TUJIULIZE: Tumetoka wapi, tupo wapi, na tunakwenda wapi

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
Nalazimika kuyaandika haya kutokana na hali ya sintofahamu inayoendelea kutawala miongoni mwa watanzania wengi, juu ya demokrasia ya Nchi yetu Mama Tanzania.

TANGAZO LA SERIKALI NA.215 La Tarehe 12/10/2007, Sheria ya Vyama vya Siasa (SURA YA 258), KANUNI (Zilizotungwa Chini ya fungu la 22(h)) KANUNI ZA MAADILI ZA VYAMA VYA SIASA ZA MWAKA 2007 (Na zilianza kutumika mara tu baada ya kutangazwa kwenye gazeti la Serikali).

Kanuni hizi zimetafsiri Chama cha Siasa kuwa ni: "Chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kwa mujibu wa Sheria"

SEHEMU YA PILI ya Kanuni Hizi Inahusu HAKI ZA CHAMA (Haki za vyama vya siasa) ambazo ni kama ifuatavyo:

4-(1)
(a) Kutoa elimu ya Uraia na elimu ya Uchaguzi kwa wananchi kwa kufuata Sheria na kanuni za nchi;
(b) Kutoa maoni ya kisiasa kadri itakavyoona inafaa ili kutekeleza sera zake, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar;
(c) Kujadili na kushindanisha Sera zake na zile za Chama cha siasa kingine kwa lengo la kutaka kukubalika na wananchi;
(d) Kuwa na Uhuru wa kutafuta wanachama na kama ni wakati wa kampeni basi kuwe na uhuru wa kutafuta kuungwa mkono na wapiga kura; na
(e) Kila chama cha siasa kitakuwa na Haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Sheria ya vyama vya siasa.
5-(2)
Kwa kuzingatia Sheria, kila chama cha siasa kitakuwa na uhuru wa kushirikiana na chama cha siasa kingine kwa nia njema kwaajili ya kupanga vikao, mikutano ya hadhara kwa pamoja au maandamano kwa wakati mmoja kama kwamba mambo hayo yamefanywa na chama cha siasa kimoja au bila kuvunja sheria za nchi.

Tangazo hili lilisainiwa na Waziri mkuu mstaafu Mhe. Edward Ngoyai Lowassa Tarehe 1 Oktoba, 2007.

KATIBA ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 3.
(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
(2) Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.

Sheria Na.5 ya Mwaka 1992 ya Vyama vya siasa inaweka bayana kuwa; "Chama cha Siasa" maana yake ni chama cha Siasa kilichoandikishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Siasa, ya Mwaka 1992;

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mapema kabisa, mara tu baada ya kuundwa kwa Sheria ya vyama vya siasa nchini mwaka 1993, ambapo bado vyama vya siasa vilikuwa vichanga na wanasiasa walikuwa wachache, na katika wachache hao wengi walikuwa CCM, aliandika kitabu kilichoitwa 'Uongozi na Hatima ya Tanzania', Mwalimu alionesha mtazamo chanya juu ya demokrasia nchini, na wala hakufumbia macho uozo aliouona ndani ya Chama cha mapinduzi CCM, na alionesha wazi dhamira yake juu ya uwepo wa vyama vya upinzani, na alitamani vije kuongoza nchi, badala ya CCM.

Nitanukuu baadhi ya maneno yake;

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwl. Julius K. Nyerere aliendelea kusema kuwa;

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni dhahiri, Mwalimu alikuwa muwazi na mwenye kulipenda Taifa kuliko kujinasibu na Chama chake alichokiasisi yeye Mwenyewe, Chama cha mapinduzi CCM. Nakubaliana na Mwalimu kuwa Vyama vya siasa wakati huo vilikuwa bado ni vichanga, tofauti na sasa ambapo vyama vya siasa vimekua, vimeungwa mkono na wananchi wengi, na vina hazina ya viongozi wazuri na wenye kuaminika... Hivyo, bila kumung'unya maneno, kama Mwalimu Nyerere angelikuwepo leo, asingekiunga mkono tena Chama cha mapinduzi, kwani alionesha kuipenda sana nchi kuliko Chama chake.

Watanzania, wengi mwayafahamu yanayoendelea kujiri kwenye utando huu wa kisiasa nchini, na mmezisikia kauli za Rais Magufuli juu ya vyama vya siasa nchini, ikiwa ni pamoja na kuvitukana kwa kuviita ni vya hovyo hovyo alipokuwa Singida kwenye maadhimisho ya Miaka 39 ya CCM tarehe 6 mwezi februari, na kutamka kuwa havita tawala, pia hivi karibuni kutamka wazi kuwa hakuna kufanya siasa kwa kipindi chote cha miaka mitano, mpaka 2020. Na zaidi, mmeshuhudia Polisi wakizuia shughuli za kisiasa kufanyika nchini, kukwamisha mikutano na vikao vya ndani vya vyama vya siasa, mpaka kuzuia mahafali ya vijana wa vyuo vikuu.

TUJIULIZE: TUMETOKA WAPI, TUPO WAPI, NA TUNAKWENDA WAPI.

Wako katika demokrasia na maendeleo
Goodluckies Good
 
Back
Top Bottom