Tukio la kifo cha Sheikh Abeid Karume hatua kwa hatua

Mkuu hiyo ilikua ni 1972, usilinganishe na mazingira ya sasa
Hata ingekua mwaka 1800 huwezi kuinga kwa kiongozi wa nchi hata kama ni ndugu yako ukawa na silaha za kivita... Ulinzi haujaanza leo tangu enzi za machifu huko ulikuepo
 
hata ingekua mwaka 1800 huwezi kuinga kwa kiongozi wa nchi hata kama ni ndugu yako ukawa na silaha za kivita... Ulinzi haujaanza leo tangu enzi za machifu huko ulikuepo

Mkuu masuala ya kidunia kila siku yanaboreka, usifikirie mambo ya miaka 40 nyuma yalikua ni sawa na mazingira ya sasa.
 
Dubai, UAE
Simulizi za mhanga wa mapinduzi Mzee Aman Thani toka



Jaha Ubwa alipokua gerezani Zanzibar watu wa Makunduchi wakamkejeli; "Tulipotaka kusali Ijumaa ukatukataza na ukasema dhambi zenu leo nitazichkua mimi." Jaha Ubwa alilia machozi.


Mzee Aman aliyepata kupelekwa gerezani akiwa na wenzie wengi kina Mdungi Ussi, Jimmy Ringo, Jaha Ubwa , Mzee Mbaba, Alhalifa Misry...Hashim Bahruan , Saleh Master ..
Source : MzeeBarwani


Makala maalum ya kurasa 76 ya shajara (diary) ya Mzee Aman Thani Fairooz:

UKWELI NI HUU (KUUSUTA UWONGO) Nimelichagua jina hili la UKWELI NI HUU KUUSUTA UWONGO, baada ya kuyasikia na kuyasoma me ngi ya uwongo na hata yakafika kusomeshwa watoto wetu katika maskuli ya Zanzibar kukhusu hayo yenye kuitwa "MAPINDUZI" yaliyofanyika katika visiwa vyetu vya Zanzibar mnamo taarikh 12 Januari 1964. Kabla ya kuingia katika hayo, ningependa ku waambia wasomaji wangu wote kuwa mimi si mjuzi hata kidogo wa fani hii ya uandishi; tena ni mbovu sana katika "spellings" na ka tika "nahau" za Kiswahili cha kisasa.

Pia nawaomba radhi kwa Kiswahili changu cha kizamani. Bali, kutokana na huo uzushi na kupotezwa kwa makusudi ukweli wa hayo yaliofanyika kukhusu hayo yenye kuitwa "mapinduzi" nimeona sina budi illa ni kujitolea hivyo hivyo juu ya upungufu wangu katika fani hii ya uandishi. Lakini ukweli lazima niudhihirishe ili vichipukizi vyetu viweze kuyaelewa vilivyo yaliyotendeka katika nchi yao.

Kwani wengi walikuwa wadogo na wengine walikuwa hata hawajazaliwa katika wakati huo. Ilivyokuwa Kiswahili ni lugha yangu ya kuzaliwa, basi ninaiandika kama ninavyoisema. Si shughuliki na "kua au kuwa, aliniambia au aliniambiya, ameuawa au ameuwawa kenda au kaenda, amekwenda au ameenda". Hayo kwa wataalamu wa lugha ni mambo muhimu lakini kwa mimi nakutakeni msamaha juu ya hayo.

Muhimu ya kuyaangaliya na kuyazingatiya ni yale nikusudiayo kuyaeleza, kwani hayo ndio muhimu na ndio ya kweli tupu isiyokuwa na dosari hata chembe. La mwanzo nitakalo kuombeni mlifahamu uzuri ni ile hakika kuwa hayo yaliyofanyika katika visiwa vyetu taarikh 12 Januari 1964, hayakuwa "MAPINDUZI" wala hayafai hata kidogo kuitwa 'mapinduzi' kwa maana asili ya neno. Bali kwa maana zote yalikuwa khasa ni "MAVAMIZI", yaani kwa Kiingereza "INVASION".


Mapinduzi lazima yapangwe, yaongozwe na yatekelezwe na wananchi wenyewe kwa maslaha ya nchi na wananchi wake. Sasa tukiangalia hayo yaliotendeka Zanzibar, yalipangwa, yaliongozwa na yalitekelezwa na WAGENI kutoka nchi za nje za jirani zetu. (Ni wao wala si wananchi ndio waliochukua ngawira kubwa kubwa).

Haya yanathibitika zaidi kwa vile kuwa huyo jamadari aliyeyaongoza hayo 'mavamizi' ni John Okello na wa chini yake walikuwa Injini na Mfaranyaki. Nani kati ya hao aliyekuwa kitovu chake kimezikwa visiwani? Okello amezaliwa na amekulia kwao Uganda, Injini amezaliwa na amekuliya kwao Kenya na Mfaranyaki amezaliwa na amekuliya kwao Tanganyika. Wote hao walikuja Zanzibar wakiwa watu wazima na shughuli zao, wamekuja kutafuta kibarua na kukimbia kodi za kichwa katika nchi zao. Liangalie hilo waliloliita "Baraza la Mapinduzi".


Utaona sehemu kubwa ya wanachama wa Baraza hilo la Mapinduzi na wajumbe wao waanzilishi walikuwa si Wazanzibari, laa kwa kuzaliwa wala kwa kuchukua Tajnisi (Kuandikisha Uraia). John Okello, Khamis Darweshi, Seif Bakari, Said Natepe, Said Washoto, Muhammed Mfaume, Edington Kisasi, Mohammed Abdalla Kaujore.

Ukiwaacha wengineo ambao nao vile vile walikuwa si wananchi wa Zanzibar kwa kuzaliwa, bali wao walikuja Zanzibar wakiwa katika migongo ya wazee wao na waliendelea kuishi humo visiwani kwa maisha yao yote. Na wakachukuliwa kama ni Wazanzibari. UTUKUFU NA NEEMA YA ZANZIBAR Mwenyezi Mungu amevipa visiwa hivi viwili yaani Unguja na Pemba bahati ya utukufu kwa kila jambo lake......


Katika nchi za jirani zetu, Tanganyika, Kenya na Uganda kote huko kulikuwepo na ubaguzi uliyokuwa ukiongozwa na serikali za nchi hizo. Malipo ya mishahara ya wafanyakazi yalikuwa yakilipwa kutokana na makabila yao wala si kutokana na ujuzi wao wa kazi. Kulikuwepo "African Scale, Asian Scale na European Scale".


Madaktari, Mainjinia, Waalimu na wowote nawawe wana elimu na ujuzi na maarifa ya namna moja, yaani wote sawa sawa kwa elimu na ujuzi wa kazi zao, lakini mishahara yao ilikuwa tafauti kutokana na makabila yao. Waafrika ndio wenye kulipwa malipo ya chini kabisa kuliko wote. Wazungu walikuwa ndio wenye kulipwa mishahara minono (hata baadhi yao walikuwa hawana elimu yoyote isipokuwa huwo Uzungu wao), waliowafuatia ni Waasia.


Vyoo vya njiani (Public Toilets) na sehemu za kungojelea usafiri wa reli navyo vile vile vilikuwa vikitumika kwa ubaguzi wa kikabila. Waafrika waliekewa vyoo vyao na sehemu zao za kungojelea usafiri. Wazungu walikuwa na sehemu zao na Waasia walikuwa na sehemu zao, wote mbali mbali. Lilikuwa ni kosa na kuvunja sheria ikiwa imetokea kwa yoyote kuingia katika sehemu isiyo kuwa amekhusika nayo. Khasa Muafrika awe ameingia au amekaa katika sehemu za Waasia au za Wazungu.

Katika Tanganyika, Kenya na Uganda kote huko kulikuwa na Kodi ya Kichwa. Kodi hiyo ilikuwa ikilipwa na kila mtu aliyekwishafika balegh katika umri wake. Nayo pia ikitekelezwa kwa njia za ubaguzi wa kikabila. Waasia na Wazungu, wao hata ikiwa wamechelewa kulipa kodi zao, basi walikuwa hawakamatwi majiani wala hawaendewi majumbani mwao kukamatwa.


Lakini, Waafrika walikuwa wakisakwa majiani na wakiendewa majumbani mwao mnamo pinga pinga za usiku. Na wakikamatwa, basi walikuwa wakifungwa kamba za viunoni au hufungwa ncha ya shati la huyu na la huyu kisha walikuwa wakiongozwa mmoja nyuma ya mmoja na huku wakipigwa mateke na kusukumwa mpaka wakifikishwa Bomani.....


Kutokana na hali kama hizo, ndipo wengi kati ya wananchi wa nchi hizo, khasa kutoka Tanganyika walikimbia kutoka makwao na kuhamia Zanzibar kwa sababu ya kufuata hali njema za kimaisha. Zanzibar hakukuwepo kodi za kichwa wala ubaguzi wa vyooni wala malipo ya mishahara wala wa namna yo yote. Ilikuwa njema atakae naaje. UBAGUZI UMEANZISHWA ZANZIBAR WAKATI WA SERIKALI YENYE KUJIITA YA "MAPINDUZI" Mara tu baada ya kufika hiyo serikali ya 'mavamizi' katika Zanzibar ubaguzi wa ukabila ulianzishwa.


Kila "mrangi rangi" kama walivyokuwa wakiwaita wenyewe, yaani wenye asili za Kiarabu, za Kihindi na za Kingazija walianza kutolewa makazini bila ya kupewa hata haki zao za ufanyaji wa kazi. Mashamba, majumba na hata mabiashara yao yalichukuliwa kwa nguvu na kupewa wageni ikiwa ni tunzo la ukatili na maovu waliyowafanyia wananchi katika nchi yao.

Serikali ya 'mavamizi' ya Zanzibar ilitangaza rasmi kupitia vyombo vya khabari vya serikali kukhusu ubaguzi katika Taalimu. Waafrika, wakipasi au wasipasi bali idadi yao ya kuingia katika "Form One" ya "secondary school" ilikuwa ni 77 katika mia (77%), Waarabu 16 katika asili mia (16%), Wahindi 6 katika mia (6%), na Wangazija MMOJA katika mia! (1%).

Si hayo tu, bali serikali ya 'mavamizi' imetumia fedha za umma kwa ajili ya kujijengea hospitali yao wao tu Wanachama wa Baraza la Mapinduzi na familia zao na wameita, "Mapinduzi Wing". Vitanda, mabetishiti, foronya za mito, vyombo vya kulia kama sahani, vikombe, visu na nyuma (forks) vyote viliagiziwa kutoka Ulaya.

Ilikuwa ikitokea Mheshimiwa kulazwa huko, basi na mkewe alikuwa akihamia huko huko na kulala kitanda kimoja kama kwamba wamo katika siku za fungati! Haya yakitendeka wakati wananchi wanyonge hawana hata dawa mahospitalini! Huo ulikuwa ndio usawa, sio ubaguzi!


ELIMU NA MATIBABU BURE! Tunaambiwa na serikali yenye kujiita ya 'mapinduzi' kuwa elimu na matibabu yameanza kuwa bure kwa wananchi baada ya kupatikana kwa Serikali ya 'mapinduzi'!

Huu ni uwongo uliokuwa hauna hata kifuniko. Toka lini elimu na matibabu yalikuwa kwa malipo katika Zanzibar? Tangu kuanzishwa kwa skuli ya serikali na Sayyid Ali bin Hamoud na toka kuanzishwa kwa matibabu katika mahospitali, kamwe hayajapata kuwa ya malipo. Toka kwa kuangaliwa na madaktari mpaka kwa madawa, chakula, na mpaka kulala kwa kutibiwa katika mahospitali kulikuwa bure.


TAALIMU Wananchi na wageni, kuanzia chumba cha kwanza yaani (standard one) mpaka kufikia chumba cha nane (standard eight), masomo yalikuwa bure kwa wote. Sio hivyo tu, kila mwanafunzi alikuwa na deski lake peke yake la kukalia na kila mwanafunzi alikuwa akipewa madaftari ya kuandikia bure, vitabu vya 6 kusomea bure, kalamu za kuandikia bure, vidawa vya wino na wino wake bure hata blotting papers (la kukaushia wino) pia wakipewa bure. Na kila Ijumaa wanafunzi walikuwa wakipewa sabuni za kufulia bure. Skuli za mashamba, wanafunzi walikuwa wakipewa kifungua kinywa kunde na uji kabla ya kuingia katika vyumba vya masomo, bure.


Kuanzia chumba cha tisa mpaka cha 12, na baada ya muda katika miaka ya 1950 kuanzia chumba cha saba mpaka cha 12, wazee walitakiwa wasaidie kitu kidogo katika masomo ya watoto wao. Malipo hayo yalikuwa ya kitu kidogo sana na si kila mzee alikuwa akilipa ada hizo. Wengi sana katika wazee walikuwa hawalipi hata senti moja. Na hao waliokuwa wakilipa, wengi wao walikuwa wakilipa kuanzia Shs. tano mpaka Shs. 20 kwa wingi kila baada ya miezi mitatu au mine. Kabla ya mzee kuwa alipe au asilipe, kulikuwepo taratibu maalumu zilizokuwa zikifanywa. Mzee wa mtoto alikuwa akipelekewa "questionnaire" (karatasi) yenye masuala yaliyokhusu mapato yake, kazi yake na idadi ya watu wake wa nyumbani. Kwa kutaka kuhakikisha uwezo wa mzee huyo, basi akipelekewa waraka huo kwanza Sheha wa mtaa kuhakikisha yale yalioandikwa na akisha Sheha humpelekea Mudiri wake na Mudiri humpelekea D.C. wake. Baada ya khatuwa hizi ndio tena hapo hutolewa uamuzi wa kulipa au wa kutokulipa, na kama kulipa alipe kiwango gani. Kutokana na mipango kama hiyo, zaidi ya 70 katika mia (70%) ya wazee watoto wao walikuwa wakisoma bila ya kulipiwa kitu chochote na kiasi cha 20 katika mia (20%) walikuwa wakilipiwa kitu kidogo na kiasi cha 10 katika mia (10%) ndio waliyokuwa wakilipiwa idadi kamili ambayo ilikuwa chini ya Shillingi 200, kwa mwaka mzima. Wengi waliokuwa wakilipa kima hicho, walikuwa ni wazee wenye asili za Kihindi. Wanaoitwa Waafrika na wanaoitwa Waarabu hayo yalikuwa si maji yao.....


Aliyekuwa Mfalme wa nchi, Seyyid Abdulla Bin Khalifa Bin Haroub, alipopata maradhi, alilala katika hospitali hiyo hiyo na alifanyiwa operesheni katika hospitali hiyo hiyo wanayotibiwa watu wa kawaida. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sehemu yao ya kutibiwa waliita "European Wing".

Kutokana na makelele ya wananchi, khasa kutokana na makala yaliyokuwa yakiandikwa katika gazeti la wananchi la "Mwongozi", sehemu hiyo ilibadilishwa jina na badala ya kuitwa "European Wing", ikaitwa "West Wing". Kutokea wakati huo ilikuwa wazi kwa yoyote mwenye kupenda kwenda katika sehemu hiyo ikiwa yutayari kulipa ada zilizowekwa.


Leo baada ya mapinduzi ya kuleta usawa na kuondoa usultani na ubwanyenye, mheshimiwa akiumwa na mdudu upande basi mbio anachukua ndege anakwenda zake Uingereza au Ujarumani kwa matibabu. Ikiwa matibabu yapo nchini bure, mbona wao wanayakimbia na kuyafuatia ya malipo, tena katika nchi za n'gambu na kwa kutumia pesa za wanyonge kwa matibabu yao? Sasa ipi inayostahiki kuitwa serikali ya kibwanyenye? Hii ya waheshimiwa waliyojitenga mbali na umma au ile ya waliyokuwa wakiishi pamoja na umma? Mwenye macho haambiwi tizama! Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu baadhi ya siku, lakini huwezi kuwadanganya watu wote siku zote...


NEEMA ZILIKUWEPO Katika huo wakati unaoitwa wa kikoloni, Serikali ya Zanzibar ilikuwa ikiendesha mambo yake yote kama kujenga maskuli, mahospitali, mabarabara, kununua meli za usafiri, pamoja na kuyahudumia na kulipa mishahara ya wafanyakazi tokea wa kigeni mpaka wananchi. Na hao wafanyakazi wa kigeni ambao wengi wao walikuwa Wazungu, basi juu ya mishahara yao walikuwa wakipewa posho maalumu (Inducement Allowances), pia walikuwa wakilipiwa nauli za kuwaleta na kuwarejesha na za wakati wa likizo zao. Yote hayo na mengineyo yakifanywa kutokana na mapato ya ushuru tu wa forodha. Serikali hii yenye kujiita ya "Mapinduzi", ni wao peke yao ndio wenye kununua bidhaa muhimu zote za nchi kama vile, karafuu, mbata na pilipili hoho kutoka kwa wananchi kwa bei wazitakazo wao wenyewe na wakaziuza kwa bei ziliopo katika masoko ya ulimwengu. Isitoshe, serikali hii haina gharama za kuwalipa hao Wazungu kama ilivyokuwa hapo zamani, sasa ilikuwaje hata ifike serikali kuwa haina fedha hata za kuwalipa mishahara wafanyakazi wake wa kienyeji?

Hapana shaka sababu kubwa ya hayo ni hii dhulma iendeleayo hadi hii leo, uwendeshaji mpotofu, ukiongozwa na siasa ya husda na uroho wa madaraka na kipato, siasa ya "Chukuwa Chako Mapema"! (CCM). Siasa ambayo immefanya mwananchi kuwa hana uwezo wala itibari yoyote katika nchi yake. Kwa hali za kimaisha nchini mwananchi hawezi kukaa akatua na kufikiri na kupanga juu ya maendeleo ya nchi yake, yeye anafikiri juu ya cha jiyo tu! Siasa mbovu hii iliopangwa makusudi imemzuiliya na kumnyima mwananchi uwezo na njia za kujiendeleza, laa si katika kimaisha, walaa si katika kiutamaduni au kielimu....


"Mwenye Elimu ni Aduwi" KUANZA HARAKATI ZA SIASA Kabla ya Serikali ya Kiingereza kuiingiza Zanzibar chini ya Himaya yake, Zanzibar ilikuwa ni Dola kamili iliyokuwa ina shughuli zake (ikiamiliana) na ulimwengu wote.


Mara tu Muingereza alipoitia Zanzibar katika makucha yake mnano mwaka 1890, kila jambo kubwa na dogo lilikuwa lazima liamuliwe kutoka Uingereza. Mfalme wa nchi alifanywa kuwa ni alama tu ya Dola, hakuwa na uwezo katika kukata shauri juu ya uwendeshaji wa nchi.

Kama ilivyo kawaida ya wakoloni popote ulimwenguni wanapotawala, lazima watumie mbinu za kuwagawa wananchi (ili waendeleze utawala wao) kutokana na hali za namna fulani ziliopo katika nchi. Ikiwa kwa njia za kidini, ukabila, urangi, utajiri, uwezo wa kimaisha na hata umadhehebu.

Katika Zanzibar Muingereza alitumia njia za kuwagawa wananchi kwa kutumia asili za makabila yao. Aliwafanya wenye asili za Kiarabu wajione kuwa wao tu ndio wenye haki za utawala kwa vile ilivyokuwa Mfalme wa nchi anatokana na asili zao.


Aliwafanya Washirazi yaani, Wahadimu, Watumbatu na Wapemba wajione kuwa wao tu ndio wenye kila haki za nchi kwa vile ilivyokuwa wao ndio waliyokwenda kuwaita Waarabu (kutoka kwao Oman) kuja kuwasaidia kumuondoa Mreno.


Aliwafanya Waafrika (weusi) wajione kuwa wao tu ndio wenye kusitahiki utawala wa Zanzibar kwa vile Zanzibar imo katika Bara la Afrika. Na alichukua uchumi wote wa nchi na kuuweka katika mikono ya wenye asili za Kihindi kuwa wao ndio raia wa Kiingereza sahihi wa tangu asli, kwa uwezo wao wa kimaisha wakajiona kuwa wao ni wabora kuliko wengine katika nchi.


Kutokana na hali kama hizo, wananchi walianza kujigawa mafungu kwa mafungu na walianza kufungua Jumuiya zao za Kikabila. Waarabu walifungua yao, Washirazi walifungua yao, Waafrika walifungua yao na Wahindi walifungua yao na Wangazija wakafungua yao. Na ndani ya hizo hizo, zilijitokeza zengine na kila moja ilikuwa ikijitapa kwa upande wake.


Kwa muda mkubwa jumuiya hizo zilikuwepo katika nchi na hazikuweza kupata wala kufanya lolote kwa maslahi ya nchi. Kubwa walilokuwa wakilipata ni kualikwa chai ya alaasiri kwenye Bustani ya Jumba la Balozi wa Kiingereza, na kualikwa katika siku ya kuzaliwa Mfalme wa Kiingereza na Mfalme wa nchi na kualikwa kutembelea manuwari za Kiingereza zinapofanya ziara kuitembelea Zanzibar...


1920 Muingereza katika njama zake za kuzidi kuwafarikisha wananchi ili aendelee kuwatumia katika kuendeleza utawala wake, alianzisha kuwateuwa (appoint) wananchi kwa kuwatia katika Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) kwa njia za kikabila. Aliwateua hatimaye Waarabu wane, Waafrika wane, Wahindi watatu na Mzungu mmoja. Na upande wa Serikali walikuwemo wakurugenzi wa idara wa Kiingereza kutoka idara mbali mbali za serikali walioteuliwa vile vile, hao walizidi kwa wingi katika baraza hilo kuliko raia.


Mwendo huo uliendelezwa kwa muda wa miaka 28 na hapakuweza kupatikana lolote la maslaha ya nchi. Miaka nenda miaka rudi, nchi haikuwa na maendeleo yoyote kukhusu mabadiliko ya Katiba itayo wawezesha wananchi kuendesha wenyewe shughuli za nchi yao bila ya kuingiliwa na yoyote.


Katika mwaka 1953 na 1954, Jumuiya ya Waarabu (Arab Association) iliamua kumpelekea Balozi wa Kiingereza madai ya kutaka yaletwe mabadiliko ya Katiba yatayo wawezesha wananchi wa Zanzibar kuchagua wajumbe wao wa kuwapeleka katika Baraza la Kutunga Sheria kwa njia ya uchaguzi wa Kura Moja Kwa Mtu Mmoja (One Man One Vote).


Na miongoni mwa madai yao, walidai uondolewe mtindo wa kuwateua wananchi kwa njia za kikabila katika kila jambo la nchi. Pia walitaka baada ya kupatikana kwa matokeo ya uchaguzi huo, paanzishwe mazungumzo ya taratibu za kupatikana kwa Uhuru kamili wa Zanzibar.

Balozi wa Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar wakati huo akiitwa Mr. Renkin. Balozi huyo alikataa hata kuyatia maanani madai hayo.


Jumuiya ya Waarabu walipoona hawakuweza kupata natija yoyote katika madai yao, bali hata hayakuzingatiwa, waliamua kuanzisha mgomo kwa kuwazuia wajumbe wao kushiriki katika vikao vya Baraza la Kutunga Sheria na katika vikao vya Kamati za Mabaraza yote waliyoteuliwa kushiriki. Mgomo huo ulichukua muda wa miezi 18 bara bara.


Jambo la kulizingatia katika suala hili ni kuwa, madai hayo kutokana na Jumuiya ya Waarabu hawakuyafanya kwa maslahi yao binafsi zao, bali kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari wote bila ya kujali asili za makabila yao. Haya yanajithibisha zaidi kwa vile ukiangaliya idadi ya hao waliyokuwa wakiitwa (au wanaoitwa) Waarabu katika Zanzibar, walikuwa ni kiasi cha 16 katika 100 (16%). Juu ya hivyo waliamua kuziachilia mbali nyadhifa walizopewa, sio hivyo tu, bali kutoa muhanga nafsi zao wakiweka mbele maslahi ya nchi.


Bahati mbaya hawakupata kuungwa mkono na wananchi wenziwao wenye asili za makabila mengine juu yakuwa walizungumza nao na waliwataka washirikiane katika madai hayo. Mmoja kati yao (alioteuliwa kushiriki katika Baraza la Kutunga Sheria akiwa ni mwenye asili ya Kiarabu), alipinga uamuzi wa Jumuiya yake na alihudhuria katika kikao cha Baraza la Kutunga Sheria wakati wenzake walipokuwa wamesha amua kugomea. Matokeo yake, alitokea mwananchi mwenye uchungu na nchi yake na kumpiga bwana huyu kwa visu. Kwa bahati mbaya alikufa kutokana na pigo hilo....


SHEIKH ALI MUHSIN KWENDA NCHI ZA ULAYA IKIWEMO NA UINGEREZA KUPIGANIA UCHAGUZI WA "COMMON ROLL" (MTU MMOJA KURA MOJA). Wakati Jumuiya ya Waarabu ilipokuwa katika hekaheka za mgomo wao wa kuto kushiriki katika Mabaraza yote ya Serikali kwa madai ya kutaka papatikane mabadiliko ya Katiba yatayo wawezesha wananchi kuchagua wawakilishi wao wa Baraza la Kutunga Sheria kwa njia ya uchaguzi wa "One Man One Vote" na kusita kuteuliwa kutokana na asili ya makabila yao, mwananchi mwenzao mwenye uchungu wa nchi yake alifunga safari (kwa gharama zake mwenyewe) kwenda kupigania maslahi ya nchi yake, akiendeleza madai ya wananchi wenziwe huko nyumbani.


Wakati Sheikh Ali Muhsin alipokuwa katika hekaheka hizo huko Uingereza, alikutana na Seyyid AbdulRahman Mohammed (Babu) na waliweza kushirikiana katika juhudi hizo. Katika harakati hizo Sheikh Ali alikutana na waongozi mbali mbali wa kisiasa na wengi wao walimshajiisha juu ya kuendelea na juhudi za ugombozi wa nchi yake na walimpa kila msaada (moral support).

Huko Uingereza alipata kuzungumza na wakuu wa Serikali ya Kiingereza, wakuu wa upande wa Upinzani na wakuu wa Vyama vya Wafanyakazi. Pia alikutana na wakuu wa vyama na jumuiya mbali mbali zenye kupigania kuondoka kwa ukoloni katika Afrika na katika sehemu zengine za ulimwengu...


KUASISIWA HIZBULWATTAN (ZANZIBAR NATIONALIST PARTY) Wakati Sheikh Ali Muhsin akiwemo katika safari zake huko nchi za Ulaya, huko nyumbani walichomoza wananchi wengine waliokuwa nao na ghera na mapenzi ya nchi yao. (wote, isipokuwa mmoja tu kati 11
yao Sheikh Abdalla Mahmoud walikuwa si Waarabu) Wananchi hao walikutana kuzingatia na kutafakari juu ya kupotea kwa nchi yao kutokana na mbinu za mkoloni za kuwagawa wananchi kwa kutumia asili za makabila yao.


Wananchi hao waliibuka na amuo la kuanzisha Umoja wa Wananchi wa Unguja na Pemba. Umoja ambao kila raia wa Zanzibar atastahiki kuwemo bila ya kujali asili ya kabila yake wala Imani ya Dini yake, la umuhimu ni URAIA wake. Hichi kilikuwa ndio chama cha kwanza na pekee katika nchi kuasisiwa kwa kufuatia misingi ya Uwananchi.


Wananchi waasisi hao walikuwa ni, Sheikh Vuai Kiteweo, Sheikh Miraj Shaalab, Maalim Zaid Mbarouk, Maalim Maksud Fikirini, Maalim Mwandoa Khamis, Maalim Wazir Ali bin Maalim, Sheikh Haji Hussain Ahmed, Sheikh Othman Soud, Sheikh Abdulla Mahmoud Kombo (wa Makunduchi), Sheikh Ramadhan Tosir (Ramadhan Madafu), Maalim Hija (wa Ndijani), Sheikh Ame, Sheikh Abdulla Mali, Sheikh Haji Kombo (wa Kiboje), Sheikh Abdalla Mahmoud na wenziwe wachache. Kwahivyo wale wenye kusema na kutangaza kuwa Hizbu (ZNP) iliasisiwa na Waarabu au kilikuwa chama cha Waarabu, hapana shaka wanakosea, amma kwa kutokujuwa ukweli ulivyo au wanasema hivyo kwa makusudio ya kutafuta maslaha yao.


Ukweli na hakika ilivyo ni kuwa Hizbu haikuasisiwa na Waarabu wala hakijapata kuwa Chama cha Waarabu. Na kama Hizbu kingelikuwa ni Chama cha Waarabu, basi kisingeweza kupata ushindi katika chaguzi zilizofanyika za (One Man One Vote) kwani idadi ya hao wenyekuitwa Waarabu nchini ilikuwa ndogo; kwahivyo idadi yao hiyo haingaliwezesha kukipa (hicho kisemwacho ni chama chao) voti za ushindi. Madai hayo ni miongoni mwa maneno na mbinu za kufitinisha na kuwagawa wananchi kwa kuuwogopa umoja wao. Hapana shaka zimetungwa na wakoloni na kuimbwa na vibaraka vyao, kwa maslahi yao. Mabwana hao tuliowataja hapo juu wakiwa ndio waasisi wa Chama cha HizbulWattan, wao ndio waliyomuendea Sheikh Ali Muhsin nyumbani kwake baada ya kurejea kutoka safarini na kumueleza kukhusu kuasisi kwa chama chao na nini dhamiri zilizo wapelekea kuasisi chama hicho. Baada ya kumueleza, walimtaka na yeye awaunge mkono kwa kujiunga katika chama.


Sheikh Ali Muhsin alipoona kuwa hayo wayatakayo wananchi wenzake ndio hayo hayo ayatakayo na kuyapigia mbio daima basi, hapo hapo aliamua kujiunga na kushirikiana nao. Baada yakujiunga, waasisi hao walimtaka Sheikh Ali Muhsin aanze kuzungumza na nduguze wenye asili za Kiarabu bali na kila anaefahamiana nae ili wajiunge na wananchi wenziwao. Sheikh Ali aliupokea na kuanza kuutekeleza ujumbe huo.


Miongoni mwa wa mwanzo (kati ya hao wenye kuitwa Waarabu) kujiunga na Umoja huo ni, Sheikh Badr Muhammed Barwani, Sheikh Ahmed Seif Kharusi, Sheikh Amour Zahor Ismaily, Sheikh Ali Ahmed Riyamy Sheikh Nassor bin Isa Ismaily na Sheikh Ahmed Khalfan Naamani haikuchukuwa muda ila nao walijiunga....

MAKAO MAKUU YA HIZBU Kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa "Common Roll Election, yaani, "Mtu Mmoja Kura Moja", katika Zanzibar mnamo mwaka 1957, mwananchi, mzalendo Sheikh Mahmoud wa Mtendeni aliyekuwa mwishoni akijishughulisha na utengezaji wa saa, alijitolea kwa kukipa Chama jumba lake la ghorofa moja lililokuwepo mtaa wa Mwembetanga kuwa ni Makao Makuu ya Chama. Alilitoa jumba hilo bila ya kupokea kodi hata senti moja.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwanzo wa 1957, Hizbu iliyaondoa Makao Makuu yake kutoka Mwembetanga na kuhamia Mkunazini karibu na Msikiti Gofu. Baada ya kuwepo hapo kwa muda, ndio iliweza kununua jumba lake wenyewe katika mtaa wa Darajani na kulifanya ndio Makao Makuu ya Chama. Jumba hilo, baada ya 'Mavamizi' ya Januari 12, 1964, liliporwa na Serikali ya 'Mavamizi' na kufanywa Makao Makuu ya AfroShirazi Youth League.....


HIZBU KUMLETA ZANZIBAR SEYYID ABDULRAHMAN (BABU) Miezi michache kabla ya uchaguzi wa mwanzo wa 1957, Chama cha HizbulWattan kilimleta Babu Zanzibar ili ashirikiane na wananchi wenziwe katika harakati za kisiasa. Baada ya kufika Zanzibar, Hizbu ilimteuwa kuwa Katibu Mtendaji wa Chama (Excutive Secretary). Kutokana na maarifa aliyokuwa nayo katika mipango ya kuendesha chama cha kisiasa, Babu baada ya muda mdogo alianzisha Umoja wa Vijana (Youth Own Union) (YOU). Kwa msaada na ushirikiano wa waongozi wenziwe na wananchi Babu alifanya kazi kubwa katika kukijenga Chama cha Hizbu ndani na nje ya nchi.

Lakini, kwa bahati mbaya, kama alivyokuwa hodari katika kukijenga, ndivyo alivyojaribu kwa uhodari au ilivyo khasa kwa kiujanja kutaka kukibomoa baada ya kushindwa kufikilia maslahi yake binafsi kwa kukitumilia chama. (Baadae tutaeleza aliyoyatenda katika kukibomoa chama na kuifisidi nchi). Alipojiunga Sheikh Ali Muhsin katika chama cha HizbulWattan Zanzibar Nationalist Party (ZNP) aliwapa shauri wakuu wa Chama kumtaka Babu achukue mafunzo katika kuendesha chama na baadae aje asaidie katika uendeshaji wa ZNP. Wakuu wakapendezewa na shauri hiyo, na Babu akawafik. Sheikh Ali hapo tena aliiomba Labour Party ya huko Uingereza kwa kupitia kwa (wasta wa) Mr. John Hatch na Mrs. Eirene White M.P. na Labour Party ikakubali kumpokea Babu kwa mafunzo. Mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi sita. ZNP (Hizbu) ililipia gharama zote za kimaisha kwa muda huo na za safari. Katika muda huo pia aliendelea kulipwa mshahara akiwa ni Executive Secretary wa Chama ZNP. Utaona dhahiri kuwa imani ya Hizbu juu ya elimu na maarifa haikufungika sehemu mmoja tu, bali ilikuwa ni kwa kila upande.


Hizbu iliamini kuwa uwongozi mwema wa chama na nchi utapatikana kutokana na watu wenye ujuzi na maarifa, kwa hivyo iliona umuhimu wa kumpatia mafunzo na elimu ifaayo Katibu Mtendaji wake khasa, na wengine wafuatie...


NATIJA YA SAFARI YA SHEIKH ALI MUHSIN Kama tulivyoeleza hapo mwanzoni kuwa Sheikh Ali Muhsin alizitembelea baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na Uingereza kwa ajili ya kugombania kupatikana kwa mabadiliko ya Katiba ya Kuanzishwa kwa uchaguzi wa "Common Roll" yaani "One Man One Vote" katika Zanzibar.

Natija ya safari hiyo, Serikali ya Kiingereza, ilimleta Zanzibar Mr. Coutts akiwa ni mchunguzi juu ya maendeleo ya Katiba. Mchunguzi huyo alifika Zanzibar kati ya mwaka wa 1956. Chama cha Hizbu kilifanya maandamano makubwa kwa kumpokea Mr. Coutts hapo kiwanja cha Ndege cha Kiembe Samaki siku aliyofika Zanzibar.


Waandamanaji walichukuwa mabango yaliyokuwa yameandikwa: "TUNATAKA UCHAGUZI WA ONE MAN ONE VOTE" "TUNATAKA UHURU WA NCHI YETU" "TUMECHOKA KUTAWALIWA'' ''TUNAPINGA "UBAGUZI WA RANGI NA WA UKABILA" Mjumbe huyo alipokuwa nchini alikutana na wananchi pamoja na wakaazi mbali mbali wa nchini. Alionana hata na watu binafsi. Na alipokea risala (za maandishi na za mdomo) kutoka vyama mbali mbali vya kikabila na vya kidini.


Chama cha Hizbu nao walionana na mjumbe huyo na walimkabidhi risala yao yenye kutilia nguvu matakwa yao, matakwa ambayo ndio msingi wa ujumbe wake wa kuja Zanzibar. Inafaa ifahamike kuwa tangu kufika kwa mchunguzi huyo na mpaka kuondoka hapakuwepo chama cha kisiasa nchini isipokuwa kimoja tu HizbulWattan. Vyama vyote vya kisiasa vyengine viliasisiwa baadae.


Kwahivyo HizbulWattan ndicho chama cha mwanzo cha kisiasa kuasisiwa Zanzibar. Mr. Coutts alipomaliza shughuli zake alirejea kwao. Baada ya muda alileta mapendekezo ya uchunguzi wake kwa Balozi wa Serikali ya Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar. Katika mapendekezo yake hayo, Mr. Coutts alikubali kuwa Zanzibar inafaa kuanzishwa uchaguzi wa "Common Roll" yaani uchaguzi wa kwa pamoja, bila ya kujali khitilafu za kabila. Lakini alipendekeza kuwa uchaguzi uanzie kwa viti sita na vilivyobakia viendelee katika mpango ule ule wa kuteuliwa na Balozi wa Serikali ya Kiingereza kwa kushauriana na Mfalme wa nchi. Pia katika mapendekezo yake, Bwana Coutts alitaka Balozi wa
Kiingereza aendelee kuwa Mwenye Kiti wa Baraza la Kutunga Sheria na watumishi wa Serikali ya Kiingereza waendelee kuwa waongozi wa upande wa Serikali.


Hizbu haikuridhika hata kidogo na mapendekezo hayo, kwa vile asli ya madaai yao ni kuwa Wawakilishi wote wa Baraza la Kutunga Sheria wawe ni wananchi waliyo chaguliwa na wananchi kwa uchaguzi wa "One Man One Vote". Juu ya hivyo, Hizbu ilikubali kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuona kuwa msingi wa matakwa yao ulipatikana; nao ni kuanzishwa kwa uchaguzi wa "Common Roll". Kwa kukubaliwa misingi hii Zanzibar ikawa ndiyo nchi ya mwanzo katika Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na ya Kusini kuanzishwa uchguzi kama huo. Baada ya kupatikana haya HizbulWattan ilizidisha juhudi za kuwafahamisha wananchi misingi na faida ya kuchaguwa Wawakilishi wao kwa kupitia uchaguzi huo...


WAKOLONI NA NYERERE NDIO WAASISI WA AFROSHIRAZI Wakuu wa Serikali wa Idara ya Utawala, Zanzibar baada ya kuona kuwa mpaka kuondoka kwa mchunguzi Coutts Zanzibar na mpaka kuleta mapendekezo ya uchunguzi wake, hapakuweza kuasisiwa chama chengine cha kisiasa nchni ili kipate kushindana na HizbulWattan (ZNP), waliamua kumtumilia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wakoloni walimtumilia Mwalimu kwa kuja Zanzibar kujaribu kuwashawishi waongozi wa vyama viwili vya kikabila waweze kuungana na kuasisi chama kimoja cha kisiasa ili kiweze kushiriki katika uchaguzi na kiweze kuwa pingamizi kwa Chama cha Hizbu.


Katika ripoti ya Mr. Penny aliyekuwa Muangalizi wa Uchaguzi aliandika, "Ofisi yangu na Idara ya Utawala zilisaidia kuundwa kwa AfroShirazi na kwahivyo ikaokolewa Zanzibar na kuwa na utawala wa chama kimoja wa namna ya khatari."


Mwalimu Nyerere alikuja Zanzibar pamoja na Sheikh Zubeir Mtemvu mnamo mwisho wa mwaka 1956. Mwalimu pamoja na ujumbe wake alikutana na waongozi wa African Association, Sheikh Abeid Amani Karume, Bwana Mtumwa Borafia na Bwana Boniface. Waongozi wa Shirazi Association aliokutana nao Nyerere katika ujumbe wake huo ni, Sheikh Ameir Tajo, Sheikh Thabit Kombo Jecha na Sheikh Othman Shariff Musa.

Mkutano huo ulifanyika katika nyumba ya Sheikh Abeid Amani Karume iliyokuwepo mtaa wa Kachorora, Mwembe Kisonge. Nyumba hiyo kwa wakati huo, ilikuwa ikikaliwa na Maalim Haji Ali Mnoga na Bwana Hija Saleh Hija.


Njama hizo za wakoloni pamoja na Mwalimu Nyerere zilifanikiwa.
Taarikhi 2 Februari 1957, miezi michache tu kabla ya kufikia uchaguzi wa mwanzo wa Juni, 1957 Chama cha AfroShirazi kiliasisiwa rasmi (kikiwa ni muungano wa jumuiya mbili za kikabila yaani "African Association na Shirazi Association"). Karume akawa Rais wa chama, Sheikh Ameir Tajo Makamo wa Rais na Sheikh Thabit Kombo Katibu Mkuu. Uwongozi wa chama haukwenda kwa mzalendo, haukwenda laa kwa Sheikh Ameir Tajo walaa kwa Sheikh Thabit Kombo, walaa kwa Sheikh Othaman Shariff, bali kwa Mzee Karume. Mbinu na njama za kuuwangamiza Uzanzibari zilianzwa zamani...


UCHAGUZI WA MWANZO JUNI 1957 Kutokana na mapendekezo ya uchunguzi wa Bwana Coutts kukhusu uchaguzi, uchaguzi wa mwanzo ulifanyika, June, 1957. Na kwa uchaguzi huo ndio wananchi wa Unguja na Pemba kwa mara ya kwanza waliweza kushiriki katika kuwachagua Wawakilishi wao wa Baraza la Kutunga Sheria la nchi yao. Uchaguzi huu ulikuwa wa viti sita. Majimbo mane yalikuwa kwa Unguja na mawili Pemba. Majimbo sita hayo yaligaiwa kama hivi: Unguja: Majumba ya Mawe Unguja: N'gambo Unguja: Kaskazini Unguja: Kusini Pemba: Kaskazini Pemba: Kusini Sheikh Ali Muhsin alisimama katika jimbo la N'gambo akiwa ni Mwakilishi wa HizbulWattan, akishindania na Sheikh Abeid Karume akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi, na Sheikh Ibuni Saleh alisimama katika jimbo hilo hilo akiwa ni mgombea huru. (independent candidate). Bwana Rutti Bulsara alisimama katika jimbo la Majumba ya Mawe akiwa Mwakilishi wa Hizbu na washindani wake wakiwa, Bwana Choudhry, Mwakilishi wa Muslim Association, Bwana Anverali Hassan Virji, mgombea huru na Bwana AbdulQadir Mukri, akiwa naye pia ni mgombea huru. Sheikh Amour Zahor alisimama jimbo la Kusini akiwa ni Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh Ameir Tajo akiwa ni Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo. Sheikh Haji Muhammad alisimama katika jimbo la Kaskazini akiwa mgombea huru akiungwa mkono na Hizbu, Sheikh Daud Mahmoud yeye alikuwa Mwakilishi wa AfroShirazi katika jimbo hilo.


Hizbu ilimuunga mkono Sheikh Haji Muhammad kwa kuamini kuwa ana fikra za kizalendo, na kutarajia kuwa hayuko mbali bali naye atajiunga na wananchi wenziwe ndani ya HizbulWattan; na hakika ikawa hivyo.


Pemba Kusini alisimama Sheikh Rashid bin Ali Khaify akiwa Mwakilishi wa Hizbu na Sheikh Muhammed Shamte Hamad alisimama jimbo hilo akiwa mgombea huru. Pia alisimama katika jimbo hilo Sheikh Abdalla bin Suleiman Busaidy, akiwa naye ni mgombea huru. Pemba Kaskazini, alisimama Sheikh Rashid Hamad Othman akiwa Mwakilishi wa Hizbu, Sheikh Ali Shariff Musa akiwa mgombea huru na Sheikh Shaaban Soud Mponda akiwa Mwakilishi wa AfroShirazi.


Matokeo ya uchaguzi huo, Chama cha AfroShirazi kilipata viti vitatu Unguja na hakikuweza kupata hata kiti kimoja Pemba. HizbulWattan ilishindwa kupata hata kiti kimoja laa Unguja wala Pemba. Viti viwili vya Pemba vilichukuliwa na wagombea huru wake, yaani Sheikh Muhammed Shamte na Sheikh Ali Shariff, baadae waliviunga viti vyao kwenye AfroShirazi na kuwa na viti vitano katika Baraza jipya la Kutunga Sheria. Kiti kimoja cha Nyumba za Mawe, kilichukuliwa na Bwana Chodhry Mwakilishi wa Muslim Association.



Natija hii ya uchaguzi inathibitisha kuwa Hizbu ni chama kilicho asisiwa bila ya kutokana na asili ya chama au jumuiya ya kikabila iliyokuwepo nchini kwa muda, kama vile ilivyokuwa hali kwa AfroShirazi. Na kwa vile HizbulWattan ilikuwa ndio kwanza chama kichanga haikustaajbu kwa kutopata hata kiti kimoja katika uchaguzi huu, kwani kilikuwa bado hakijawafikilia wananchi kwa wingi.


Amma AfroShirazi ambayo ni muungano wa jumuiya mbili za kikabila, jumuiya ambazo kwa muda zilikuwa zishakuwepo nchini hakikupata taabu kupata ushindi wa uchaguzi huu, kwani wanachama wake ndio walewale. Tafauti na HizbulWattan ambayo ilibidi ikuwe kwa kupitia kwa wananchi pole pole...


KUGAWANYIKA KWA AFROSHIRAZI Mwanzoni mwa 1959 kulitokea mgawanyiko wa waongozi wa Chama cha AfroShirazi. Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Ali Shariff waliamua kujitoa katika chama na kwa kutoka kwao, kulifuatiwa na wanachama wengi nyuma yao khasa Pemba.



Katika wakati huo huo, Chama cha AfroShirazi kilimfukuza katika chama Sheikh Ameir Tajo kwa singizio la kuwa alikwenda kuwaombea msaada wa fedha vijana wa YASU (Young African Social Union) kwa Sir Tayabali Karemjee kwa ajili ya ujenzi wa klabu (club) yao iliyokuwepo Miembeni, bila ya kuiarifu kamati kuu ya AfroShirazi. Sababu kubwa zilizompelekea Sheikh Mohammed Shamte na wenziwe kujitoa katika Chama cha AfroShirazi ni zenye kutokana na hisia za uwananchi khalisi kwa nchi yake. Hisia zake za kisiasa na nyendo zake pamoja na matarajio yake juu ya nchi yake yalikuwa ya kutaka kutumikia upatikane uhuru wa Zanzibar.


Uhuru utaongozwa na Wazanzibari wenyewe bila ya kuchukua amri au shauri kutoka pahala pengine popote. Sheikh Karume yeye alikuwa hawezi kufanya lolote bila ya kuzungumza na Mwalimu Nyerere na kama itavyoamuliwa na Mwalimu, ndivyo hivyo hivyo atavyofuata hata ikiwa si maslahi kwa Zanzibar (na mara nyingi hivyo ndivyo ilivyokuwa). Sheikh Mohammed Shamte, hayo yeye alikuwa hayakubali; kwahivyo daima walikuwa wakibuburushana mpaka mambo yalipofika hadi ya kufanywa mikutano ya Kamati Kuu ya Chama bila ya kuarifiwa Sheikh Mohammed kwa kukhofiwa kuwa akiwepo ataleta upingaji juu ya baadhi ya mambo. Ilipofika kiwango hichi, maji kuzidi unga, Sheikh Mohammed na Sheikh Ali Shariff walijitoa katika AfroShirazi.



KUASISIWA KWA ZANZIBAR AND PEMBA PEOPLES' PARTY (ZPPP) Chama cha Z.P.P.P. kiliasisiwa Novemba, 1959. Raisi wa Chama alikuwa Sheikh Mohammed Shamte Hamad na Naibu Raisi alikuwa Sheikh Ameir Tajo. Makao Makuu ya Chama yalikuwa Malindi Zanzibar. Z.P.P.P. kilikuwa Chama cha wananchi wa Unguja na Pemba. Kwa Unguja hakikuweza kupata wanachama wengi kwa wakati huo lakini kwa Pemba kiliweza kupata wananchi wengi kujiunga katika chama. Misingi na dhamiri ya Z.P.P.P. ikilingana na ya HizbulWattan. Nayo ni kufanyakazi kwa pamoja Wazanzibari wote, bila ya kubali rangi, kabila au imani zao za kidini katika kugombania kupatikana Uhuru wa Zanzibar kwa ajili ya mslahi ya wananchi wote.


Waongozi wa HizbulWattan hawakuwa na shaka yoyote juu ya uzalendo wa Sheikh Muhammed Shamte na wenziwe, kwahivyo walikuwa wakiamini kuwa iko siku wataweza kufanyakazi pamoja....


TUME YA SIR HILLARY BLOOD Katika Mei, 1960 Serikali ya Kiingereza baada ya juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na Chama cha Hizbu juu ya kutaka yapatikane maendeleo zaidi juu ya mabadiliko ya Katiba katika nchi, walimleta Sir Hillary Blood kutoka Uingereza akiwa ni mchunguzi wa mabadiliko ya Katiba. (Huyu ni wa pili, wa kwanza alikuwa Mr. Coutts).


Hizbu kama kawaida yao waliandaa maandamano makubwa kutoka kiwanja cha ndege cha Kiembe Samaki mpaka mbele ya nyumba ya Balozi wa Kiingereza. Waandamanaji wote wa kike na wa kiume, walichukuwa mabango yaliyoandikwa neno moja tu, "UHURU 1960".


Mapendekezo aliyoyatoa Sir Hillary Blood katika uchunguzi wake ni kuwa viti 22 tu viwe vya kuchaguliwa katika uchaguzi wa "Common Roll Election" na viti vinane viendelee kuwa vya kuteuliwa na Balozi wa Kiingereza kwa kushauriana na Mfalme wa nchi, yaani vyote viwe 30. Mapendekezo yake haya hayakuwa mbali na yale ya Chama cha AfroShirazi. Kama tulivyoona hapo juu katika risala yao, AfroShirazi wao walipendekeza kuwa viti vyote visizidi 25, kati ya hivyo vitatu viwe vya wajumbe wa kuteuliwa na kuchukuwa nafasi muhimu katika serikali.



UCHAGUZI WA PILI, JANUARI 1961 Baada ya miaka mitatu unusu tokea kufanyika kwa uchaguzi wa mara ya mwanzo, Juni 1957, ulifanywa uchaguzi mwengine, katika Januari, 1961. Safari hii, mabibi nao walipata fursa ya kushiriki katika uchaguzi. Uchaguzi huu ulikuwa wa viti 22. Vyama vyote vitatu vilishiriki kwa ukamilifu. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa, AfroShirazi walipata viti 10, Hizbu viti tisa na ZPPP viti vitatu. Kwa natija hii, hapakuwa na chama kilichoweza kuunda Serikali ila kwa kushirikiana na chama chengine.


Balozi wa Kiingereza Sir George Mooring aliwaalika waongozi wa vyama viwili vikubwa, yaani Hizbu na AfroShirazi kwa kuzungumzia tatizo liliokuwepo juu ya utaratibu wa kuweza kuunda serikali. Baada ya mazungumzo marefu ya hivi na hivi mwongozi wa Chama cha Hizbu, Sheikh Ali Muhsin alitoa shauri la kutaka ifanywe serikali ya pamoja ya vyama vyote vitatu.



Mwongozi wa Chama cha AfroShirazi, Sheikh Abeid Amani Karume, yeye aliipinga shauri hiyo na badala yake alitaka matokeo ya uchaguzi huo yafutwe na pafanywe uchaguzi mwengine. Baada ya kuzozana zozana na pasipatikane natija yoyote ya kurahisisha tatizo hilo, Balozi wa Kiingereza, Sir George Mooring alimpa kila kiongozi katika hao wawili muda wa wiki moja ajaribu kupata waakilishi waliyochaguliwa kuchanganya viti vyao pamoja naye ili aweze kupata wingi wa viti vya kumuwezesha kuunda serikali.


Fursa hiyo kwanza alipewa Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuwa Chama chake kilipata kiti kimoja zaidi kuliko Chama cha Hizbu. Wakati Karume alipokuwa katika juhudi za kuzungumza na Chama cha ZPPP, kwa kuwataka waviunge viti vyao vitatu upande wa Chama cha AfroShirazi, baadhi ya watumishi wa Serikali wa kikoloni na khasa wa Idara ya Utawala, nao waliingia kazini kwa kufunga njuga kwa njia za siri siri. Miongoni mwa utumishi wao ilikuwa ni kukisaidia Chama cha Afro waweze kupata viti vya kutosha waunde serikali. Kwa kutaka kutekeleza utumishi wao huo walizungumza na Sheikh Othman Shariff na walimtaka afanye kila njia na kila jitihada mpaka ampate Sheikh Mohammed Shamte akubali kuvipeleka viti vyao (vya ZPPP) vitatu upande wa AfroShirazi.


Kwa ilivyokuwa Sheikh Othman aliahidiwa malipo fulani fulani kama vile kulipiwa deni la nyumba yake ya "Kijipu House" iliyokuwepo Gongoni, Zanzibar, na mengineyo yaliyokhusika na mambo ya kisiasa, aliukubali utumwa huo. Na kwa kuwepo makhusiano ya kuowana baina yake na Sheikh Mohammed Shamte, yaani Sheikh Mohammed Shamte alimuowa binti wa Sheikh Issa Shariff (mtoto wa kaka yake Sheikh Othman Shariff), na vilevile mmoja katika hao washindi watatu wa ZPPP, alikuwa ni kaka yake yeye Othman, yaani, Sheikh Ali Shariff, basi Sheikh Othaman aliona itamuwiya rakhisi kufuzu utumwa huo. Othman aliingia mbioni kwa "Full speed". Baada ya kuona jitihada zake zote alizozifanya za kumtaka Sheikh Mohammed Shamte ayakubali matakwa yake zimefeli, alianza kumtishia kaka yake Sheikh Ali Shariff kwa kumwambia....


Sheikh Karume akiwa keshakuwa na mipango na matakwa yake, mbali na maslahi ya nchi, yote haya aliyakataa katakata na alishikilia fikra iliyotolewa na Balozi wa Kiingereza ya kufanywa Serikali ya Mshikizo na kufanywa uchaguzi baada ya miezi sita. Baada ya kuwa hakuna jengine isipokuwa kutekelezeka shauri hiyo iliyotolewa na Balozi, lilizuka tatizo jengine nalo ni, nani ataye kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali hiyo ya Mshikizo? Sheikh Ali Muhsin alipendelea nafasi hiyo apewe raia aliyekuwa na uzowevu juu ya mambo au uwendeshaji wa serikali.


Kwahivyo, alipendelea nafasi hiyo ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mshikizo apewe Sheikh Ahmed Lakha, ambaye ni Mzanzibari, mwenye ujuzi, maarifa, itibari na hakuwa mwenye kujiambatisha na chama chochote.


Mwongozi wa AfroShirazi Sheikh Abeid Amani Karume alikataa katakata kukhusu nafasi hiyo kupewa Sheikh Ahmed Lakha. Yeye alitaka nafasi hiyo apewe Bwana Roberts, mfanyakazi wa Serikali ya Kiingereza ambaye wakati huo alikuwa ni "Chief Secretary" wa Serikali ya Zanzibar na pia ndiye aliyekuwa akikamata nafasi ya Ubalozi wa Kiingereza wakati Balozi akiwa katika likizo. Shauri ya mzee Karume ndiyo iliyokubaliwa na Balozi, Sir George Mooring na Bwana Roberts akawa Waziri Kiongozi wa mwanzo wa Serikali ya Mshikizo ya Zanzibar.


Ukifuatia na kuzingatia utatambua kuwa katika harakati za kisiasa hizi zilizopita muda wote huu, fikra za ASP daima zilikuwa zikilingana na kukubaliana na fikra na matakwa ya kikoloni...



UCHAGUZI WA TATU JUNI 1961 Kwa kuchelea natija ya uchaguzi huu kutokea kama ile ya uchaguzi uliopita (wa Januari, 1961) hata kutokumkinika chama kimoja pekee kuunda Serikali kwa idadi ya viti walivyokuwa navyo, katika uchaguzi huu liliongezwa jimbo moja na kufanya idadi ya viti vyote 23 badala ya 22.


Ushirikiano Wa ZNP/ZPPP Katika uchaguzi huu, Hizbu na ZPPP walikubaliana na walitangaza rasmi kuwa watashirikiana katika kusimamisha wagombea wao kwa pamoja. Yaani, jimbo litalo simamiwa na mgombea wa Hizbu, ZPPP haitoweka mgombea wake bali wanachama wote wa Hizbu na wa ZPPP watampigia kura mjumbe huyo na hivyo hivyo kwa mgombea wa ZPPP. Fikra hii ilifanyika kwa kuzidi kutilia nguvu umoja na vile kila siku idhihirivyo kuwa misingi na matakwa ya ZNP/ZPPP juu ya maslahi ya nchi yakilingana. Ndugu zetu ASP wao daima muelekeo wao (kama tulivyoona na tutavyozidi kuoona) ulikuwa kinyume na hivyo, maslahi yao binafsi ndio yaliokuwa mbele....


AfroShirazi Iliandaa Machafuko Siku ya Uchaguzi Waongozi wa Chama cha AfroShirazi walipoona ushirikiano wa Hizbu na ZPPP katika uchaguzi, walijua kuwa hawatoweza kushinda, kwa hivyo waliandaa kufanya machafuko katika vituo vya uchaguzi. Walianza kwa kuwasukuma sukuma wanachama wa Hizbu na wa ZPPP khasa mabibi na vizee.


Waliendelea katika mipango yao hiyo ya fujo kwa kuwatowa wanachama wa ZPPP/ZNP katika mistari waliyokuwa wamejipanga kwendea kwenye masanduku ya kutilia kura. Ilipokuwa wanachama wa Hizbu na ZPPP hawakukubali kutolewa katika mistari, hapo tena wanachama wa AfroShirazi walianza kuwapiga wanachama wa ZNP/ZPPP kwa magumi, mateke na mwisho walianza kutumia silaha kama visu, mapanga na mawe.


Michafuko hiyo ilianza katika vituo vya uchaguzi na baadae iliendelea majumbani, mitaani na viamboni. Waongozi wa Hizbu na ZPPP, walipoona wenziwao wao wanauliwa na kujeruhiwa, waliwatangazia wao wote waondoke katika vituo vya upigaji kura na waliwazuia waliyokuwa bado hawajafika katika vituo vya upigaji kura, wasende mpaka watapoambiwa na chama chao ZNP/ZPPP kuwa wende ndio wende.


Michafuko hiyo ilimalizikia kwa kuuawa MaHizbu na MaZPPP 68 na mamia kujeruhiwa vibaya vibaya. Wengi wao walibakia na vilema vya muda na wengine vya milele. Michafuko hiyo ilianza tokea saa 12 za asubuhi kabla hata kufunguliwa hivyo vituo. Na tokea wakati huo, askari wa polisi walikuwa wamesha kuwepo katika vituo vyote vya mjini na mashamba lakini walijifanya kama hawayaoni yenye kutokea.


Serikali ya kikoloni walipoona mambo yamezidi watu wanauliwa na kujeruhiwa kwa wingi, ndipo walipoagizia kikosi cha askari wa kuzuwia fujo (GSU) kutoka Kenya. Askari hao walifika Zanzibar kiasi cha saa saba za mchana. Baada ya kuingia mitaani waliweza kutuliza michafuko na kurejesha hali ya kawaida. Lakini wakati huo waliyokuwa wameuliwa, wamesha uliwa na waliyokuwa wamejeruhiwa, wameshajeruhiwa.


Juu ya fujo hilo lililoandaliwa na AfroShirazi katika uchaguzi huo kwa kufikiria kuwa kwa kufanya hivyo watapata ushindi, wanachama wa ZPPP na Hizbu walisema, Mungu Mmoja kheri tufe lakini hatutowacha kwenda kuzitia kura zetu. Baada ya kuhisabiwa kura, AfroShirazi walijikuta na viti vyao vilevile 10 walivyovipata katika uchaguzi wa Januari 1961. ZNP/ZPPP walijipatia viti 13. Katika sehemu ya Zanzibar kulikofanywa ukatili mkubwa sana siku hiyo ya uchaguzi wa taarikh moja Juni 1961, hapakutokea kuliko Bambi.


Huko Mwalimu mmoja wa skuli, anayeitwa Bwana Ali Muhsin Mshirazi (bwana huyu pia alishiriki katika mauwaji ya Januari 12, 1964) alishirikiana na makatili wenzake kwa kuwachukua vijana wadogo, ambao wengi wao walikuwa ni miongoni mwa wanafuzi wake na kuwatia ndani ya tanuri la kuchomea mbata kwa kuwadanganya ati kuwa "anawahifadhi na ghasia ziliopo katika mji". Baada ya kuwatia humo, waliiondoa ngazi waliyo wateremshia kisha waliwamiminia geloni kwa mageloni ya petroli kisha wakawawasha moto. Vijana hao waliachwa wakiteketea mpaka kuwa majivu. Tanuri hilo ndilo lililokuwa kaburi lao. Jee nini kosa la vijana hao? Na wawe wana makosa ya aina yoyote, jee ulimwenguni huu tuishio iko kanuni ya adhabu ya aina hiyo? Kwa Kiislamu haifai kuadhibu kwa moto hata kwa mnyama mwenye kudhuru. Seuze binaadamu, tena watoto wadogo! Malipo ya Mwenyezi yanaanza tangu hapa duniani, natunayaona, kesho ndio hesabu na malipo ya milele. Kwa bahati, mmoja kati ya vijana hao ambaye siku yake ilikuwa bado Mwenye Enzi Mungu hajamuandikia, aliweza kupenya wakati walipokuwa wenzake wana teremshwa ndani ya tanuri mmoja mmoja. Kijana huyo, ndiye baadae aliyeweza kuzifikisha khabari hizo katika mikono ya polisi na kuweza kukamatwa mikatili hiyo.


Jambo la kustaajabisha na kusikitisha ni kuwa mahakama iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu Jaji Mkuu mkoloni, Muingereza haikuweza kupata hata mshitakiwa mmoja kati ya wote waliyopelekwa mbele yake kwa mashitaka ya kuuwa, kuwa ni mukhalifu. Hakutokea hata muuwaji mmoja aliyepewa adabu ya kuuliwa au hata ya kufungwa gerezani kifungo kikubwa. Wote waliachiliwa huru. Katika kesi ya mwalimu (Ali Muhsin Mshirazi) na mikatili wenzake, ushahidi aliyoutoa kijana yule mdogo mbele ya ...


KUTOKUFAULU MAZUNGUMZO YA MWANZO YA KATIBA YA UHURU Baada ya miezi 10 mpaka 11 tokea Serikali ya Muungano wa ZPPP/ZNP "Serikali Ya Madaraka" kuwa katika madaraka, Serikali ya Kiingereza ilikubali baada ya kushikiliwa na serikali hiyo ya madaraka kufanya mkutano wa mazungumzo ya uhuru.


Mkutano huo wa Katiba ya Uhuru ulifanywa katika miezi ya Machi na April 1962 huko Lancaster House, London. Pande zote mbili yaani upande wa Serikali na upande wa Upinzani walihudhuria kwenye mkutano huo. Kwa bakhti mbaya mkutano huo haukuendelea kwa siku nyingi illa ulivunjika bila ya kukubaliana kwa kuwekwa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa AfroShirazi walikataa kuzungumzwa chochote kilicho khusika na kutolewa taarikh ya Uhuru mpaka kwanza pafanywe uchaguzi mwengine. Baada ya matokeo ya uchaguzi huo, ndio yafuatie mazungumzo ya kutolewa kwa taarikh ya Uhuru. Waongozi wa upande wa Serikali waliwanasihi mwisho wa uwezo wao waongozi wa upande wa Upinzani yaani AfroShirazi waache kuleta vizingiti vitavyo sababisha kuchelewa kwa Uhuru wa Zanzibar. Bali waongozi wa AfroShirazi walin'gan'gania uzi wao huo huo wa kupinga kuzungumzwa chochote kitachofikilia kutolewa kwa taarikh ya Serikali ya Ndani kabla ya kufanywa uchaguzi mwengine.


Waongozi wa upande wa Serikali, walipoona waongozi wa upande wa Upinzani hawataki kubadili msimamo wao, walijaribu kuzungumza nao nje ya mkutano. Katika mazungumzo hayo, upande wa Serikali waliutaka upande wa Upinzani wakubali kufanyika serikali ya pamoja, yaani "Government of National Unity" (hii ni mara ya pili ASP kupewa shauri na wenzao ZNP/ZPPP kufanya serikali ya pamoja.)...


Baada ya kufuzu hayo yenye kuitwa 'mapinduzi' ya Januari 12, 1964, Katibu Mkuu wa AfroShirazi, Sheikh Thabit Kombo alisema wakati akikhutubia mkutano wa hadhara mbele ya Makao Makuu ya AfroShirazi, hapo Mapipa ya Ngozi, Kisiwandui: "Tunamshukuru Mwalimu Nyerere kwa kutuvua mtego waliyotaka kutunasa Mahizbu wakati wa mkutano wa mwanzo wa Katiba, huko Uingereza. Mahizbu walitaka kutufanyia ujanja wa kutaka tuungane pamoja katika kuendesha serikali na kwa kutaka kutimiza ujanja wao, walikiri kutupa wizara tatu katika serikali yao. Lakini mzee Karume kabla ya kusema lolote, alizungumza na Mwalimu kwa simu kumtaka shauri yake juu ya jambo hilo. Mwalimu alimwambia mzee Karume asikubali kufuata shauri hiyo ya Hizbu kwani huo ni ujanja tu wakutaka kusiwepo na upinzani. Mkitaka shauri yangu kataeni. Ndipo mzee alipokataa", alisema Thabit Kombo.


Mara nyingi utamsikia Mwalimu akisema kuwa yeye hakukhusika na lolote katika mizozo ya kisiasa ya Zanzibar. Hatujui Mwalimu anataka akhusike namna gani zaidi ya hivyo alivyokhusika (alivyo jikhusisha).


Yeye Mwalimu ndiye aliyekiasisi Chama cha AfroShirazi na ni yeye aliyekuwa, "master mind" katika kuyaandaa hayo yenye kuitwa 'mapinduzi'. Wavamizi walioivamia Serikali ya halali ya Zanzibar wengi wao wameletwa Zanzibar kutoka katika nchi yake Tanganyika, na huko ndiko walikopewa mafunzo ya kutumia silaha; na hizo silaha zenyewe zilitoka huko huko kwake Tanganyika. Naiwe hakukhusika na fisadi zote hizi zilizofanyika Zanzibar kama adaivyo, bali huo ufisadi mmoja tu unatosha, nao ni wa huko kuiburura Zanzibar ndani ya huo muungano wake, muungano uhange, miezi minne tu baada ya kufuzu hayo 'mavamizi' yake.....



Kwa kuhudhuriya mazungumzo ya Uhuru huko London, Hizbu ilitengeneza mipango maalum ili baadhi ya waongozi wa Chama nawo wawepo huko London wakati wa mazungumzo hayo ya Uhuru. Miongoni mwa waliokuwepo huko ni Babu akiwa ndiye Katibu Mtendaji wa Chama, Suleiman Malik na mimi Aman Thani tukiwa ndio wenye dhamana ya Ofisi ya ZNP iliyokuwepo Cairo wakati huo. Pia walikuwepo huko London, Bwana Ali Sultan Issa, Sheikh AbdulRazak Mussa (Kwacha) na Bwana Ali Mahfoudh akiwa ndiye aliyekuwa na dhamana ya Ofisi ya ZNP Cuba na Bwana Salim Said Rasdhid Mauly ambaye ndiye aliyekuwa na dhamana ya Ofisi ya ZNP hapo London.


Kwa ajili ya matengenezo fulani fulani, ujumbe huo ulitangulia kufika Uingereza kabla ya kufika Mawaziri. Waziri aliyefika mbele kabla ya wenziwe, alikuwa Dr. Ahmed AbdulRahman Idarus Baalawy. Siku moja kabla ya kufika Mawaziri wengine, Babu alitaka tukutane kwa kuzingatia mambo muhimu ya kazi zetu.


Katika kuendelea na mkutano huo, Babu alieleza kuwa amepata khabari za kuaminika kuwa nyumbani Zanzibar kumeasisiwa Kamati ya watu 14. Kazi ya Kamati hiyo ni kumpa nasaha Sheikh Ali Muhsin katika uwongozi khasa katika wakati kama huu wa kukaribia kupatikana kwa Uhuru wa nchi. Aliendelea kueleza Babu kuwa, "Kamati hiyo inamtaka Sheikh Ali Muhsin ajaribu kama awezavyo kutafuta njia zitazowezesha kuwaepuka baadhi ya waongozi wa Hizbu, mimi (Babu) nikiwa ni mmoja na kila wanaye muona kuwa anazo fikra za kimaendeleo, yaani hata wewe Dr. Idarus umo katika hao wenye kutakiwa waepukwe". Maneno hayo ya Babu yalitushangaza na kutusitusha baadhi yetu, ama wengine kati yetu walikuwa tokea mwanzo wanayajuwa.


Baada ya kuyazungumza kwa urefu maneno hayo tulikubaliana tuyaakhirishe mazungumzo hayo mpaka baada ya mazungumzo ya mkutano wa Uhuru, baada ya hapo tutakaa na Sheikh Ali Muhsin pamoja na Mawaziri wote tuyazungumze. Babu aliwafiki rai hii. Baada ya kumalizika kwa mkutano, baadhi yetu tulimkumbusha Babu kukhusu kukutana na Sheikh Ali Muhsin pamoja na Mawaziri wengine juu ya masala aliyoyaeleza kabla ya mkutano wa Uhuru.....


KUFUNGWA GEREZANI KWA SEYYID ABDULRAHMAN BABU Serikali ya kikoloni ilikuwa daima dawamu dhidi ya misingi na msimamo wa Chama cha Hizbu, haikutokea hata mara moja kukipa uso mzuri. Kwa vile hawakupendelea kiendelee, kila wakati walikuwa wakikitafutia kila njia ya kukivuruga ili kisiweze kuwa na nguvu, na ikiyumkinika hata kitoweke kabisa.


Lakini kila wakizidisha njama zao ndio umma ukizidi kuwafahamu na jitihada zao zikifeli. Babu wakati huo alikuwa ni miongoni mwa waliyokuwa hawapendiza machoni mwa wakoloni, kwa hivyo naye pia alikuwa katika mipango ya njama zao. Walipopata kipengee kutokana na makala aliyoyaandika katika gazeti lake la ZANEWS, wakoloni waliona sasa mtego wao umeweza kumnasa Babu. Pia waliona kuwa natija yake itafaa kutumika dhidi ya Hizbu.


Wakoloni walimshitaki Babu kwa kosa la kuwa makala yake ni matusi ya kumtukana Mkuu wa Polisi kwa jambo la uwongo wala si kwa maslahi ya umma. Kamati Kuu ya Hizbu bali hata wananchi wengi ilifahamu wazi kuwa wakoloni wamechukua khatua hiyo ya kumshitaki Babu si kwa sababu yoyote illa ni kutaka kukidhoofisha Chama katika wakati muhimu kama huo katika juhudi za ugombozi wa nchi kutokana na ukoloni.


Kamati Kuu ya Hizbu iliamua kushirikiana na Babu katika kesi hiyo kwa hali na kwa mali, juu ya kuwa gazeti hilo la ZANEWS halikuwa gazeti la Chama bali lilikuwa la Babu binafsi....

Kwa vile wakoloni walikuwa wamekwisha dhamiria kuitumia fursa hii kwa azma ya kuleta michafuko katika Chama, walitekeleza azma yao kwa kumfunga Babu gerezani kifungo cha miezi 18. Chama kilikata rufaani kwa hapo Zanzibar na baada ya kushindwa hapo, kilichukua rufaani kutoka "East African Court of Appeal" na huko pia kilishindwa na Babu aliendelea na kifungo chake kwa muda wa miezi 18, kama ilivyokwisha pangwa.


KUTOLEWA GEREZANI BABU Baada ya Babu kumaliza kifungo chake, alitolewa gerezani mnamo saa nne za usiku na ilikuwa kwa njia za siri siri. Jambo ambalo si la kawaida. "BABU'S WEEK" Chama cha Hizbu kwa furaha ya kutolewa Katibu wake kifungoni kwa salama, kiliandaa mapokezi yake kwa sherehe kubwa kubwa. Sherehe hizo zilikuwa kwa muda wa wiki mbili, wiki moja zilifanywa Unguja na wiki ya pili zilifanywa Pemba. Kwa kusherehekea siku hio, Makao Makuu ya Chama na Matawi yake yote, Unguja na Pemba, mjini na mashamba, yalipambwa kwa mabendera na mataa ya kila rangi. Sherehe hizo zilikuwa kwa kusomwa Maulidi, kwa Dhikiri, kwa magoma na hata kwa mashindano ya ngalawa. Babu akibebwa juu ya mabega ya wananchi na huku kukiimbwa "SOTE TWAMPENDA BAABU!".


"Babu's Week" (wiki ya shereha za kufunguliwa Babu) ya Unguja ilimalizika kwa Hizbu kufanya karamu kubwa katika uwanja wa Bustani ya Seyyid Khalifa Hall (sasa ati inaitwa Karume House). Baada ya hapo, Babu alikwenda Pemba na huko alifanyiwa kama alivyofanyiwa Unguja na zaidi. Wananchi wa Ziwani kwa furaha zao, walimtunukia Babu awe ni mgombea kiti cha jimbo lao la Ziwani katika uchaguzi wa 1963. Kiti hicho kilikuwa ni kiti cha hakika kwa ushindi wa Hizbu.


BABU NA FISADI YAKE YA MWISHO Babu alirejea kutoka Pemba siku ya Jumaane kiasi cha saa mbili za usiku. Usiku huo huo, alikutana na kamati ya uchaguzi ya Chama. Kamati hiyo ilimkabidhi Babu orodha ya wagombea uchaguzi wa Hizbu katika Unguja kama walivyo teuliwa na majimbo yao kwa mjini na kwa mashamba. Babu baada ya kupokea orodha huo, naye alitoa orodha wa wagombea uchaguzi wa Hizbu kwa Pemba, naye akiwa ni miongoni mwao. Kamati ilifurahikiwa na matokeo yalivyokwenda vizuri kukhusu uteuwaji wa wagombea uchaguzi, Unguja na Pemba.


Siku ya pili yake, Jumaatano, Kamati Kuu ya Hizbu ilikutana. Babu alitoa ripoti yake ya Pemba na kuiarifu Kamati Kuu kuwa yeye ameteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha Ziwani Pemba. Kamati Kuu ilifurahikiwa na matokeo yote yaliyotokea Pemba...


Ikabidi wanafunzi hao kukatiwa "skolashipu" zao. Wengine walirudi Zanzibar, na baadhi wakatokomea nchi za Kikomunisti kwa matengenezo ya Komredi Ali Sultan, mpwawe Rashad. Hata hivyo, wengi waliendelea na masomo yao, na kila baada ya muda wengine walikuwa wakipelekwa mpaka ikawa idadi kubwa sana. Juu ya hizo "skolashipu" wazazi walio kuwa wakijiweza waliwapeleka watoto wao kwa gharama zao, na kuwalipia kuwakimu kutokana na mifuko yao wenyewe.


Yalipotokea mavamizi ya Zanzibar katika mwaka 1964 Baraza la Mavamizi lilipasisha kuwakatia masomo vijana wote hao na kudai warejeshwe Zanzibar. Nyerere na Karume walitoka mguu mosi mguu pili mpaka Misri kwa ajili ya kuukomesha ule mradi wa kufadhiliwa "skolashipu" wanafunzi wa Zanzibar. Wakati huo Diria ndiye alikuwa Balozi wa Tanzania Cairo. Maalim Hija Saleh alikuwa wakati huo katika Ubalozi. Wao hao walivaa njuga katika kuwasaka wanafunzi majumbani na majiani, na kuwataka wawarejeshe Zanzibar. Waliwapata baadhi, na wengine wakaendelea na masomo yao kwa shida na taabu, mpaka wakamaliza....


Lakini, wakati ulipo pasishwa uamuzi huo wa kuwakatia masomo wanafunzi walikuweko Profesa Babu, Al Haji Aboud Jumbe, Komred Ali Sultan, Komred Badawi, Komred Khamis Abdulla Ameir, Komred Salim Rashid, Kanali Komred Ali Mahfoudh, Komred Kassim Hanga, Maalimu Saleh Saadala na Twala. Vipi wote hao viongozi wataalamu waliweza kuunga mkono jambo kama hilo? Kutokana na mambo kama hayo na mengineyo mfano wa hayo, ndipo wananchi wa kweli wenye uchungu wa nchi yao na wenziwao, wanaposema kuwa waongozi wote wa serikali yenye kujiita ya "Mapinduzi" tokea wa awamu ya kwanza, hadi ya pili, hadi ya tatu, na..na...Mwenyezi Mungu anajua hapana hata mmoja aliyekuwa amesimama kwa ajili ya maslaha ya nchi, wala ya wananchi. Kila mmoja, kuanzia Rais mpaka Komisar, wote walikuwa mbioni kujitengenezea maslaha ya nafsi zao tu. Naitoshe kuwa siku ya pili tu baada ya hayo yenye kuitwa mapinduzi kufanyika katika nchi kila mheshimiwa alikimbilia kwiba motokari, na kuhamia katika majumba ya watu, mbali ya kukimbilia mabanati wa Kiarabu na wa Kihindi.


Leo, baada ya kuwa wengi katika hao walio kuwa katika Awamu ya kwanza na ya pili hata na ya tatu kuwa wapo nje ndio utasikia wakisema maneno kama kwamba wao walikuwa hawakuwamo katika kufanyika hayo!....


YALIYO NIFIKA NAFSI YANGU NA HAYO YENYE KUITWA "MAPINDUZI" Kiasi cha saa 12 za magharibi siku ya Jumaatatu taarikh 13 Januari 1964, siku ya pili ya hayo yenye kuitwa 'mapinduzi', mimi pamoja na mke wangu na chungu ya wananchi wenzetu wa kike na wa kiume, wakubwa na wadogo, tulikuwepo katika klabu ya wazee wa Kingazija "Comorian Club" iliyokuwepo Kisiwandui, Unguja. (klabu hiyo kwa wakati huo, wakuu wa mavamizi waliifanya kuwa ni miongoni mwa vituo vya wakimbizi).


Ghafla tulisikia mlango ukigongwa kwa vishindo vikubwa na baada ya kufunguliwa, tuliwaona vijana watatu wametuingilia, wawili walikuwa wamechukua bunduki na mmoja alikuwa na bastola, huyu alikuwa ni Mzanzibari, kwa jina ni Ahmed Bushir Aboud na hao wenzake walikuwa vijana wa Kibara.


Kwanza waliwachukua, Sheikh Ameir Tajo na Sheikh Ali Ahmed Riyami na baada ya muda walirejea na walinichukua mimi (Aman Thani) na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa. Wote hao wenzangu wameshafika mbele ya haki. (Mungu awape malazi mema, Amin). Safari yetu hiyo ilimalizikia katika jumba la Raha Leo (Civic Centre) Miafuni. Jumba hilo kwa siku hizo za mavamizi, 35

lilifanywa ndio Makao Makuu ya Wavamizi. Mbele ya uwanja wa jumba hilo, tulikuta umati wa watu mkubwa sana na kila mmoja alikuwa na silaha mkononi mwake. Wengine walikuwa na mabunduki, wengine walikuwa na mapanga, mashoka, mishale, na mipinde pamoja na mikuki. Wengine walikuwa kama ni vichekesho kwani walikuwa wamejiremba marangi mwilini mwao na wamejizongeresha majani na magozi, na huku mtu mmoja huyo huyo amechukua bunduki mkono mmoja, panga mkono wa pili na upinde ameuvaa shingoni na mishale ameichomeka kiunoni.


Ndani ya hilo jumba la Raha Leo, kulikuwa kumejaa watu, wake kwa waume wakubwa kwa wadogo hata vitoto vichanga, pamoja na mama zao, hao pia walichukuliwa kutoka majumbani mwao na kuletwa hapo ati kwa usalama wao...


Baada ya muda walitujia, Comrade Ali Mahfoudh na Comrade Badawi Qulatain na walitutaka mimi, Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, Sheikh Issa Mohammed Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi tuwafuate. Walituongoza, Ali Mahfoudh akiwa mbele na Badawi akiwa nyuma na sisi tukiwa katikati mpaka nje ya jumba; na hapo tulitiwa ndani ya gari aina ya "pickup" kubwa (Lori) na tulifuatanishwa na walinzi wanane, wote wakiwa na bunduki, na wote pamoja na dereva wetu walikuwa wamelewa. Hao walinzi waliwauliza mabosi wao, "Hawa wa wapi?" Comrade Ali Mahfoudh alijibu, "Wapelekeni Kilimani"....


MAAFA YA GEREZANI Tulifika katika Gereza la Kiinua Miguu, ambalo sasa linaitwa, Chuo cha Mafunzo, kiasi cha saa nne za usiku na hapo tulimkuta Comrade Hemed Hilal Barwani, ambaye yeye ndiye aliyekuwa na dhamana ya gereza hilo kwa wakati huo. Comrade Hemed Hilal alitutaka tuvue nguo zetu zote, na tulizivua na tukabaki kama tulivyotoka matumboni mwa mama zetu. Hakuweza kumwekea sitaha hata mzee wake, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani. Baada ya kwisha kusachiwa, Comrade Hemed Hilal alitoa amri tupelekwe kwenye vyumba vya "security" vya kuwekewa mahabusi. Tulipewa virago vya kulalia, (kirago ni kizulia cha usumba urefu wake kiasi cha futi nne mpaka tano na upana wake ni kiasi cha futi mbili mpaka tatu) shuka mbili za bafta na kopo la kunywia maji, uji na kunawia baada ya kwenda haja ndogo au kubwa, ndio hilo hilo. Baada ya kupewa vitu hivyo, tuliongozwa na sajin wa gereza mpaka katika hivyo vyumba. Mimi na Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa tulitiwa katika chumba kimoja na Sheikh Issa na Sheikh Mwinyi Nemshi walitiwa katika chumba kimoja. Sehemu hiyo ilikuwa na vyumba sita, kila upande vyumba vitatu na katikati ujia. Tulifungiwa kwa kufuli, lango la nje pia lilitiwa kufuli. Baada ya kuondoka huyo sajin aliyetupeleka, tulisikia sauti ikitoka katika chumba kimoja ikiuliza, "Ni nani wenzangu mliyoletwa"? Sauti ilikuwa si ngeni kwetu lakini kwa mughma tuliyokuwa nao wakati huo, tulishindwa kuitambua. Tulimuuliza kwani wewe ni nani mwenzetu? Alitujibu, "Mimi Suleiman Said Kharusi, na chumba chengine yumo Sheikh Humoud Ali Harthi, na chumba chengine yumo Sheikh Mohammed Idi Mjasiri, na chumba cha mwisho yumo mwanangu Edi Kharusi". (Mohammed Ali Said Kharusi) Na mimi nilimjibu, "Mimi Aman Thani, na mwenzangu Sheikh Mohammed Aboud Mkandaa, tumo katika chumba cha pili mkono wa kulia kutokea mlangoni". "Na wenzetu wawili, Sheikh Issa Mohammed Issa Barwani na Sheikh Mwinyi Nemshi, wao wametiwa katika chumba cha mwisho katika mkono huu ...


KUFUNGWA KIFUNGO CHA MIAKA 10 GEREZANI Taarikh 1 Januari, 1965 kiasi ya saa nne za asubuhi, Karume Raisi wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar akifuatana na wenzake wa Baraza lake la Mavamizi walikuja gerezani. Walipofika walitukuta sisi wachache tuliyokuwa tumebakia kiziwizini tumesimama kwa kungojea kwa matumanio makubwa sana ya kuachiliwa huru kama walivyo achiliwa wa kabla yetu. Alipofika mbele yetu, Karume alisema, "Leo tumekuja kuwaachilia huru wote waliyokuwa wamewekwa humu ndani kuanzia siku za mwanzo za mapinduzi". Kiasi ya kusema hivyo tu, tuliwaona baadhi ya waongozi wa Baraza la Mavamizi, wakiwemo Ibrahim Mbwana (Ibrahim Makungu), Said Natepe, Seif Bakari na Khamis Darwesh wamevutana upande na wakinon'gonezana. Baadae walimnon'goneza Karume; na hapo hapo mpira uligeuzwa kuelekea upande mwengine. Tuliona tunatolewa mmoja mmoja na kuwekwa upande mpaka tulitimia watu 25. Karume na kikosi chake waliondoka na kutuacha sisi watu 25 upande mmoja na wenzetu wengine wachache waliachwa upande wao. Baada ya muda alitujia Ofisa wa Gereza, Bwana Oliver Fernandes akifuatana na sajini (sergeant) Nyankabwa pamoja na askari wao wawili. Oliver alikuwa akitwambia na huku ameinamisha uso wake chini kwa kutuonea taabu kututizama kwa namna alivyokuwa akiona dhulma na unyonge tuliyopitishiwa ambao tokea kuanza kwake kazi hajapata kuuona wala kuusikia. Alisema kutwambia, "Baraza la Mapinduzi, limeamua kukufungeni gerezani kifungo cha miaka 10 kwa kila mmoja wenu kuanzia hii leo Januari 1, 1965...huu wa kulia."....


Yafuatayo ndio majina ya hao wadhulumiwa 25 tuliofungwa miaka 10 gerezani bila ya makosa na bila ya kupelekwa mbele ya mahakama: Suleiman Sultan Malik Hassan Usi Walid Fikirini Ali Issa Ali (Mataa) Mohammed Rajab (Machungwa) Haji Hussain Ahmed Yahya Mohammed Ali Shambe Hussain Bachu Ramadhan Khamis Shariff AbdulRahman Othman Mzee Maalim Mwita Rashid Mohammed Marjeby Ali Raza Nathani (Ali Bomu) Omar Hamad (Mkame Ndume) Sheha Abdulqadir Thiney Sheha Suleiman Khamis Ali Mohammed Suleiman Wazir Ali bin Maalim Mzee Ismail Salim Said Halua Nasser Mohammed Husein Jessa Bhaloo Ali Mdungi Ahmed Abdulqadir (Qullatain) Aman Thani Fairooz Kwa hakika siku hiyo ilikuwa ni siku ngumu sana katika maisha yetu. Tulishindwa kula na tulikesha usiku kucha bila ya kufumba jicho hata muda mdogo.


Kulipokucha siku ya pili taarikh 2 Januari 1965, baada ya kupewa uji wa sembe na chembe mbili tatu za maharagwe, tulipelekwa kuonana na Mkuu wa Magereza. Wakati huo alikuwa Bwana Kilonzi. Lakini, aliyetukabili alikuwa Bwana Oliver Fernandes, msaidizi wake. Oliver alitupa Daftari kubwa lenye kuwekwa majina ya wafungwa pamoja na makosa yao na muda wa vifungo vyao. Tulipo litupia jicho, tuliyaona majina yetu yamesha andikwa pamoja na makosa yetu na mahakama yaliyotuhukumu na hakimu aliyetuhukumu na muda wa vifungo vyetu.


Maelezo ya hukumu ya kufungwa kwetu huko kama yalivyoandikwa katika Daftari hilo yalikuwa kama hivi: Kosa Letu: Kutia choko choko za kutaka kuipinduwa Serikali ya Wananchi. Hakimu Aliye tuhukumu: Mkuu wa Jeshi la Taifa. Mahakama Iliyotuhukumu: Makao Makuu ya Jeshi Muda wa Vifungo Vyetu: Miaka 10 Kila Mmoja (tangu Januari 1, 1965 mpaka Desemba 31, 1974).....


KUTOLEWA GEREZANI Kila lenye mwanzo lina mwisho, na hakuna marefu yasiyo ncha na baada ya dhiki ni faraji. Wanasema wasemao: Akushutuao wewe sishutuke Yupi awezao kukwetea lake Watu wanayao Mungu ana lake Taarikh 10 Januari 1967 ikiwa taarikh 28 Ramadhani kiasi cha saa 10 za alasiri, wafungwa wote tuliokuwa tukiitwa "wafungwa wa kisiasa" tuliyokuwepo katika gereza la Langoni tulikusanywa, na waliletwa pamoja na sisi wenzetu kutoka gereza la Kinu Moshi. Haikupita muda ila tuliyaona magari mawili ya magereza yametufikilia. Sote tulipakiwa na kupelekwa Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu (Mjini). Tulifika huko na kin'gora cha magharibi kinalia. Tulitawadha na baada ya kumaliza kusali, tulifuturu kwani sote tunamshukuru Mwenye Enzi Mungu tulikuwa tukifunga. Baada ya kumaliza kufuturu, tuliachwa kukaa katika njia ya kupitia baina ya vyumba na vyumba. Tuliachwa hapo mpaka baada ya kusali Taraweh ndipo tulitiwa vyumbani na kufungiwa ndani.


Taarikh 11 Januari ikiwa taarikh 29 Ramadhani, kiasi cha saa tatu za asubuhi, Karume na kikosi chake cha Baraza la Mavamizi walifika hapo gerezani, walitukuta tumewekwa tayari, tukingojea maamuzi yao juu yetu. Upande mmoja roho zilikuwa na tamaa kuwa hwenda ikawa mkusanyo huu ni wa kuachiliwa huru, na upande wa pili roho zilikuwa zikidunda dunda kwa khofu za kuwa hwenda ikiwa wengine wasiachiwe. Muradi kila mmoja alikuwa akivuta uradi moyoni mwake na kumuomba Mwenyezi Mungu atufaraji. Lakini kwa hakika tamaa za kuachiliwa sote hazikuwemo katika nyoyo zetu.

Karume alikuja moja kwa moja mpaka upande tuliowekwa na alituambia, "Leo tumekuja kwa makusudio ya kukutoeni gerezani ili mupate kwenda kusherehekea Sikukuu ya EidelFitr na Sikukuu ya Mapinduzi pamoja na aila zenu. Tumefurahi kupata ripoti ya ukaaji wenu gerezani kuwa mmekaa kwa adabu na kufuata kila amri za gereza mlizokuwa mkipewa na waliyo khusika. Kwahivyo, leo tunakuachilieni huru, na kila mmoja atapewa Shs. 1000 mpate kufurahikia Sikukuu pamoja na watoto wenu! Lakini ninakuonyeni na nakutakeni mkakae uzuri huko nje. Ikiwa mtajitia kuchanganyika na makundi ya watu wakorofi, mkaja mkakumbwa na kuletwa tena gerezani, basi adabu itayokuwa ni kifo wala si chengine...

NAKIMBILIA DARESSALAAM Kutokana na hali kama hizo zilizokuwepo nchini, namiye niliamua kuikimbia nchi yangu. Taarikhi 10 Juni, 1967 niliondoka Zanzibar kwa kuhamia DaresSalaam na huko nilifikia, na nilipokelewa na ndugu yangu mpenzi Mzee Mohammed MBABA. Tuliishi pamoja kwa muda mkubwa na baada ya kupata kazi, niliondoka kwa kuhamia pahala pangu peke yangu lakini kila wakati tulikuwa pamoja kwa mashauri na kwa mazungumzo.


Baada ya kupata kazi na baada ya kutamakani kidogo, nilileta aila yangu na kuishi pamoja katika maisha yetu mapya. Ole wangu! Kumbe nimeondoka kwa wachinjaji, nimekwenda kwa wala nyama!


Baada ya muda wa miezi 16, yaani tangu Juni 1967 mpaka September 1968, tokea kuishi DaresSalaam, nilisitukia ghafla mlango wa nyumba niliyokuwa nikiishi ukigongwa kwa vishindo vikubwa mnamo usiku wa manane, kiasi cha saa saba na nusu hivi. Nilipofungua mlango, waliniingilia ndani watu saba kwa jumla. Watano walikuwa wamevaa nguo za kiaskari wa polisi na walikuwa wame chukua marungu mikononi mwao na wawili, walikuwa wamevaa nguo za kiraia yaani shati na suruali. Wao walikuwa na bastola mikononi mwao. Kiasi cha kuingia ndani tu, waliniuliza, "Jina lako nani?" Niliwajibu, "Aman Thani". Mmoja katika hao wawili waliokuwa wamevaa nguo za kiraia, aliniambia kuwa, "Tokea sasa tumekukamata, na umo katika dhamana ya Polisi". Niliwauliza, "kwa kosa gani?" Nilijibiwa kuwa, "Utaambiwa utapofika Makao Makuu ya Polisi".


Niliwaomba waniruhusu kuvaa nguo kwani wakati huo nilikuwa nimevaa shuka na fulana tu. Kwanza walinikatalia na kwa kuwaomba sana, walinikubalia na walimtaka mke wangu aniletee nguo. Niliwahi kuvaa shati na suruali. Nilipokuwa nataka kuvaa soksi na viatu, askari mmoja alinizuwia na alivichukuwa yeye hivyo viatu na aliniambia, "Utavivaa utapokuwa ndani ya gari huko nje". Niliongozwa na kutolewa nje nikawaacha nyuma mke wangu na mtoto wangu mchanga wa mwaka mmoja katika nchi ya kigeni na katika nyakati za usiku kama huo. Unyonge ulioje! Nilipofika nje, nilizikuta gari mbili za polisi, na nilitiwa katika moja ya hizo. Yule askari aliyechukuwa viatu vyangu, yeye aliingia katika gari nyengine hakuingia pamoja na mimi.

Nilipofika Makao Makuu ya Polisi baada ya kuandikwa jina langu nilisachiwa mwilini na nguoni. Nilipokuwa nikisachiwa nilimwambia huyo aliyekuwa akinisachi kuwa viatu na soksi zangu amechukua mmoja katika askari waliyokuja kunichukuwa kutoka nyumbani kwangu na aliniambia kuwa atanipa wakati nitapokuwepo katika gari nje, lakini sijamuona tena, kwahivyo naomba nipewe viatu vyangu. Jawabu la huyo aliyokuwa akinisachi, lilikuwa, "Hilo mimi halinikhusu, atapokuja, atakuletea". Niliondolewa hapo na nilipelekwa katika vyumba wanavyowekwa mahabusi. Nilipofika huko, niliwakuta baadhi ya Wazanzibari wengine wameshaletwa na ilikuwa kila baada ya muda, wakiletwa wengine mpaka kulipokucha, tulitimia watu 17. Wote isipokuwa mmoja tu, walikuwa ni Wazanzibari. Huyo mmoja, yeye alikuwa ni mtu wa Tanganyika na hajawahi hata mara moja kwenda Zanzibar wala alikuwa haijui khasa ....



Wengi ya hao Wazanzibari waliyokamatwa usiku huo, waliondoka Zanzibar na kuishi DaresSalaam miaka mingi nyuma. Wengine zaidi ya miaka 40 walikuwa wakiishi Tanganyika na kufanyakazi huko huko kwa maisha yao yote na hata baadhi yetu hatukuwa tukiingiliana kwa lolote bali hata tulikuwa wengine hatujuani. Usiku kucha tulikuwa macho hapana hata mtu mmoja aliyekuwa angalau amesinzia. Tulikuwa tukiulizana na hapana aliyeweza kumjibu mwenziwe, kwanini tumekamatwa? Tumefanya kosa gani? Kiasi cha saa mbili za asubuhi, alitujia Sajini mmoja pamoja na askari wake na alimwambia huyo askari wake, "Waletee hawa watu chai 'special'". Baada ya muda, tuliletewa chai katika mabirika na vikombe, maziwa, siagi na mikate. Hakika chai ilikuwa chai ya kweli, iliyokuwa imetimia kwa kila kitu. Wakati sisi tukipewa chai kama hiyo, tuliwaona mahabusi wenzetu wengine wakipewa chai kavu na maandazi ya mkahawani! Tulimuuliza yule askari aliyetuletea hiyo chai, kuwa, mbona sisi tunapewa chai nzuri kama hivi na wale wenzetu wanapewa chai kavu na maandazi na ilhali sisi sote ni mahabusi? Askari alitujibu, "Kweli nyote ni mahabusi lakini nyie ni mahabusi wa kisiasa, na wale ni makriminali. Lazima iwepo tafauti kati yenu".


Kwa kusikia tu neno "wa kisiasa" basi hapo hapo hiyo chai "special" ilitutumbukia nyongo, tuliiona ni "special" kweli! Hapo tena tulianza kutizamana na kila mmoja aliingiliwa na khofu moyoni mwake. Tulikuwa tukiulizana tu wenyewe kwa wenyewe, siasa hizo tumezifanya wapi au za namna gani? Mradi hatukuweza kujijibu kwa lolote. Ilipofika saa sita na nusu mchana, tuliletewa wali wa pilau nzuri na baada ya kumaliza kula, tulichukuliwa mpaka kwenye ofisi moja na huko tulitilishwa vidole (finger prints) na baada ya hapo, tulitiwa katika gari kubwa la polisi na tulipelekwa moja kwa moja mpaka kwenye kiwanja cha ndege za kijeshi.


Tulipofika kiwanjani, tulipokelewa na maofisa wawili waliyokuwa hawakuvaa nguo za kiaskari na baada ya kukaa hapo kwa muda mchache, tulitiwa katika ndege ya kijeshi ya aina ya "caribou", tukifuatanishwa na askari watatu wa polisi wote wakiwa wamechukua bastola mikononi mwao. Ndege iliruka na baada ya kiasi cha nusu saa, tuliteremka kiwanja cha ndege cha Zanzibar. Hapo, tulipokewa na askari wa magereza na tulitiwa katika gari la magereza na kupelekwa Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu.


Tulipofika gerezani, tulisachiwa kisha tuliandikwa majina yetu na baada ya hapo, tulikutana na Mkuu wa Magereza, Bwana Adam Taib naye alituambia kama hivi: "Ndugu zangu, mimi nimeambiwa nikopokeeni na nikuwekeni mpaka watapo kuja wenyewe wakubwa. Sijui lolote baada ya hapo. Kwahivyo, msiniulize lolote. Ninalo kuombeni ni kuwa mkae kwa salama mpaka mtapokutana na wenyewe, mtaweza kujua kila jambo"....


MAHABUSI WADHULUMIWA WA MWALIMU NYERERE Maalim Harun Ustadh Maalim Mohammed Mattar Seyyid Hassan Sheikh Seyyid Mohammed Adnan Mzee Mohammed Mbaba AhmedRashad Ali Hashim Haji Abdalla Seyyid Hashim Abdalla Baharun AbdulLatif Binbrek Mohammed Shioni Seyyid Mohammed Mattar Mohammed Ali Abbas Ali Abdalla (Admeri) Ali Jaffer Ali Khalifa Miskiry Ali Manara (Mtu wa Tanganyika) Aman Thani Fairooz Baada ya kumaliza kutukhutubia, Mkuu wa Magereza, aliondoka na sisi kila mmoja alipewa kirago chake pamoja na shuka mbili na kopo la kunywiya maji na ndio hilo hilo la kutumia kwa kujisafishia baada ya kwenda haja kubwa na ndogo. Tulipomalizika sote kupewa vitu hivyo, tuliongozwa mpaka kwenye vyumba vya kulala mahabusi. Siku ya pili, waliletwa wenzetu wawili wengine, mmoja alikuwa mwanamke, Bibi Mbarawa Bakari, yeye alipelekwa katika upande wa mahabusi wa kike na mwengine alikuwa Seyyid Harun Abdalla Baharun, yeye aliletwa upande wetu. Sote kwa jumla tukawa watu 19, mmoja mwanamke na 18 wanaume. Hawa wenzetu wawili, Bibi Mbarawa na Seyyid Harun wao walikamatwa hapo hapo Zanzibar...


Baada ya kuuliwa Karume, April 7, 1972 na kutawalishwa AlHaj Aboud Jumbe, wananchi hao wadhulumiwa, wote walichukuliwa kutoka magerezani na kwenda kuuliwa kwa kupigwa marisasi siku moja. Baada ya kuuliwa, wote walitumbukizwa katika shimo moja. Yale yaliyofanyika hivi karibuni huko Ruwanda si ajabu kuwa wameyaiga kwa yaliofanyika Zanzibar. Kuiga maovu ni rahisi! Baadhi ya hao maofisa waliokubali kusema uwongo kuwazulia ndugu zao wakati huo, hivi sasa baada ya kuwa na wao yeshawafika ya kuwafika kwa matokeo ya kuuliwa Mzee Karume, ati ndio wanasema kwa sauti za majuto na za kusikitika kuwa, "Yale yote tulioyasema siku ile mbele ya mkutano ule yalikuwa ni maneno ya kupangiwa na wakubwa wetu tuyaseme, kwa hakika yote yalikuwa ni maneno ya uwongo"!! Hao ndio "progressives" wetu, wapenda maendeleo.


Wametumiliwa kuivamia Serikali ya halali iliyochaguliwa na wananchi kwa uchaguzi wa kidemokrasi wa "One Man One Vote". "Progressives" hao hao ndio waliotumiliwa kwa maslahi ya nafsi zao kwa kusema uwongo uliopelekea kuuliwa kwa wananchi wenziwao bila ya kuwa na makosa yoyote.


"Progressives" hao hao ndio waliotumiliwa tena, mara hii katika mipango ya kumuuwa Karume!! Si ajabu kuwa hivi sasa "progressives" hao hao wamo mbioni wakitumiliwa, wakijuwa au bila ya kujuwa, katika mipango na njama za kuleta vurugu kupitia huu "Mfumo wa Vyama Vingi" tulioletewa, bali na katika mengineyo. Watu kama hawa khatari kuwanao. Daima yafaa kuepukwa.


ALIYONIZUNGUMZIYA TWALA Mimi na Bwana AbdulAziz Twala kabla ya kuwa watumwa wa Karume na Serikali yake ya Mavamizi katika magereza yake hatukupata kuwa na maingiliano ya namna yoyote....


Idrisa Majura ni kijana wa Kihaya amezaliwa Bukoba, Tanganyika bali amelelewa Zanzibar na Sheikh Said Komba Nyongo na amesoma katika skuli za Serikali za msingi Zanzibar. Kijana huyo baada ya Mavamizi aliondoka Zanzibar na kurejea kwao Bukoba. Alipokamatwa Othman Shariff na kurejeshwa Zanzibar, na yeye alikamatwa huko huko kwao Bukoba na aliletwa Zanzibar, walikuwa pamoja huko kwa "Ba Mkwe". Katika karasa za mbele, nitaeleza aliyotendewa yeye Idrisa wakati akiwa mfungwa wa Karume katika gereza la Langoni...


KARUME KUANZA KUMBADILIKIA TWALA Katika kuendelea na mazungumzo yetu baina yangu na AbdulAziz Twala, Twala aliniambia kuwa mwanzoni yeye alikuwa katika hao watoto wazuri mbele ya Mzee Karume, na ilikuwa kila alichokuwa akikitaka kwa Karume akikipata bila ya taabu yoyote. Mambo yalianza kuharibika wakati ujumbe wa Serikali ya Mavamizi ulipoalikwa Misri. Twala amesema kuwa alipokuwa akitengeneza kutoa matumizi ya safari (travelling allowances) kwa wajumbe wa safari hiyo, aliwacha kumtia katika orodha ya matumizi ya safari Bibi Fatma Karume kwa sababu Bibi Fatma alikuwa anachukuliwa na mumewe kwa matembezi tu, sio katika ujumbe rasmi. Mzee Karume, alipoona mkewe hakutengenezewa sehemu yake ya matumizi, alimuuliza Waziri wake wa Nchi kukhusu posho la mama Fatma Karume.


Twala alipigiwa simu na Waziri wa Nchi, AlHaj Aboud Jumbe na alimwambia, "Mbona umesahau kuleta posho la mama Fatma Karume?" Twala alimjibu, "Laa, sikusahau lakini nimeona kuwa yeye si katika wajumbe rasmi wa safari. Lakini, ikiwa unaona na yeye anastahiki, basi nitamtengenezea". Twala amesema haukupita muda baada ya mazungumzo hayo ila alipata simu nyengine kutoka kwa Katibu wa Waziri wa Nchi kumwambia kuwa, "Unaambiwa na Mzee basi usilete posho la mama Fatma. Yeye mwenyewe atampa kutoka mfukoni mwake". Twala amesema kutokana na jawabu hilo la Mzee, alihisi kuwa amesha mtonesha Mzee kidonda; na kweli ndivyo ilivyokuwa.


Kutoka wakati huo mambo yalianza kuharibika, alisema Twala. Ujumbe uliporejea Misri, Twala amesema kuwa kila alipokuwa akikutana na Mzee Karume alikuwa hampi mkabala mwema. Jambo jengine ameniambia Twala lililozidi kutimua mavumbi lilitokea wakati mmoja alipokuwa Mwalimu Nyerere amehudhuria kikao cha Baraza la Mavamizi. Katika kikao hicho, amesema Twala, Mwalimu alilaumu kukhusu namna zilivyotumiwa fedha za kigeni kwa kununulia vitu kwa wingi kama peremendi, tofi, chakileti, ubani wa kutafuna na vyenginevyo ambavyo havikuwa na umuhimu katika maisha ya binaadamu wakati yapo mambo mengi muhimu yanayohitajia fedha za kigeni.


Twala amesema kuwa Karume alivyomuona Mwalimu akilaumu kiasi hicho, alinigeukia na aliniambia, "Mheshimiwa Waziri wa Fedha, unasikia maneno hayo? Usijitumilie mapesa ovyo ovyo tu". Twala amesema, siku hiyo alishindwa kunyamaza kimya, alisema kujibu hayo, "Kweli mimi ndiye niliyempa amri Waziri wa Biashara na Viwanda, Sheikh Shaaban Soud Mponda aagizie vitu hivyo, lakini nimefanya hivyo, baada ya kupata amri kutoka katika ofisi yako ya kunitaka mimi nitowe idadi fulani ya fedha kwa kuagizia vitu hivyo kutoka Ujarumani ya Mashariki. Sasa mimi Mzee, kosa langu ni lipi hapo?" Twala ameniambia kuwa, alivyokuwa amesema hivyo, alimuona Karume amesawijika uso, na alikuwa akipuma kama n'gombe jike.


Mwalimu Nyerere alipoona hali haikuwa nzuri, alijaribu kuyageuza mazungumzo na kuleta maudhui nyengine. Mkutano ulipomalizika, Mwalimu Nyerere aliondoka kurejea DaresSalaam. Siku ya pili yake, amesema Twala, kiasi cha kuingia katika ofisi yake, alipata simu kutoka kwa Waziri wa Nchi ya kumwambia kuwa kutakuwepo na mkutano wa dharura katika Peoples' Palace na wote wahudhurie. Twala amesema kwa kupata khabari kama hizo tu basi nusra alikuwa atokwe na mkojo suruwalini! ...


KWANINI MWALIMU NYERERE ALIKATAA KUWAPELEKA ZANZIBAR WATUHUMIWA WA KESI YA UKHAINI? Alipouliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume, Wazanzibari wengi walikamatwa na kutiwa viziwizini vya Magereza ya Zanzibar na ya Tanzania Bara. Wazanzibari waliyotuhumiwa zaidi kwa mauwaji ya Karume, walikuwa ni hao wajiitao, "progressives" au makomredi.


Wao, "progressives" au makomredi. walibakishwa viziwizini kwa muda mkubwa baada ya Wazanzibari wengine kuachiliwa huru. Baada ya muda tokea kuwekwa humo viziwizini, Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar iliwafungulia mashitaka watuhumiwa wote waliyokuwepo Zanzibar na waliyokuwepo Bara.

Lakini, inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alikataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Tanzania Bara. Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, walipoona Mwalimu amekataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo Bara kuhudhuria katika mashitaka yao, waliendelea na mashitaka na waliwapeleka Mahakamani watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Zanzibar. Mashitaka yalichukuwa muda mkubwa, mwisho Mahakama yalitoa uwamuzi wake juu ya watuhumiwa wote wa Zanzibar na wa Bara (ambao walihukumiwa bila ya wenyewe kuhudhuria Mahakamani).


Hukumu iliyotolewa na Mahakama hayo ilikuwa, wengine wapewe adabu ya vifo na wengine wafungwe gerezani kwa vifungo vya muda mbali mbali. Miongoni mwa waliohukumiwa vifo ni huyo mkuu wao "progressives", Abdulrahman Babu.



Sisemi kuwa Mahakama hayo na Mahakimu hao waliyoendesha mashitaka hayo walikuwa ni wenye kufaa au wenye ujuzi uliyokhusika na sheria, hashaa! Sote tukijuwa kuwa Mahakimu hao hawakuwa na ujuzi wowote juu ya mambo ya sheria, bali tu walikuwa na ujuzi wa kuuza samaki wakavu na kushona kofia za viuwa. Lakini, kwa vile hao wahukumiwa, wao wenyewe ni washiriki katika kuleta hiyo serikali ya mavamizi, na kwa kiasi fulani walikhusika na nyendo za seikali hiyo ambayo matokeo yake ndiyo kuwepo kwa Mahakama kama hayo na Mahakimu kama hao, kwahivyo, washitakiwa hao kuhukumiwa na Mahakimu kama hao itakuwa wanafaidika kwa matunda waliyoyapanda kwa mikono yao wenyewe. Ama wananchi wanyonge waliopata mateso kutokana na hukumu za mahakama hizo, wao ni waliyodhulumiwa .....


Kwa hakika mipango na matokeo yaliyopitishwa mpaka kuuliwa kwa Mzee Karume yana kitandawili kikubwa. Kama si hivyo, Mwalimu asingekataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo katika Magereza ya Tanzania Bara na wasingeachiliwa huru baada ya muda mdogo tokea kuhukumiwa. Mwalimu aliona ndivyo kuwapeleka Zanzibar Othman Shariff, Abdalla Kassim Hanga, Idrisa Abdalla Majura, Bibi Titi Mohammed, Kamaliza, Chipaka, (hao watatu wa mwisho ni Watanganyika) bila ya kujuulikana makosa yao au kuhukumiwa na yoyote. Nyerere huyo huyo akiwa ni mwalimu wa mipango aliona ni busara kutowapeleka hao wajiitao, "progressives" waliyokuwemo ndani ya mikono yake na waliyokuwa wakitakiwa na Serikali yake ya Mavamizi ya Zanzibar kwa kumuuwa aliiyekuwa Makamo Raisi wake Makamo Raisi wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jee, haya ni bure bure tu! Haiwezi kuwa! Lazima lipo, lakini ikiwa si leo, kesho na ikiwa si kesho, keshokutwa; bali ikiwa hata si mwaka huu, miaka ijayo. Lakini lazima siku moja ukweli utajichomoza. Vyovyote vile ilivyo lakini, Karume alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Afike kuuliwa, na waliyo tuhumiwa kuwa ndio wauaji wamekamatwa na kuwepo katika mikono ya Serikali, kisha wakahukumiwa na pakatolewa hukumu juu ya washitakiwa hao, na baada ya hukumu wakaachiliwa huru kama kwamba hapana lililotendeka! Oh!, Kweli hayo?!! Ni hakika ingelikuwa kauliwa mwanachama tu wa ASP basi mtuhumiwa huyo angelikiona cha mtema kuni, leo kauliwa Raisi wa Nchi ndio imekuwa si chochote si lolote! Si hayo tu yenye kuwasangaza wananchi wa Zanzibar bali yapo na mengineyo. Lishangazalo zaidi ni kuwa huyo aliyetajwa na ikakubalika kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakiendeshwa kuwa ndiye aliyekuwa mwongozi wa hayo machafuko yaliyotendeka nchini (Zanzibar) katika taarikh 7 April, 1972 na kumalizikia kwa kuuawa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar awe ameruhusiwa bila ya viziwizi vyovyote kuondoka na kurejea katika nchi wakati wowote aupendao. Si hayo tu, bali Serikali hiyo hiyo iliyomuhukumu kifo, ikawa inamualika kushiriki katika mikutano yenye kufanywa katika nchi, akiingia na kutoka maridhawa!!...


SIRI HII NI KUBWA SANA!! Leo ni miaka 30 tokea kufanyika kwa hayo yenye kuitwa, "Mapinduzi" na mpaka hii leo baadhi ya waongozi wa Serikali ya Hizbu na ZPPP, hawaruhusiwi hata kuikanyaga nchi yao, Zanzibar. Na ilhali wao hawakumuuwa yoyote, licha kumuuwa Raisi wa Nchi, wala hawakunya'ganya mali ya mtu wala hawakuiba au kupoteza mali ya Nchi, hawakufanya kosa lolote dhidi ya sheria ya nchi. Ilivyo khasa ni wao ndio waliodhulumiwa tokea kuvamiwa kwa Serikali, kuuliwa watu, kufungwa magerezani, kuteswa na kubidi kutoka nchini. Isitoshe, kwa kuchukuliwa mali zao, tokea majumba mpaka mashamba ambayo wameyachuma kwa jasho lao au kwa majasho ya wazee wao. Ingalikuwa yuko mmoja katika wao aliyekuwa na kosa lolote basi Serikali ya Mavamizi ingaliwapeleka Mahakamani, lakini hakuwaona na kosa lolote, kwa hivyo waliamua kuwafanya "wafungwa wa kisiasa"na kuwaweka magerezani kwa muda wa miaka 10 bila ya kuhukumiwa. Lakini waliothibiti mahakamani kuwa walikhusika na kuuliwa kwa Rais wa Nchi na Kiongozi wa Chama cha AfroShirazi hawakuguswa, bali walitunzwa! Jee, tuseme wanaogopwa, au wanayajuwa yale yenye kuogopwa yakisemwa ....


NILITAKIWA NITOKE NCHINI Mimi, muandishi wa kijitabu hiki, baada ya muda wamiaka 20 toka kutoka nchini naliomba niruhusiwe kuizuru nchi yangu. Nchi nilyozaliwa mimi na wamezaliwa wazee wangu wawili. Kwa shida niliruhusiwa kwa kupewa muda wa miezi mitatu kukaa katika nchi! Kwa kupewa ruhusa hiyo, taarikhi 9 Januari, 1992 nilizuru Zanzibar na 18 Februari, 1992 nilirejea katika masikani yangu, Dubai. Baada ya miezi sita, yaani taarikh 9 Agosti, mwaka huo huo wa 1992, nilikwenda tena Zanzibar na wakati huo nilidhamiria kukaa kwa muda wa miezi mitatu kwa kuendelea na mipango ya miradi yangu ya ukulima na ufugaji niliyo kusudia kuifanya.


Niliambiwa nilipofika kiwanja cha ndege siku nilioingia nchini, kuwa ikiwa nitataka kukaa nchini kwa muda zaidi, nenda Idara ya Uhamiaji nikaombe kuongezewa muda. Baada ya mwezi mmoja, nilikwenda huko Idara ya Uhamiaji kutaka niongezwe muda wa kukaa. Nilipofika, walinizuilia paspoti yangu na kisha nikaambiwa nikaonane na "boss". Nilipelekwa mpaka kwa huyo "boss" anaeitwa Ali Daud. "boss" baada ya kunitilia mijiti hii na hii, aliniambia, "Njoo keshokutwa kwani Boss leo hayupo kenda mkutanoni DaresSalaam". Nilimuuliza huyu boss, "Kwani pana jambo gani?" Alinijibu, "boss anataka kukuona". Nilinyamaza na niliondoka. Ilipofika hiyo keshokutwa niliyoambiwa, nilifika Idara ya Uhamiaji na safari hii nilipelekwa kwa "boss" mwengine, Himid Yusuf Himid. Huyu ni kijana mdogo, Mzee wake tulikuwa tukifahamiana sana. Juu yakuwa tulikuwa na tafauti zetu kukhusu msimamo wa fikra za kisiasa, lakini tulikuwa tukihishimiana na tukisikilizana. Nilipofika ofisi ya kijana huyo Himid, aliniambia, "Mambo yako bado hayajamalizika, ikiwa utaweza, kusubiri hapo nje au unaweza kwenda na kurejea kiasi cha saa sita za mchana". Niliporejea mnamo saa sita, aliniuliza, "Ndege ya Arabuni inaondoka hapa siku gani?" Nilimwambia, "Inategemea ndege gani uitakayo, kwani zipo ndege mbili zinazo kwenda Arabuni, na kila moja inayo siku yake na wakati wake". Aliniambia, "Hiyo unayo safiria wewe". Nilimwambia, "Inaondoka hapa kuelekea Dubai kila siku ya Jumaapili asubuhi saa tatu". Baada ya kumjibu hivyo, aliniambia, "Nifuate!" Nilimfuata mpaka ofisi nyengine na huko alimpa kijana aliyekuwa akifanyakazi sehemu hiyo pasipoti yangu na alimwambia, "Mpe muda wa kukaa Zanzibar mpaka Jumaapili tarehe 3 9 92 na muuandikie, 'Final Extension'." Nilimuuliza huyo kijana Himid, "Kwa nini yakawa yote haya kwani nimefanya jambo gani katika nchi hata ikawa nanyimwa kupewa muda zaidi, na kufika hadi kuondolewa katika nchi?" Jawabu aliyonijibu na huku anakwenda zake, "Huo ndio uwamuzi uliyofikiwa". Nilinyamaza na nilingojea pasipoti yangu nilipoipata niliondoka na kwenda kutenegeneza safari. Siku hiyo ilikuwa siku ya Ijumaa taarikhi 1 8 92. Utaona kuwa nimepewa muda wa kasoro kuliko saa 36 niondoke katika nchi yangu niliyokuwa nimezaliwa! Bila ya kuambiwa nimekosa nini ....

Baada ya kurejea kwangu Dubai nilianza kuyazingatiya haya niliofanyiwa, na nalikata shauri kuwaandikia wakuu wa Serikali ya Zanzibar khasa kwa vile wao wenyewe ndio walionipa ruhusu kuizuru Zanzibar. Kwa hakika sikuweza kupata jawabu lolote kwa maandishi ila nilikuwa nikisikia maneno tu, kuwa wakuu wa serikali wanasema kuwa wao hawajui lolote nililolitenda wakati nilipokuwepo nchini lakini watazidi kuchungua. Mimi kwa upande wangu nilikuwa nakwenda mbio katika kujiombea ili nipate tena kuingia Zanzibar bila ya taabu na shida yoyote. Nawashukuru shemegi zangu na baadhi ya wananchi wenzangu kwa shida walizozichukuwa za kupanda na kushuka kunitakia ruhusa, mpaka mwisho Mungu akayafungua na kukubaliwa kuingia Zanzibar tena. Taarikhi 24 Julai, 1994 nilifika Zanzibar na baada ya kukaa kwa muda wa mwezi mmoja na siku chache niliondoka mnamo taarikhi 27 Agosti, 1994 kwa kurejea kwenye masikani yangu Dubai. Nashukuru kuwa safari hii nimeingia katika nchi kwa salama na nimeachiwa kukaa mpaka nimetoka kwa salama na Inshaallah itaendelea kuwa salama daima dawamu....



NAMNA NILIVYOONDOKA KUUKIMBIA WATTANI WANGU Tokea nilipokuwepo kifungoni, nilikuwa nikipanga njia za kuondoka katika Wattani wangu, Zanzibar, nikijaaliwa kuachiliwa huru kwa salama. Baada ya kutolewa gerezani Januari 12, 1972, nilianza kutafuta pasipoti lakini nilikuwa nikihangaishwa huku na huku, mwisho niliambiwa kwa njia za kiundugu zisizokuwa rasmi kuwa, "Haitokuwa rahisi kwako kupata pasipoti kwa wakati huu". Nilipoambiwa hivyo, nilianza kutupa nyavu kila kipembe. Ilipofika taarikhi 7 Mei, 1972 (mwezi mmoja tokea kuuliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar) nilimuomba Mwenyezi Mungu nikifuatana na wenzangu wawili, Sheikh Mohammed Ali Abbas na mwanawe Ali Mohammed Ali Abbas.


Katika wakati huo, yaani baada ya kuuliwa Karume, usafiri wa namna yoyote ulikuwa na shida kubwa bali hata hivyo tulimuomba Mwenyezi Mungu. Ilipofika saa tatu za usiku wa taarikhi hiyo 7 Mei, tuliondoka. Kulipo pambazuka asubuhi yake, tuliingia katika moja ya bandari za kivuvi ziliopo pwani pwani ya sehemu ya bahari ya Tanganyika.

Tulisali alfajiri katika msikiti wa kiambo hicho, kisha tulifungua vinywa kwa chai na maandazi katika kijikahawa kidogo kilichokuwepo hapo. Tulingojea "bas" la kuendea Tanga kwa kupitia Pangani. Kiasi cha saa mbili za asubuhi "bas" lilifika na tuliingia. Jumla yetu tulikuwa watu wane. Sisi watatu na kijana mmoja tuliyepewa na wazee atufikishe Tanga. Tulipoingia katika "bas", tulimkuta kijana wa kiZanzibari kafatana na kijana wa kiTanganyika. Kijana huyu (wa kiTanganyika) alikuwa amevaa nguo za Tanu Youth League. Huyo kijana wa kiZanzibari tulijuana tulipokuwa gerezani, Langoni. Yeye alikuwa amefungwa kwa 'kumnajisi' n'gombe. Alitulahiki kwa uzuri na tulikaa naye mpaka kufika Pangani. Tulipofika Pangani tulipokuwa tunakula chakula cha mchana, huyo kijana wa kiZanzibari alitujia kwenye meza yetu na alitwambia, "Yule mwenzangu niliyekaa naye, amewekwa sehemu hizi kuchungua watu wanaoingia kwa magendo na wenye kusafirisha karafuu kwa magendo. Alinambia kuwa ana wasiwasi juu yenu na tulipofika hapa, alitaka kukupelekeni kwenye kituo cha polisi cha hapa Pangani, mimi nimemuomba asifanye hivyo. Lakini amesema kuwa anataka kuona vitambulisho vyenu, basi nipeni nimpelekee. Tulimwambia kuwa sisi hatuna vitambulisho vyovyote hatukuona kuwa ni muhimu kuchukuwa vitambulisho wakati tunasafiri katika nchi moja....


Lakini, tulipofanikiwa kufika Kenya, kwanza tulijisalimisha kwa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa upande wa wakimbizi wa kisiasa, Sheikh Salim Muhasham. Sheikh Salim alitupokea uzuri na la mwanzo alitutengezea warka wa safari wa kutokea nchini (one way travelling document) kutoka Idara ya Uhamiaji ya Kenya, pia alikuwa akitusaidia kwa kila yaliyokuwa yanahitajia. Kwa kupata warka huo, ukaaji wetu wa hapo Kenya ulikuwa wa kihalali.

Baada ya muda wa miezi mine tokea kufika hapo Mombasa, Mwenyezi Mungu alinijaalia kutengenekewa na mambo yangu na kuweza kuondoka Kenya mwanzo kuelekea Dubai kabla ya wenzangu wawili. (tulikubaliana kuwa mimi nitangulie). Niliondoka Kenya taarikhi 29 Septemba, 1972 kwa kupata msaada wa safari tokea tikti ya ndege mpaka pesa kidogo za matumizi kutoka katika mfuko wa Umoja wa Mataifa unao shughulikia wakimbizi wa kisiasa (UNHCR). Kiasi cha saa mbili za usiku wa taarikh 30 Septemba, 1972 nilifika Dubai ....


Baada ya mimi kutoroka katika nchi yangu, ahli zangu waliwekewa vikwazo vikubwa vya kuwazuwia kuondoka kwa njia yoyote. Wakati ulipofika, Mwenyezi Mungu aliteremsha Rehema Zake. Kama msemo wa nzi, "Ukiujuwa huu, naujuwa huu". Taarikhi 28 Disemba, 1976 ahli zangu wote tokea mke wangu mpaka watoto wangu walifika Dubai kwa kupata msaada wa Umoja wa Mataifa (UNHCR). Namshukuru Mwenyezi Mungu, hivi sasa tunaishi pamoja. Watatu kati ya watoto wangu wameshatuletea vijukuu vya kucheza nao. Namuomba Mwenyezi Mungu awakuze, kwa raha na furaha na atuletee na wengine kwa wao, na kwa waliyokuwa bado hawajajaaliwa kutuletea....


Hapa nimefikilia kikomo cha kuyaeleza niliyokuwa yamenikaa moyoni kuwaeleza wananchi wenzangu. Lakini khasa wale chipukizi zetu ambao kwa kutokuujuwa ukweli wa yaliotokea katika nchi yao, tangu kuanza kwa harakati za siasa na mpaka kufikishiwa tuliyofikishiwa kwa hayo yenye kuitwa mapinduzi, wakidanganywa kwa kuambiwa na kwa kusomeshwa uwongo mwingi sana. Kwahivyo, huu ndio ukweli wa mambo yalivyokuwa kwa kiasi nilichojaaliwa kukijuwa na kujaaliwa kukielezea. Kama nilivyotangulia kusema, natumai watatokea wengine baada ya kukisoma kijitabu hiki, wataingiwa na mori na kuhisi waajib wao wa kuyaandika yale wayajuwayo na ambayo sikujaaliwa kuyaandika, amma kwa kutokuyajuwa au kwa kuyasahau. Kukamilika ni Kwake Subhanahu Wataala.

Soma kwa urefu mwandishi na msimulizi Mzee Aman Thani Fairooz source : Ukweli Ni Huu, (Kuusuta Uwongo) - Aman Thani Fairooz - PDFCOFFEE.COM
 
"Humud acha utani Humud hio ni bunduki imeshika, Humud msalie Mtume una nini Leo? "

"Sitanii mie Leo ndio mwisho wako Karume"

Hamna watu watano kuvamia wala nini, ilikuwa ni kazi ya Humud mwenyewe

Na alikuwa mtu wake wa karibu
 
Mmejuaje kazi yake na cheo chake, kwamba ni Koplo, kama hamjui ni nani mpaka leo ?

Na ni tume gani au mahakama gani ilichunguza mauaji na kutoa hizo nadharia za kifo, vyanzo vyako ni nini?

Na Mungu amlaze pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani?

Karume alimuua baba yake Umudi aliyekuja kulipiza kisasi, Karume alimuua Makamu wa Rais Kassim Hanga, Karume alimuua balozi wa Tanzania Marekani na Waziri wa Elimu Othman Sharrif, na wengine leke leke walitupwa baharini wamefungwa mgongoni mizigo ya mawe, waliteswa na vikosi katili vya bwana Mandera kwenye jela ya Bamkwe...mikono ya Karume imejaa damu.....

Tumedanganywa mashuleni, tulikuwa watoto, na ukubwani pia mtudanganye ? Hell freaking no. Alazwe pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani ? Rote in hell.
Umenikumbusha Kwa ba mkwe na 'Kumbakumba' kwenye kitabu cha Haini
 
Mmejuaje kazi yake na cheo chake, kwamba ni Koplo, kama hamjui ni nani mpaka leo?

Na ni tume gani au mahakama gani ilichunguza mauaji na kutoa hizo nadharia za kifo, vyanzo vyako ni nini?

Na Mungu amlaze pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani?

Karume alimuua baba yake Umudi aliyekuja kulipiza kisasi, Karume alimuua Makamu wa Rais Kassim Hanga, Karume alimuua balozi wa Tanzania Marekani na Waziri wa Elimu Othman Sharrif, na wengine leke leke walitupwa baharini wamefungwa mgongoni mizigo ya mawe, waliteswa na vikosi katili vya bwana Mandera kwenye jela ya Bamkwe mikono ya Karume imejaa damu.

Tumedanganywa mashuleni, tulikuwa watoto, na ukubwani pia mtudanganye? Hell freaking no. Alazwe pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani? Go burn in hell.
Hii mkuu nilisoma katika makala ya Joseph mihangwa kwamba kilikuwa kifo cha kisasi na ndio maana alikufa kama hakukuwa na walinzi kwani walifahamiana sana na muuaji. Alimsomesha na almchukulia kama mwanae kumbe jamaa alishaapaga kulipa kisasi.
 
Hii mkuu nilisoma katika makala ya Joseph mihangwa kwamba kilikuwa kifo cha kisasi na ndio maana alikufa kama hakukuwa na walinzi kwani walifahamiana sana na muuaji. Alimsomesha na almchukulia kama mwanae kumbe jamaa alishaapaga kulipa kisasi.
Ni kweli kabisa, Karume na Umudi walikuwa wanajuana, I mean, Wazanzibar wote wanajuana, nusu yao ni ma cousins anyhow. Kwa saab ka Zanzibar kenyewe ni kadogo kuliko Mbagala Kizuiani.

Karume was a blood soaked, unrestrained dictator. But one thing I credit Karume for, ni alikuwa hafagilii wageni, hakutaka Mwarabu, Mhindi, Msomali, ajitenge na asujudiwe kama ilivyo huku Bara.

Kwa hiyo akafanya social engineering ya kuzaliana na Waarabu ili tuchanganyike na kumvuta chini Mwarabu, iwe ni kwa kuwaoa au kwa kuwa repu. Na yeye mwenyewe akachukua Mwarabu mmoja. Ndio mana mpaka leo Mwarabu wa Zanzibar yuko sawa na Mnyamwezi wa Zanzibar, kwa utajiri na umaskini. Na huwezi kujua nani Mwarabu nani chotara, including the Mwinyi's and the Samia's of the world.
 
Mmejuaje kazi yake na cheo chake, kwamba ni Koplo, kama hamjui ni nani mpaka leo?

Na ni tume gani au mahakama gani ilichunguza mauaji na kutoa hizo nadharia za kifo, vyanzo vyako ni nini?

Na Mungu amlaze pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani?

Karume alimuua baba yake Umudi aliyekuja kulipiza kisasi, Karume alimuua Makamu wa Rais Kassim Hanga, Karume alimuua balozi wa Tanzania Marekani na Waziri wa Elimu Othman Sharrif, na wengine leke leke walitupwa baharini wamefungwa mgongoni mizigo ya mawe, waliteswa na vikosi katili vya bwana Mandera kwenye jela ya Bamkwe mikono ya Karume imejaa damu.

Tumedanganywa mashuleni, tulikuwa watoto, na ukubwani pia mtudanganye? Hell freaking no. Alazwe pema peponi mpendwa wetu Abeid Karume, mpendwa wetu wewe na nani? Go burn in hell.
Sultan akihojiwa alijisikaje baada ya Karume kuuwawa? Anasema"I was delighted to hear that the dictator is gone"
 
Mambo ya ki-Magu ? Magu ni malaika wa bwana mbele ya Karume...

Magu kampoteza Ben Saa Nane, inasemwa, hatuna hakika

Karume kawapoteza mawaziri wazi wazi... Mabalozi wa Nyerere... Karume kampoteza Vice President! Kassim Hanga, who was he, Vice President no less...

baba Humudi, a true blue Zanzibar revolutionary, aliwekwa kwenye gunia, gunia likaburuzwa kwenye kokoto huku linatandikwa fimbo, wakamtoa roho. Kisa? Alihoji mikopo ya Karume na deni la Taifa, for all we can think of. Mtoto kaja kutafuta haki kwa njia anazozijua yeye, halafu wanatuambia Karume aliuliwa na wapinga mapinduzi, get the hell outta here...
Mkuu naomba tufafanulie kidogo jinsi hao viongozi walivyopotea nasi tupate faida
 
Back
Top Bottom