Tujikumbushe: Vijana na uchaguzi

Mar 2, 2012
57
17
Takwimu.jpg

Wakati zikiwa zimebaki siku tano (5) kuelekea siku ya kupiga kura katika uchaguzi Mkuu mwaka huu (25 Oktoba 2015) nachukua nafasi hii kuwakumbusha Vijana wenzangu kuwa sisi (Vijana) ndio kundi kubwa katika jamii yetu na kundi linaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi zenye uhitaji wa mikakati makini na shirikishi, nia thabiti ya Viongozi na ushiriki madhubuti wa vijana wenyewe kuweza kuzitatua changamoto zinazotukabili.

Moja kati ya namna ambayo vijana wa Tanzania tunaweza kushiriki kutengeneza taswira ya maendeleo yetu na mustakabali wa taifa kwa ujumla ni kushiriki mchakato wa kisiasa uliopo mbele yetu wa Uchaguzi Mkuu.

Vijana tuna nafasi ya kipekee kushiriki katika ujenzi wa demokrasia kwa namna ileile tuliyojitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, namna tulivyojitokeza kuomba ridhaa za uwakilishi wa nafasi mbalimbali na ngazi za maamuzi wakati wa kutafuta uwakilishi kupitia vyama na itikadi zetu mbalimbali za siasa.Vivyo hivyo tujitokeze kupiga kura siku ya Uchaguzi.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Takwimu (NBS) na ripoti mbalimbali zinaonyesha idadi ya wastani wa vijana Nchini ni asilimia sitini na tano (65%) ya idadi ya watanzania wote, hivyo basi mchakato huu wa kisiasa kwa kiasi kikubwa unawahusu Vijana na unawapasa kushiriki kwa maendeleo endelevu.

Kwa maana hiyo hakuna jambo lolote pasipo sisi (vijana), hivyo kwa vijana mchakato huu wa uchaguzi ni muhimu sana katika kuhakikisha msingi bora wa ustawi na maendeleo yetu.

Licha ya ushiriki usioridhisha wa watanzania katika michakato ya kisiasa, takwimu zinaonyesha vijana ndilo kundi kubwa la watu ambao wamekua hawajitokezi vya kutosha kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, kuomba ridhaa za kugombea nafasi za kisiasa katika vyombo vya maamuzi na pengine kupiga kura, ikiwepo ukosefu wa elimu ya uraia na demokrasia, kukithiri kwa rushwa, kutokua na imani na siasa na wanasiasa, hali ngumu ya maisha na ukosefu wa Ajira, kususia Uchaguzi na vitisho, fujo na vurugu katika uchaguzi ambazo vijana hunyooshewa vidole kwa vurugu hizo.

Kipindi cha Uchaguzi Mkuu ndiyo nafasi pekee na fursa adhimu kwa Vijana kufanya maamuzi dhidi yao na Taifa. Kupima na kutathmini Viongozi wanaowatumikia au kuwaomba ridhaa katika nafasi mbalimbali za uwakilishi kwa kusikiliza kwa makini na kupima sera zao za kuongoza au kuratibu juhudi za maendeleo katika jamii.

Changamoto zetu Vijana zimekua zikipigiwa chapuo na baadhi ya watangaza nia wakiwa na malengo ya kujihakikishia kura au kuungwa mkono na kundi la Vijana. Wasiwasi wangu ni kwa namna gani sehemu ya changamoto hizo zimekwisha tatuliwa hapo awali na kufanikiwa kwa kiasi gani.Tunahitaji kulitafakari na kulitathimini sana suala hili ili kuweza kufanya maamuzi sahihi na kuchagua Viongozi madhubuti watakaoongoza gurudumu la mabadiliko chanya na yenye tija kwa sisi (Vijana) na kuliwezesha Taifa letu kusonga mbele pia.

Uchaguzi Mkuu unaambatana na visa na mikasa mbalimbali ambayo inaweza kuondoa maana nzima ya zoezi hilo kama, rushwa, maneno ya kashfa na uchochezi yanayoweza kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini: Pasi na changamoto zote hizo, Vijana hatuna budi kushiriki zoezi hili kwa uadilifu na kusimamia amani kama tunu ya Taifa letu. Madhara ya ukosefu wa amani Nchini yatakuwa makubwa mno kwetu Vijana na watoto ambao tutaishi nayo kwa muda mrefu kuliko makundi mengine.

Namalizia kwa kunukuu msemo wa kiswahili usemao "Asiyekuwepo na lake halipo" nikiwa na maana kuwa vijana tunapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu; kinyume chake itakuwa kuwa endapo ushiriki wetu usipoonekana na maslahi yetu pia yatakanyagwa.

Imeandaliwa na S.Khalfan,A.Lukanza na G.Mwakijungu.
 
kwa takwimu tu, atakaye kuwa amewekeza kwa vijana na wanawake atakuwa na mteremko kama wote wamemuelewa na kuamua kumpigia kura. Ila sio tuwatumie kuingia ikulu na kuwadump baada ya uchaguzi.
 
Back
Top Bottom