SoC01 Tukio lililonifumbua macho kuhusu changamoto huduma ya dharura katika hospitali zetu

Stories of Change - 2021 Competition

Mazima1

Member
Dec 31, 2020
20
47
Huduma ya dharura katika hospitali zetu imekuwa sio dharura tena badala yake kumfanya mgonjwa asubiri hali ambayo ni hatari kwa afya na usalama wa mgonjwa anayehitaji huduma hiyo

Binafsi mara nyingi nimekuwa nikisikia malalamiko juu ya ya uzorotaji wa huduma ya dharura katika hospitali nyingi hali ambayo hupelekea watu kupoteza wapendwa wao au kusababisha madhara kuwa makubwa zaidi ya ilivyotakiwa kuwa,binafsi nilikuwa sijawahi kushuhudia kwa macho yangu.

Ushuhuda wangu
Wiki chache zilizopita nilimpeleka hospitali mgonjwa ambaye aliumia katika shughuli za ujenzi baada ya kujiumiza na ncha kali ya sururu katika maeneo ya utosi,kwa mujibu wa daktari aliyemuhudumia ni kuwa ile ncha ya sururu ilitoboa kidogo mshipa mmojawapo kichwani hali ambayo ilipelekea mgonjwa kutokwa na damu nyingi,binafsi kwa kuona hali ile niliogopa kwani damu ilikuwa inatoka spidi sana mithili ya mfereji,

Kwa maelezo ya daktari yule ni kuwa endapo ncha ile ingechimba ndani kidogo badi hadi muda ule tungekuwa tunazungumza habari nyingine

Basi katika kutafuta namna ya kumnusuru mgonjwa tulimfunga kitambaa na kumkimbiza katika hospitali fulani inayomilikiwa na serikali(sitoitaja)baada ya kufika mapokezi tuliruhusiwa kuwapita wagonjwa wengine waliokuwa wakisubiri huduma katika foleni ya mapokezi,wagonjwa wenyewe hawakuwa na hiyana juu ya hilo,pengine kwa sababu ya utu na ukarimu wa mtanzania ambao ni sehemu ya utamaduni wetu wa kila siku.

Tafrani ilianza pale tu tulipofika dirisha la mapokezi na kuongea na mhudumu ambaye kwanza hakuonekana kuwa na haraka kwani kwa karibia dakika moja aliendelea kutumia simu yake ya mkononi,nikiwa nimeghafirika kidogo nikamwambia mgonjwa wangu anahitaji huduma ya dharura, akanielekeza kuwa mgonjwa akae chini na mimi nimwandikishie taarifa zake,muda huo mgonjwa damu zinaendelea kumbubujika hadi lile tambara alilofungwa limeloana.

Basi baada ya kujaza taarifa za mgonjwa muhudumu akanieleza kuwa inahitajika shilingi elfu mbili, nikamueleza kwamba tumekurupuka kutoka eneo la kazi hivyo hela niliyonayo mfukoni ni shilingi elfu moja tu ila bosi wake nimekwisha wasiliana naye hivyo angefika kama baada ya dakika ishirini hivi na kulipia gharama zote,pasipo wasiwasi muhudumu yule akanijibu "basi msubiri bosi wake akifika na kulipia ndipo tutamuhudumia"nilipatwa na hali ya hasira lakini sikuwa na namna,nikajaribu kuwaomba wahudumu wanikopeshe shilingi elfu mbili ila niweke simu yangu kama dhamana lakini kila muhudumu alidai hana hela yoyote nilijaribu kumuomba huyo muhudumu wa mapokezi lakini yeye aliona kama namsumbua hivyo akanitenga na himaya ya majibu na mdomo wake haukufunguka tena kunijibu
Baada dakika kama tano za kuhangaika bosi alimpigia bodaboda aliyekuwepo karibu akaja na shilingi elfu kumi ndipo nikalipia nikakabidhiwa fomu na kuelekezwa niende duka la dawa.

Nikiwa pale nikaelezwa kuwa inahitajika shilingi elfu ishirini na nne kwa ajili ya kununua vifaa vya oparesheni yaani gloves,nyuzi,sindano na kadhalika,nikajihisi kuchoka kabisa sasa nikajaribu kuhoji kwanini mgonjwa asihudumiwe kwanza halafu malipo yatafanyika baadaye nikajibiwa kwamba huo ndio utaratibu basi tukamsubiri bosi wake ambaye alifika karibia baada ya kama nusu saa hivi ndipo mgonjwa akahudumiwa.

Namshukuru Mungu mgonjwa alipona na hadi muda huu naandika makala hii anaendelea vizuri

Changamoto za kimfumo
Mfumo wa kuratibu huduma za dharura ni mbovu isivyomithilika,kitendo cha mgonjwa mwenye dharura ya hali ile kusubirishwa kwa takribani nusu saa na sehemu ni sawa na kumsogeza karibu mgonjwa na himaya ya Israel mtoa roho,je hilo ndilo lengo la kuanzishwa kwa huduma ya dharura katika hospitali zetu?tukiwa tunaendelea kujiuliza hilo,akilini mwetu tukumbuke kuwa hospitali hizi zimejengwa kwa kodi zetu hilo pia linaweza likatupeleka kwenye majibu ya hilo nililouliza hapo juu

Lakini pia kwanini wizara husika isibadili mfumo kutoka pesa kwanza huduma baadaye na kuwa huduma kwanza pesa baadaye hasa kwa huduma nyeti kama huduma za dharura? serikali ilitazame suala hili.

Utu na ukarimu
Utu na ukarimu vimebaki kama msamiati katika kamusi na sio tendo waliishilo baadhi ya wahudumu katika ofisi za umma,ni dhahiri wahudumu wale waliogoma kunisaidia shilingi elfu mbili kwa kiasi fulani walikosa utu ukizingatia hali aliyokuwa nayo mgonjwa nafikiri suala la "utu na ukarimu" litiliwe mkazo huko vyuoni wanakofundishwa japo utu haufundishwi ila sio vibaya binadamu kukumbushwa juu ya hilo,wafundishwe kuvaa viatu vya mhanga wa tatizo husika hii itasaidia kurahisisha huduma katika hospitali zetu.

Ukosefu wa vifaa tiba
Baada ya kumaliza oparesheni ile tuliandikiwa dawa ambazo zote tulizikosa katika duka la dawa la hospitali ile na kuelekezwa kuzitafuta wenyewe kwenye maduka binafsi ya madawa
Ni ukweli usiopingika kuwa hospitali zetu bado zinakabiliwa na tatizo la upungufu wa madawa na vifaa tiba,wizara ya afya ilitazame kwa jicho la tatu suala hili.

Mwisho kabisa,nimeandika makala hii sio kwa lengo la kuwabeza wahudumu au hospitali zetu bali kuonesha maeneo yenye changamoto ili yaweze kufanyiwa maboresho kupitia yale niliyoyashuhudia mwenyewe kupitia tukio lile, ni dhahiri kuwa wahudumu wetu wa afya wamekuwa kiungo muhimu katika ustawi wa afya zetu na bila wao safari ya kufika mbinguni ingekuwa fupi sana kama kutoka tandika hadi buza.

Wasalaam,hadi wakati mwingine.
 
Jambo ulilozungumzia ni la muhimu Sana maana dharura humpata yeyote mahalo po pote tukilinyamazia ipo siku utajikuta linakusibu ukawa umechelewa.Nilishuhudia mgonjwa asiyeweza hata kutembea na zaidi ni mzee na anapumu anapumua kwa tabu ndugu walomleta wanachukua wheel chair waloikuta mbovu, wanaomba wasaidiwe hakuna mhudumu anayejali mpaka wagonjwa walokuwa wanasubiri huduma wakainuka kwenda kusaidia.Yaan niliishiwa na usemi.
 
Wahudumu walio wengi hawaijui TRIAGE na management ya vituo havijaipa kipaupembele
 
Back
Top Bottom