 2021 Competition
Sep 6, 2021
24
109
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Umeme ni nishati muhimu sana katika karne hii ya leo. Shughuli nyingi za majumbani, viwandani, ofisini na sehemu zingine, zinategemea sana nishati hii ili kufanya kazi.

Matumizi yake ni mengi mno na umuhimu wake hauelezeki.
Heko kwa Serikali ilijitahidi na inajitahidi kufikisha nishati hii muhimu kwenye vijiji vingi vya Tanzania.

Juhudi ni kubwa ila tuongeze juhudi zaidi ili tupeleke umeme kwenye vijiji vyote vya Nchi yetu ili Watanzania wa vijijini wapate umeme na kuweza kufaidika na fursa nyingi zitokanazo na umeme.

Hadi kufikia Februari 2, 2020, jumla ya vijiji 8,587 kati ya vijiji 12, 268 vilipelekewa umeme katika Mradi wa Usambazaji wa umeme vijijini (REA).

Juhudi ni kubwa ila tuongeze juhudi zaidi ili tupeleka umeme vijijini kwa asilimia miamoja (100%).

TUKIPELEKA UMEME VIJIJINI, TUTAUAJE NDEGE WAWILI KWA JIWE MOJA?

Kwanza, vijiji vya Nchi yetu vitapata nishati ya umeme kwa ajili ya matumizi ya mwanga.

Baadhi ya vijiji vya Nchi yetu bado vina changamoto ya ukosefu wa umeme kwa ajili ya mwanga. Wananchi wengi wanatumia sola, taa, vibatari na kadhalika kwa ajili ya kupata mwanga. Wanatumia sola kwa ajili ya kuendesha shughuli zingine za majumbani na biashara.

Nishati hizi za sola na taa, bado zina udhaifu mkubwa na zenye kero kubwa katika matumizi. Hivyo, ni muhimu vijiji hivi kufikishiwa nishati ya umeme ili kutatua udhaifu wa changamoto hizo.

Pili, tukipeleka umeme vijijini, tutatengeneza fursa nyingi zitokanazo na umeme kama ifuatavyo.

Umeme vijijini utasaidia watu kuona na kuonyesha michezo ya mpira wa miguu (Ligi kuu na Ulaya), michezo ya ngumi, michezo ya magari na michezo mingine chungu mzima, kwa wingi ukilinganisha na sasa. Kitendo hiki cha kuonyesha michezo, kina matokeo chanya kwenye uchumi wa watu na pato la Taifa.
Idadi kubwa ya watu itaongezeka kununua ving'amuzi, kununua runinga, kununua umeme na kadhalika.
Manunuzi yote haya, yatahusisha kodi katika bidhaa hizo, hivyo kuongeza wigo wa kukusanya mapato ya Serikali.

• Wigo wa uuzaji na ununuaji wa vinywaji (vileo) baridi utaongezeka maradufu.
Ununuaji na uuzaji wa vinywaji baridi kama vile soda, bia, juisi na kadhalika, utaongeza pato la Taifa kupitia kodi ya vinywaji hivyo.
Ni ukweli ulio wazi kuwa, vinywaji (vileo) vinachangia kiasi fulani katika pato la Taifa.
Hata msingi wa lile wazo la kiuchumi la Serikali kutaka kupunguza bei ya vinywaji na vileo, ni kutaka kukusanya kodi katika bidhaa hiyo ya vinywaji kwa mzunguko mkubwa zaidi.
Hivyo tukipeleka umeme vijijini, tutaongeza wigo wa watu kutumia vinywaji hivyo na kutanua wigo wa Serikali kukusanya kodi maradufu kupitia bidhaa hiyo.
Soda ya moto hainyweki wala bia ya moto hainogi.

• Umeme vijijini utatoa fursa kwa akina mama na watu wengine, kugandisha barafu majumbani mwao na kisha kuwauzia wanafunzi wa shule na watu wengine.
Hii ni fursa muhimu sana kwa akina mama wa nyumbani, kwani ataweza kugandisha barafu na kujipatia kipato kwa ajili ya matumizi ya familia.
Hii itapunguza utegemezi wa mama kwa baba.
Mama kupitia fursa ya umeme vijijini, anaweza kutengeneza juisi baridi ya matunda hivyo kujipatia fedha ya matumizi ya familia.
Hakika, umeme ukienea vijijini, utawasaidia akina baba kutua baadhi ya mizigo midogo midogo ya familia kama vile pesa ya mboga, chumvi na kadhalika.

Uwepo wa nishati ya umeme vijijini, utapanua wigo wa vijana wa kike na kiume kujiajiri kwa kufungua saluni za kike na kiume.
Vijana wengi kupitia ajira hii ya saluni ambayo msingi wake mkubwa ni umeme, wataweza kuendesha familia zao na kupata fedha za kujikimu maisha.
Umeme vijijini utasaidia vijana hawa kuweka vivutio vya kibiashara kama vile redio na runinga kwenye saluni zao.
Hii itawarahisishia wao kuvuta wateja kwenye biashara zao.

Tuhakikishe tunapeleka umeme vijijini ili Watanzania wa vijijini wafaidike na fursa za umeme.

Ahsante.
 
Back
Top Bottom